Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Iran vilichangiaje kukamatwa mmoja wa wahalifu wakubwa wanaotafutwa Ulaya?
Vita ya Iran haikubadilisha tu mizani ya kikanda katika eneo la Mashariki ya Kati, bali pia ilikuwa na athari nyingine zisizotarajiwa.
Mojawapo ya athari hizo ilitokea katikati ya mwezi Aprili huko Dubai, ambapo Daniel Kinahan, raia wa Ireland ambaye kwa miaka mingi alikuwa akijulikana kama mhusika muhimu katika njama za uhalifu wa kimataifa, alikamatwa.
Mnamo Aprili 2022, serikali ya Marekani iliweka vikwazo dhidi ya mtu huyo, ikimtaja yeye pamoja na baadhi ya wanafamilia wake kama viongozi wa "Kinahan Cartel," mtandao unaodaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa silaha, na mauaji.
Daniel Kinahan anachukuliwa kuwa mmoja wa wahalifu wenye nguvu na ushawishi mkubwa barani Ulaya, kwa mujibu wa Idara ya fedha ya Marekani na mashirika ya usimamizi wa sheria barani Ulaya.
Pia alikuwa na uhusiano na ulimwengu wa michezo kupitia kampuni yake ya usimamizi ambayo sasa imekoma kufanya kazi, iliyofanya kazi na zaidi ya mabondia 100, wakiwemo Tyson Fury na Carl Frampton.
Kukamatwa kwake katika Umoja wa Falme za Kiarabu kulikuja wakati wa kilele cha hatua kali za usalama katika eneo la Mashariki ya Kati, huku kukiwa na wasiwasi kwamba mitandao ya uhalifu ya kimataifa inatumia hali ya kutokuwa na utulivu iliyosababishwa na vita ya Iran.
Tukio hilo linaonyesha jinsi migogoro ya kikanda inavyoweza kuwa na athari zisizotarajiwa, ikiwemo kuathiri usalama wa kimataifa na juhudi za kupambana na uhalifu uliopangwa.
Nicola Tallent, mwandishi wa habari wa uchunguzi anayebobea katika uhalifu uliopangwa, anasema kukamatwa huko ni pigo kubwa kwa familia ya Kinahan na anaona tukio hilo kuwa la muhimu.
"Mamlaka zimewekeza muda na rasilimali nyingi katika kuvunja mtandao wa Kinahan Cartel, na hili ni mafanikio makubwa," aliiambia Idhaa ya Kihispania ya BBC.
"Hata hivyo, huu ni mtandao mkubwa sana, wenye fedha nyingi, na sidhani kwamba kumwondoa mtu mmoja kunaweza kuutokomeza. Kwa maoni yangu, tayari kuna watu walio tayari kuchukua uongozi wa cartel hiyo. Hawatakata tamaa wala kutoweka kwa sababu Daniel amekamatwa."
Polisi wa Ireland walisema katika taarifa kwamba kukamatwa kwa watu hao kunaonyesha umuhimu na "haja ya ushirikiano wa kimataifa wa polisi ili kupambana na mipango ya uhalifu wa kimataifa."
Kukamatwa kwa Kinahan kulitokea baada ya mamlaka za Ireland kutuma faili ya kisheria kwenda UAE, iliyoonyesha tuhuma za uhalifu wake na nafasi yake katika mtandao wa uhalifu wa kimataifa.
Kwa kuzingatia kesi hiyo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Umma Dubai ilitoa hati ya kukamatwa kwa Kinahan ili kuanza mchakato wa kisheria kabla ya kurudishwa (extradition) kwake.
Daniel Kinahan alikamatwa chini ya saa 48 baada ya hati hiyo kutolewa.
Polisi wa Ireland walisema mchakato huo unafanyika ndani ya mfumo wa makubaliano ya pande mbili ya kuwarejesha wahalifu kati ya Ireland na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo ni muhimu sana kwa operesheni za pamoja kama hizi.
Familia ya Kinahan
Historia ya familia ya Kinahan na uhusiano wao na biashara ya dawa za kulevya inaanza katika miaka ya 1980, wakati Christopher Kinahan, baba yake Daniel, alihusika kwa kiasi kikubwa katika biashara hiyo.
Mnamo mwaka 1986, Christopher Kinahan alikamatwa kwa kujihusisha na usafirishaji wa heroini na akahukumiwa kifungo cha miaka sita jela. Hata hivyo, hatimaye alitumikia vifungo vifupi katika nchi za Ireland, Uholanzi, na Ubelgiji.
Hata hivyo, inasemekana kwamba hatua kwa hatua alipanua mtandao wake wa mawasiliano na kuanzisha muundo unaojulikana katika duru za polisi kama "Kundi la Uhalifu uliopangwa la Kinahan" (Kinahan Organized Crime Group).
Kundi hilo lilikuwa likielekeza shughuli zake huko Marbella, kusini mwa Uhispania, hadi mwaka 2010. Daniel na Christopher Jr., wana wa Christopher Kinahan, walituhumiwa kumsaidia baba yao kuendesha mtandao huo wa familia.
Wakati huo, Daniel Kinahan alikuwa tayari mtu anayejulikana sana.
Nicola Tallent, mwandishi wa habari wa uchunguzi ambaye amekuwa akifuatilia familia ya Kinahan kwa miaka mingi, anasema Daniel aliishi Hispania hadi mwaka 2016, ambapo alianzisha kampuni ya uzalishaji wa ndondi iitwayo MGM Boxing na akaanza kujenga taswira ya kuwa mfanyabiashara halali.
Tangu wakati huo, genge la Kinahan limekuwa likijihusisha na uhasama mkali wa umwagaji damu na genge pinzani lijulikanalo kama "Hutch."
"Mojawapo ya matukio makubwa yaliyotokea wakati wa mgogoro huu ni jaribio la mauaji katika Hoteli ya Regency mjini Dublin, ambalo lilisababisha hatua kali kutoka kwa polisi wa Ireland," anasema Bi. Tallent.
Katika shambulio hilo, David Byrne, mmoja wa washirika wa Kinahan, alipigwa risasi na kuuawa huku wengine wawili wakijeruhiwa. Mgogoro kati ya magenge ya Hutch na Kinahan umesababisha takriban watu 18 kupoteza maisha hadi sasa.
Tallent anasema majaribio ya awali ya kuvunja mtandao huo (operesheni ya mwaka 2010 nchini Hispania) yalishindwa kutokana na kasi ndogo ya mfumo wa mahakama na utetezi mkali wa kisheria kwa kundi hilo.
Hata hivyo, baada ya tukio la ufyatuaji risasi katika Hoteli ya Regency mwaka 2016, ushirikiano kati ya mashirika ya polisi barani Ulaya ulibadilika kwa kiasi kikubwa, na Uholanzi pamoja na Ufaransa zikaanza kushirikiana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi zaidi.
Mamlaka za Ireland ziliweza kuvunja sehemu kubwa ya muundo wa ndani wa kundi hilo na kuwafunga gerezani takribani wanachama 70 katika kipindi cha miaka kadhaa kwa makosa kama mauaji na utakatishaji fedha.
Hata hivyo, kumfuatilia Daniel Kinahan ilikuwa zoezi gumu zaidi alipohamia Dubai pamoja na kaka yake mwaka 2016. Baba yao alikuwa tayari ameishi katika jiji hilo hapo awali.
Huko Dubai, Kinahan aliimarisha nafasi yake, akijikita katika duru za biashara na kuwa mtu mwenye ushawishi katika ndondi za kimataifa.
Wakati huohuo, utafiti uliendelea katika nchi mbalimbali.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa waandishi wa habari na vyanzo vya kijasusi vinavyonukuliwa kwenye vyombo vya habari, mtandao wa Kinahan ulikuwa ukidhibiti sehemu ya usafirishaji wa cocaine kutoka Amerika Kusini kuelekea Ulaya.
Idara ya Hazina ya Marekani pia inaelezea kundi hilo kama "shirika la uhalifu."
Nicola Tallent anaeleza kwamba biashara ya dawa za kulevya barani Ulaya ilienea kutoka vituo vya jadi kama Amsterdam, ambayo ilianza kuwa "soko kuu la dawa za kulevya" kutokana na nafasi yake ya kimkakati na mtazamo wake mlegevu, hadi maeneo mengine kama pwani ya kusini ya Hispania, eneo linalojulikana kwa rushwa, ukaribu wake na Morocco na uwepo wa magenge ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Bi. Tallent, katika miaka ya hivi karibuni Dubai imekuwa makazi mapya ya wahusika wa uhalifu uliopangwa; wanavutwa na maisha ya anasa, mkusanyiko wa utajiri na mazingira ambayo, kwa maoni yake, yaliruhusu mtiririko wa fedha haramu kuingia nchini kabla ya hukumu za mahakama za kimataifa kutolewa.
Anasisitiza: "Dubai inazunguka fedha, maisha ya anasa na utajiri usiofikirika, sehemu yake ikiwa ni matokeo ya uhalifu uliopangwa. Hakuna shaka kwamba makundi mengi ya uhalifu yanajihisi salama na tulivu katika jiji hili."
Tahadhari za kikanda kutokana na vita ya Iran
Inaonekana kwamba mazingira ya mvutano wa kikanda kutokana na vita ya Iran na hisia nyeti kuhusu shughuli zinazohusiana na nchi hiyo yamekuwa na athari hasi kwa Daniel Kinahan.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mamlaka za UAE zilianza msako wao baada ya kuibuka kwa uwezekano wa uhusiano kati ya mtandao wa Kinahan na mitandao inayohusishwa na Iran, hasa katika shughuli haramu kama biashara ya mafuta ili kukwepa vikwazo vya Marekani dhidi ya mauzo ya nje ya mafuta ya Iran.
Ripoti ya tovuti ya uandishi wa habari za uchunguzi ya Bellingcat yenye makao yake Uholanzi inaonyesha kwamba baadhi ya watu wanaohusishwa na mtandao huo walihusika katika mitandao ya kusafirisha na kuuza mafuta yaliyo chini ya vikwazo.
Gazeti la Uingereza The Times pia lilinukuu tathmini za kiusalama zikidai kwamba mtandao huo ulikuwa na "mahusiano na huduma za kijasusi za Iran, hasa katika biashara haramu ya mafuta."
Kwa mujibu wa The Times, hali hii iliongeza shinikizo la kidiplomasia kwa UAE na kuifanya mamlaka zake kuchukua hatua.
Katika mazingira haya, inaonekana kwamba hisia nyeti za kikanda zinazohusiana na vita ya Iran na mashambulizi ya Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya nchi za Ghuba ya Uajemi zilichangia kuimarisha ushirikiano wa maafisa wa UAE na Ireland na kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya viongozi wakuu wa kundi hilo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari Nicola Tallent, kukamatwa kwa Kinahan kunakuja ndani ya muktadha mpana unaojumuisha migogoro ya Iran na madai ya uhusiano wa mtandao huo na makundi kama Hezbollah ya Lebanon.
Bi. Tallent anarejea ripoti zinazodai kwamba mtandao huo ulisaidia kufadhili shughuli za makundi hayo kwa kuwezesha usafirishaji na uwekezaji unaohusiana na biashara ya dawa za kulevya, jambo ambalo anasema limeathiri mwelekeo wa kesi hiyo kisiasa.
Kesi ya Kinahan inaonyesha jinsi migogoro ya kimataifa inavyoweza kuongeza shinikizo kwa mitandao ya uhalifu.
Kwa serikali ya Ireland, kukamatwa kwa Daniel Kinahan ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu uliopangwa na mfano wa kuongezeka kwa umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya usalama.