Kwanini Kylian Mbappé anachukiwa Real Madrid?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Jumapili hii ya Mei 10, macho ya dunia yatakuwa Hispania wakati Real Madrid wakivaana na Barcelona katika El Clasico yenye presha kubwa ya ubingwa pale Camp Nou. Lakini safari hii, mjadala mkubwa ndani ya Madrid haupo tu kuhusu matokeo ya mchezo huo, upo kwa mtu mmoja: Kylian Mbappé.

Miaka miwili iliyopita, ujio wa Mbappé Santiago Bernabéu ulionekana kama mwanzo wa zama mpya za Real Madrid. Mashabiki waliamini nyota huyo wa Ufaransa angeirudisha Real Madrid kileleni mwa soka la Ulaya na kuongeza nguvu kwenye historia ya klabu yenye mataji 15 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji 36 ya La Liga. Lakini badala ya furaha ya makombe, Madrid sasa wako kwenye hatari ya kumaliza msimu wa pili mfululizo bila kutwaa La Liga wala Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hasira za mashabiki zimefikia kiwango kipya baada ya kampeni ya mtandaoni ya kutaka Mbappé aondoke klabuni (Mbappé Out) kusambaa kwa kasi kubwa. Ombi la mtandaoni lililoanzishwa na mashabiki likiwa na lengo la kukusanya saini 200,000 pekee, lilivuka zaidi ya saini milioni 12 ndani ya saa 24 za mwanzo.

Moto uliongezeka zaidi baada ya picha za Mbappé akiwa kwenye mapumziko huko Sardinia nchini Italia pamoja na mwigizaji Ester Expósito kusambaa mtandaoni, wakati Real Madrid walikuwa kwenye kipindi kigumu cha msimu na yeye akiwa nje kutokana na majeraha. Ingawa safari hiyo iliruhusiwa rasmi na klabu, mashabiki wengi walikerwa na muda aliouchagua kwenda mapumzikoni.

Kampeni ya kumtaka Mbappé aondoke ilivyotikisa Madrid

Katika historia ya Real Madrid, mastaa wengi wamewahi kukosolewa. Lakini si mara nyingi mashabiki wamefikia hatua ya kuanzisha kampeni kubwa ya mtandaoni dhidi ya mchezaji mwenye hadhi ya Mbappé.

Ndani ya muda mfupi, ujumbe wa kutaka nyota huyo aondoke ulianza kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii huku maelfu ya mashabiki wakieleza kutoridhishwa kwao na mwenendo wa timu.

Ripoti zinaonyesha kampeni hiyo ya mtandaoni imeungwa mkono na zaidi ya mashabiki milioni 50. Hata hivyo, hakuna njia rasmi ya kuthibitisha kama wote waliosaini ni mashabiki halisi wa Real Madrid, kwani mfumo huo ulihitaji kubofya mara moja tu bila uthibitisho wa utambulisho. Huenda Mashabiki wa wapinzani wao wakubwa, Barcelona wakatumia mwanya huo kumuondoa, nyota huyo anayeipa nguvu Madrid.

Lakini hata kama si wote ni mashabiki wa madrid (Madridistas), ujumbe umefika wazi ndani ya Bernabéu, kuna sehemu ya mashabiki ambao wameanza kupoteza imani na Mbappé ndani ya klabu hiyo.

Na hali hiyo imekuja katika kipindi kigumu zaidi kwa Real Madrid. Klabu hiyo ipo nyuma ya Barcelona kwa tofauti ya pointi 11 katika mbio za La Liga, tayari imetolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali, na ipo kwenye hatari ya kumaliza msimu bila taji kubwa kwa mara nyingine tena. Na mabya zaidi katika siku chache zilizopita kumeripotiwa uwepo wa ugomvi wa wachezaji kwa wachezaji.

Federico Valverde alikimbhizwa hospitali kufuatia ugomvi wake na Aurelien Tchouameni, ugomvi uliomalizwa kwa vikao na Valverde kusema ugomvi hutokei na yameisha. Ijumaa klabu hiyo ilisema wachezaji hao wameombana msamaha na kuwaomnba wachezaji wenzao msamaha na pia wamepigwa faini ya 500,000 euros kila mmoja. Nyota wengine, Alvaro Carreras na Antonio Rudiger na wao walikuwa na tofauti zao ambazo wamejitokeza kusema zimekwisha.

Mabao pekee hayatoshi Real Madrid

Kinachofanya mjadala huu kuwa mgumu zaidi ni ukweli kwamba Mbappé hajawa na msimu mbaya kwa upande wa takwimu binafsi.

Tangu ajiunge na Real Madrid mwaka 2024, nyota huyo mwenye miaka 27 tayari amefunga mabao 85 katika mechi 100 akiwa na jezi ya klabu hiyo kabla ya Mei 10, 2026. Msimu huu pekee amefunga mabao 41 katika mechi 41 za mashindano yote.

Kwa klabu nyingi duniani, takwimu hizo zingemfanya mchezaji kuonekana shujaa mkubwa wa msimu. Lakini Real Madrid si klabu ya kawaida.

Ukiwa Madrid, mafanikio hupimwa kwa makombe makubwa, si mabao pekee. Kwa klabu iliyojenga historia yake kupitia mafanikio ya Ulaya, kumaliza misimu miwili bila kutwaa ubingwa wa La Liga wala Ligi ya Mabingwa Ulaya ni jambo ambalo mashabiki hawawezi kulikubali kirahisi.

Ndiyo maana mjadala nchini Hispania sasa umehamia mbali zaidi ya takwimu zake za mabao. Wachambuzi wengi wanauliza kwanini Mbappé hakimbii zaidi uwanjani, kwanini ushirikiano wake na Vinicius Jr hauonekani kuwa wa kawaida, na kwanini Madrid wameonekana kupoteza uwiano tangu ujio wake.

Baadhi ya wachambuzi wanaamini mfumo wa timu umeathirika kwa sababu Mbappé na Vinicius wote wanapenda kucheza maeneo yanayofanana uwanjani. Wengine wanaamini lawama hizo ni kubwa kupita kiasi na kwamba matatizo ya Madrid hayawezi kubebwa na mchezaji mmoja pekee.

'Kujivinjari' huko Sardinia, Italia kumeongeza hasira

Katika mazingira ya kawaida, mchezaji kwenda mapumzikoni wakati wa kuuguza majeraha isingeonekana kama jambo kubwa sana. Lakini mazingira ya Madrid kwa sasa si ya kawaida.

Mbappé alikuwa nje ya kikosi baada ya kupata majeraha ya misuli ya paja dhidi ya Real Betis mwishoni mwa Aprili. Lakini wakati Madrid wakicheza dhidi ya Espanyol, picha zake akiwa kwenye boti ya kifahari huko Sardinia, Italia pamoja na mwigizaji Ester Expósito zilianza kusambaa mtandaoni.

Ingawa klabu iliruhusu safari hiyo rasmi, mashabiki wengi waliona muda aliouchagua ulikuwa mbaya kwa nyota mkubwa wa timu kuonekana akifurahia maisha wakati klabu ikiwa kwenye kipindi kigumu.

Kocha Álvaro Arbeloa alijaribu kupunguza mjadala huo kwa kusema:

"Katika muda wake binafsi, Mbappé anaweza kufanya anachotaka kama mchezaji mwingine yeyote."

Lakini kauli hiyo haikutosha kupunguza hasira za mashabiki waliotaka kuona kujitolea zaidi kutoka kwa mchezaji wao muhimu zaidi. Wnapiga kura kusema hatukutaki.

Kwa mashabiki wengi, tatizo halikuwa safari yenyewe, bali ujumbe uliotumwa kwa mashabiki katika kipindi ambacho timu ilikuwa inapoteza mwelekeo wa msimu.

Nini mustakabali wa Mbappé?

Sasa macho yote yanaelekezwa kwenye El Clasico dhidi ya Barcelona katika dimba la Spotify Camp Nou.

Mbappé alikuwa nje kwa wiki mbili kutokana na majeraha, jambo lililozua hofu kuwa angekosa mchezo huo mkubwa wa msimu.

Baada ya vipimo vya awali, Arbeloa mwenyewe alikiri kuwa hali yake ilionekana kuhitaji muda zaidi wa kupona na Ijumaa alianza mazoezi na wenzake.

"Tutaona hali ya Mbappé ilivyo wiki hii," alisema Arbeloa baada ya mchezo wa mwisho wa Madrid.

"Baada ya vipimo vya wiki iliyopita, ilionekana huenda angehitaji muda zaidi."

Hata hivyo, habari njema kwa Real Madrid ni kwamba Ijumaa, Mbappé alirejea mazoezini na kushiriki sehemu ya mazoezi ya pamoja siku mbili kabla ya safari ya Barcelona.

Kurejea kwake kunakuja wakati presha ikiwa kubwa ndani ya kikosi, huku ripoti mbalimbali zikieleza kuwepo kwa hali ya taharuki ndani ya timu kutokana na uwezekano wa kumaliza msimu bila taji.

Na kwa Mbappé mwenyewe, El Clasico ya Jumapili hii inaweza kuwa zaidi ya mchezo wa kawaida. Inaweza kuwa nafasi ya kuwanyamazisha wakosoaji wake, kurejesha imani ya mashabiki wa Bernabéu na kubadilisha simulizi zote linalomzunguka.

Kwa sababu ndani ya Real Madrid, jambo moja ambalo mashabiki hawawezi kusamehe ni kuona timu yao ikishindwa bila kupigana hadi mwisho.