Wasanii wa Afrika Mashariki wanavyoishi katikati ya vita ya Marekani na Iran

s

Chanzo cha picha, Dogo Skills

    • Author, Na Ahmad Haji
    • Akiripoti kutoka, BBC Swahili - Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika kipindi hiki ambacho dunia imejaa tahadhari za kikanda na changamoto mbalimbali za kiusalama, wengi hujiuliza kuhusu hali ya maisha ya wasanii wa sekta ya ubunifu na wanamuziki kutoka Afrika Mashariki wanaoishi katika maeneo ya Mashariki ya Kati, maeneo ya Iran, israel, Lebanon, Kuwait, Oman, Yemen na hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na jiji la Dubai, ambao wasanii wengi wanakwenda huko.

Dubai imejijengea sifa kama kitovu kikuu cha burudani, utalii, muziki, ubunifu na biashara, huku ikiwa na uhusiano mkubwa na ukanda wa Afrika Mashariki. Kuna wasanii, mapromota na mashabiki wengi kutoka Afrika Mashariki wanaoishi na kufanya shughuli zao jijini humo.

Wanamuziki wengi wa Afrika Mashariki hupenda kufanya matamasha Dubai kwa lengo la kupata malipo mazuri pamoja na kutumia jukwaa hilo kuwafikia mashabiki wa kimataifa.

Lakini katika nyakati hizi za hofu kutokana na mvutano wa Marekani na Iran, maisha ya wasanii hao yakoje? Je, wanaendelea na kazi zao kama kawaida au matamasha yamepungua kutokana na tahadhari za kiusalama?

s

Chanzo cha picha, Dogo Skills

Maelezo ya picha, Gabriel Mumbo maarufu kama Dogo Skills

Gabriel Mumbo maarufu kama Dogo Skills ni mwanamuziki wa kizazi kipya na mjasiriamali kutoka Kenya aliyewahi kutamba na vibao kama Nakupenda na Nana. Aliamua kuhama Kenya na kuichagua Dubai kama makazi yake mapya ili kutafuta fursa zaidi katika muziki na biashara.

Akizungumzia hali ilivyokuwa mwanzoni mwa mvutano huo wa Marekani na Iran, Dogo Skills anasema kuwa wao pia waliingiwa na hofu kufuatia tahadhari za kiusalama na kusimamishwa kwa baadhi ya safari za ndege.

"Kwa msanii, mjasiriamali na mkaazi wa Dubai, ninaiona UAE kama moja ya maeneo yenye uthabiti mkubwa duniani. Licha ya changamoto za kikanda, maisha yanaendelea kwa utulivu, usalama na mpangilio wa hali ya juu," anasema.

Anaongeza kuwa:

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Watu wanaendelea kufanya kazi, biashara zinaendelea kukua, matukio yanaendelea kufanyika na jamii ya kimataifa inaendelea kuishi pamoja kwa mshikamano mkubwa. Hilo ndilo lililonifanya niamini kuwa Dubai si sehemu ya kuishi tu, bali ni sehemu ya kujenga ndoto na kupeleka vipaji kwenye kiwango cha dunia."

Mwezi uliopita, wakati mvutano wa Marekani na Iran ulipokuwa umeongezeka, tahadhari za kiusalama pamoja na vikwazo vya usafiri vilisababisha kusimamishwa kwa safari kadhaa za ndege kuelekea Dubai. Hali hiyo iliathiri sekta ya burudani kwa muda, huku baadhi ya matamasha yakiahirishwa.

Hata hivyo, baada ya hali kutulia na safari za ndege kurejea, shughuli za burudani zilianza kushika kasi tena, zikihusiaha wasanii, watayarishaji wa muziki, waandaaji wa filamu pamoja na wajasiriamali kutoka Afrika, Ulaya, Asia na Marekani.

Dogo Skills anasema baada ya hali kutulia aliandaa tamasha la mwanamuziki maarufu Mkenya, Bien, anayefanya vizuri kupitia wimbo wake Finally aliomshirikisha Ali Kiba wa Tanzania. Tamasha hilo lilihudhuriwa na maelfu ya mashabiki.

Mwanamuziki huyu anaibeba vita kwa namna ya kipekee akiendelea kusaidia vijana wasiojiweza wa Afrika.

"Naamini mafanikio ya kweli hayapimwi kwa pesa pekee, bali kwa athari unayoiacha katika maisha ya wengine. Kupitia miradi ya kijamii na ushirikiano mbalimbali, ninaendelea kujenga daraja kati ya Afrika, UAE na Dubai," anasema.

Muziki unapigwa, wasanii wanakuja kubnurudisha na yeye na wengine licha ya hofu iliyoko, wamechagua kuendelea na maisha Mashariki ya kati.

Muziki unaendelea, maisha yanaendelea pia, na ndivyo wanavyoishi wasanii huko, burudani vitani.

Wasanii wa Tanzania wanapendwa Mashariki ya Kati

Diamond Platnumz

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Diamond Platnumz

Kwa mujibu wa Dogo Skills, muziki unaopendwa zaidi na mashabiki wanaohudhuria matamasha Mashariki ya Kati hasa Dubai kwa sasa ni Bongo Flava kutoka Tanzania.

Muziki wao 'unasahulisha' vita na kinachoendelea Mashariki ya Kati. Watu wanasikiliza nyimbo na kufuatilia licha ya ukanda huo kuwa na mgogoro. Anasema wasanii wa Tanzania wanapendwa sana kutokana na uhalisia wa muziki wao na uwezo wao wa kuwavutia mashabiki kutoka mataifa mbalimbali.

Anamtaja mwanamuziki Diamond Platnumz kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wengi jijini Dubai, huku akisema pia kuwa Bien kutoka Kenya anaendelea kupata mapenzi makubwa kutoka kwa mashabiki.

Licha ya hofu iliyotokana na mvutano huo wa kisiasa, Dogo Skills anasema hana mpango wa kurejea kuishi Kenya kwa sasa. Anaamini Dubai bado ni sehemu muhimu ya kutimiza ndoto zake kupitia muziki na ujasiriamali.

"Lengo langu ni kutumia muziki na biashara kuonyesha kuwa Afrika ina vipaji vikubwa vinavyoweza kushindana katika soko la dunia, huku Dubai ikiwa moja ya njia muhimu kuelekea mafanikio hayo," anasema.

Pamoja na changamoto za kisiasa zinazojitokeza katika ukanda huo, Dubai inaendelea kubaki kuwa moja ya vituo muhimu duniani kwa wanamuziki na wajasiriamali kutoka Afrika Mashariki kutokana na uwezo wake wa kuunganisha vipaji vya Afrika na mashabiki wa kimataifa.