Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Uingereza yapeleka meli ya kivita Mashariki ya Kati kwa ajili ya operesheni katika Mlango bahari wa Hormuz

Meli hiyo ya kivita, HMS Dragon, ambayo ni aina ya Type 45 destroyer, itawekwa tayari katika eneo hilo kabla ya jukumu lake katika operesheni ambayo Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imeeleza kuwa ni “ya kujihami pekee na ya kujitegemea.”

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu kwa leo...mpaka kesho panapo majaaliwa.

  2. Uingereza yapeleka meli ya kivita Mashariki ya Kati kwa ajili ya operesheni katika Mlango bahari wa Hormuz

    Jeshi la majini la Uingereza linatuma meli ya kivita Mashariki ya Kati ambapo inaweza kujiunga na ujumbe wa kimataifa wa kulinda usafirishaji wa meli katika Mlango bahari wa Hormuz.

    Meli hiyo ya kivita, HMS Dragon, ambayo ni aina ya Type 45 destroyer, itawekwa tayari katika eneo hilo kabla ya jukumu lake katika operesheni ambayo Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imeeleza kuwa ni “ya kujihami pekee na ya kujitegemea.”

    Keir Starmer, ambaye pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanaongoza juhudi za ujumbe huo, amesema operesheni ya kulinda usafirishaji haitaanza hadi mapigano katika eneo hilo yatakapomalizika.

    Kwa miezi kadhaa sasa, Iran imekuwa ikidhibiti Mlango bahari wa Hormuz kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Marekani na Israel.

    HMS Dragon ni moja ya meli sita za kivita aina ya Type 45 destroyer za jeshi la majini la Uingereza zilizotengenezwa mahsusi kwa ajili ya vita dhidi ya mashambulizi ya anga na makombora, na ni miongoni mwa meli za kisasa zaidi za kivita za nchi hiyo.

    Unaweza kusoma;

  3. Mkuu wa WHO awahakikishia usalama wakazi kabla ya kuwasili kwa meli ya kitalii iliyokumbwa na Hantavirus

    Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amewahakikishia wakazi wa Tenerife kwamba hatari ya kuambukizwa ni ndogo kabla ya kuwasili kwa meli ya kitalii iliyokumbwa na mlipuko wa hantavirus.

    Tedros alisema kuwa “hii si Covid nyingine” na kwamba kwa sasa hakuna abiria wenye dalili ndani ya meli ya MV Hondius, katika ujumbe wake kwa wakazi wa visiwa vya Canary.

    Meli hiyo inatarajiwa kuwasili katika bandari ya Granadilla mapema Jumapili asubuhi, jambo ambalo limezua wasiwasi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

    Watu sita wamethibitishwa miongoni mwa abiria wa meli hiyo, ikiwemo mmoja kati ya watu watatu waliofariki dunia wakati meli hiyo ya Uholanzi ilipokuwa ikisafiri kutoka Amerika ya Kusini.

    Maafisa wa Hispania wamejaribu kupunguza hofu kuhusu kuwasili kwa meli hiyo kwa kueleza hatua za tahadhari na udhibiti zinazochukuliwa.

    Virusi vya hantavirus kwa kawaida hubebwa na panya, lakini maambukizi kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu yanawezekana kwa aina ya Andes strain, ambayo WHO inaamini baadhi ya abiria waliipata walipokuwa Amerika Kusini.

    Dalili za ugonjwa huo zinaweza kujumuisha homa, uchovu mkubwa, maumivu ya misuli, maumivu ya tumbo, kutapika, kuharisha na matatizo ya kupumua.

    “Ninajua mna wasiwasi,” Tedros aliwaambia wakazi wa Tenerife.

    “Ninaelewa kwamba mnaposikia neno ‘mlipuko’ na kuona meli ikielekea kwenye mwambao wenu, kumbukumbu zinaibuka ambazo bado hatujazisahau kabisa. Maumivu ya mwaka 2020 bado yapo, na siyapuuzi hata kwa sekunde moja.

    “Lakini nahitaji mniskie vizuri: hii si Covid nyingine. Hatari ya sasa ya kiafya kutoka kwa hantavirus bado iko chini.”

    Aliongeza kuwa kwa sasa kuna mtaalamu wa WHO, Dkt. Freddy Banza-Mutoka, ndani ya meli ya MV Hondius.

    Kwa kushirikiana na madaktari wawili kutoka Uholanzi, wanafanya tathmini za afya na uchunguzi wa uwezekano wa maambukizi kwa kila mtu aliyepo ndani ya meli hiyo.

    WHO imesema hadi sasa hakuna abiria wengine wanaoonesha dalili za hantavirus.

    Shirika hilo pia lilisema kuwa Tedros amesafiri hadi Tenerife kufuatilia operesheni hiyo moja kwa moja.

    Abiria wataendelea kubaki ndani ya meli hiyo na wataruhusiwa kuondoka kwa kutumia boti ndogo pale tu ndege za kuwarudisha makwao zitakapokuwa tayari uwanjani.

    Maafisa wamesema ndege zimepangwa kuwapeleka abiria hao kurejea Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji na Ireland.

    Umoja wa Ulaya pia umetuma ndege mbili zaidi kwa ajili ya raia wengine wa Ulaya waliobaki.

    Unaweza kusoma;

  4. Ndege yagonga na kumuua mtu aliyekuwa akitembea katika njia ya kurukia ndege

    Ndege ya Shirika la Frontier Airlines imegonga na kumuua mtu mmoja aliyekuwa akitembea kwa miguu wakati ilipokuwa ikijaribu kupaa kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Denver usiku wa Ijumaa.

    Mamlaka zimesema ajali hiyo ilisababisha moto mdogo kwenye injini, ambao ulizimwa haraka na Idara ya Zimamoto ya Denver. Moshi pia ulionekana ndani ya ndege.

    Abiria wote 224 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walihamishwa kwa kutumia njia za dharura kama tahadhari, kulingana na taarifa ya Frontier Airlines.

    Inaelezwa kuwa mtu huyo aliruka uzio wa uwanja wa ndege na aligongwa takriban dakika mbili baadaye alipokuwa akivuka njia ya kurukia ndege.

    Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Los Angeles wakati tukio hilo lilipotokea. Shirika la ndege limesema lina huzuni kubwa kuhusu tukio hilo.

    Mamlaka za uwanja wa ndege wa Denver zimesema mtu huyo haaminiki kuwa mfanyakazi wa uwanja huo na bado hajafahamika utambulisho wake.

    Taarifa ya uwanja huo imesema kuwa uzio wa eneo la uwanja umechunguzwa na kubainika kuwa uko salama na haujavunjwa.

    Aidha, abiria 12 waliokuwa ndani ya ndege ya Frontier Airlines walipata majeraha madogo kutokana na tukio hilo, ambapo watano kati yao walipelekwa hospitali zilizo karibu kwa matibabu.

    Njia ya kurukia ndege imefungwa kwa muda wakati uchunguzi ukiendelea kufanywa na mamlaka.

  5. “Hatufurahishwi na Pakistan kusimamia mazungumzo kati ya Iran na Marekani”

    Pakistan inatajwa kuwa na jukumu la upatanishi katika juhudi za kusitisha vita kati ya United States na Iran. Hata hivyo, Israel haionekani kufurahishwa na jukumu hilo.

    Balozi mdogo wa Israel mjini Mumbai, Yaniv Revach, alisema: “Sidhani kama serikali yangu inafurahishwa na ukweli kwamba Pakistan inaongoza mazungumzo kati ya Iran na Marekani.”

    Aliongeza kuwa Israel haishiriki mazungumzo yoyote na Pakistan, akisisitiza kuwa ni Marekani chini ya Donald Trump ndiyo inayoendesha mazungumzo hayo, na Israel inaamini Marekani italinda maslahi yake ya kiusalama.

    Kwa upande mwingine, Trump pamoja na viongozi wa Iran wameripotiwa kuishukuru Pakistan kwa jitihada zake za upatanishi.

    Pia, nchi hizo mbili zilituma wawakilishi wake katika mazungumzo yaliyofanyika Islamabad, mji mkuu wa Pakistan. Israel haikuwa na mwakilishi katika mazungumzo hayo.

    Hali hiyo inaonesha tofauti za kimkakati katika eneo hilo, huku Pakistan ikijaribu kujitokeza kama mpatanishi kati ya mataifa makubwa yenye mvutano mkubwa.

    Unaweza kusoma;

  6. Iran yakanusha madai kwamba ilihusika katika shambulio dhidi ya meli ya mafuta iliyokuwa na wafanyakazi wa China

    Iran imekanusha taarifa kwamba jeshi lake lilishambulia meli ya mafuta iliyokuwa imewabeba mabaharia wa China.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, balozi wa Iran nchini China, Abdulreza Rahmani Fazli, alisema: “Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi alitembelea China, hivyo habari kama hizi zinasambazwa ili kupunguza umuhimu wa ziara hiyo.”

    Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilithibitisha siku ya Ijumaa kuwa meli ya mafuta iliyokuwa na wafanyakazi wa China ilishambuliwa katika Mlango bahari wa Hormuz.

    Wizara hiyo ilisema kuwa hatari kwa meli za biashara inaongezeka kutokana na mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati na ikaeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali hiyo.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba raia wa China walikuwemo ndani ya meli hiyo, lakini hadi sasa hakuna taarifa za majeruhi miongoni mwa wafanyakazi.

    Kwa sasa, Mlango bahari wa Hormuz umefungwa kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israel na Iran. Marekani pia imeweka mzingiro katika eneo hilo.

    Unaweza kusoma;

  7. Hakuna duru mpya ya mazungumzo iliyopangwa kati ya Ukraine na Urusi

    Msaidizi wa rais wa Urusi, Yuri Ushakov, amesema kuwa Ukraine na Urusi bado hazijakubaliana kuhusu duru inayofuata ya mazungumzo.

    “Hakuna aliyezungumzia mazungumzo hayo; hadi sasa mapumziko yamechukuliwa, na hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu duru inayofuata ya mazungumzo,” Ushakov alisema, kwa mujibu wa Interfax.

    “Ni wazi kila upande unatakiwa kufanya nini kabla ya duru inayofuata ya mazungumzo. Kila upande, namaanisha hasa upande wa Ukraine. Na wao wanajua kinachopaswa kufanywa ili duru inayofuata iwe na mafanikio,” aliongeza.

    Mapema, Ushakov alisema kuwa mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine hayana maana ikiwa Kyiv haitakubali kuondoa wanajeshi wake kutoka eneo lote la Donbass, ikiwemo maeneo ambayo bado yako chini ya udhibiti wake. Ukraine imekuwa ikikataa mara kwa mara masharti hayo na kuyaita hayakubaliki.

    Duru inayofuata ya mazungumzo ya pande tatu kati ya wajumbe wa Ukraine, Urusi na Marekani ilikuwa iwe mwishoni mwa majira ya baridi katika Mashariki ya Kati, lakini ilifutwa baada ya kuanza kwa vita nchini Iran.

  8. Vladimir Putin aishutumu Nato katika gwaride la Siku ya Ushindi

    Vladimir Putin ametumia hotuba yake ya kila mwaka ya maadhimisho ya Siku ya Ushindi katika Red Square mjini Moscow kuhalalisha vita vya Urusi dhidi ya Ukraine na kuishutumu Nato.

    Akizungumza mbele ya mamia ya wanajeshi na akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa dunia, Putin alisema kuwa anapigana “vita vya haki” na akaieleza Ukraine kuwa “vikosi vya uchokozi” vinavyoungwa mkono na kupewa silaha na muungano mzima wa Nato.

    Kauli zake zimekuja wakati maadhimisho ya Siku ya Ushindi yakifanyika kwa kiwango cha chini katika baadhi ya maeneo ya Urusi. Sikukuu hiyo ni moja ya matukio makubwa ya kitaifa nchini humo na huadhimisha ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Nazi katika Vita vya Pili vya Dunia.

    Kabla ya maadhimisho hayo, Urusi na Ukraine zilikubaliana kusitisha mapigano kwa siku tatu, hatua iliyotangazwa na Donald Trump siku ya Ijumaa.

    Kwa mara ya kwanza katika miaka kadhaa, hakukuwa na magari ya kivita wala makombora ya masafa marefu yaliyooneshwa katika gwaride la Siku ya Ushindi mjini Moscow.

    Hata hivyo, chini ya ulinzi mkali, wanajeshi wengi walipita katika Red Square wakati wa gwaride hilo.

    Akilihutubia taifa, Putin alianza hotuba yake kwa kuwakumbuka wanajeshi wa Umoja wa Kisovieti walioyatoa maisha yao katika Vita vya Pili vya Dunia.

    “Ushujaa mkubwa wa kizazi cha washindi unawapa hamasa wanajeshi wanaotekeleza malengo ya operesheni maalum ya kijeshi leo,” alisema Putin akirejelea vita vya Ukraine.

    “Wanakabiliana na vikosi vya uchokozi vinayopatiwa silaha na kuungwa mkono na muungano mzima wa Nato. Na licha ya hayo, mashujaa wetu wanaendelea kusonga mbele.”

    Kiongozi wa Urusi, Vladimir Putin, aliendelea kuwasifu raia wake kwa mchango wao katika juhudi za vita, akiwataja wafanyakazi mbalimbali kama wanasayansi, wavumbuzi, waandishi wa habari za kijeshi, madaktari na walimu.

    “Haijalishi mbinu za kijeshi zinabadilika vipi, mustakabali wa nchi unaandaliwa na wananchi,” alisema.

    Mara baada ya hotuba hiyo, mizinga ilifyatua risasi kadhaa mfululizo huku muziki ukipigwa na bendi ya kijeshi.

    Nyuma ya Putin alikuwepo kiongozi wa Belarus, Alexander Lukashenko.

    Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais wa Laos, Thongloun Sisoulith, Mfalme wa Malaysia Sultan Ibrahim, Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev, pamoja na Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev.

    Pia Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico, alionekana akikutana na Putin katika Kremlin kabla ya gwaride hilo.

    Idadi ya viongozi wa dunia waliohudhuria ilikuwa ndogo zaidi ikilinganishwa na maadhimisho ya mwaka uliopita ya miaka 80, ambayo yalihudhuriwa na viongozi 27 akiwemo Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva.

    Unaweza kusoma;

  9. Donald Trump amesema kuwa Urusi na Ukraine zitasitisha mapigano kwa siku tatu

    Donald Trump ametangaza usitishaji wa mapigano wa siku tatu kati ya Urusi na Ukraine, baada ya nchi hizo mbili kushutumiana kwa kukiuka usitishaji wa mapigano uliotangazwa na kila upande kwa ajili ya maadhimisho ya ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Nazi.

    “Usitishaji huu wa mapigano utahusisha kusimamishwa kwa shughuli zote za kivita, pamoja na kubadilishana wafungwa 1,000 kutoka kila nchi,” rais huyo wa Marekani alisema.

    Muda mfupi baadaye, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alithibitisha ushiriki wa Ukraine katika makubaliano hayo, huku vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vikisema kuwa Urusi pia imekubali pendekezo hilo.

    Awali, pande zote mbili zilidai kuwa upande mwingine uliendelea kushambulia maeneo yao, na meya wa Moscow alisema mji huo ulikuwa umelengwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani usiku kucha.

    Katika ujumbe wake, Trump alisema aliomba binafsi usitishaji huo wa mapigano wa siku tatu na “anathamini sana kukubaliwa kwake na Rais Vladimir Putin pamoja na Rais Volodymyr Zelenskyy.”

    Putin alikuwa ametangaza usitishaji wa mapigano kwa tarehe 8 hadi 9 Mei kabla ya maadhimisho ya Siku ya Ushindi yaliyopangwa kufanyika Jumamosi. Kyiv hapo awali ilikuwa imetoa wito wa usitishaji wa mapigano usio na kikomo kuanzia tarehe 6 Mei.

    Urusi imeionya Ukraine kutofanya jaribio lolote la kushambulia gwaride la Siku ya Ushindi litakalofanyika katika Red Square mjini Moscow.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imetishia kufanya “shambulio kubwa la kulipiza kisasi kwa makombora” katikati mwa mji wa Kyiv ikiwa Moscow itashambuliwa. Pia imewaonya wanadiplomasia wa kigeni kuondoka katika mji mkuu wa Ukraine kabla ya tarehe 9 Mei.

    Unaweza kusoma;

  10. Iran yaishutumu Marekani kwa “hatua za kijeshi zisizo na tahadhari”

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameishutumu Marekani kwa kuchagua “hatua za kijeshi zisizo na tahadhari” kila mara “suluhisho la kidiplomasia linapowekwa mezani.”

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye X, Araghchi alisema kuwa Wairani “hawatasalimu amri kwa shinikizo,” siku moja baada ya pande zote mbili kushutumiana kwa kufanya mashambulizi katika Mlango Bahari wa Hormuz, huku Marekani ikiendelea kushambulia vyombo zaidi vya Iran.

    “Je, hii ni mbinu ya shinikizo la moja kwa moja?” alihoji mwanadiplomasia huyo wa Iran. “Au ni matokeo ya mtu anayeharibu mambo kumdanganya tena Rais wa Marekani Donald Trump na kumuingiza katika mgogoro mwingine?”

    Licha ya mapigano hayo, Trump alisema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano bado yanaendelea kuheshimiwa. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwezesha mazungumzo ya kumaliza vita ambavyo Marekani na Israel walivianzisha mwezi Februari.

    Iran ilitarajiwa kujibu mapendekezo ya Marekani siku ya Ijumaa, kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio.

    “Natumaini ni pendekezo la dhati, kweli natumaini hivyo,” Rubio alisema akiwa katika ziara nchini Italia.

    Iran imekuwa ikidhibiti Mlango bahari wa Hormuz pamoja na kushambulia washirika wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi kama kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Marekani na Israel.

    Takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia duniani hupitia katika njia hiyo muhimu ya maji, na kuzuiwa kwake kumesababisha bei kupanda kwa kasi.

    Mapema wiki hii, Trump alianzisha, kisha kusitisha operesheni ya kijeshi ya Marekani iliyolenga kusaidia kuachilia zaidi ya meli 2,000 ambazo zimekwama katika eneo hilo tangu Februari.

    Unaweza kusoma;

  11. Waziri Mkuu Starmer akabiliwa na shinikizo la kujiuzulu, huku Labour ikipoteza kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer amesisitiza kuwa hatajiuzulu na “kuitumbukiza nchi kwenye mgogoro,” wakati chama cha Labour kikikabiliwa na hasara kubwa katika uchaguzi.

    Matokeo ya uchaguzi nchini England, Scotland na Wales yameongeza shinikizo kwa Sir Keir, huku baadhi ya wabunge wa Labour wakimtaka kuweka ratiba ya kuondoka kwake madarakani, ingawa kwa sasa washirika wake wa baraza la mawaziri wanaendelea kumuunga mkono.

    Labour imepoteza madaraka nchini Wales, na hivyo kumaliza utawala wake wa miaka 27, huku chama cha SNP kikiendelea kuwa chama kikubwa zaidi nchini Scotland.

    Chama cha Reform UK ndicho kilichopata mafanikio makubwa zaidi nchini England, kikitwaa zaidi ya viti 1,400 na kuchukua udhibiti katika maeneo ambayo kihistoria yalitawaliwa na Labour na Conservatives.

    Chama cha Labour kimepoteza zaidi ya viti 1,100 vya halmashauri nchini England, ikiwemo katika ngome zake za kisiasa kaskazini mwa England na maeneo ya Midlands, na kinatarajiwa kukumbana na matokeo mengine magumu.

  12. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo