Ibrahim Traoré: Kwa nini Burkina Faso imepiga marufuku maneno 'nchi maskini' na 'nchi ndogo'?

Chanzo cha picha, Presidency of Burkina Faso
Tangu kuanza kwa mwaka wa masomo tarehe 1 Oktoba 2026, mamlaka za Burkina Faso zimeanza mchakato wa "kuondoa athari za ukoloni" katika historia inayofundishwa ndani ya mfumo wake wa elimu.
Nchini Burkina Faso, mapambano dhidi ya ubeberu yanayohimizwa na mamlaka tangu kutangazwa kwa Mapinduzi ya Kimaendeleo ya Umma mwezi Aprili 2025 na Kapteni Ibrahim Traoré, pia yanahusisha mapinduzi ya kumbukumbu na historia, kulingana na mamlaka hizo.
Katika taarifa ya Septemba 7, 2026, Waziri wa Elimu ya Sekondari na Mafunzo ya Ufundi na Teknolojia, Profesa Moumouni Zoungrana, alisema kuwa kuna "misemo katika masomo ya historia na jiografia ambayo haitoi heshima kwetu."
"Hii ina maana kwamba hata katika vitabu vyetu vya kiada kuna taarifa za uongo zilizorekodiwa kwa lengo la kutufanya tuonekane kama watoto, kutudhalilisha na kutufanya tusifikirie kwa kina. Na tumetumia muda wetu mwingi kukuza maadili haya potofu ambayo tumeyapitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine," alisema.
Aliendelea kwa kuialika jamii ya elimu ya Burkina Faso kuwa na "uthubutu wa kuvunja kabisa mifumo ya zamani na kuibadilisha kwa msingi mpya."
Profesa Zoungrana kisha alitangaza marekebisho ya mitaala, ikiwemo masomo ya Historia, Jiografia na Elimu ya Uraia, kwa lengo la kuondoa, kwa mujibu wake, misemo na maudhui yanayoonekana kuwa "hayana mantiki" au yasiyolingana na uhalisia wa taifa la Burkina Faso.
Masomo haya matatu yanaonekana kuwa ya dharura zaidi wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa mageuzi makubwa ya mfumo wa elimu wa Burkina Faso yanayojulikana kama "Mkataba wa Neekre", uliozinduliwa tarehe 17 Oktoba.
Wakati wakisubiri kukamilika kwa uandishi upya wa vitabu vya Historia, Jiografia na Elimu ya Uraia, waraka maalumu wenye mabadiliko ya haraka tayari umesambazwa kwa walimu.
Mabadiliko hayo yanahusisha kubadilishwa kwa baadhi ya misemo na istilahi, kuanzishwa kwa sura mpya za masomo, pamoja na kupigwa marufuku kwa baadhi ya misemo na mada zilizokuwa zikifundishwa hapo awali.
Hapa kuna baadhi ya misemo na mwelekeo (au mabadiliko) ambayo yamebadilika nchini Burkina Faso tangu tarehe 1 Oktoba:

Chanzo cha picha, DCRP/MESFPT
1.Misemo iliyobadilika
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika somo la Historia, maneno na misemo ishirini na saba imeondolewa kwenye msamiati wa walimu na wanafunzi.
Wavamizi na majasusi: Miongoni mwa dhana zilizobadilishwa, ukoloni sasa unaitwa uvamizi wa kiimla, mkoloni au mkaazi wa kikoloni anaitwa mvamizi, na wagunduzi wanaitwa majasusi. Aidha, makoloni sasa yanatajwa kama maeneo yaliyovamiwa.
Uvamizi wa Kifaransa wa Kiimla nchini Burkina Faso: Huu sasa ndio msemo unaotumika kuelezea ukoloni wa Kifaransa nchini Burkina Faso.
Ukombozi wa Afrika: Dhana ya kuondoa ukoloni na kupata uhuru sasa inatajwa kama Ukombozi wa Afrika. Vivyo hivyo, vipindi vya historia vinagawanywa katika kabla ya uvamizi na baada ya uvamizi, badala ya enzi za kabla na baada ya ukoloni.
Vita vya uvamizi wa kurejea: Kuanzia sasa, ugaidi unaelezewa kama vita vya uvamizi wa kurejea. Neno wapiganaji wa bunduki wa Senegal limebadilishwa kuwa wapiganaji wa vita wa Afrika, huku wanajeshi wastaafu wa vita wakitajwa kama maveterani wa vita wa Afrika.
Masomo ya historia kuhusu biashara ya watumwa ya Mashariki na biashara ya watumwa ya Atlantiki sasa yanaitwa uhamishaji wa lazima wa Waafrika wa Mashariki na wa Atlantiki.
Katika somo la Jiografia, takribani dhana kumi zilizochukuliwa kuwa za kudhalilisha pia zimeondolewa.
Burkina Faso, ambayo hapo awali ilielezwa kama nchi isiyo na bandari ya bahari, sasa inatajwa kama nchi ya bara.
Neno makabila limebadilishwa na makundi ya kijamii na kitamaduni.
Udhaifu na vikwazo vya nchi sasa vinaelezwa kama changamoto na fursa.
Dhana ya maendeleo imepewa mtazamo wa kienyeji na sasa inajulikana kama maendeleo yanayotokana na rasilimali na uwezo wa ndani.
Somo la Elimu ya Uraia na Maadili (ECM) limebadilishwa jina kabisa na sasa linaitwa Elimu ya Uraia na Uzalendo (ECP).

Chanzo cha picha, Prime Minister's Office of Burkina Faso
2. Misemo na Mada za masomo zinazoondolewa
Misemo kadhaa yenye maelezo yanayoonekana kuwa ya kudhalilisha, hasa katika somo la Jiografia, sasa imepigwa marufuku kutumika shuleni. Maneno kama nchi maskini, nchi yenye madeni, nchi ndogo, hali ya hewa isiyofaa, na mengineyo, hayaruhusiwi tena kutumika.
Pia, hairuhusiwi tena kuweka makundi ya kijamii na kitamaduni katika asilimia za makabila au dini.
Baadhi ya mada za Jiografia, hasa zile zinazofundishwa katika kidato cha pili (darasa la 8), zinaondolewa kwenye mtaala. Miongoni mwa mada zilizoondolewa ni somo la biashara ya pembetatu (triangular trade).
Aidha, sura iliyokuwa imejitolea kwa uchunguzi wa jiografia ya kimaumbile ya Ulaya imeondolewa kabisa.
Mwalimu mmoja aliyezungumza na BBC Africa alisema:
"Msisitizo sasa umewekwa zaidi kwenye mazingira ya asili na maendeleo ya Afrika."
Alieleza kuwa lengo ni kuelekeza zaidi ufundishaji katika hali za kiasili na maendeleo ya bara la Afrika badala ya kuangazia maeneo mengine kama Ulaya.
3. Mada mpya katika Mtaala
Wakati huo huo, masomo mapya ya Historia na Jiografia yanaanzishwa katika ngazi za elimu ya msingi ya juu na sekondari.
Katika darasa la sita, somo jipya linaloitwa "Dhana ya Mapinduzi" limeongezwa. Hii ni mada ambayo mamlaka zinaiona kuwa muhimu katika kuleta mabadiliko makubwa nchini.
Akizungumza na vijana wa Burkina Faso wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana mwezi Agosti uliopita, Waziri Moumouni Zoungrana alisema kwamba:
"Mapinduzi ndiyo chaguo pekee linalowezekana la kuvunja urithi wa zamani na kuhakikisha uhuru kamili wa Burkina Faso katika nyanja za uchumi, fedha na siasa."
Masomo mawili mapya pia yameongezwa katika mtaala wa Historia wa darasa la tano. Haya ni:
- Maarifa na Ujuzi wa Kiafrika
- Mapinduzi ya Burkina Faso
Somo la "Mapinduzi ya Burkina Faso" linahusu misingi na malengo ya Mapinduzi ya Kidemokrasia na Kijamii (RDP) ya Kapteni Thomas Sankara, aliyeiongoza Burkina Faso kati ya mwaka 1983 na 1987, pamoja na Mapinduzi ya Maendeleo ya Umma (RPP) ya Kapteni Ibrahim Traoré, yanayoendelea tangu mwishoni mwa mwaka 2022.
Kwa wanafunzi wakubwa wa darasa la nane, somo jipya linaloitwa "Mapinduzi ya Haiti" limeanzishwa. Somo hili linarejelea harakati za kupigania ukombozi wa watu wa Haiti, mafanikio yao pamoja na makosa yaliyotokea katika harakati hizo.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na vyombo vya habari mwishoni mwa Septemba, Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, aliwahimiza wananchi wake:
"Someni historia ya Haiti na muelewe kwamba si jambo la busara kucheza na watu hao," akirejelea mataifa yaliyokuwa madola ya kikoloni hapo awali.



































