Kwa nini China imebadili sheria yake ya ulinzi wa taifa?

.
Maelezo ya picha, China imefanya mabadiliko katika Sheria yake ya Uhamasishaji wa Ulinzi wa Taifa, hatua inayotajwa kuwa inalenga kurahisisha mchakato wa kuhama kutoka kipindi cha amani hadi kipindi cha vita.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

China imefanya marekebisho ya kwanza baada ya miaka 16 katika Sheria yake ya Uhamasishaji wa Ulinzi wa Taifa.

Baadhi ya watu nchini Taiwan wanaona hatua hiyo kama maandalizi ya kuelekea "mgogoro mkubwa."

Sheria hiyo mpya itaanza kutumika tarehe 1 Oktoba. Ilipitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge la Taifa la China (NPC) tarehe 28 Agosti. Sheria ya awali ilianza kutumika tarehe 1 Julai 2010.

Sheria mpya imehifadhi muundo wa uhamasishaji wa ulinzi wa taifa uliokuwepo kabla ya marekebisho.

Hii inajumuisha masuala kama vile wakati wa kupeleka wanajeshi, majukumu ya idara mbalimbali za serikali wakati wa uhamasishaji, uandikishaji wa wanajeshi wa akiba na usafirishaji wa kimkakati, pamoja na kuchukua vifaa vya kiraia kwa matumizi ya kijeshi.

Hata hivyo, baadhi ya mabadiliko muhimu yamefanywa.

Ripoti hii inajaribu kuelewa mabadiliko hayo na namna vyombo vya habari vya China na Taiwan vimeyapokea.

Mabadiliko makubwa ni yapi?

Neno "maslahi ya maendeleo" limeongezwa kwenye sheria hiyo, jambo linaloipa China mamlaka zaidi katika suala la uhamasishaji.
Maelezo ya picha, Neno "maslahi ya maendeleo" limeongezwa kwenye sheria hiyo, jambo linaloipa China mamlaka zaidi katika suala la uhamasishaji.

Mabadiliko moja ya kuvutia ni kuongezwa kwa "maslahi ya maendeleo" katika orodha ya sababu zinazoweza kusababisha uhamasishaji.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Sheria ya mwaka 2010 ilisema China inaweza kuanzisha uhamasishaji "wakati mamlaka yake, umoja, uadilifu wa eneo na usalama vinapotishiwa."

Sheria mpya haijaeleza ni nini hasa kinachomaanishwa na "maslahi ya maendeleo," jambo ambalo linaweza kuipa Beijing mamlaka zaidi ya kuamua lini uhamasishaji unahitajika.

Hii inaweza kuiwezesha China kuhamasisha wanajeshi hata wakati wa operesheni za kijeshi zinazolenga kulinda maslahi yake ya kibiashara yanayokua nje ya nchi, ingawa sheria hiyo haisemi hivyo moja kwa moja.

Ufafanuzi wa "Sheria ya Uhamasishaji wa Ulinzi wa Taifa" pia umeongezwa katika Kifungu cha 2 cha sheria ya mwaka 2026.

Inasema hii inamaanisha serikali kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha mabadiliko ya haraka kutoka wakati wa amani kwenda wakati wa vita, pamoja na kubadilisha nguvu za kiuchumi na kijamii kuwa nguvu za ulinzi wa taifa.

Wazo hili jipya la kubadilisha "nguvu za wakati wa amani kuwa nguvu za wakati wa vita" linaonekana katika sehemu mbalimbali za sheria hiyo.

Pia imeongezwa sharti jipya kuhusu miradi na bidhaa za kiraia zinazohusiana kwa karibu na ulinzi wa taifa.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, hasa miradi na bidhaa za kiraia ambazo hazikidhi viwango vya kiraia zitatakiwa kufuata viwango vya kijeshi.

Miundombinu kama reli, bandari na viwanja vya ndege, pamoja na vyombo kama meli za mizigo na ndege za kiraia, vinaweza kuangukia katika kundi hilo.

Sheria hizo mpya zitaiwezesha jeshi kutumia uwezo huo kwa urahisi na kwa haraka zaidi wakati wa uhamasishaji.

Katika mabadiliko mengine, kampuni, taasisi za umma na mashirika ya kijamii yamehimizwa "kuhifadhi kwa kiwango cha kutosha bidhaa za kimkakati" na "kuimarisha uwezo wa kiteknolojia na uzalishaji" ili kukidhi mahitaji ya uhamasishaji wa ulinzi wa taifa.

Sehemu nyingine mpya inaitaka miili miwili ya juu ya kijeshi nchini China — Baraza la Serikali na Tume Kuu ya Kijeshi — kufanya tathmini za kiusalama kuhusu minyororo ya usambazaji wa bidhaa za kijeshi na kuchukua hatua za kuimarisha uimara na usalama wake.

Hii inaendana na juhudi za China za kujitegemea katika bidhaa na teknolojia muhimu ili kukabiliana na vikwazo vya kigeni na vizuizi vya usafirishaji wa bidhaa na teknolojia.

Hata hivyo, sheria ya mwaka 2026 imeondoa kipengele kilichosema Baraza la Serikali na Tume Kuu ya Kijeshi "zitaongoza kwa pamoja" uhamasishaji wa ulinzi wa taifa kote nchini.

Badala yake, inasisitiza uongozi wa pamoja na wa kati wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China katika shughuli za uhamasishaji wa ulinzi wa taifa.

Tetesi kuhusu umri wa kuandikishwa jeshini

Kifungu cha 3 cha sheria hiyo pia kinajumuisha utekelezaji wa "Fikra za Xi Jinping kuhusu Kuimarisha Jeshi."

Mabadiliko haya katika lugha inayohusu uongozi yanaakisi juhudi za Rais Xi Jinping kuimarisha udhibiti wake juu ya jeshi. Sheria ya mwaka 2010 ilitungwa kabla hata hajawa rais.

Kama ilivyokuwa katika sheria ya zamani, sheria mpya imetumia lugha isiyo wazi kuhusu suala la kuandikishwa jeshini.

Kifungu cha 33 kinasema Baraza la Serikali na Tume Kuu ya Kijeshi zitaamua "idadi, aina na mbinu" za kuandikisha wanajeshi wa akiba kulingana na mahitaji ya uhamasishaji wa ulinzi wa taifa.

Umri wa kuandikishwa bado ni miaka 18 hadi 60 kwa wanaume na miaka 18 hadi 55 kwa wanawake, bila mabadiliko kati ya mwaka 2010 na 2026.

Hata hivyo, sheria mpya inasema watu hao "watatakiwa kisheria" kutekeleza majukumu yanayohusiana na ulinzi wa taifa.

Kumekuwa na wasiwasi mkubwa mtandaoni kuhusu suala hili la umri wa kuandikishwa.

Shirika la AFP lilichapisha uchunguzi wa ukweli uliobaini kuwa hakukuwa na mabadiliko katika umri wa kuandikishwa, licha ya tetesi mtandaoni kwamba umri huo ulikuwa umebadilishwa.

Vyombo vya habari vya China vinasema nini?

Mabadiliko katika Sheria ya Uhamasishaji wa Ulinzi wa Taifa yanaangaliwa kwa mashaka na nchi kadhaa.
Maelezo ya picha, Mabadiliko katika Sheria ya Uhamasishaji wa Ulinzi wa Taifa yanaangaliwa kwa mashaka na nchi kadhaa.

Vyombo vya habari vya China kwa ujumla vimewasilisha mabadiliko hayo kama masasisho ya kawaida yanayolenga kuendeleza uboreshaji wa mfumo wa nchi na jeshi.

Madai kutoka nje kwamba China inajiandaa kwa vita maalumu pia yamepuuzwa.

Shirika la habari la serikali, Xinhua, lilisema mabadiliko hayo makubwa yalifanywa ili kukabiliana na "hali mpya" ya uhamasishaji wa ulinzi wa taifa.

Makala ya maoni katika gazeti la serikali la Global Times ilijibu ukosoaji kutoka nje kwa kuuita mjadala kuhusu sheria hiyo kuwa ni wa "wachochezi wa vita."

Ilisisitiza kwamba sheria hiyo "inaakisi kwa uthabiti sifa za msingi za kuwa ya kujihami, ya kawaida na inayofanya kazi kwa mujibu wa sheria."

Kwa mujibu wa tahariri hiyo, lengo ni kuwa tayari kwa uhamasishaji, si kupanga uhamasishaji kwa ajili ya vita.

Iliwashutumu "baadhi ya watu wa Magharibi" na "makundi yanayounga mkono uhuru wa Taiwan" kwa kuipotosha na kutoielewa sheria hiyo.

Ilisema kuweka kisheria uwezo wa kubadilika kutoka hali ya amani kwenda hali ya vita ni "mchakato wa kawaida wa kimataifa" unaofuatwa Marekani na Ulaya.

Jin Canrong, mchambuzi maarufu kutoka Chuo Kikuu cha Renmin, pia alisema mabadiliko hayo hayamaanishi maandalizi ya moja kwa moja ya kuishambulia Taiwan.

Aliwataka watu wa nje "kutotafsiri kupita kiasi" sheria hiyo.

Alisema lengo lake ni kuboresha tu mfumo wa uhamasishaji kwa ajili ya "hali mbaya zaidi inayoweza kutokea", na si suala lolote maalumu.

Vyombo vya habari vya Taiwan vinasema nini?

Vyombo vya habari vya Taiwan vinasema kuwa hatua hii ni maandalizi ya China kwa ajili ya vita.
Maelezo ya picha, Vyombo vya habari vya Taiwan vinasema kuwa hatua hii ni maandalizi ya China kwa ajili ya vita.

Vyombo vya habari vya Taiwan, hasa vinavyounga mkono uhuru wa Taiwan, vinasema mabadiliko hayo ni sehemu ya juhudi za China za kuunganisha Taiwan na China.

Kwa mujibu wa gazeti la lugha ya Kiingereza la Taipei Times, afisa mmoja wa Taiwan alisema sheria hiyo mpya iliundwa kumsaidia Rais Xi Jinping kutimiza "jukumu lake la kihistoria la kuunganisha taifa."

Afisa huyo alilinganisha uwezo wa kujihami wa Taiwan na juhudi za China za kuongeza "uwezo wa kushambulia."

Alisema sheria hiyo imeundwa kuhakikisha kwamba hakuna "vikwazo wala vikwazo vya kimataifa" vinavyoweza kuzuia shambulio lolote la China.

Ripoti nyingine ya shirika la habari la Central News Agency (CNA), linalohusishwa na serikali ya Taiwan, ilimnukuu Hung Pu-chao wa Chuo Kikuu cha Taipei akisema sheria hiyo inaweza kuiwezesha China kupata msingi wa kisheria wa hatua zake iwapo kutatokea vita na Taiwan na kujaribu "kuhalalisha" hatua zake mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Alisema Beijing kwa muda mrefu imekuwa ikitumia sheria za ndani kuwasilisha Taiwan kama suala lake la ndani.

Hung pia alisema mabadiliko hayo yanaweza kulenga nchi nyingine ambazo China ina migogoro ya mipaka nazo, zikiwemo Ufilipino, India na Japan.

Wachambuzi wengine wanasema hatua hiyo imepangwa kwa wakati unaoweza kumsaidia Xi Jinping kudumisha udhibiti wake wa madaraka kabla ya kutangaza uwezekano wa kuhudumu kwa muhula wa nne ambao haujawahi kutokea mwaka 2027.

Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Ambia Hirsi