Chanjo ya saratani ya ngozi yaonyesha matokeo ya kutia moyo katika majaribio

Chanzo cha picha, ETH ZURICH
Chanjo ya saratani iliyoundwa kulingana na vinasaba vya kila mgonjwa imepunguza kwa asilimia 42 hatari ya saratani ya ngozi kujirudia au mgonjwa kufariki, inapotumiwa pamoja na matibabu ya kawaida yanayochochea mfumo wa kinga ya mwili kupambana na saratani.
Matokeo hayo yametokana na utafiti mkubwa uliofanywa na kampuni za dawa za Moderna na MSD.
Utafiti huo ulihusisha wagonjwa zaidi ya 1,100 waliokuwa na melanoma, aina hatari ya saratani ya ngozi. Vivimbe vya saratani kwa wagonjwa hao vilikuwa vimeondolewa kwa upasuaji.
Washiriki wote walipatiwa Keytruda, dawa ya tiba ya kinga inayosaidia mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kushambulia seli za saratani.
Takriban theluthi mbili ya washiriki pia walipatiwa chanjo ya majaribio inayoitwa intismeran.
Watafiti walibaini kuwa wagonjwa waliopokea chanjo hiyo pamoja na tiba ya kinga walikuwa na uwezekano mdogo zaidi wa saratani kujirudia. Pia, katika kipindi cha miaka miwili, hatari ya saratani kusambaa hadi sehemu nyingine za mwili ilipungua kwa asilimia 38 ikilinganishwa na wagonjwa waliopokea tiba ya kinga pekee.
Chanjo hiyo inatumia teknolojia ya mRNA, inayotumika pia katika baadhi ya chanjo za Covid 19.
Hata hivyo, tofauti na chanjo za kawaida, chanjo hii hutengenezwa mahsusi kwa kila mgonjwa kwa kutumia taarifa za kijenetiki kutoka kwenye uvimbe wake wa saratani. Lengo ni kuufundisha mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kuharibu seli za saratani iwapo zitajirudia.
Wanasayansi walioshiriki katika utafiti huo wanasema matokeo hayo yanaweza kuwa hatua muhimu katika kuendeleza matibabu ya saratani yanayolenga mahitaji ya kila mgonjwa.
Profesa Pippa Corey, daktari bingwa wa saratani aliyeshiriki katika utafiti huo, ameelezea matokeo hayo kuwa uthibitisho wa umuhimu wa teknolojia hiyo.
Mbinu hiyo pia inafanyiwa majaribio kwa wagonjwa wenye aina nyingine za saratani, zikiwemo za figo, kibofu cha mkojo na mapafu.
Hata hivyo, wataalamu huru wameonya kuwa bado kuna haja ya kufuatilia wagonjwa kwa muda mrefu zaidi ili kubaini iwapo matibabu hayo yanaongeza muda wa kuishi kwa ujumla.
Profesa Alan Melcher wa Taasisi ya Utafiti wa Saratani amesema matokeo hayo ni ya kutia moyo, lakini mafanikio katika kutibu melanoma hayamaanishi kuwa mbinu hiyo itafanya kazi kwa kila aina ya saratani.
Moderna na MSD zimesema zinaendelea kujadiliana na mamlaka za udhibiti kuhusu matokeo hayo, huku uwezekano wa kuwasilisha maombi ya kuidhinisha chanjo hiyo ukitarajiwa ndani ya mwaka ujao.
Utafiti huo utaendelea kuwafuatilia wagonjwa kwa muda mrefu zaidi. Matokeo kamili yanatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa saratani utakaofanyika Madrid. Hata hivyo, matokeo hayo bado hayajachapishwa katika jarida la kitaalamu la tiba linalopitia tafiti kabla ya kuchapishwa.
Soma Pia:

































