Kwa nini makamanda wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani wanajiuzulu?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kujiuzulu kwa Waziri wa Jeshi la Marekani, Dan Driscoll, kumeibua tena mjadala kuhusu mwenendo wa mambo ndani ya Pentagon.
Ingawa Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amewafukuza au kuwaondoa maafisa kadhaa waandamizi wa jeshi na serikali katika miezi ya karibuni, wakosoaji wanasema tofauti zinazoonekana sasa hazihusu tu kuunga mkono au kupinga sera za utawala wa Marekani. Badala yake, zinahusiana pia na kiwango ambacho maafisa hao wanaafikiana na mtindo wa uongozi wa Hegseth pamoja na namna anavyofanya maamuzi.
Mabadiliko hayo yamegusa baadhi ya viongozi wa juu kabisa wa vikosi vya Marekani. Miongoni mwa walioondolewa ni Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu (Army), Jenerali Randy George; kamanda wa majeshi ya Marekani barani Ulaya na Afrika, Jenerali Christopher Donahue; Katibu wa Jeshi la Wanamaji, John Fallon; Kamanda wa Southern Command, Admirali Alvin Holsey; Kamanda wa Jeshi la Anga, Jenerali David Alvin; na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi wa Pamoja (Joint Chiefs of Staff), Jenerali Charles Q. Brown Jr.
Kujiuzulu kwa Driscoll kumevutia umakini mkubwa zaidi kwa sababu alikuwa mteule wa Rais Donald Trump na mmoja wa watu waliokuwa karibu na Makamu wa Rais J.D. Vance. Hapo awali, Ikulu ya White House ilikuwa imemsifu kwa mchango wake katika kusukuma mbele baadhi ya mipango ya utawala wa Trump.
Hata hivyo, tofauti zake na Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth ziliongezeka na kuwa kubwa kiasi kwamba hatimaye aliamua kuachia wadhifa wake.
Lakini tofauti hizo zilihusu nini hasa?

Chanzo cha picha, Adam Gray/Getty Images
Je, ni migogoro binafsi au mvutano kuhusu mustakabali wa jeshi?
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani, chanzo kikuu cha mvutano kati ya Dan Driscoll na Pete Hegseth kilikuwa namna ya uongozi na maamuzi yaliyokuwa yakifanywa ndani ya Wizara ya Ulinzi.
Ripoti hizo zinasema kuwa Driscoll alimweleza moja kwa moja Rais Donald Trump kuhusu wasiwasi wake juu ya baadhi ya hatua za Hegseth, zikiwemo uamuzi wa kuwaondoa makamanda kadhaa wa ngazi za juu wa jeshi. Hatua hiyo, kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, ilimkasirisha Hegseth na kuongeza mvutano kati yao.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, tofauti hizo hazikuhusu tu mahusiano binafsi au mtindo wa usimamizi. Driscoll alikuwa akiongoza juhudi za mageuzi makubwa ndani ya Jeshi la Nchi Kavu la Marekani, akihimiza matumizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani pamoja na mifumo mingine ya kisasa isiyoendeshwa na binadamu.
Msukumo wa mabadiliko hayo ulitokana kwa kiasi kikubwa na mafunzo yaliyopatikana katika vita vya Ukraine, ambako teknolojia ya ndege zisizo na rubani imekuwa na mchango mkubwa katika uwanja wa mapambano. Driscoll aliamini kuwa Jeshi la Marekani lilihitaji kubadilika haraka ili kuendana na mazingira mapya ya kivita.
Pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia hiyo, alitaka pia kufanyika kwa mabadiliko ya kimuundo ndani ya vikosi vya nchi kavu ili kuvifanya kuwa vya kisasa zaidi na vyenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za baadaye.
Lakini kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, Driscoll aliona kuwa Hegseth alikuwa akikwamisha mara kwa mara au kupunguza upeo wa baadhi ya mipango hiyo ya mageuzi. Hali hiyo ilizidisha tofauti zilizokuwapo kati ya viongozi hao wawili, na hatimaye ikachangia uamuzi wa Driscoll kujiuzulu.
Kuondoka kwake sasa kumeibua maswali mapya kuhusu mwelekeo wa uongozi ndani ya Pentagon na namna ambayo mageuzi ya jeshi la Marekani yataendelea katika kipindi kijacho.
Vita dhidi ya Iran vilitajwa pia kuwa moja ya vyanzo vya mvutano kati ya viongozi hao wawili. Driscoll, pamoja na baadhi ya wakosoaji wengine, walikuwa na wasiwasi kwamba mabadiliko makubwa katika safu za juu za uongozi wa kijeshi wakati wa operesheni za kijeshi yangeweza kudhoofisha uwezo wa jeshi kuongoza, kuratibu na kusimamia majukumu yake kwa ufanisi.
Wakati huo huo, gazeti la The Washington Post liliripoti kuhusu kile lilichokieleza kama "pengo la uongozi" katika baadhi ya maeneo ya jeshi la Marekani. Ripoti hiyo pia ilieleza kuwepo kwa hali ya kutokuwa na uhakika na wasiwasi miongoni mwa baadhi ya maafisa wa ngazi za juu kufuatia mabadiliko ya mara kwa mara katika uongozi wa kijeshi.

Chanzo cha picha, Alex Wong/Getty Images
Hegst anatafuta nini?
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa suala hilo linavuka mipaka ya mvutano wa kibinafsi kati ya Pete Hegseth na Dan Driscoll.
Kwa mtazamo wao, Waziri wa Ulinzi wa Marekani anaonekana kujaribu kuimarisha ushawishi wake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na utungaji sera ndani ya Pentagon. Katika muktadha huo, kuondolewa kwa makamanda na maafisa waandamizi kunatazamwa na baadhi ya wachambuzi kama sehemu ya juhudi pana za kurekebisha muundo wa uongozi wa jeshi la Marekani, hata kama hatua hizo zinahusisha kuondoka kwa baadhi ya viongozi wenye uzoefu mkubwa na nafasi zao kuchukuliwa na maafisa wenye uzoefu mdogo.
Ripoti kadhaa pia zimeashiria kwamba, mbali na kuunga mkono sera za utawala wa Trump, uwezo wa maafisa kuendana na mtindo wa uongozi na mbinu za Hegseth katika utekelezaji wa sera hizo umekuwa jambo muhimu katika kuamua mustakabali wao ndani ya Pentagon.
Katika mazingira hayo, mjadala unaoibuka si tena kama viongozi waandamizi wa jeshi wanaunga mkono sera za utawala huo au la. Badala yake, swali kuu ni ni kwa kiwango gani wanaweza kutofautiana na mbinu, maamuzi na vipaumbele vya Waziri wa Ulinzi huku wakiendelea kubaki katika nyadhifa zao.
Je, Pentagon inapoteza sauti huru?
Kwa miaka mingi, tawala tofauti za Marekani zimekuwa zikitegemea ushauri wa kitaalamu kutoka kwa maafisa wa kijeshi na watumishi waandamizi wa Wizara ya Ulinzi, hata pale ambapo ushauri huo ulikuwa unatofautiana na msimamo wa viongozi wa kisiasa.
Katika mfumo huo, makamanda wa jeshi na wataalamu wa masuala ya ulinzi walitarajiwa kutoa tathmini zao kwa uwazi na kwa msingi wa taaluma, bila kuzingatia iwapo maoni hayo yangepokelewa vyema na Waziri wa Ulinzi au Rais. Uamuzi wa mwisho ulipofikiwa, taasisi nzima ya ulinzi ilitarajiwa kuutekeleza.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa wimbi la hivi karibuni la kuondolewa kwa maafisa waandamizi linaweza kuwa linadhoofisha utamaduni huo.
Kwa mujibu wa mtazamo huo, ikiwa maafisa wa kijeshi na wataalamu wa ulinzi wataanza kuhisi kuwa kutoa maoni yanayotofautiana na yale ya viongozi wa kisiasa kunaweza kuhatarisha nafasi zao, huenda wakasita kuwasilisha tathmini ambazo haziendani na matarajio ya wakubwa wao.
Wachambuzi hao wanasema hatari ya hali kama hiyo ni kwamba viongozi wa kisiasa, akiwemo rais, wanaweza kukosa maoni mbadala na tathmini huru zinazohitajika katika kupima chaguzi mbalimbali kabla ya kufikia maamuzi muhimu ya usalama wa taifa.
Katika mazingira hayo, kujiuzulu kwa Dan Driscoll kumezua maswali mapya. Ikiwa mtu aliyekuwa akionekana kuwa mshirika wa kisiasa wa Donald Trump ameona kuwa haiwezekani kuendelea na majukumu yake, baadhi ya wachambuzi wanauliza ni kwa kiwango gani maafisa wa kijeshi na viongozi wengine ndani ya Pentagon wanaweza kutoa maoni ya kitaalamu yanayokinzana na mbinu za Waziri wa Ulinzi au sera za Ikulu bila kuhofia athari kwa taaluma zao.












