"Pomboo wa kujitoa mhanga" wanaodaiwa kutumiwa na Iran kutega mabomu ya majini

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi ya wizara ya ulinzi nchini Marekani, maarufu Pentagon, katika maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari, moja ilikuwa "Je, Iran inatumia pomboo wa kujitoa mhanga?

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alijibu kwa kusema "Siwezi kuthibitisha wala kukanusha matumizi ya pomboo wa kujitoa muhanga, lakini naweza kuthibitisha kwamba hawana wanyama hao."

Jenerali Dan Caine pia alisema hajawahi kusikia ripoti kama hizo, na akauliza kama hii ni hadithi.

Kauli hizi zilikuwa zinarejelea ya makala ya Wall Street Journal yaliyochapishwa siku tano zilizopita yenye mada "Iran Inatafuta suluhisho la kukabiliana na kizuizi cha kijeshi"

Chapisho hilo liliandika kuwa vizuizi vya majini vya Marekani vimeonyesha mapungufu katika mkakati wao wa kudhibiti Mlango bahari wa Hormuz, na kwamba Iran inatafuta njia ya kutumia mwanya huo.

Taarifa ya wall street Journal pia inasema kuwa

"Maafisa wa Iran walisema Tehran inaweza kutumia silaha ambazo haijawahi kutumia hapo awali, kuanzia manowari hadi pomboo wanaobeba mabomu ya kutegwa baharini, kushambulia meli za kivita za Marekani. Jeshi la IRGC limetishia kuongeza mvutano huo kwa kukata nyaya za mawasiliano za fiber-optic katika Mlango bahari wa Hormuz, hatua ambayo inaweza kuvuruga mtandao wa intaneti duniani."

Ingawa matumizi ya kijeshi ya pomboo yanaweza kuonekana kama hadithi, zoezi hilo limekuwepo kwa miongo kadhaa.

Miaka 26 iliyopita, mwezi Machi tarehe 8, mwaka 2000, BBC iliripoti kwamba Iran ilinunua pomboo wa "kujitoa muhanga".

Ripoti hiyo ilisema kuwa pomboo hao waliopewa mafunzo na Jeshi la Wanamaji la Kisovieti waliuzwa kwa Iran, lakini wakati huo haikujulikana wazi wangefanya nini katika Ghuba ya Uajemi.

Wataalamu wa Urusi walikuwa wamewafundisha pomboo hao na wanyama wengine wa majini kushambulia meli za adui na wapiga mbizi, lakini kutokana na kupungua kwa ufadhili, wengi wao walihamishwa kwenda kwenye majumba ya makumbusho.

Boris Jurid, alikuwa mwalimu wa pomboo hizo na alianza kazi yake kama afisa wa manowari .

Wakati huo ilisemekana kuwa aliwauza wanyama hao wa majini kwa Iran kwa kushindwa kugharamia chakula na matunzo yao.

Ripoti ya BBC wakati huo ilisema kwamba jumla ya wanyama 27, wakiwemo pomboo, simba wa baharini na nyangumi aina ya beluga, walisafirishwa kutoka Sevastopol katika Rasi ya Crimea kwenda Ghuba ya Uajemi kwa ndege ya mizigo.

Pomboo wanne na nyangumi aina ya beluga walikuwa wamefunzwa na Jurid katika kambi ya jeshi la wanamaji katika Bahari ya Pacific kabla ya kuhamishiwa kutoka Crimea mwaka wa 1991. Wanyama hao walifundishwa kushambulia wapiga mbizi wa adui kwa kutumia mikuki iliyofungwa mgongoni mwao au kuwavuta juu ya maji ili wakamatwe.

Pomboo waliofunzwa pia wangeweza kulenga meli za adui kwa kutekeleza mashambulizi ya kujitoa muhanga, wakibeba mabomu ya kutegwa ambayo yangelipuka yakigonga meli.

Inasemekana kwamba pomboo hao waliweza kutofautisha manowari za Kisovieti na za kigeni kwa sauti ya propela zao.

Mbali na Urusi, nchi nyingine pekee inayojulikana kufundisha pomboo kwa matumizi ya kijeshi ni Marekani, ambayo inaendesha programu ya wanyama wa baharini huko San Diego, California.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ripoti zisizo rasmi za juhudi za baadhi ya nchi, zikiwemo Korea Kaskazini kuwafunza pomboo.

Tangu uvamizi wake wa Ukraine, Urusi inaripotiwa kuongeza matumizi ya pomboo za kijeshi katika bandari ya Sevastopol ili kukabiliana na wapiga mbizi wa adui na kulinda meli zake za kijeshi katika Bahari Nyeusi.

Akbar Hashemi Rafsanjani, katika kumbukumbu zake "Reforms in Crisis", aliandika kuhusu matukio ya Farvardin 2 1990.

"Pomboo ni wanyama wenye akili na hutekeleza maagizo vizuri, isipokuwa inapofikia suala la muziki."