Je, Nchimbi na Gachagua wameponzwa na misimamo yao kisiasa?

S

Chanzo cha picha, BBC Via EPA

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika siasa za Afrika Mashariki, nafasi ya Makamu wa Rais mara nyingi huonekana kama daraja kati ya Rais na serikali.

Katika mifumo ya kisiasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais ndiye mwenye mamlaka makubwa zaidi katika utendaji wa serikali. Makamu wake anatarajiwa kumsaidia katika kutekeleza majukumu ya serikali, lakini pia inaweza kuwa nafasi yenye mipaka mikali, hasa pale makamu anapoanza kujenga msimamo unaotofautiana hadharani na mkuu wa nchi.

Emmanuel Nchimbi wa Tanzania na Rigathi Gachagua wa Kenya wamejikuta kwenye dhoruba inayofanana kutokana na cheo chao cha kuwa wa pili katika uongozi wa ngazi ya juu.

Wote waliingia madarakani kama manaibu wa marais waliokuwa na ushawishi mkubwa kisiasa. Wote walikuwa sehemu ya serikali zilizokuwa madarakani. Na wote waliishia katika mgogoro wa kisiasa na marais wao.

Lakini, hakuna ushahidi kwamba kujiuzulu kwa Nchimbi kulitokana na mazingira kama yale yaliyomkabili Gachagua. Badala yake, Nchimbi amewasilisha uamuzi wake kama wa hiari, akisema ametimiza ahadi aliyowahi kutoa kwa Rais Samia.

Naye Gachagua aliondolewa madarakani kupitia mchakato wa bunge mwaka 2024, baada ya Bunge na Seneti kuunga mkono kuondolewa kwake.

Hivyo, hakuna sababu ya kusema kwamba Nchimbi amepitia kilichompata Gachagua.

Lakini visa vyao vinaibua swali moja kubwa kuhusu nafasi ya Makamu wa Rais katika siasa za Afrika Mashariki: Ana uhuru kiasi gani wa kuwa na msimamo wake pale anapotofautiana na Rais?

Gachagua na mgongano wa wazi na Ruto

h

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gachagua aliingia serikalini akiwa mshirika muhimu wa William Ruto katika uchaguzi wa 2022. Lakini uhusiano wao ulianza kuzorota kadiri tofauti za kisiasa zilivyozidi kuonekana.

Kauli yake kwamba serikali ilikuwa kama kampuni yenye wenye hisa, ambapo jamii zilizomsaidia Ruto kushinda zilipaswa kunufaika zaidi, ilizua mjadala mkubwa kuhusu siasa za kikabila na mgawanyo wa rasilimali za taifa.

Pia alikosolewa kwa kuingilia masuala yaliyohusu serikali za kaunti na kwa kauli zake kuhusu taasisi za usalama.

Katika kile kilichokuwa moja ya migongano mikubwa, Gachagua aliikosoa hadharani Idara ya Taifa ya Ujasusi, NIS, kuhusu namna ilivyomjulisha Rais kuhusu maandamano ya vijana ya 2024.

Bunge lilitaja pia mashambulizi yake dhidi ya NIS kama sehemu ya tuhuma zilizokuwa katika mchakato wa kumuondoa madarakani.

Hatimaye, Bunge la Kitaifa lilipitisha hoja ya kumng'oa madarakani kwa kura 282 dhidi ya 44. Seneti baadaye ilimpata na hatia katika mashtaka matano kati ya 11, na kumuondoa madarakani.

Gachagua mwenyewe baadaye alisema alijaribu kwanza kumweleza Ruto kwa faragha kuhusu sera alizoona hazikubaliki kwa wananchi. Alisema alipoanza kuzungumza hadharani ndipo uhusiano wao ulipozidi kuvurugika.

Nchimbi na safari iliyokatika ghafla

n

Chanzo cha picha, MWANANCHI

Kwa Nchimbi, simulizi ni jipya lakini lina maswali mengi.

Nchimbi alichukua nafasi ya Makamu wa Rais baada ya uchaguzi wa 2025, lakini hakudumu hata mwaka mmoja. Tarehe 25 Agosti 2026 alitangaza kujiuzulu na pia kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma. Rais Samia alikubali uamuzi huo.

Kilichofanya kujiuzulu kwake kuvutia zaidi ni mazingira yaliyotangulia uamuzi huo.

Nchimbi alikuwa ameibua hadharani suala la Katiba mpya katika tukio la haki za binadamu jijini Dar es Salaam. Alisema Tanzania inahitaji Katiba inayolinda maendeleo ya wananchi pamoja na utu na haki zao. Kauli hiyo ilikuja wakati ambapo mjadala kuhusu utawala, uchaguzi na haki za kisiasa nchini Tanzania ulikuwa tayari umeongezeka.

Kisha, baada ya kujiuzulu, CCM ilimvua uanachama. Uamuzi huo ulifikiwa na Kamati Kuu ya chama katika kikao cha dharura jijini Dar es Salaam. CCM pia ilimteua Deogratius Ndejembi kuwa mgombea wake wa nafasi ya Makamu wa Rais.

Hapa ndipo simulizi la Nchimbi linatofautiana na la Gachagua.

Gachagua alipambana na mfumo hadi mwisho na akaondolewa kupitia Bunge. Nchimbi aliondoka kwa barua ya kujiuzulu, lakini hatua iliyofuata ya kufukuzwa CCM imeongeza maswali kuhusu kilichotokea ndani ya chama na serikali.

Lakini je, kweli simulizi zao zinafanana?

Kwa kiasi fulani, ndiyo.

Wote walikuwa manaibu wa marais ambao uhusiano wao na wakuu wa nchi ulifikia hatua ya kuvurugika.

Wote waliingia kwenye mijadala ya kisiasa ambayo iliwafanya waonekane kuwa na msimamo binafsi wenye uzito.

Na wote walijikuta wakiondoka katika nafasi zao katika mazingira ambayo yalizua mjadala kuhusu mipaka ya mamlaka ya Makamu wa Rais.

Gachagua alikabiliwa na mchakato rasmi wa bunge uliokuwa na tuhuma 11, zikiwemo madai ya kuchochea mgawanyiko wa kikabila, kudhoofisha taasisi za serikali, kukiuka Katiba na utovu wa nidhamu.

Nchimbi amejiuzulu mwenyewe na hakutoa sababu ya moja kwa moja ya kuondoka kwake. Taarifa rasmi ya serikali haikutaja sababu ya kujiuzulu, ingawa ripoti mbalimbali zimeeleza kuhusu mvutano wa kisiasa na misimamo yake kuhusu mageuzi ya Katiba.

Mamlaka ya Makamu wa Rais Afrika Mashariki

Kisa cha Gachagua na Nchimbi kinaibua swali kubwa zaidi kuliko hatima ya watu wawili.

Je, Makamu wa Rais ana nafasi gani ya kuwa na msimamo wake binafsi katika serikali ambayo yeye ni sehemu yake?

Gachagua alionyesha wazi gharama za kuingia katika mgongano wa hadharani na Rais. Nchimbi sasa anaacha swali hilo likiwa wazi zaidi, hasa baada ya kujiuzulu na baadaye kuvuliwa uanachama wa CCM.

Tofauti zao pia zinaonyesha tofauti za mifumo ya kisiasa ya Kenya na Tanzania.

Nchini Kenya, mgogoro kati ya Rais na Naibu Rais unaweza kufika moja kwa moja Bungeni kupitia mchakato wa bunge. Nchini Tanzania, nafasi ya Makamu wa Rais imefungamana kwa karibu zaidi na mfumo wa urais na muundo wa chama tawala.

Matokeo ni tofauti, lakini visa vyote vinaweka ofisi ya Makamu wa Rais katika mjadala mpana wa kikanda kuhusu mamlaka, uaminifu wa kisiasa na nafasi ya pili katika uongozi wa nchi.

Ni funzo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

D

Chanzo cha picha, EAC

Kujiuzulu kwa Nchimbi kunatokea wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, ikijaribu kusukuma mbele ajenda yake ya muungano wa kisiasa.

Jumuiya hiyo inaendelea na mchakato wa kuandaa Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, ambalo limekusudiwa kuwa hatua ya mpito kuelekea lengo kubwa la Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.

Mchakato huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, amani na usalama, sera za nje na utawala wa kikanda.

Ikiwa nchi wanachama zinakabiliwa na misukosuko kuhusu urithi wa uongozi, mamlaka ya Makamu wa Rais na mgawanyo wa madaraka ndani ya serikali, taasisi za Afrika Mashariki zitakuwa imara kiasi gani kadiri mchakato wa kuunganisha kisiasa unavyozidi kusonga mbele?

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa kisiasa, mazingira waliojipata Nchimbi na Gachagua yanaonyesha kwamba kuwa mtu wa pili katika uongozi wa nchi si lazima kumaanishe kuwa na nafasi ya pili katika siasa.