Matukio 8 yaliyoipa Arsenal ubingwa wa EPL msimu huu

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sam Drury
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Baada ya miaka 22 ya kusubiri, hatimaye Arsenal wamerejea rasmi kileleni mwa soka la England kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2025/26.
Kikosi cha Mikel Arteta kilifanikiwa kuhimili ushindani mkali kutoka kwa Manchester City na kufuta maumivu ya misimu mitatu mfululizo ya kumaliza nafasi ya pili nyuma ya mabingwa hao wa zamani pamoja na Liverpool.
Katika safari hiyo ya kihistoria, kulikuwa na matukio kadhaa muhimu yaliyoibeba Arsenal kuelekea ubingwa huo mkubwa. Haya manane yalibadili kabisa mwelekeo wa mbio za EPL msimu huu:
Usajili mkubwa na kikosi kipana cha Arsenal

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya kuona Liverpool wakitwaa ubingwa msimu uliopita kwa kutumia kikosi kipana chenye ubora mkubwa, Arsenal waliamua kufanya maboresho makubwa ya kikosi chao katika dirisha la usajili.
Kwa ujumla, Arsenal waliongeza wachezaji wanane wapya huku Thomas Partey akiwa mmoja wa majina machache yaliyoondoka ndani ya kikosi cha kwanza.
Usajili mkubwa zaidi ulikuwa wa mshambuliaji wa Sweden Viktor Gyokeres aliyesajiliwa kutoka Sporting CP kwa pauni milioni 64, jambo lililowapa mashabiki mshambuliaji namba tisa ambaye walikuwa wakimhitaji kwa muda mrefu.
Mbali na Gyokeres, Martin Zubimendi aliongeza ubora mkubwa katikati ya uwanja, huku Piero Hincapie akiimarisha safu ya ulinzi. Noni Madueke na Eberechi Eze pia waliongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji.
Arsenal walitumia zaidi ya pauni milioni 250 kufanya maboresho hayo, na kadri msimu ulivyokuwa ukiendelea, umuhimu wa usajili huo ulizidi kuonekana wazi.
Goli la Martinelli dhidi ya Manchester City

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika moja ya mechi muhimu mapema msimu huu, Arsenal walinusurika kupata kipigo dhidi ya Manchester City kupitia bao la kusawazisha la Gabriel Martinelli dakika ya 93.
Wakati huo ilikuwa ni mechi ya tano ya msimu, lakini bao hilo lilikuja kuwa moja ya matokeo muhimu yaliyoamua mbio za ubingwa mwishoni mwa msimu.
Manchester City walikuwa wamepata bao la mapema kupitia Erling Haaland na walionekana kuwa karibu kushinda mechi hiyo muhimu dhidi ya wapinzani wao katika mbio za ubingwa.
Pep Guardiola hata alibadilisha mfumo wa mchezo na kuongeza mabeki wengi ili kulinda ushindi huo, akiamini Arsenal wasingeweza kupata nafasi ya kurudi mchezoni.
Hata hivyo, nguvu ya kikosi kipana cha Arsenal ilionekana mwishoni mwa mchezo ambapo Eberechi Eze na Martinelli walionana vizuri na kuipa Arsenal bao muhimu la kusawazisha.
Bao la Gabriel dhidi ya Newcastle dakika za 'jioni'

Chanzo cha picha, Getty Images
Wiki moja baadaye, Arsenal walionyesha tena moyo wa kupambana walipocheza ugenini dhidi ya Newcastle katika Uwanja wa St James' Park.
Kabala ya mchezo huo, Arsenal walikuwa wamepoteza mechi tatu mfululizo kwenye uwanja huo bila hata kufunga bao.
Mambo yalizidi kuwa magumu baada ya Newcastle kupata bao la kuongoza kipindi cha kwanza katika mchezo uliokuwa na presha kubwa.
Arsenal pia walinyimwa penalti baada ya VAR kubadilisha maamuzi ya awali ya mwamuzi, hali iliyowaacha mashabiki wengi wakihofia kupoteza mchezo huo.
Lakini dakika za mwisho zilibadili kila kitu. Mikel Merino aliisawazishia Arsenal dakika ya 84 kabla ya Gabriel kufunga bao la ushindi dakika ya 96 na kupeleka shangwe kubwa kwa mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi.
Baada ya Liverpool kupoteza alama siku moja kabla, ushindi huo uliifanya Arsenal kusogea karibu zaidi na kileleni mwa msimamo. Ulikuwa ushindi muhimu
Hat-trick ya Eze dhidi ya Tottenham
Miezi miwili baadaye, Arsenal walikuwa kwenye kiwango bora kabisa baada ya kushinda mechi 10 mfululizo katika michuano yote.
Katika dabi muhimu ya London Kaskazini dhidi ya Tottenham, Arsenal waliingia uwanjani wakijua ushindi ungewafanya waongoze kwa alama sita kileleni baada ya Manchester City kufungwa na Newcastle.
Arsenal walitawala mchezo huo tangu mwanzo na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0 kabla ya kuongeza bao la tatu mapema kipindi cha pili.
Ingawa Tottenham walipata bao moja kupitia Richarlison, Arsenal walitawalahuku Eberechi Eze akitimiza 'hat-trick' yake ya kwanza akiwa na timu ya wakubwa.
Hat-trick hiyo ilimfanya Eze kuwa mmoja wa mastaa muhimu zaidi wa Arsenal msimu huu na ushindi huo uliwaongezea imani kubwa ya kutwaa ubingwa.
Manchester City kuanza mwaka 2026 vibaya
Wakati Arsenal wakizidi kuimarika, Manchester City wao walipoteza mwelekeo mwanzoni mwa mwaka 2026.
Baada ya kurejea kwenye mbio za ubingwa kipindi cha Krismasi, kikosi cha Pep Guardiola kilishindwa kushinda mechi zake nne za kwanza za ligi mwaka mpya.
Walitoa sare dhidi ya Sunderland kabla ya kupoteza alama nyingine dhidi ya Chelsea na Brighton.
Matokeo hayo yaliipa Arsenal nafasi ya kujenga tofauti ya alama saba kileleni mwa msimamo licha ya wao pia kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya mechi.
Gabriel kunusurika kadi nyekundu dhidi ya Haaland
Mwezi Aprili, Arsenal walikabiliana tena na Manchester City katika mchezo mkubwa uliokuwa na presha kubwa kwenye mbio za ubingwa.
City walishinda mchezo huo kwa bao la Erling Haaland, lakini moja ya matukio yaliyojadiliwa zaidi lilikuwa lile la Gabriel na Haaland kutunishiana misuli uwanjani.
Mabeki hao walikutana uso kwa uso kabla Gabriel hajaonekana kumpiga kichwa Haaland.
Wengi waliamini Gabriel alipaswa kupewa kadi nyekundu kwa tukio hilo, lakini Haaland kutoanguka baada ya kuguswa kichwa na Gabriel kulimsaidia beki huyo kunusurika adhabu.
Kama Gabriel angelamwa kadi nyekundu, angekosekana katika mechi kadhaa muhimu za Arsenal za mwisho wa msimu.
Kosa la Guehi dhidi ya Everton liliipeleka 'wodini' Manchester City

Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester City walipoteza alama muhimu sana walipolazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Everton.
City walikuwa mbele katika mchezo huo na walionekana kuwa njiani kuelekea kupata ushindi muhimu kabla makosa ya safu yao ya ulinzi hayajabadilisha mchezo.
Marc Guehi alipiga pasi mbaya ndani ya eneo la hatari na Everton wakatumia nafasi hiyo kusawazisha kabla ya kufunga mabao mengine mawili kwa muda mfupi.
Ingawa City walifanikiwa kusawazisha dakika za mwisho na kupata alama moja, kosa la mlinzi huyo yalisababisha matokeo yaliyoipa Arsenal faida kubwa zaidi katika mbio za ubingwa.
Mechi hii ni kama iliwarudisha 'wodini' Man City, katika mbio za ubingwa. Ingawa walirejea na kupata ushindi dhidi ya Crystal Palace na Brentford, sare na Bournemouth ikahitimisha safari yao.
Uhodari wa Raya na VAR dhidi ya West Ham
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika moja ya mechi ngumu zaidi za mwisho wa msimu, Arsenal walipata ushindi muhimu dhidi ya West Ham uliokuja kwa presha kubwa.
Mchezo huo ulikuwa mgumu huku West Ham wakitengeneza nafasi nyingi za kusawazisha.
Kipa wa Arsenal David Raya aliokoa hatari kubwa sana baada ya kuzuia shuti la karibu la Matheus Fernandes katika dakika muhimu za mchezo.
Dakika chache baadaye, Leandro Trossard aliifungia Arsenal bao la kuongoza lililoonekana kuwa la ushindi.
Hata hivyo, West Ham walidhani wamesawazisha dakika za majeruhi kupitia Callum Wilson kabla ya Video Assistant Referee (VAR), teknolojia ya video inayosaidia uamuzi wa uwanjan, kuingilia kati na kulifuta bao hilo kwa madai ya Raya kuchezewa faulo.
Maamuzi hayo yaliwakasirisha West Ham pamoja na mashabiki wa Manchester City, lakini Arsenal walifanikiwa kulinda ushindi huo muhimu hadi mwisho.
Hatimaye, matukio haya yanaipa ubingwa Arsenal baada ya miaka 22 ya kusubiri. Arsenal wameandika historia mpya chini ya Mikel Arteta na kurejea tena kileleni mwa soka la England. Wanasubiri kucheza fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya PSG Mei 30, 2026.












