Iran haiko tayari kuiacha Hezbollah nje ya makubaliano yake na Marekani, Kwa nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kama mtu yeyote angekuwa ametabiri katika siku za mwanzo za mwezi Machi kwamba mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran yangesababisha hatimaye makubaliano ya kusitisha mapigano ambapo maafisa wa Iran wangehusisha kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kusitishwa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, watu wachache sana wangeamini.
Lakini baada ya maelezo ya makubaliano ya maelewano kati ya Iran na Marekani kuchapishwa, ilibainika kwamba Lebanon ilichukua nafasi muhimu katika maandishi na vipengele vya makubaliano hayo.
Kwa mtazamo wa juu juu, mada kuu ya maelewano hayo ilikuwa kumaliza vita kati ya Iran na Marekani, kufungua tena njia za usafirishaji wa baharini, kudhibiti mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, na kufungua njia ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia. Hata hivyo, Iran ilisisitiza kwamba Lebanon na kundi la Hezbollah zijumuishwe katika mpangokazi.
Upande mmoja hii inaweza kuiweka Iran katika nafasi yenye nguvu, na kwa upande mwingine, inaweza kusababisha kuvunjika kwa makubaliano haya na kurejea kwa mapigano katika eneo lote.
Lakini kwa nini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiko tayari kuiacha nje Hezbollah katika makubaliano yake na Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Inaonekana kwamba Hezbollah si tu nguvu ya kijeshi kwenye mpaka wa Israel kwa Iran. Kundi hilo pia ni sehemu ya nguvu ya Iran katika mazungumzo ya kisiasa, ishara ya uaminifu wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati, na kipengele muhimu katika mtazamo wa wafuasi wa kiitikadi wa utawala kuhusu sera ya nje ya Iran.
Wakosoaji wengi wa sera za kikanda za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huuliza kwa nini Tehran iko tayari kuhatarisha makubaliano yake na Marekani ili kudumisha uhusiano huu, hasa wakati uchumi wa Iran uko chini ya shinikizo kubwa.
Hata hivyo, uchambuzi wa misimamo ya maafisa wa Iran na maoni ya wataalamu unaonyesha kwamba, kwa mtazamo wa Tehran, suala hili halihusu tu mustakabali wa Hezbollah.
Badala yake, linafungamana pia na:
- Ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.
- Uaminifu na uthabiti wa mtandao wa washirika wake wa kikanda.
- Mtazamo wa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu mustakabali wa vita na mvutano dhidi ya Israel na Marekani.
Kwa hiyo, kwa viongozi wa Iran, kuitenganisha Lebanon na Hezbollah katika makubaliano yoyote makubwa ya kisiasa au kiusalama kunaweza kuonekana kama kupunguza ushawishi wao wa kikanda na kudhoofisha imani ya washirika wao kwamba Tehran itaendelea kuwaunga mkono katika nyakati za migogoro
Lebanon iliingiaje katika maelewano kati ya Iran na Marekani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuingizwa kwa Lebanon katika maelewano kati ya Iran na Marekani, kwa mtazamo wa wakosoaji wa makubaliano hayo mjini Washington, ni moja ya ishara kwamba Tehran imeweza kulazimisha baadhi ya matakwa yake katika mchakato wa kidiplomasia.
Wakosoaji kama Mark Dubowitz, Jonathan Schanzer, na Michael Doran, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitetea sera ya kuongeza shinikizo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wanaona makubaliano hayo kama ishara kwamba utawala wa Donald Trump umefanya maridhiano makubwa mno kwa Iran.
Kwa maoni yao, Marekani imeipa Iran baadhi ya makubaliano yanayozidi kusitishwa kwa muda kwa mapigano, kwa lengo la kuhakikisha kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kupunguza gharama za kiuchumi zilizotokana na vita.
Michael Young, mtafiti mwandamizi katika Carnegie Middle East Center, alifikia hitimisho linalofanana lakini kutoka mtazamo tofauti kwenye mahojiano na BBC Persian.
Mchambuzi huyo wa Lebanon anasema kwamba kwa sasa ni Marekani inayohitaji mafanikio ya mazungumzo hayo zaidi kuliko Iran, kwa sababu kufungwa au kuwekewa vikwazo kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kumesababisha gharama kubwa kwa uchumi wa Marekani pamoja na uchumi wa dunia kwa ujumla.
Kwa mujibu wa mtazamo huu, uwezo wa Iran wa kuhusisha masuala ya Lebanon na Hezbollah katika mazungumzo mapana unaonyesha kwamba Iran bado inaona ushawishi wake wa kikanda kama sehemu muhimu ya nguvu zake za mazungumzo na haitaki kuutenganisha na makubaliano yoyote makubwa na Marekani.
Mtazamo huu unaweza kuwa mojawapo ya sababu zilizoiwezesha Iran kuingiza suala la Lebanon katika mahesabu ya mazungumzo hayo. Iran inataka kuhakikisha kwamba Israel haipewi uhuru wa kufanya inavyotaka nchini Lebanon ikiwa vita kati ya Iran na Marekani vitasitishwa.
Kwa mtazamo wa watunga maamuzi mjini Tehran, makubaliano ambayo yanapunguza shinikizo la moja kwa moja dhidi ya Iran lakini yakairuhusu Hezbollah kuendelea kushambuliwa na Israel yanaweza kuonekana kama makubaliano yasiyokamilika. Sababu ni kwamba hali hiyo ingeweza kudhoofisha moja ya nyenzo muhimu zaidi za Iran katika makabiliano yoyote ya baadaye na Israel.
Kwa hiyo, viongozi wa Iran wanaweza kuona usalama na uwezo wa Hezbollah kama sehemu ya mkakati mpana wa kuzuia na kujilinda kikanda.
Kwa mtazamo wao, kulinda nafasi ya Hezbollah nchini Lebanon kunahusiana moja kwa moja na kudumisha ushawishi wa Iran katika eneo na uwezo wake wa kujibu vitisho vya baadaye.
Hali ya Hezbollah iko vipi sasa hivi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Msisitizo wa Iran juu ya Hezbollah unaendelea licha ya kwamba kundi hilo haliko tena katika nafasi lililokuwa nayo kabla ya vita vya Gaza.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Hezbollah imepata pigo kubwa kutoka kwa Israel: kuanzia kuuawa kwa viongozi wake wakuu na makamanda wake, kushambuliwa kwa mtandao wake wa uongozi na udhibiti, hadi kuharibiwa kwa sehemu ya miundombinu yake ya kijeshi na kupunguzwa kwa uwezo wake wa kufanya operesheni na kujihamisha kusini mwa Lebanon.
Hamid Reza Azizi, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati katika mahojiano na BBC Persian, alisema:
"Hezbollah iko katika hali dhaifu zaidi ikilinganishwa na kabla ya vita vya Gaza. Moja ya sababu zilizofanya Israel ihitimishe kwamba ingeweza kushambulia Iran kwa gharama inayoweza kudhibitiwa ilikuwa ni kudhoofika kwa Hezbollah."
Kwa mujibu wa Azizi, hapo awali Hezbollah ilionekana kama nguvu iliyokuwa kubwa kuliko jeshi la Lebanon na yenye uwezo mkubwa kuliko majeshi mengi katika eneo hilo. Hata hivyo, uwezo wake wa makombora na muundo wake wa kivita umepungua baada ya vita na mashambulizi ya hivi karibuni.
Anaendelea kusema: "Hezbollah leo kwa kiasi fulani imerudi katika mbinu zilizotumiwa katika miaka ya mwanzo ya kuanzishwa kwake na katika mapambano yake ya kwanza dhidi ya Israel."
Hii inajumuisha:
- Muundo wa uongozi uliogatuliwa zaidi
- Kutegemea vikundi vidogo vya wapiganaji.
- Matumizi ya mbinu za vita visivyo vya kawaida
- Kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia mpya, kama vile ndege zisizo na rubani za aina ya FPV.
Jukumu la Hezbollah limebadilikaje?
Kwa miaka ya hivi karibuni, wachambuzi wengi wamekuwa wakiitazama Hezbollah ya Lebanon kwa namna ya pekee, na kile kinachoitwa "mhimili wa upinzani" kwa ujumla, kama sehemu ya mkakati wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuimarisha uwezo wake wa kuzuia mashambulizi kutoka kwa maadui wake.
Mkakati huu ulijengwa juu ya nadharia ya kuzuia adui kwa kufanya hatua za kijeshi kuwa ngumu na za gharama kubwa.
Katika mfumo huu, Iran ilijaribu kuongeza gharama, hatari na ugumu wa hatua yoyote ya kijeshi kutoka kwa Israel au Marekani kwa kutegemea mtandao wake wa washirika wa kikanda. Miongoni mwa washirika hao, Hezbollah ilichukua nafasi muhimu.
Lengo lilikuwa kuimarisha uwezo wa Iran wa kuzuia mashambulizi kwa kuunda kile ambacho wachambuzi wengine wamekiita "ulingo wa moto" inayozunguka Israel. Ndani ya mfumo huu:
Vikundi hivyo ni pamoja na Hezbollah huko Lebanon, vikundi vya Iraqi, Wahouthi huko Yemen, na vikosi vya washirika huko Syria vyote vilikuwa sehemu ya ukanda huu wa shinikizo.
Lakini cahngamoto kutokana na kile kinachoitwa "mhimili wa upinzani" katika miaka ya hivi karibuni, hasa kilichotokea nchini Syria na kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad, kimevunja sehemu muhimu ya mnyororo huo wa ushawishi wa kikanda.
Iran sasa imeingia kwenye mtindo mpya, lengo si tu kufanya mashambulizi ya adui kuwa magumu au ya gharama kubwa, bali pia kuonyesha kwamba shambulio lolote dhidi ya yake litakabiliwa na jibu la moja kwa moja na lenye maumivu makubwa kwa mshambuliaji.
Kwa maneno mengine, badala ya kutegemea sana mtandao wa washirika wa kikanda kama Hezbollah, makundi ya Iraq, au washirika wa Syria ili kuzuia maadui wake, Iran imeanza kuweka mkazo zaidi kwenye uwezo wake wa moja kwa moja wa kulipiza kisasi kupitia makombora ya masafa marefu, ndege zisizo na rubani, na mifumo mingine ya kijeshi.
Mabadiliko haya yanaonyesha jinsi mazingira ya kimkakati ya Iran yamebadilika baada ya kudhoofika kwa baadhi ya washirika wake wa kikanda. Hata hivyo, licha ya mabadiliko hayo, Hezbollah bado inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa Iran, si tu kama nguvu ya kijeshi bali pia kama sehemu ya ushawishi wake wa kisiasa na wa kimkakati katika Mashariki ya Kati.
Kwa mtazamo huu, Hezbollah imechukua jukumu jipya katika mkakati wa Iran; huenda isiwe tena nguzo kuu ya kuzuia maadui lakini bado ni sehemu ya mfumo wa shinikizo.
Kulingana na Bw. Azizi, Hezbollah iliweza kutingisha kwa kiasi fulani sehemu ya uwezo wa ulinzi wa Israel wakati wa vita vya hivi karibuni, na jambo hili liliisaidia Iran kuelekeza mashambulizi yake dhidi ya Israel kwa kiwango kikubwa zaidi katika nusu ya pili ya vita.
Hata hivyo, Michael Young anaamini kwamba Hezbollah haina tena "uwezo wa kumzuia adui" kwa ajili ya Iran.











