Wanasayansi wanaweza kujifunza nini roketi ya SpaceX iliyoanguka mwezini?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Roketi ya SpaceX iliyopoteza mwelekeo inaaminika kugonga uso wa Mwezi na kutengeneza shimo jipya karibu na bonde maarufu la Einstein, jambo linalowapa wanasayansi fursa adimu ya utafiti inayoweza kusaidia safari za anga za juu za siku zijazo.

Sehemu ya juu ya roketi ya Falcon 9, ambayo ilikuwa imejitenga, iligonga uso wa Mwezi karibu na Shimo la Einstein siku ya Jumatano kwa kasi ya takriban kilomita 8,700 kwa saa.

Mwangaza mdogo lakini wa kuvutia uliotokana na mgongano huo ulikuwa mgumu kuonekana hata kwa wanaastronomia wasio wataalamu wenye darubini za kisasa, lakini vituo vikubwa vya uchunguzi wa anga katika mabara ya Marekani sasa vinachunguza taarifa hizo.

Huenda ikachukua siku au hata wiki kuelewa kikamilifu tukio hilo na yale yanayoweza kujifunza kutoka nalo, lakini kwa wanasayansi wanaochunguza muundo na nyuso za sayari, tukio hili ambalo halikutarajiwa ni fursa adimu ya kisayansi.

Falcon 9 ya SpaceX ni roketi inayoweza kutumika tena na ambayo imeshatumika katika safari mbalimbali za anga. Roketi hiyo imeundwa kwa namna ambayo sehemu yake moja hurejea Duniani, huku sehemu nyingine zikiachwa angani.

Roketi hiyo ilirushwa kutoka Florida mwezi Januari mwaka jana, ikiwa imebeba vyombo viwili vilivyokusudiwa kutua mwezini.

Jukumu la roketi hiyo lilikuwa kusukuma sehemu yake ya juu kwa nguvu ya kutosha ili kuviondoa vyombo vyote viwili kutoka kwenye mzunguko wa Dunia na kuviingiza katika njia inayoelekea Mwezini—lengo ambalo lilifanikiwa.

Sehemu ya roketi hiyo iliyomaliza kazi yake—ambayo ina ukubwa unaokaribia ule wa jengo la ghorofa tano na uzito wa takribani kilo 4,000—iliachiliwa katika njia ndefu ya duara iliyoielekeza kuelekea Mwezini na kisha kuirejesha ikizunguka Dunia.

Kwa muda wa miezi 18 iliyofuata, mvutano wa Dunia, Mwezi, na Jua, na hata shinikizo dogo sana kutoka kwa mwanga wa jua, vililitumia nguvu hafifu lakini endelevu.

Wataalamu wa nyota waliokuwa wakifuatilia roketi hiyo hatimaye waligundua kuwa athari hizo japo ni ndogo sana zilikuwa zimeiweka katika mkondo wa kugongana na Mwezi, na kusababisha iongeze kasi kila siku.

Mgongano huo ulitokea mwendo wa saa 1:35 asubuhi (kwa Saa za Mashariki) siku ya Jumatano. Wakati huo, anga lilikuwa wazi katika maeneo mengi duniani, lakini mwanga uliotokana na mgongano huo ulikuwa hafifu sana na haungeonekana hata kwa kutumia darubini.

Wapenda-astronomia waliokuwa wakitazama kutoka maeneo yenye giza pia walikuwa na nafasi ndogo ya kuona mwanga huo, kwani ulidumu kwa muda mfupi sana—sehemu tu ya sekunde.

Hata hivyo, huenda waliona wingu la vumbi lililoenea hadi umbali wa takribani kilomita 100 na kusalia angani kwa dakika chache.

Hata vyombo vya anga vilivyokuwa vikizunguka Mwezi havikuwa katika nafasi nzuri ya kushuhudia tukio hilo la mgongano moja kwa moja.

Chombo cha Korea Kusini kiitwacho Danuri kilikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kunasa tukio hilo, kwani kilipita karibu na eneo la mgongano muda mfupi kabla ya tukio hilo kutokea. Timu ya wataalamu wa mradi huo iliambia vyombo vya habari vya Korea kuwa picha zozote zitakazopatikana zitatolewa baada ya tafiti za kisayansi kukamilika.

Katika siku zijazo, chombo cha NASA kama Lunar Reconnaissance Orbiter kitakuwa katika nafasi ya kupiga picha eneo la mgongano, jambo litakalowezesha kulinganisha picha za kabla na baada ya tukio hilo.

Huenda taarifa za kwanza za kisayansi na picha zikatoka kwenye darubini zenye nguvu zilizoko katika mabara ya Amerika, ambapo bado kulikuwa na giza wakati mgongano huo ulipotokea.

Hata hivyo, kurekodi kitu chenye urefu wa mita 14 kikigonga uso wa Mwezi kutoka umbali wa kilomita 385,000 si kazi rahisi.

Kuchakata picha ili kuondoa kasoro na kuboresha ubora wake kunaweza kuchukua saa, siku, au hata wiki, kwani ni lazima wanasayansi wachunguze na kuchambua taarifa hizo kwa uangalifu.

Kwa kuwa watafiti wanajua mapema ukubwa kamili wa kombora hilo, kasi yake, na eneo la mgongano, tukio hilo limebadilika kutoka kuwa ajali ya bahati mbaya na kuwa jaribio adimu na lililodhibitiwa.

Hii ni fursa ya kipekee kwa wanasayansi wanaochunguza sayari, kwani inawawezesha kujaribu mifumo yao ya kuelezea jinsi mashimo yanavyotokea kutokana na migongano, jinsi vifaa vinavyosambaa juu ya uso wa mwezi, na jinsi mitetemo inavyosafiri ndani ya mwezi.

Suala hili pia lina umuhimu mkubwa katika nyanja ya vitendo.

Kujua kiasi cha miamba na vumbi vinavyotawanywa na mgongano kutawasaidia wahandisi kubuni vyombo vya kutua na vituo vya mwezini kwa usalama zaidi. Wanaweza kukokotoa umbali ambao vifaa vilivyotupwa nje husafiri na kiwango cha mtetemo wa ardhi karibu na eneo la mgongano.

Vifaa vilivyotupwa nje kutoka chini ya uso wa mwezi pia vinatoa taarifa mpya kuhusu jiolojia ya mwezi, na hivyo kuongeza uelewa wa wanasayansi kuhusu jinsi mfumo wa Dunia na Mwezi ulivyoundwa takriban miaka bilioni 4.5 iliyopita.

Hii si mara ya kwanza kwa kifaa kilichotengenezwa na binadamu kugonga mwezi. Tangu mwaka 1959, vyombo vingi vya anga vimegonga uso wa mwezi; vingine kwa bahati mbaya na vingi kwa makusudi kwa ajili ya utafiti wa kisayansi.

Chombo cha Luna 2 cha Umoja wa Kisovieti ndicho kilikuwa cha kwanza. Kilifuatiwa na vyombo vya Ranger vya NASA katika miaka ya 1960, sehemu mbalimbali za roketi za enzi ya Apollo, na hivi karibuni zaidi, dhamira ya LCROSS mwaka 2009.

Chombo cha anga cha LCROSS kiligongeshwa kwa makusudi kwenye uso wa mwezi ili wanasayansi waweze kutafuta uwepo wa barafu ya maji.

Mgongano wa mwisho uliothibitishwa kutokea kwa bahati mbaya ulikuwa mwaka 2022. Wakati huo, kifaa kilichogonga kilidhaniwa kuwa sehemu ya mabaki ya roketi ya China ya kwenda mwezini iliyozinduliwa mwaka 2014.

Tukio hili ni ukumbusho kwamba taka kama hizo za anga zimekuwa zikikusanyika kimya kimya katika anga inayozunguka Dunia kwa zaidi ya nusu karne.