Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zijue nchi 7 ndogo zaidi duniani
Duniani kuna nchi ambazo ni ndogo sana kiasi kwamba unaweza kuzizunguka kwa muda mfupi ajabu hata ndani ya siku moja. Wakati wengine wanapanga safari za wiki au miezi ili kutalii nchi fulani, hizi ni tofauti kabisa.
Kwa msomaji wa Afrika Mashariki, inaweza kuwa vigumu kufikiria nchi nzima ikiwa ndogo kuliko hata Kata au Wilaya. Lakini ukweli ni kwamba baadhi ya mataifa haya yana ukubwa unaolingana na maeneo madogo kabisa ya Tanzania, Kenya au Uganda.
Ingawa ni ndogo kwa ukubwa, nchi hizi zina historia kubwa, utamaduni wa kipekee na vivutio vinavyovutia watalii kutoka kote duniani. Ukubwa wao mdogo haupunguzi umuhimu wao katika ramani ya dunia.
Hapa chini ni orodha ya nchi 7 ndogo duniani ambazo kwa moja moja, unaweza kuitembelea karibu yote ndani ya siku moja ama kwa saa chache.
7. Malta
Malta ina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 316. Hii ni kubwa kidogo ukilinganisha na nchi nyingine kwenye orodha hii, lakini bado ni ndogo vya kutosha kuizunguka ndani ya siku moja ukiwa na mpango mzuri.
Kwa Afrika Mashariki, Malta inaweza kufanana na eneo la mji mkubwa kama Arusha na viunga vyake.
Hii ina maana kuwa unaweza kusafiri kutoka upande mmoja wa nchi hadi mwingine kwa muda mfupi kwa gari, na kutembelea vivutio vikuu ndani ya siku moja.
Malta ina historia ndefu sana, majengo ya kale, fukwe nzuri na miji ya kuvutia. Ingawa ni ndogo, ina mambo mengi ya kuvutia, lakini kwa mpangilio mzuri, unaweza kutembelea maeneo muhimu yote ya nchi hii ndani ya siku moja.
6. Liechtenstein
Liechtenstein ina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 160. Inapakana na Uswisi na Austria na ni moja ya nchi ndogo lakini zilizoendelea sana kiuchumi.
Ukubwa wake unaweza kulinganishwa na Thika na maeneo yake ya karibu hasa kwa eneo la mji na viunga vyake, huko Kenya.
Unaweza kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine ndani ya muda mfupi kwa gari.
Licha ya ukubwa wake, ina milima mizuri, vijiji vya kupendeza na uchumi imara. Ni nchi ambayo unaweza kuitembelea kwa siku moja lakini bado ukaona vivutio vyake vyote vikuu vilivyoko kila upande.
5. San Marino
San Marino ina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 61. Ipo Ulaya na ni moja ya nchi kongwe zaidi duniani.
Kwa ukubwa, inakaribiana vizuri na mji wa Moshi, Kilimanjaro, Tanzania.
Ingawa kilomita za mraba 61si haba lakini unaweza kuizunguka kwa siku moja, ukiwa na gari na ukatumia saa kadhaa tu.
Nchi hii ina milima na majengo ya kihistoria yanayovutia sana watalii. Ndani ya siku moja unaweza kutembelea maeneo mengi muhimu na kufurahia mandhari yake.
4. Tuvalu
Tuvalu ina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 26 na ni moja ya nchi ndogo na zilizo hatarini kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Ukilinganisha na Afrika Mashariki, inaweza kufanana na eneo la miji ya ukubwa wa kati aua hata jiji la Kampala, Uganda kwa maeneo ya katikati.
Ni ndogo kiasi kwamba unaweza kuitembelea sehemu kubwa kwa muda mfupi sana.
Tuvalu ina fukwe nzuri na maisha ya utulivu. Hakuna msongamano wa magari wala majengo mengi, jambo linaloifanya kuwa tofauti kabisa na miji mikubwa ya Afrika Mashariki.
3. Nauru
Nauru ni kisiwa kidogo katika Bahari ya Pasifiki chenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 21. Ni moja ya nchi zisizojulikana sana lakini pia ni miongoni mwa ndogo zaidi duniani.
Ukubwa wake unaweza kulinganishwa na Kisiwa cha Chumbe. Kisiwa hiki cha Zanzibar na pamoja na eneo lake la hifadhi, kinakaribia ukubwa wa Nauru.
Kwa gari, unaweza kuizunguka nchi hii ndani ya saa moja hadi mbili tu.
Nauru haina miji mikubwa au majengo marefu, lakini ina mandhari ya asili na utulivu wa kipekee unaovutia watu wanaopenda mazingira yasiyo na pilika nyingi.
2. Monaco
Monaco ina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 2 tu. Ni moja ya nchi tajiri zaidi duniani, maarufu kwa maisha ya kifahari, magari ya gharama kubwa na mashindano ya Formula 1.
Ukubwa wake unaweza kulinganishwa na eneo la Westlands jijini Nairobi, ambapo Monaco ni karibu nusu ya eneo hilo nchini Kenya.
Hii ina maana unaweza kutembea kutoka upande mmoja hadi mwingine kwa muda mfupi sana.
Pamoja na kuwa ndogo, Monaco imejaa majengo ya kifahari, hoteli na fukwe nzuri. Ni nchi unayoweza kuitembelea kikamilifu ndani ya siku moja na bado ukaona mengi.
1. Vatican City
Vatican City ndiyo nchi ndogo kuliko zote duniani, ikiwa na ukubwa wa takriban kilomita za mraba 0.49 tu. Iko ndani ya mji wa Roma nchini Italia na ndiyo makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani.
Kwa ukubwa, eneo hili ni dogo sana kiasi kwamba linaweza kulinganishwa na eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, kule kwenye maduka ya biashara, hivyo Vatican ni ndogo hata kuliko hata eneo lote la Kariakoo.
Hata kwa kutembea kwa miguu polepole, unaweza kuzunguka nchi nzima ndani ya saa moja au mbili tu.
Licha ya udogo wake, Vatican ina vivutio vikubwa kama Kanisa la Mtakatifu Petro na makumbusho maarufu. Watalii wanaweza kuona sehemu kubwa ya nchi hii kwa siku moja bila haraka.
Makala hii imetokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo mentalfloss