Farhia Elmy: Kutoka ndoto ya udaktari hadi malkia wa bahari

    • Author, Martha Saranga
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

'Nina uwezo wa kukaa chini ya maji baharini kwa saa mpaka mbili", anasema Farhia Elmy, binti mwenye mapenzi na maji, aliyegeuza mapenzi hayo kuwa fursa.

Tena anazama baharini na mavazi ya staha, anavaa hata ushungi ama kitambaa kichwani kama ambavyo angekuwa nchi kavu.

Akiwa na umri wa miaka 26, binti huyu kutoka Tanzania amechagua njia ambayo wengi hawaioni ama wanaiona ni hatari: Sayansi ya bahari. Kwa wengi, bahari ni mandhari ya kupendeza au eneo la kupumzikia. Kwa Farhia, ni mapenzi na maisha, na pia ni dunia yenye siri, hazina, na maswali yasiyoisha.

Farhia ambaye mara zote amejawa tabasamu la utulivu, anaeleza kwa msisitizo, kwamba "Bahari ni kitu cha kipekee sana ambacho watu wengi hawakiangalii.

Imenipa fursa kubwa sana kuwa mdadisi mzuri."

Anasimulia kuwa safari yake ilianza kwa mshangao mdogo lakini wenye athari kubwa. "Kuna siku nilikuwa nasoma nikakutana na sentensi kwamba asilimia 95 ya bahari haijawahi kuangaziwa. Nilihisi kama dunia imenifungulia mlango mpya. Nikatamani kufahamu zaidi."

Hata hivyo, ndoto yake haikuwa ile iliyopangwa na familia yake.

Wazazi wake walitamani awe daktari wa binadamu. "Nilikuwa tayari hata kupelekwa China kusomea udaktari," anakumbuka.

Lakini janga la COVID-19 lilibadilisha mkondo wa maisha yake. Badala ya kusafiri nje ya nchi, alibaki na kuanza kusomea sayansi ya bahari uamuzi ambao leo unaonekana kuwa wa hatima yenye matumaini kwake.

Farhia alisomea sayansi ya bahari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na tangu hapo hajawahi kuangalia nyuma. Leo hii, yeye ni mtaalamu wa uhifadhi wa mazingira ya bahari na mwanzilishi wa kampuni ya Seablue Innovators, inayolenga kuboresha maisha kupitia rasilimali za bahari.

Anatumia muda wake mwingi baharini, tena chini ya maji, akitafiti, akilima, akivinjari na shughuli nyingine muhimu za chini ya bahari.

"Chini ya bahari ni kuzuri sana. Ukienda, stress zote zinakwisha," anasema kwa furaha. "Ni tiba. Kuogelea hadi chini ya bahari si tu mazoezi ya mwili, bali pia ya akili. Mara nyingi nabana pumzi hilo lenyewe ni zoezi la akili."

Chini ya bahari wakati mwingine hutumia mtungi wa gesi hasa kama anakaa muda mrefu, wakati mwingine hatumii. Siri kubwa ni mazoezi, dhamira na kuondoa uoga.

Tofauti na simulizi za kale kuhusu viumbe wa ajabu, Farhia anabaki kuwa mkweli wa kisayansi. "Stori kuhusu majini sijawahi kuona wala siamini. Bahari ni dunia nyingine kabisa, lakini ya kweli, yenye uhalisia wake."

Niliwahi kushushwa kwenye boti kisa tu mwanamke

Lakini safari yake haikukosa changamoto. Katika jamii ambayo haijaizoea taaluma yake, alijikuta akipambana kuthibitisha uwezo wake hasa kama mwanamke.

Kuna wakati anatumia boti za watu kawaida kuzamia majini kufanya shughuli zake ambazo, pia zina mchango mkubwa sana kwenye kuboresha mazingira. Wakati anaaza kwenda baharini kutengeneza fursa kwa kuzamia chini alikuwa akikutana na changamoto:

"Nimewahi kufukuzwa na wavuvi nisipande mashua yao," anasema bila kusita. "Haikuwa rahisi wanaume kunielewa. Waliona kama si sehemu yangu." Lakini hakukata tamaa.

Aliomba msaada kwa mamlaka, akatambulishwa rasmi, na polepole akaanza kupata ushirikiano.

Hata familia yake ilihitaji muda kuelewa. "Kila nikimuaga mama yangu kuwa ninaenda chini ya maji, huogopa sana na kunifanyia dua," anasema kwa upole. Lakini mambo yalibadilika. "Baba ananiamini sana sasa. Anajivunia mimi, na hiyo inanipa nguvu ya kuendelea."

Katika jamii pana, Farhia anaonekana kama mtu wa kipekee. Wapo wanaoshangaa, na wapo wanaopongeza. "Marafiki zangu wengine wananishangaa, lakini wengi pia wananipa moyo kupitia mitandao ya kijamii," anaeleza.

"Ninajivunia kutambulika,"

Licha ya vikwazo, mafanikio yake yanaonekana wazi. Wazazi wangu walionekana kukataa mapenzi yangu kwenye baharini. Na hata jamii waliona kama baharini ni kazi isiyostahili wanawake tena binti mdogo kama yeye.

Lakini sasa ana kiwanda kidogo kigamboni Dar es salaam, kinachozalisha mazao ya baharini na kimeweza kutoa ajira kwa vijana na wanawake, hasa katika shughuli kama upandaji wa matumbawe na uzalishaji wa bidhaa za mwani katika eneo la Kigamboni.

Hii si tu biashara ni harakati ya kijamii.

"Ninajivunia kutambulika," anasema kwa msisitizo. "Nimetamani siku zote kuwa muhamasishaji wa mambo ya bahari."

Juhudi zake pia zimemtambulisha kimataifa. Amepokea tuzo mbalimbali, ikiwemo tuzo ya wanawake katika sayansi, pamoja na tuzo ya ubunifu unaotoa ajira kwa jamii kupitia miradi yake ya kuwawezesha wanawake wakulima na vijana visiwani.

Hata hivyo, bado anakumbana na mitazamo hasi. "Mara nyingi mwanamke anaonekana kama kiumbe very delicate," anasema.

"Hadi leo, mara nyingi najikuta mimi peke yangu mwanamke kwenye boti. Lakini hainiogopeshi."

'Ninatamani kuwa muongoza watalii baharini'

Anapoulizwa anajiona wapi katika miaka mitano ijayo, Farhia alijibu kwa matumaini kwamba anatamani kuwa muongoza watalii binafsi haswa baharini.

" Pia nataka kuzalisha video nyingi zitakazoonyesha maisha ya chini ya maji, kuwaelimisha watu kuhusu mambo ambayo bado hawajayafahamu."

Kwa Farhia, bahari si tu taaluma ni wito.

Ni nafasi ya kugundua yasiyojulikana, kuhamasisha jamii, na kubadilisha maisha. Katika kina chake, amepata si tu kazi, bali kusudi la maisha.

Farhia anasema kupitia sauti yake, dunia itaanza kuiona bahari si kama ukingo wa ardhi bali kama mwanzo wa maarifa mapya.