Chapisho katika mtandao wa kijamii linaweza kusababisha kufungwa jela au kupokonywa uraia katika mataifa ya Ghuba

Muda wa kusoma: Dakika 4

Miezi miwili iliyopita, tangu vita vya Marekani na Israel kuanza dhidi ya Iran, mataifa ya Ghuba yamekuwa yakiwakamata, kuwafungulia mashtaka, na kuwafukuza watu wanaotuhumiwa kuchapisha taarifa zinazosemekana kuathiri usalama wa taifa.

Mamlaka za mataifa hayo, zimezuia kukata rufaa kwa yeyote atakayepatikana na hatia, na hata kuwanyanganya uraia wao.

Baada ya Bahrain kuwapokonya uraia watu 69, Wizara ya usalama wa ndani ya taifa la Bahrain ilitangaza kuwa "Uraia wa Bahrain wa watu hawa umefutwa kwa sababu ya kusifu vitendo vya uhasama vya Iran au kuonyesha uungwaji mkono kwa Iran."

Vyombo vya usalama vinawafuatilia kwa karibu watumiaji wa mitandao ya kijamii na wanaharakati, hatua ambayo mashirika ya haki za binadamu yanasema ni ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.

Nchini Bahrain na Kuwait, waliokamatwa wanatoka katika makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, watu maarufu mitandaoni, wanaharakati wa haki za binadamu, na raia wa kawaida.

Nchi hizi zinasema mashtaka yanayowakabili watu hao yanahusisha kuchochea mgawanyiko wa kidini, kusambaza habari za uongo, matumizi mabaya ya simu za mkononi, na vitendo vingine vinavyoonekana kuhatarisha usalama wa taifa.

Nchi kadhaa katika Ghuba ya Uajemi zilikuwa zimeonya mwanzoni mwa mzozo huo kuwa, kupiga picha, video au kuchapisha taarifa zinazohusiana na mashambulizi ya Iran katika mataifa hayo imepigwa marufuku.

Familia za waliokamatwa nchini Bahrain na Kuwait zinasema zina wasiwasi kuhusu kunyimwa haki ya kusikilizwa kwa haki mahakamani na kupokonywa uraia wao.

Haya yametokea baada ya kutekelezwa kwa sheria mpya ya uraia nchini Kuwait na amri ya hivi karibuni ya serikali ya Bahrain.

Mwanaharakati mmoja wa Kuwait, ambaye aliomba kutotajwa jina lake, aliiambia BBC kuwa mamlaka za taifa hilo zimekuwa zikifuatilia kwa karibu mitandao ya kijamii wakati wa vita.

Mamlaka za mataifa hayo zimeweka vituo vya ukaguzi wa usalama barabarani, ambapo maafisa hukagua simu za mkononi na kuangalia ujumbe, picha na kusikiliza ujumbe wa sauti.

Kufutiwa mashtaka kwa mwandishi wa habari nchini Kuwait

Baada ya wiki kadhaa za kuzuiliwa wakati uchunguzi unafanywa kuhusu madai ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, mahakama ya usalama ya Kuwait iliwahukumu watu 135 tarehe 23 mwezi Aprili.

Washtakiwa 17 walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela katika kesi zinazohusiana na mitandao ya kijamii. Mshtakiwa mmoja, ambaye anaishi nje ya nchi, alihukumiwa bila kuwepo mahakamani kifungo cha jumla cha miaka 10 jela.

Mahakama haikutoa adhabu kwa washtakiwa 109, lakini iliamuru wafute baadhi ya machapisho yao. Wengine tisa waliondolewa mashtaka. Wote walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuchochea migawanyiko ya kidini na kusambaza habari za uongo.

Miongoni mwa waliondolewa mashtaka ni Ahmed Shahabuddin, mwandishi wa habari wa Kuwait na Marekani ambaye alizuiliwa Kuwait mapema mwezi Machi akiwa ameenda kuitembelea familia yake.

Shahabuddin, alishtakiwa kwa kusambaza taarifa za uongo, kuhatarisha usalama wa taifa, na matumizi mabaya ya simu ya mkononi.

Wasiwasi kuhusu kunyanganywa uraia

Mwezi Machi, Kuwait ilipitisha sheria inayotoa adhabu ya kifungo cha miaka 3 hadi 10 jela pamoja na faini, kwa kuchapisha taarifa, video au picha inayoonyesha udhaifu wa jeshi au "kuchochea kuharibu utulivu wa taifa"

Serikali ya taifa hilo pia ilitangaza kuwa itaanzisha mahakama maalum za usalama wa taifa na kupambana na ugaidi.

Mahmoud Shalabi kutoka shirika la Amnesty International anasema hatua hizi zimesababisha watu wengi kujidhibiti kuchapisha vitu mitandaoni na imefanya uandishi huru wa habari kuwa mgumu zaidi nchini humo.

BBC ilizungumza na raia mmoja wa Kuwait ambaye ndugu yake alikamatwa mwanzoni mwa vita.

Alieleza kuwa kukamatwa huko, kulihusiana na taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kupenda machapisho, na kuonyesha huzuni kuhusu kuuawa kwa kiongozi wa Iran Ali Khamenei.

Raia huyo wa Kuwait, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliongeza kuwa wengi wa waliokamatwa ni waislamu wa Kishia, na hali hiyo imefanya watu wengi kuwa na hofu ya kutoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii.

Wafungwa wasio raia wa Kuwait wamehamishiwa katika vituo maalum vya kuwarejesha nchini kwao baada ya kurejea kwa safari za ndege ambazo zilikuwa zimesitishwa kutokana na vita vya Iran.

Bahrain yawapokonya uraia watu kadhaa

Bahrain pia iliwakamata watu waliokuwa wakichapisha taarifa zinazohatarisha usalama wa taifa katika mitandao ya kijamii.

Shirika la Amnesty International linasema kuwa wengi wa waliokamatwa katika nchi zote mbili wameshtakiwa kwa kutumia haki yao ya uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na mashtaka kama kusambaza "habari za uongo" au matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Mahmoud Shalaby, mtafiti wa kikanda wa shirika hilo Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, aliambia BBC kuwa kuna "wasiwasi mkubwa" kuhusu mchakato wa kesi hizo. "Nchini Bahrain, baadhi ya waliokamatwa wamezuiwa kupata wakili"