Madaktari Uganda waipa serikali siku 14 kushughulikia maslahi ya madaktari wanafunzi
Chama cha Madaktari Uganda, UMA, kimeipa Serikali siku 14 kutatua mzozo kuhusu ajira, upangaji wa vituo vya kazi na maslahi ya madaktari wanafunzi.
Chama cha UMA kimeonya kuwa iwapo Wizara ya Afya haitatoa majibu ya maandishi na ya kuridhisha ndani ya muda huo, madaktari nchini kote watafanya mgomo nchini kote.
Rais wa UMA, Daktari Frank Asiimwe, amesema: “Ili kulinda heshima ya taaluma ya udaktari pamoja na ubora na usalama wa utoaji wa huduma za afya, madaktari kote Uganda wataanza mgomo baada ya siku 14 kumalizika iwapo Wizara ya Afya itashindwa kutoa mawasiliano ya wazi, ya maandishi na ya kuridhisha kuhusu upangaji na uwezeshaji wa madaktari wanafunzi.”
Daktari Asiimwe amesema madaktari wataondoa huduma zao baada ya muda huo kumalizika, ingawa huduma za dharura na zile muhimu kwa kuokoa maisha zitaendelea kutolewa.
UMA pia inataka Serikali kuongeza ufadhili katika sekta ya afya, kuondoa zuio la kuajiri wahudumu wa afya, kushughulikia tofauti za mishahara kwa madaktari wasaidizi na kuwapandisha vyeo madaktari ambao wamebaki katika nafasi zao kwa zaidi ya muongo mmoja licha ya kupata tajriba ya juu.
Hatua hiyo inakuja baada ya wanachama wa UMA kupiga kura kuunga mkono madaktari wanafunzi na kuidhinisha kufanya mgomo iwapo Serikali itashindwa kushughulikia malalamiko yao.
Soma Zaidi hapa: