'Vita vya nani mwenye ushawishi' katika mlango bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, Getty Images
Vyombo vya habari vya kikanda na vya ndani katika ulimwengu wa Kiarabu viliripoti kwa kina taarifa zinazokinzana kutoka Iran na Marekani kuhusu hali katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Vituo vikuu vya televisheni vya Kiarabu vinavyotangaza kwa lugha ya Kiarabu na vilivyoko katika nchi za Ghuba ya Uajemi vilianza matangazo yao ya habari kwa kuzungumzia maendeleo yanayohusu Mlango-Bahari wa Hormuz, huku vingine vikirejelea "vita vya ushawishi" katika njia hii muhimu ya kimkakati.
Vingine vilijikita katika tangazo la hivi karibuni la Oman kuhusu njia ya muda ya baharini kwa meli zinazojaribu kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz, pamoja na uratibu unaoendelea kati ya Oman na Iran kuhusu usimamizi wa njia hiyo ya maji.
Taarifa zinazokinzana
Vyombo vingi vya habari vilijadili mgongano kati ya taarifa zilizotolewa na Marekani na Iran.
Baadhi yao waliripoti kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump, alihakikishia kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz utaendelea kubaki wazi.
Wakati huohuo, chombo cha habari cha Iran Al-Alam na RT Arabic ya Urusi vilimnukuu Mohammad Baqer Qalibaf akisema kwamba "usimamizi wa Mlango-Bahari wa Hormuz hautarudi tena katika hali ya kabla ya vita," akiongeza kuwa mlango huo utasimamiwa na Iran kwa mujibu wa sheria za kimataifa na taratibu za Iran.
Gazeti la Saudi "Asharq Al-Awsat", linalochapishwa London, liliandika katika kichwa cha ukurasa wa mbele wa taarifa zake za moja kwa moja: "Mitazamo kinzani ya Marekani na Iran kuhusu ukaguzi wa nyuklia, Mlango-Bahari wa Hormuz na Lebanon."
Vilevile, gazeti la serikali la Misri Al-Ahram lilimnukuu Donald Trump kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social akisema kwamba alikuwa amekubaliana "kuufanya Mlango-Bahari wa Hormuz ubaki wazi na kutoweka vizuizi zaidi vya kijeshi baharini."
Kwa upande mwingine, gazeti la Al-Ahram liliripoti kwamba Iran imeendelea kusisitiza kuwa "itachukua jukumu la kusimamia Mlango-Bahari wa Hormuz" baada ya kumalizika kwa duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Washington na Tehran yaliyofanyika Uswisi.
Kurejesha usafirishaji katika hali ya kawaida
Mtandao wa Sky News Arabia ulioko Abu Dhabi uliripoti kwamba meli kadhaa zimepitia Mlango-Bahari wa Hormuz tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya maelewano kati ya Washington na Tehran tarehe 17 Juni ya kumaliza vita, jambo lililofikia "rekodi mpya."
Mtandao huo uliongeza kuwa idadi hiyo ni sawa na takriban theluthi moja ya kiwango cha kabla ya vita kuanza.
Sky News Arabia pia iliripoti taarifa kutoka Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) kwamba shirika hilo limeanzisha operesheni ya kuwahamisha takriban mabaharia 11,000 waliokwama katika Mlango-Bahari wa Hormuz, hatua inayofanywa ndani ya mfumo wa "jitihada za kikanda na kimataifa za kurejesha usafirishaji katika hali ya kawaida."

Chanzo cha picha, Getty Images
"Vita vya ushawishi"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sky News Arabia iliripoti kwamba licha ya kupungua kwa mvutano wa kijeshi, mgogoro huo haujamalizika kikamilifu, kwa kuwa Marekani na Iran bado wana mitazamo "kinzani".
Mtandao huo unaona kwamba sasa mzozo huo umegeuka kuwa "mashindano ya ushawishi na udhibiti juu ya mojawapo ya njia muhimu zaidi za kimkakati za baharini duniani."
Wataalamu waliozungumza na Al Jazeera Qatar walisema kwamba makubaliano kati ya Marekani na Iran bado ni "dhaifu," na kwamba kuvunjika kwa mazungumzo kunaweza kusababisha kufungwa upya kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Walieleza kuwa makubaliano ya kuufanya mlango huo ubaki wazi yanaweza kurahisisha mchakato wa mazungumzo, lakini hayahakikishi urejeshwaji kamili wa usafiri wa baharini na biashara, ambao umeathirika sana kutokana na kufungwa kwa mlango huo.
Kwa upande mwingine, mtandao wa Qatar Al Arabi uliripoti kwamba: "Mapambano ya shinikizo na nguvu yanaendelea; Tehran na Muscat wanatayarisha mpango wa kusimamia Mlango-Bahari wa Hormuz, huku Washington ikipinga kuwekwa kwa ushuru wowote."
Vilevile, mtangazaji wa Saudi Al Arabiya aliangazia kauli ya Waziri Mkuu wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, katika mahojiano na Financial Times, akisema kuwa kuanzishwa kwa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran ni "muhimu ili kuzuia wahusika wasio na udhibiti kuzuia kufunguliwa kwa mlango huo."
Aliongeza pia kuhusu matarajio ya kurejea kwa "uzalishaji wa kawaida wa gesi asilia iliyosafishwa (LNG)" nchini Qatar.















