Majengo 8 yenye rangi za kuvutia zaidi duniani

Chanzo cha picha, Pompidou Center, Malaga/Getty Images
Kwa muda mrefu, wabunifu wa majengo wamekuwa wakitumia rangi kama nyenzo muhimu ya kuongeza mvuto na ubunifu katika kazi zao.
Matumizi ya rangi kuwasilisha hisia za furaha na uzuri yamekuwepo kwa maelfu ya miaka.
Jamii za kale za Neanderthal zilipamba kuta za mapango kwa rangi zilizotengenezwa kutoka kwenye udongo na madini mbalimbali.
Baadaye, ustaarabu wa Misri na Ugiriki ya kale ulijenga mahekalu yenye rangi ang'avu, huku Waroma wakitumia marumaru za rangi tofauti kupamba majengo yao makubwa.
Katika vipindi vyote hivyo vya historia, rangi ilikuwa sehemu muhimu ya usanifu na ilionekana karibu kila mahali.
Rangi ilitekeleza jukumu muhimu katika madirisha ya vioo vya makanisa ya enzi za kati, pamoja na dari na kuta zilizopambwa kwa michoro ya fresco wakati wa kipindi cha Renaissance nchini Italia.
Pia imekuwa sehemu muhimu ya majengo ya kisasa yenye nyuso angavu na zinazong'aa katika karne ya 20 na 21. Mfano mmoja ni lango lenye umbo la mchemraba la Kituo cha Pompidou mjini Malaga, lililobuniwa na Daniel Buren, ambalo linajulikana kwa matumizi yake ya kipekee ya mwanga na rangi.
Mbunifu Adam Nathaniel Furman na mwandishi Kate Mazade, katika kitabu chao Chromatic Architecture: The Craft of Colour in Design, wanaeleza kwamba rangi ni "kipengele muhimu kinacholiinua jengo na kulifanya livutie na kuleta furaha kwa namna ambayo haiwezi kufanikishwa kwa njia nyingine."
Majengo haya manane yanadhihirisha jinsi rangi zinavyoweza kubadilisha sura na hisia za majengo, huku zikiwapa wasanifu majengo msukumo wa kutumia rangi kwa ujasiri zaidi katika kazi zao.
Hekalu la Sri Ranganatha Swamy, Tamil Nadu, India

Chanzo cha picha, Rupesh Maurya/ Creative Commons
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hekalu la Sri Ranganatha Swamy huko Tamil Nadu ni miongoni mwa majengo yanayotambulika zaidi nchini India.
Mchanganyiko wake wa rangi angavu za bluu, kijani, njano, nyekundu na zambarau hulifanya kuwa mfano bora wa jinsi rangi zinavyoweza kutumika kuonyesha utamaduni, imani na utambulisho wa eneo husika.
Muonekano wake wa kuvutia umeifanya hekalu hilo kuwa moja ya alama maarufu za usanifu wa Kihindu duniani.
Ujenzi wa Hekalu la Sri Ranganatha Swamy ulianza katika karne ya kwanza BK na kuendelea kupanuliwa na tawala mbalimbali kwa muda wa karne nyingi, hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 20.
Leo, ni moja ya majengo makubwa zaidi ya kidini duniani, likiwa na eneo la zaidi ya hekta 60.
Eneo hilo limezungukwa na malango 21 ya kuingilia yanayojulikana kama gopuram, ambayo yamepambwa kwa mamia ya sanamu za rangi angavu na za kuvutia. Mapambo hayo ya pande tatu huifanya hekalu hiyo kuwa moja ya mifano maarufu zaidi ya usanifu wa jadi wa Kihindu.
2. Palau de la Musica Catalana, Barcelona, Hispania

Chanzo cha picha, Consuelo Borroni/ Pexels
Uzuri wa ukumbi wa tamasha wa Palau de la Música Catalana, uliojengwa mwaka 1908, umekuwa ishara ya utambulisho wa Catalonia, eneo la Uhispania lenye utajiri wa kitamaduni na historia ya maendeleo ya viwanda.
Jengo hilo, lililobuniwa na mbunifu Lluís Domènech i Montaner, linaunganisha mitindo mbalimbali ya usanifu ikiwemo Art Nouveau, Romanesque na Neo-Gothic, pamoja na athari za usanifu wa Mudéjar na mila za Valencia.
Kwa mwanahistoria wa usanifu Geoffrey Furman, kila sehemu ya Palau de la Música imejaa ishara na alama zinazolipa jengo hilo sura ya ulimwengu wa hadithi za kichawi.
"Kila jiwe, nguzo, ukingo na mapambo ya jengo hili yamepambwa kwa rangi na maumbo ya kuvutia yanayoonekana kuyaingiza maisha kwa namna ya ajabu na ya kichawi," anaeleza Furman.
3. Jengo la Guardian, Detroit, Michigan, Marekani

Chanzo cha picha, Guardian Building
Jengo hili la ofisi lililojengwa mwaka 1929 na kubuniwa na mbunifu Wirt C. Rowland linajulikana miongoni mwa wakazi wa eneo hilo kama "Kanisa Kuu la Fedha" kutokana na muonekano wake wa fahari na umuhimu wake wa kihistoria.
Pia linahesabiwa kuwa miongoni mwa majengo muhimu zaidi duniani yaliyobuniwa kwa mtindo wa usanifu wa Art Deco.
Akizungumza na BBC, Mazade anasema Rowland alitumia rangi kuonyesha ustadi wa hali ya juu wa mafundi wa eneo la Maziwa Makuu nchini Marekani mwanzoni mwa karne ya 20.
Sehemu ya nje ya jengo hilo imefunikwa na karibu matofali milioni mbili pamoja na vigae vya terracotta vyenye rangi ya chungwa, vinavyolipa mwonekano wake utambulisho wa kipekee.
Ndani, ukumbi mkuu una dari yenye matao ya viwango vitatu, iliyopambwa kwa vigae vya rangi za msingi vilivyopangwa katika muundo unaofanana na blanketi la viraka.
"Jengo hili lilikuwa alama ya mafanikio makubwa ya kibiashara ya Detroit katika enzi yake, na hadi leo linaendelea kuwa kumbukumbu hai ya kipindi hicho cha ustawi," anaongeza Mazade.
4.Duka la De Bijenkorf, Eindhoven, Uholanzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Inasemekana mbunifu, msanifu na msanii wa Italia, Gio Ponti, alipata msukumo wa kubuni jengo hili mwaka 1969 kutokana na mandhari ya mashamba ya Uholanzi yenye gridi za kijani kibichi alizoziona kutoka dirishani mwa ndege.
Kuipa mvuto wa kipekee jengo kubwa lisilo na madirisha kungekuwa changamoto kwa wasanifu wengi, lakini si kwa Ponti, ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi muhimu wa usanifu wa kisasa pamoja na majina makubwa kama Le Corbusier na Mies van der Rohe.
Kwa mujibu wa Geoffrey Furman, Ponti alilibadilisha jengo hilo kuwa "mandhari kubwa ya kuvutia yenye mng'aro wa zumaridi", lililoonekana tofauti kabisa na majengo mengine ya wakati huo.
Kwa kufanya hivyo, aliubadilisha uso wa kawaida wa zege uliotawala katika enzi hiyo na kuugeuza kuwa kazi bora ya sanaa ya kisasa iliyotoa sura mpya kwa jiji hilo.












