Kuondoa 30% ya uume wangu, kuliokoa maisha yangu

Muda wa kusoma: Dakika 3

Alastair Munro alipogundua ana uvimbe mdogo kwenye uume wake, alihisi kuwa huenda ni jambo hatari kwa afya yake.

Aliahirisha kwenda hospitali kwa takriban wiki sita,ila alipomuona daktari wa familia,aliambiwa huenda ni saratani.

"Ni kauli iliyotolewa na ujasiri," Alastair, mwenye umri wa miaka 49, alisema. "Nilishtuka sana. Daktari hakuweza kusema kwa uhakika wa 100%, lakini alihisi ni saratani."

"Wiki moja baadaye, daktari wa mfumo wa mkojo pia alianiambia hivyo hivyo . Kisha ikawa ni kusubiri kufanyiwa vipimo vya uchunguzi wa seli maarufu biopsy."

Miezi mitatu baada ya kugundua uvimbe huo kwa mara ya kwanza, Alastair, ambaye ni mhandisi wa ujenzi kutoka Inverness, alipata uthibitisho kuwa alikuwa na saratani ya uume {penile cancer}, huu ni ugonjwa adimu unaowapata wanaume 80 hadi 90 kwa mwaka nchini Scotland na 700 nchini Uingereza.

"Nilishtuka sana lakini tayari nilikuwa na hisia kuwa ni saratani," aliambia BBC.

"Sijawahi kabisa kusikia aina hii ya saratani "

Uchunguzi wa Tomografia au CT scan ulithibitisha kuwa saratani aliyokuwa nayo tayari ilikuwa imeanza kusambaa.

Alastair alifanyiwa upasuaji uliohusisha kuondolewa kwa uvimbe aliokuwa nao pamoja na asilimia 30 ya uume wake katika operesheni iliyochukua saa saba.

Saratani hiyo pia ilikuwa imeenea hadi kwenye tezi za limfu katika sehemu ya kinena chake, hivyo zililazimika kuondolewa pia.

Baadaye, uume wake ulitengenezwa upya kwa kutumia kipande cha ngozi kilichochukuliwa kutoka kwenye paja lake.

Wiki sita baadaye, Alastair, ambaye anatoka Kingussie, alilazimika kufanyiwa upasuaji mwingine uliodumu kwa saa tatu na nusu baada ya matokeo ya upasuaji wa kwanza kuonyesha kuwa bado kulikuwa na kiasi kidogo cha uvimbe kilichosalia.

Kulikuwa na uwezekano wa asilimia 50 kwamba saratani hiyo ingeweza kusambaa hadi kwenye eneo la nyonga lake.

"Hawawezi kujua kama ni saratani hadi wanapoingia ndani ya mwili,wanachofanya ni kukata sehemu zilizoathirika na kuzichunguza papo hapo. Ni kama wanachimba ndani yako."

"Wanaendelea kufanya hivyo hadi wanapofika mwisho wa uvimbe huo wa saratani. Ni njia ya zamani, lakini ndivyo wanavyofanya. Ni jambo la kushangaza."

Baada ya hapo, Alastair alipitia mzunguko wa tiba ya radiotherapy kwa mwezi mmoja na baadaye kuambiwa hana tena dalili za saratani mapema mwezi Februari.

Kwa sasa hawezi kufanya tendo la ndoa wala kukojoa kawaida kwa sababu ameathirika na tatizo la lymphedema kama madhara ya upasuaji na tiba ya radiology ambayo pia imesababisha uvimbe wa ngozi.

Inatarajiwa kuwa atafanyiwa upasuaji wa kufanyiwa marekebisho baada ya mwaka mmoja ili kuboresha hali hiyo.

Ameambiwa pia kuwa kuna uwezekano mkubwa wa saratani hiyo kurudi ndani ya miaka miwili.

"Kuongeza ufahamu"

Alastair anasema kuwajulisha familia yake kuhusu saratani hiyo ilikuwa vigumu sana, hasa kwa kuwa ni ugonjwa ambao watu wengi hawaujui.

"Lengo lote ni kuongeza uelewa kuhusu saratani za wanaume," alisema.

"Ni ugonjwa mgumu sana kutambuliwa mapema. Dalili zake ni chache sana. Inaweza kuwa tu doa dogo kwenye uume wako."

"Ukiona uvimbe wowote au una matatizo ya nguvu za kiume au damu, nenda ukapimwe hospitalini."

Uvimbe wa Alastair ulikuwa kwenye kichwa cha uume wake.

Haikuwa na maumivu, lakini ilikuwa ikiongezeka kwa ukubwa kila siku, na wakati mmoja aligundua pia kulikuwa na damu eneo hilo.

Upasuaji wake ulifanywa na Daktari wa upasuaji wa mfumo wa mkojo CJ Shukla katika Hospitali ya Western General eneo la Edinburgh,Uingereza.

Hii ni mojawapo ya vituo viwili pekee nchini Scotland vinavyoweza kutibu saratani adimu za wanaume.

"Nataka kuwashukuru madaktari wa upasuaji na wafanyakazi wote wa Western General Edinburgh pamoja na wauguzi wa jamii," alisema.

Kulingana na Dkt Shukla aina hii ya saratani ya uume huletwa na uvutaji sigara, unene kupita kiasa na maambukizi ya virusi vya HPV.