Hadithi ya msichana aliyebakwa na sheikh aliyekuwa 'akimtibu'

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Onyo: Makala haya yana maelezo kuhusu unyanyasaji wa kingono, ukahaba wa kulazimishwa na maneno mengine ambayo baadhi ya watu wanaweza kuyaona ya kuudhi.

"Aria" alikuwa na umri wa miaka 13 aliponyanyaswa kingono na imam aliyemwambia kuwa alikuwa "akimtibu."

Abdul Halim Khan, kiongozi wa dini aliyekuwa akiheshimika sana katika msikiti mmoja huko East London, alikuwa akiwaambia wasichana wadogo na wazazi wao kwamba walihitaji "matibabu" ili kuondoa "mapepo au roho chafu."

Kila mara alipomfanyia vibaya msichana, alimwambia asimweleze mtu yeyote, na alikuwa akimfuatilia kwa karibu, akimtisha kwamba baadhi ya watu wa familia yake wangeweza kuumizwa.

Aria ni jina la kubuni lililotumika katika simulizi hili, si jina lake halisi. Alipozungumzia jambo hilo, alisema: "Nilimwamini kabisa kwamba alikuwa na nguvu zisizo za kawaida kuliko watu wengine."

Alisema Khan alimwambia kwamba "kitu kibaya kingewapata yeye na familia yake" ikiwa angesema kuhusu unyanyasaji aliokuwa akimfanyia, na hakuwa peke yake aliyepitia hali hiyo.

Abdul Halim Khan pia aliwanyanyasa wanawake na wasichana saba katika kipindi cha miaka 11. Msichana mwenye umri mdogo zaidi aliyemnyanyasa alikuwa na miaka 12.

Aliwashawishi wasichana kukutana naye katika maeneo ya faragha kama kwenye nyumba au gari. Akiwa huko, aliwabaka au kuwanyanyasa kingono huku akijifanya kuwa ni jini, roho yenye nguvu za ajabu kupita za kibinadamu.

Abdul Halim Khan alichagua gari lenye vioo vya giza, alimpa mmoja wa waathirika simu ili aweze kuwasiliana naye, na alimshawishi mwingine kufungua dirisha la chumba chake ili waweze kukutana.

Aria alipelekwa kwa kiongozi huyo wa dini na mama yake baada ya kuugua magonjwa yasiyoeleweka na kupata matatizo shuleni, huku mama yake akiamini imam huyo angempa ushauri.

Walipokutana, Khan alimwambia aingie ndani ya gari. "Hapo ndipo alianza kunigusa kwa njia isiyofaa," Aria alisema.

"Niliwekewa kitambaa machoni, na aliniambia kutakuwa na vitu vinavyogonga dirisha la gari. Nilivisikia kweli vikigonga. Lakini bila shaka nilikuwa msichana wa miaka 13, nilikuwa na hofu sana."

Abdul Halim Khan, mwenye umri wa miaka 54, sasa amehukumiwa kifungo cha maisha jela, akiwa anatakiwa kutumikia takribanimiaka 20 gerezani kwa mashambulizi hayo ya kutisha.

Hukumu hizo zinajumuisha makosa tisa ya ubakaji pamoja na mashtaka mengine ya unyanyasaji wa kingono na ukatili dhidi ya watoto yaliyohusisha waathirika saba kutoka jamii ya Kiislamu ya eneo hilo.

Khan alitenda unyanyasaji huo kati ya mwaka 2004 na 2015, akitumia mamlaka na ushawishi wake kuwafanya waathirika wabaki kimya.

Polisi waligundua uhalifu wake mwaka 2018 baada ya mwathirika mwenye umri mdogo zaidi kuripoti tukio hilo kwa kitengo cha shule kinachoshughulikia unyanyasaji. Ilichukua miaka mingine mitano kabla ya kufunguliwa mashtaka rasmi dhidi yake.

BBC ilizungumza na waathirika wawili kusimulia madhila yaliyowakabili.

Familia yangu hainiamini

Farah, ambalo pia si jina lake halisi, alikutana na Abdul Halim Khan akiwa mtoto baada ya Khan kumshawishi mama yake kwamba alihitaji "matibabu." Farah alisema alitumia fursa ya udhaifu wa familia yake.

"Alikuwa anatunga hadithi akisema, 'Naona mambo mabaya yanakuja kwenu, mnahitaji kulindwa, ninahitaji kumlinda binti yako.'"

Khan baadaye alimfanyia Farah ubakaji na unyanyasaji wa kingono, akimwambia kuwa ilikuwa sehemu ya "matibabu" yake.

Farah alisema mwanzoni alijaribu kujishawishi kwamba kile alichokuwa akifanya hakikuwa cha makusudi. "Nilijiambia, 'Hii si sawa, unajua si sawa kukugusa hivi.' Nilichanganyikiwa sana siku hiyo, lakini sikuweza kurudi kuiaambia familia yangu kwa sababu wasingeniamini."

Hatimaye Farah alisimulia kile kilichomtokea kwa wazazi wake alipokuwa mkubwa zaidi, lakini alisema hawakumwamini.

"Familia yangu haikuniamini. Watu ambao nilitarajia wanilinde na kuniunga mkono walinigeuka, walinilaumu, na hadi leo bado wanafanya hivyo," alisema.

"Ninahisi kama ninakosa mambo mengi sana maishani. Najiuliza mimi ni nani? Ninastahili kuwa wapi?"

"Walitishwa na mawazo yao yakabadilishwa."

Melissa Garner, mwendesha mashtaka aliyefanya kazi katika kesi hiyo kwa niaba ya Crown Prosecution Service, alisema hajawahi "kuona kitu kama hiki" kuhusu unyanyasaji alioufanya Abdul Halim Khan dhidi ya wasichana wadogo na wanawake.

Alisema Khan "aliwatisha na kuwabadilisha mawazo" waathirika hadi wakaamini alikuwa akifanya kazi pamoja na mapepo. "Lilikuwa jambo la kushtua sana, na unapokutana na ushuhuda wa namna hiyo, inasikitisha mno."

Aisha K Gill, profesa wa stadi za masuala ya uhalifu katika Chuo Kikuu Bristol ambaye pia alikuwa miongoni mwa walioelezea historia ya kidini ya kesi hiyo, alisema kuwa ingawa Uislamu wa misimamo mikali haukubaliani na uchawi, bado una "ushawishi mkubwa wa kitamaduni."

"Waathirika walifanywa waamini kwamba ni Khan pekee aliweza kuwalinda wao na familia zao dhidi ya magonjwa mabaya na majanga, na kwamba wakijiondoa kwake wangekumbwa na madhara makubwa," Profesa Gill aliongeza.

"Kwa wanawake wa Kiislamu, kuzungumzia unyanyasaji wa kingono ni jambo la aibu sana. Wanawake wengi hulelewa kutokujadili masuala binafsi nje ya familia, na wanaweza kubeba aibu ambayo kwa kweli ilipaswa kuwa ya mhalifu," alisema.

"Mchanganyiko wa mamlaka ya kidini, hofu ya kiroho na udhaifu wa kitamaduni unaifanya kesi hii kuwa tofauti kabisa na nyingine."

Athari kwa waathiriwa

Farah alisema hakupitia utoto wake kama watoto wengine, akisema alichojifunza ni jinsi ya kuvumilia maisha.

Ujumbe wake kwa manusura wengine wa unyanyasaji ni kwamba thamani yao haiamuliwi na yale waliyofanyiwa, na kwamba hawapo peke yao.

"Kuokoka hakukufanyi kuwa dhaifu, kunaonesha nguvu," alisema.

Ingawa Aria alikuwa bado kijana mdogo aliponyanyaswa kingono, hakuweza kumweleza mama yake kuhusu tukio hilo hadi alipokuwa katika miaka yake ya 20. Anasema tukio hilo lilikuwa na athari ya kudumu katika maisha yake.

"Wakati mwingine unajiuliza, ningekuwa mtu wa aina gani kama jambo hili lisingenitokea?"