Utafiti: Zaidi ya nusu ya wanawake wanaamini kuna mazingira yanayoweza kuhalalisha mume kumpiga mke

Haween

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Zaidi ya nusu ya wanawake nchini Ethiopia wanaamini kuwa kuna mazingira ambayo yanaweza kumhalalishia mwanaume kumpiga mke wake, kwa mujibu wa utafiti mpya uliobaini kuwa mitazamo kuhusu ukatili wa majumbani bado imejikita katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo.

Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Takwimu ya Ethiopia uligundua kuwa asilimia 55 ya wanawake walikubali kuwa angalau sababu moja inaweza kumfanya mume awe na haki ya kumpiga mke wake. Kwa upande wa wanaume, asilimia 39 walitoa jibu kama hilo.

Matokeo hayo yalitolewa katika Utafiti wa Kitaifa wa Idadi ya Watu na Afya uliochapishwa Julai 2025, uliowashirikisha karibu watu 30,000. Utafiti huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Takwimu ya Ethiopia, wizara za Afya na Mipango na Maendeleo, pamoja na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa.

Washiriki waliulizwa kama kuna mazingira yanayoweza kuhalalisha mume kumpiga mke wake, ikiwemo chakula kuungua, ugomvi wa kifamilia, mke kutoka nyumbani bila kumjulisha mume, kupuuza watoto au kukataa kushiriki tendo la ndoa.

Utafiti huo uligundua kuwa asilimia 55 ya wanawake walikubali kuwa kuna angalau sababu moja inayoweza kuhalalisha mwanaume kumpiga mke wake. Kwa upande wa wanaume, asilimia 39 walitoa jibu hilo. Hii inaonyesha kuwa wanawake wengi kuliko wanaume bado wanaamini kuwa mazingira fulani yanaweza kuhalalisha ukatili wa majumbani.

Wengi wa wanawake na wanaume waliokubali kitendo hicho walitaja kupuuzwa kwa watoto kuwa sababu inayoweza kuhalalisha ukatili huo.

Hata hivyo, ripoti inaonyesha kuwa idadi ya wanawake wanaoshikilia mtazamo huo imekuwa ikipungua kwa miaka mingi. Miaka kumi iliyopita ilikuwa asilimia 63, huku takribani miaka 25 iliyopita ikifikia asilimia 85.

Kwa upande mwingine, idadi ya wanaume wanaoamini kuwa kuna sababu za kumpiga mke imeongezeka. Miaka kumi iliyopita ilikuwa asilimia 28, lakini sasa imefikia asilimia 39.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za wanawake la Setawit, Dkt. Sena Tefera, amesema inatia wasiwasi kuona wanawake wengi kuliko wanaume wakiamini kuwa ukatili wa majumbani unaweza kuhalalishwa.

Amesema wanawake wengi wanaopigwa na waume zao hukulia katika mazingira yanayofanya vitendo hivyo kuonekana kuwa vya kawaida.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 30 ya wanawake walio kwenye ndoa au wanaoishi na wenza wao wamewahi kukumbana na angalau aina moja ya ukatili wa kijinsia, ikiwemo vipigo, unyanyasaji wa kingono au wa kisaikolojia.

Aidha, asilimia 58 ya wanawake waliopitia ukatili huo hawakutafuta msaada wala kumweleza mtu yeyote yaliyowapata.

gabar

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dkt. Tefera amesema sababu zinazochangia wanawake kuhalalisha ukatili huo ni pamoja na ndoa za utotoni, kukulia katika familia zenye ukatili, utegemezi wa kiuchumi na umaskini.

Ameongeza kuwa katika jamii nyingi nchini Ethiopia, vipigo na unyanyasaji wa kisaikolojia bado havitambuliwi kama aina za ukatili.

Utafiti huo pia umebaini kuwa kiwango cha elimu na hali nzuri ya kipato hupunguza uwezekano wa mtu kuamini kuwa kumpiga mke kunakubalika.

Asilimia 63 ya watu wasio na elimu waliamini kuwa kuna sababu zinazoweza kuhalalisha kitendo hicho, huku miongoni mwa wanawake wenye elimu ya zaidi ya sekondari idadi hiyo ikishuka hadi asilimia 29.

Wanawake wanaoishi vijijini walionekana kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuunga mkono mtazamo huo kuliko wanaoishi mijini.

Kwa upande wa maeneo, mkoa wa Sidama uliongoza kwa kuwa na asilimia 74 ya wanawake wanaoamini kuwa kuna mazingira yanayoweza kuhalalisha mume kumpiga mke wake, ukifuatiwa na Mkoa wa Kusini Magharibi wa Ethiopia wenye asilimia 71.

Kinyume chake, eneo la Somali nchini Ethiopia lilikuwa na kiwango cha chini zaidi, ambapo ni asilimia 23 pekee ya wanawake waliokubaliana na mtazamo huo.

Watafiti wanasema kubadili mitazamo kuhusu ukatili wa majumbani kutahitaji kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kuongeza elimu kwa umma na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria, afya na ushauri wa kisaikolojia kwa waathirika wa ukatili.