Ufaransa yakabiliwa na maandamano mapya yanayopinga kupanda kwa gharama za maisha

Chanzo cha picha, Reuters
Ufaransa inakabiliwa na wimbi jipya la maandamano yanayopinga kupanda kwa gharama za maisha na kuzorota kwa hali ya elimu shuleni, huku kukiwa na hofu ya kurudiwa kwa vurugu na uporaji wa maduka ulioshuhudiwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Serikali imesema itatuma maafisa 70,000 wa polisi katika maeneo mbalimbali nchini humo na kuahidi kuchukua hatua mara moja iwapo dalili zozote za machafuko zitajitokeza.
“Hatutavumilia kitendo chochote cha uvunjifu wa sheria,” amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurent Nuñez.
Ameongeza kuwa serikali haitakuwa na msamaha kwa waharibifu wa mali, waporaji na wote wanaojihusisha na vitendo vya vurugu. Amesema pia kuwa, mbali na maandamano yaliyopangwa, kumekuwa na jumbe nyingi za uchochezi wa vurugu kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa makundi ya mrengo wa kushoto na mrengo mkali wa kushoto.
Mjini Paris, wafanyabiashara wamefunga au kuimarisha ulinzi wa maduka yao kuzuia uharibifu unaoweza kutokea. Mji wa Orléans, kusini mwa Paris, ni miongoni mwa maeneo yanayotia wasiwasi mkubwa.
Katika siku za hivi karibuni, mamia ya watu wamehukumiwa kifungo kwa uharibifu wa mali, uchomaji moto na uporaji, baada ya kusikilizwa kwa kesi zao kwa utaratibu wa haraka.
Hasira na kukata tamaa vimeongezeka miongoni mwa wananchi wa Ufaransa, ambao wanakabiliwa na gharama za maisha zinazozidi kupanda. Hali hiyo inazidishwa na tahadhari zinazotolewa kuwa serikali zijazo huenda zikapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya umma.
Maandamano hayo yalianza kwa wanafunzi wa shule za sekondari kudai kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia na kutatuliwa kwa uhaba wa walimu na wafanyakazi wengine. Hata hivyo, baadaye baadhi ya maeneo yalikumbwa na vurugu.
Chama cha mrengo wa kulia mkali cha National Rally kinafanya mkutano wake wa mwaka katika mji huo. Kiongozi wake, Marine Le Pen, anatarajiwa kutangaza rasmi nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Soma pia:



























