Aspirini inaweza kupunguza hatari ya kupata saratani – unajua ni kwa nini?

    • Author, Miriam Frankel
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Dawa hiyo ya miaka 4,000, ambayo hutumika kutibu maumivu, huzuia uvimbe fulani kujitokeza na kuenea mwilini.

Nick James, Mwingireza na mtengenezaji wa samani akiwa na umri wa miaka 40, alianza kuwa na wasiwasi kuhusu afya yake baada ya mama yake kufariki kutokana na saratani na kaka yake, pamoja na wanafamilia wengine kadhaa, baadaye kupata saratani ya utumbo.

Alichagua kufanyiwa vipimo vya kijenetiki, na akagundulika kuwa na jeni yenye hitilafu ambayo husababisha Lynch Syndrome, yaani mabadiliko ya jeni - ambayo huongeza hatari ya kupata aina hiyo ya saratani.

Hata hivyo, msaada ulitoka mahali pasipotarajiwa, wakati James alipokuwa mtu wa kwanza kujiandikisha kwa jaribio la kimatibabu lililolenga kupima kama dozi ya kila siku ya aspirini - dawa ya kutuliza maumivu - inaweza kumlinda dhidi ya kupata saratani.

Takriban 80% ya watu wenye tatizo la Lynch hupata saratani ya utumbo katika maisha yao. Lakini hadi sasa, mambo yanaonekana kuwa mazuri kwa James. "Amekuwa akitumia aspirini kwa miaka 10 bila saratani yoyote hadi sasa," anasema John Burn, profesa wa jeni katika Chuo Kikuu cha Newcastle, ambaye aliongoza jaribio hilo.

Inaonekana vigumu kuamini, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na dalili kwamba dawa hiyo inaweza kupunguza uwezekano wa kuenea kwa saratani ya utumbo mpana.

Historia ya Aspirin

Mwishoni mwa karne ya 19, wanaakiolojia waligundua vidonge vyenye umri wa miaka 4,400 kutoka mji wa kale wa Nippur huko Mesopotamia – ambayo ni Iraq ya sasa. Ni orodha ya dawa mbalimbali zilizotengenezwa kutokana na mimea, wanyama na madini.

Miongoni mwao kulikuwa na kidonge kinachotokana na mti wa msafsafi (Willow tree). Mti huu una kemikali inayoitwa salicin, ambayo mwili unaweza kuibadilisha kuwa asidi ya salicylic ambayo husaidia kutuliza maumivu. Wamisri, Wagiriki na Warumi - pia walitumia dawa hiyo.

Utafiti wa zama hizi kuhusu dawa hiyo ulianza mwaka 1763, wakati mchungaji wa Kiingereza Edward Stone alipowaandikia wanasayansi wa Royal Society kuwaelezea dawa ya kupambana na homa itokanayo na gome la mti wa Willow lililokaushwa na unga. Karibu karne moja baadaye, wanasayansi waliweza kuchanganya asidi ya salicylic na asidi ya acetylsalicylic na kutengeneza dawa ya aspirin chini ya kampuni ya Bayer.

Karne nyingine tena, wanasayansi walianza kugundua faida za aspirini katika kuzuia magonjwa ya moyo na mishipa - kupunguza hatari ya kuganda kwa damu kwa kufanya damu iwe nyepesi na chembe chembe za damu zisishikamane sana.

Kwa sababu hii, mashirika kama Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza yanapendekeza dozi ya kila siku kwa watu walio na hatari ya mshtuko wa moyo au kiharusi.

Kufikia mwaka 1972, faida zimeongezeka hadi kuzuia saratani, pamoja na utafiti juu ya panya waliodungwa seli za saratani. Wanasayansi wa Marekani waligundua kwamba kumwaga aspirini katika maji ya kunywa ya mnyama huyo kulipunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya saratani kuenea mwilini - ikilinganishwa na panya ambao hawakupewa dawa hiyo.

Mabadiliko yalitokea mwaka 2010, wakati Peter Rothwell, profesa wa neurolojia katika kliniki ya Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, alipochunguza tena kuhusu aspirini kama kinga ya ugonjwa wa moyo na mishipa. Katika uchambuzi wake, dawa hiyo ilionekana kupunguza kuenea kwa saratani.

Ushahidi wa kutosha

Mwaka 2020, John Burn alichapisha matokeo ya jaribio muhimu kwa wagonjwa 861 wenye ugonjwa wa saratani. Baada ya kushiriki kwa miaka 10, timu yake iligundua kuwa watu ambao walikuwa wakitumia dozi ya aspirini ya 600mg kila siku kwa angalau miaka miwili walipunguza kwa nusu hatari ya kupata saratani ya utumbo mpana.

Timu yake imefanya jaribio la pili. Matokeo ya awali yanaonyesha, "watu waliotumia aspirini kwa miaka miwili walikuwa na saratani chache kwa 50% kwenye utumbo mpana," anasema. "Tunachotaka kufanya ni kuendelea kwa miaka michache zaidi kwa sababu data itazidi kuwa bora kadri muda unavyosonga.”

Dozi ndogo ya (75-100mg) ni sawa na ile ambayo watu hutumia kwa ajili ya kuzuia matatizo ya moyo na mishipa. Hilo ni muhimu, kwa kuwa aspirini inaweza kuja na madhara, ikiwa ni pamoja na kusababisha chakula kutosagwa tumboni, kutokwa na damu ndani, vidonda vya tumbo na hata kutokwa na damu kwenye ubongo, lakini dozi ndogo inaweza kuvumiliwa vyema na mwili.

Sasa inapendekezwa, watu wenye tatizo la Lynch wanapaswa kuanza kutumia aspirini wakiwa na umri wa miaka 20 au 35 kutegemea na ukubwa wa tatizo.

Bado haijabainika kama aspirini inaweza kuwalinda watu na wagonjwa kutokana na saratani zingine - lakini tutapata majibu.

Kwa sasa Langley anafanya utafiti kwa washiriki 11,000 ambao wamewahi kuwa na saratani ya utumbo mpana, matiti, umio, au kibofu nchini Uingereza, Ireland na India. Timu yake itaangalia faida ya 100mg au 300mg ya aspirini kwa kila mtu, na wanatarajia kupata matokeo mwaka ujao.

"Kwa kweli sisi ndio wa kwanza kuchunguza aspirini katika aina zingine za uvimbe," anasema.

Inafanyaje kazi?

Aspirini hufanya kazi dhidi ya saratani kwa kupunguza maambukizi na kuzuia seli za saratani kuenea, hasa kwa saratani ya utumbo mpana.

Saratani mara nyingi hukua katika maeneo yenye mambukizi sugu. Aspirini huzuia enzaimu wanaoitwa COX-1 na COX-2, ambao huzalisha kemikali zinazosababisha uvimbe huu.

Aspirini husaidia urekebishaji wa DNA iliyoharibika, na kupunguza uwezekano wa seli zenye afya kugeuka kuwa seli za saratani.

Aspirini husaidia kuzuia chembe chembe za damu "zinazoganda" kuunda ngao ya kinga kwa seli za saratani, hivyo kuzizuia kutulia katika maeneo mapya ya mwili.

Ni tiba kwa wote

Ni nani hasa anayepaswa kutumia aspirini mara kwa mara, na lini, bado ni suala la mjadala. Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba faida kwa ugonjwa wa moyo na mishipa zinapaswa kufanya matumizi kuwa makubwa zaid.

Burn, ambaye ametumia aspirini kama kinga hapo awali, anasema. "Tulifanya utafiti mkubwa ambapo tulionyesha kwamba ikiwa kila mtu mwenye umri wa miaka 50 angetumia aspirini ya mtoto kwa miaka kumi, vifo vingepungua kwa 4%.”

Watafiti wengi wanasema inapaswa kutumiwa na wagonjwa maalum pekee. "Ni jambo sawa kuwapa aspirini watu wenye saratani lakini ni jambo baya kuwapa watu wenye afya njema kitu ambacho kinaweza kuwadhuru," anasema Martling.

Hiyo ni kwa sababu aspirini inaweza kuwa na athari mbaya, na kuna uwezekano mdogo wa kufanya kazi kwa watu wote au saratani zote.

Hata hivyo, ikiwa una Ugonjwa wa Lynch au umetibiwa saratani ya utumbo, unaweza kuzungumza na daktari kujua kama kipimo cha chini cha matumizi ya aspini kinafaa kwako.

"Daima zungumza na daktari au mtaalamu mwingine wa afya kabla ya kuanza kutumia aspirini," Langley anasema.