Kwa nini wazee nchini China 'hukodi watoto' ili kupata faraja?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

"Changamoto kubwa zaidi ilikuwa upweke, bila shaka. Wakati mwingine nilipotaka kuzungumza na mtu, nilikuwa nikizungumza na televisheni."

Yang, mwenye umri wa miaka 91, anaishi katika vitongoji vya Beijing, mji mkuu wa China wenye shughuli nyingi. Baada ya kifo cha mumewe, alihisi upweke mkubwa kiasi cha kufikiria hata kujiua kwa msaada wa kitabibu.

"Nilimuuliza mwanangu kuhusu jambo hilo, lakini aliniambia kuwa limepigwa marufuku. Nilimwambia kuwa iwapo siku moja litaruhusiwa kisheria, ningependa kufanya hivyo,sikutaka kuendelea kuishi katika hali hii."

Akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa glakoma unaosababisha uharibifu wa kuona, hali ya macho yake ilizidi kuwa mbaya kadri muda ulivyosonga. Hali hiyo ilimfanya ashindwe kufanya hata shughuli za kawaida, kama vile kurekebisha kiyoyozi.

Visa vya watu kama Yang vinazidi kuongezeka katika miji ya China. Kwa mujibu wa Teresa Kuan, profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Kichina cha Hong Kong, hali hiyo "inachochewa zaidi na muundo wa jamii na namna watu wanavyowasiliana."

Nchini China, kuna sababu nyingi zinazochangia upweke. Kwa mfano, watu wanaohama kutoka maeneo ya vijijini kutafuta fursa za kiuchumi huacha nyuma mitandao imara ya kijamii inayowasaidia na kwenda kuishi mijini, ambako upweke na kutokuwa na uhakika wa maisha vinaweza kuwa vigumu kukabiliana navyo. Hali kama hiyo pia huwakumba vijana wanaoondoka katika maeneo yao ya nyumbani kutafuta ajira sehemu nyingine za nchi.

"Tunajiona kuwa sehemu ya jamii," Yingwei aliiambia BBC. "Hii ina maana ya kujiweka katika nafasi ya wazee na kuzingatia kikamilifu mahitaji yao."

Kwa mfano, huenda wazee wakawa wanatumia maji ya bomba yenye ukungu na kiwango kikubwa cha chokaa. Ninaweza kutatua tatizo hilo kwa kuwawekea tangi la maji lenye kichujio. Jambo dogo kama hilo linaweza kuwafanya wawe na furaha zaidi.

"Huenda wasiweze kuoga kwa sababu vifaa vyao vimeharibika. Nitanunua kifaa kinachohitajika, nitakibadilisha, na wataweza kuoga bila matatizo yoyote."

Aliongezea kuwa "Wazee wanatuchukulia kama watoto wao, nasi tunawachukulia kama wazazi wetu."

Huduma zinazotolewa na Yingwei zinagharimu chini ya nusu ya gharama ya kumwajiri mlezi.

Hata hivyo, kwa sasa, sekta inayokua kwa kasi sana ni ya huduma zinazolenga kupunguza upweke na kuziba mapengo hayo katika maisha ya watu.

Yang anasema maisha yake yamebadilika pakubwa kutokana na mojawapo ya huduma hizo, inayotolewa na Wang Yingwei na timu yake ya wasambazaji wa chakula wanaotumia skuta za umeme.

Mwanzoni, walikuwa wakimletea chakula cha moto mara mbili kwa siku, lakini msaada wao unaenda mbali zaidi ya hapo.

.

Wazee wanaotaka kuendelea kuishi nyumbani

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwanamume huyo, ambaye hapo awali alikuwa muuzaji wa simu za mkononi, anasema alianzisha kampuni yake ili kuwasaidia wazee kuendelea kuishi katika nyumba zao bila kulazimika kuhamia katika makazi ya wazee.

Alipata wazo hilo baada ya baba yake wa kambo, aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Alzheimer, kulazimika kupelekwa katika kituo cha kulelea wagonjwa.

Yingwei anaeleza kuwa hali ya maisha katika kituo hicho ilikuwa duni kiasi cha kumfanya atake kuhakikisha kuwa watu wengine wanaweza kuepuka kupelekwa katika vituo kama hivyo kwa muda mrefu iwezekanavyo.

Biashara yake ndogo kwa sasa ina wafanyakazi wanne, lakini anasema inaweza kukua kadiri mahitaji ya huduma hizo yanavyoongezeka.

Ingawa bado hakuna takwimu za kuaminika kuhusu ukubwa wa sekta hii, ambayo watoa huduma wanasema imekua kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni, kampuni ya udalali wa masuala ya fedha ya Sinolink inakadiria thamani yake kufikia takriban dola bilioni 7.4 mwaka 2025.

Thamani hiyo inatarajiwa kuendelea kuongezeka kutokana na mabadiliko katika mitindo ya maisha ya kisasa.

Zheng Ruizhi, mteja mwingine wa Yingwei anayeishi katika vitongoji vya kaskazini mwa Beijing, alimkaribisha mlangoni kwa tabasamu pana.

"Tangu nilipostaafu, sijapata fursa nyingi za kukutana na watu," mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 75, ambaye mwanawe anaishi umbali wa saa mbili kutoka kwake, aliiambia BBC.

Alikuwa akipata nafuu baada ya kupata jeraha hivi karibuni, ambalo alisema lilikuwa limemfanya ashindwe kutekeleza kwa urahisi shughuli za kila siku.

.

Hata hivyo, kuwasili kwa Yingwei, ambaye humwita "mpendwa wangu mdogo", kulimchangamsha.

"Ninakuita 'mpenzi' kwa sababu nakupenda sana. Ninakuthamini kwa dhati kutoka moyoni mwangu. Pia ninakuheshimu na kukuamini. Unaponisaidia, sina wasiwasi wala hofu," alimwambia.

Hata hivyo, huduma zinazotolewa na kampuni katika sekta hii haziishii tu katika kutembelea watu majumbani.

Kwa mfano, Liu Yanyan, mwenye umri wa miaka 23, anafanya kazi kama "msindikizaji wa wagonjwa" hospitalini. Kazi yake ni kuwapeleka wagonjwa kwa madaktari au kuwachukulia majibu ya vipimo na dawa katika hospitali za jiji, ambazo zinaweza kuwatisha watu kutokana na ukubwa wake na urasimu uliopo.

"Baadhi ya wateja wangu ni vijana walio na umri wa miaka 20 na kitu ambao wamekuja Beijing kujenga maisha yao ya kikazi. Huenda wasiwe na marafiki hapa, au wakasita kuwaomba wenzao wa kazini waandamane nao kwa sababu ya utamaduni wa Wachina unaosisitiza kulipiana wema," alieleza.

"Kwa mfano, nikikusindikiza kwenda kwa daktari bila malipo, unaweza kuhisi kuwa una wajibu wa kunialika chakula cha mchana au kwenda nami kutazama filamu baadaye."

Aliongeza kuwa, kwa sababu hiyo, watu wengi katika jamii ya kisasa ya China huwa na tabia ya kujitenga.

"Ndiyo maana huwa wanatafuta huduma za watu kama mimi ili niwasindikize hospitalini. Iwapo wangelazimika kwenda peke yao, huenda wakahisi hofu au wasiwasi."

.

Kiini cha huduma zinazotolewa na kampuni nyingi nchini China katika kupambana na upweke ni wazo rahisi: kuunganisha watu na kuwajengea mahusiano ya kibinadamu.

Teresa Kuan alieleza kuwa baadhi ya watu hupendelea kueleza siri na matatizo yao kwa mtu wasiyemfahamu kabisa, badala ya rafiki au mtu wa karibu, kwa malipo.

Iwapo mtu huyo analipwa kwa ajili ya kukusindikiza, uhusiano huo hauwi wa usawa kabisa.

"Huu ni uhusiano wa mtoa huduma na mteja, ambao huepusha hali ya kutotabirika inayoweza kujitokeza katika mahusiano ya kawaida. Changamoto ya urafiki ni kwamba hauwezi kutabirika. Huwezi kujua ni wakati gani mtu anaweza kukukatisha tamaa. Kinyume chake, katika uhusiano wa huduma, unakuwa na picha iliyo wazi zaidi kuhusu kile unachoweza kutarajia."

Msaada wa kihisia

Wang Zhoutao anaendesha kampuni ya matembezi ya milimani inayowasaidia watu wanaotaka kupanda mlima maarufu wa Huangshan, katika jimbo la Anhui nchini China.

"Tunahakikisha tunawapa moyo, kwa mfano kwa kuwatia hamasa, kuwapiga picha au kuwasimulia vichekesho. Kwa hakika, hii ni huduma inayolenga kuwapa watu msaada," alisema.

Mwanamume huyo, ambaye hapo awali alikuwa mwanajeshi, aliongeza kuwa kwa kawaida hupanda mlima huo na wateja wake kati ya siku 10 na 15 kwa mwezi. Ratiba yake inapokuwa na shughuli nyingi, anaweza kupanda mlima huo hadi mara 30 kwa mwezi.

.

Alitoa mfano wa mwanamke kijana aliyewahi kumsindikiza kupanda mlima, ambaye alihisi kutengwa kazini.

"Alijihisi hana manufaa na alitaka kujithibitishia kuwa ana uwezo wa kufanya jambo fulani," alisema.

"Tulianza kupanda mlima, lakini safari ilikuwa ngumu kwa sababu kulikuwa na joto kali na tulikuwa tukitokwa na jasho jingi. Wakati mwingine alitaka kukata tamaa, lakini nilimwambia, 'Ukikata tamaa sasa na kushindwa hata kupanda mlima huu, utawezaje kukabiliana na changamoto nyingine maishani?' Niliendelea kumtia moyo bila kuchoka."

Baada ya kufika kileleni mwa mlima, mwanamke huyo alimtumia ujumbe mrefu wa kumshukuru, akieleza safari yake ya ndani ya kujitambua na kutoa shukrani zake.

"Maisha ya siku hizi yana shughuli nyingi kupita kiasi. Watu wanakabiliwa na shinikizo kazini, katika mahusiano na kutokana na matarajio ya familia," alisema. "Nadhani wateja wangu wengi ni watu wanaohisi kuna pengo katika mahusiano yao au ambao wamekumbana na changamoto zilizowakatisha tamaa."

Uhusiano wa kibinadamu ni hitaji muhimu, lakini katika jamii inayokabiliana na tatizo la upweke, sasa umekuwa pia bidhaa inayoweza kununuliwa.

Akiwa tena katika nyumba yake ndogo jijini Beijing, Yang anasema sasa anajisikia vizuri zaidi baada ya Yingwei kutatua tatizo lake na kufanya kiyoyozi kifanye kazi ipasavyo.

"Ni vizuri kuwa na mtu kando yako unapomhitaji, mtu ambaye unaweza kumweleza mawazo yako ya ndani kabisa," alisema.

"Nilikuwa na tatizo la upweke, lakini nimeweza kulishinda. Nina furaha kwa kiasi kikubwa."

"Siwezi kuishi bila Yingwei na wengine. Wote wana mioyo mizuri."