Iran na Marekani kwenye vita yenye washindi wawili

Muda wa kusoma: Dakika 4

Tarehe 5 mwezi Mei, Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio, alisema oparaseheni 'epic fury' ilifanikwa katika hotuba yake.

Hii ina maana kuwa huenda vita vimekwisha, lakini swali ni nani alishinda vita hivyo?

Nchini Iran, vyombo vya habari ikiwemo shirika la habari la kitaifa la Iranian Broadcasting Corporation vimeelezea uwezo wa serikali yao kuweza kustahimili na kushinda mataifa yenye nguvu kubwa za kijeshi.

Kule Washington, Donald Trump na serikali yake wamejitangaza washindi na kusema kuwa wameafikia malengo yao yote.

Ila nyuma ya pazia kwa sasa, ni misururu ya mazungumzo yanayoendelea na si vita, na hii ndiyo itaamua nani mshindi wa vita hivyo.

Kulingana na ripoti kutoka shirika la habari la Axios, Reuters na mashirika mengine ya habari nchini Marekani, Ikulu ya White House ina Imani kuwa, iko karibu kuafikia makubaliano yenye pinti 14 walizopendekeza kwa Iran.

Hati hiyo inatarajiwa kutoa mwelekezo wa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kufunguliwa kwa mlango bahari wa Hormuz.

Msemaji kutoka wizara ya mambo ya kigeni ya Iran, alisema kuwa taifa lake huenda likazingatia mapendekezo ya Marekani, na watatoa majibu yao kupitia mpatanishi Pakistan. Ila viongozi wakuu wa Iran, tayari wamekataa pendekezo hilo.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari hadi sasa, chini ya mpango huo unaopendekezwa, Iran italazimika kusitisha mpango wake wa nyuklia kwa kipindi cha miaka 20, na kusalimisha akiba yake ya urani iliyoboreshwa kubomoa vituo vyake vya nyuklia, na kukubali ukaguzi wa kina wa kimataifa.

Ripoti pia zinaonyesha kuwa makubaliano hayo yanaitaka Iran kuhakikisha kufunguliwa kikamilifu kwa Mlango bahari wa Hormuz.

Kwa upande mwingine, Marekani itaanza kulegeza vikwazo dhidi ya Iran hatua kwa hatua, kuachilia mali za Iran zilizozuiliwa, na huenda ikairuhusu Iran kuanza tena urutubishaji mdogo wa urani baada ya kipindi hicho cha miaka 20 kumalizika.

Kwa wengi ndani ya serikali ya Iran, masharti hayo yanaonekana zaidi kama kujisalimisha kuliko kufanya maridhiano.

Kulingana na baadhi ya viongozi wa Iran, Marekani ilisimamisha Operesheni Epic Fury kwa sababu ilishindwa kupata matokeo waliotarajia, na ilisimamisha ghafla Project Freedom, ambayo ilikuwa imeanzishwa kufungua tena Mlango wa Hormuz, kwa sababu iliongeza hatari ya mataifa ya Ghuba kuingizwa vitani. Ingawa Iran ililenga kambi za Marekani na miundombinu ya nishati katika eneola Ghuba, mataifa hayo hayakujibu wala kuingia vitani na Iran.

Kabla ya vita, baadhi ya maafisa na wachambuzi wa Magharibi waliamini kuwa kampeni ya kijeshi, pamoja na kuuawa kwa viongozi na makamanda wakuu wa Iran, ingeweza kuchochea wimbi jipya la maandamano dhidi ya serikali na hata kusababisha kuanguka kwa utawala wa Iran.

Ila hilo halikutokea.

Mohammad Baqer Qalibaf hivi karibuni aliandika,"Tunajua vizuri sana kwamba kuendelea kwa hali ilivyo sasa hakuvumiliki kwa Marekani wakati sisi hata bado hatujaanza."

Tehran haionekani kuwa na haraka ya kuzuia duru mpya ya vita. Maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu wanaamini kwamba Iran ina uwezo mkubwa zaidi wa kustahimili shinikizo la kiuchumi, shinikizo la kijeshi, na vita vya muda mrefu ikilinganishwa na wapinzani wake.

Iran ilipata hasara kubwa katika vita, iliwapoteza makamanda wake wa kijeshi pamoja na miundombinu muhimu, na bado inakumbana na shinikizo kali la kiuchumi na mfumuko mkubwa wa bei, hali ambayo inaweza kuchochea tena maandamano ya umma.

Marekani na Israel pia zilionyesha kwamba, kwa kutegemea silaha zao za kisasa na uwezo wa kijasusi, zina uwezo wa kushambulia maeneo ya ndani kabisa ya Iran na kufikia malengo yao kote nchini humo.

Lakini vita haviamuliwi tu katika uwanja wa mapambano.

Iwapo Washington itailazimisha Iran kusalimisha mpango wake wa nyuklia, Marekani itadai ushindi.

Ikiwa Tehran itaendelea kudumisha ushawishi wake wa kikanda na kuzuia kusitishwa kabisa kwa mpango wake wa nyuklia, Iran itajiona kuwa mshindi.

Kwa sasa, pande zote mbili zinawaambia raia wao kuwa wameshinda vita hivyo. Jibu halisi linaweza kujulikana tu baada ya mazungumzo kukamilika.