Kutoka kukimbia ndoa ya utotoni na 'mzee' hadi kuwa mke wa rais

Fatima Bio
    • Author, Megha Mohan, Maggie Latham and Alvaro Alvarez
    • Nafasi, BBC World Service
    • Akiripoti kutoka, Freetown
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Ilimchukua Fatima Bio muda mfupi tu kujibu tulipomuuliza ilikuwaje alikuwa mtafuta hifadhi mjini London.

"Bora kuliko kuolewa na mzee mpotovu," alisema kwa sauti tulivu kabla ya kucheka akirejelea mpango wa baba yake wa kumuoza akiwa binti mdogo.

Mambo mengi yamebadilika tangu wakati huo. Katika miaka iliyofuata, alikuja kuwa muigizaji, kisha akakutana na mwanaume mmoja London alipokuwa akimhoji kuhusu Wasierra Leone wenye ushawishi wanaoishi ughaibuni, na baadaye wakafunga ndoa. Mwanaume huyo alikuwa Julius Bio, ambaye sasa ni rais wa Sierra Leone.

Kama mke wa rais, Fatima Bio anaonekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa lakini pia mwenye utata.

Baadhi ya vijana wanamuona kama sauti mpya katika siasa anayewatetea wanawake na wasichana, huku wengine wakisema ameenda mbali zaidi ya wajibu wake na kwamba anazungumza sana na kujihusisha mno katika uendeshaji wa chama cha mume wake.

Amewahi kuzomewa na wabunge na kukosolewa kutokana na video aliyowahi kushiriki kwenye mitandao yake ya kijamii iliyomhusisha mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya, ambaye anasema hamfahamu.

Haraka aliacha kucheka na kujituliza ili kusimulia hadithi iliyomsukuma kupigania sheria ya kupiga marufuku ndoa za utotoni nchini Sierra Leone, iliyoanza kutumika mwaka 2024.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yeye mwenyewe alikuwa karibu kuwa bibi harusi wa utotoni. Kufikia alipofikisha miaka 13, baba yake, mchimbaji wa almasi kutoka wilaya ya Kano, alikuwa tayari amepanga aolewe na mwanaume mwenye umri wa zaidi ya miaka 30 ambaye alikuwa akimfahamu kama baba tangu akiwa mtoto mdogo.

"Hakukuwa na mjadala. Ilikuwa tayari imeamuliwa," alisema.

Lakini muda mfupi kabla ya harusi, alipofikisha miaka 16 mwaka 1996, vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sierra Leone vilisababisha vurugu zilizompa nafasi ya kutoroka kwa msaada wa ndugu zake na kuomba hifadhi nchini Uingereza.

Fatima Bio aliwasili London usiku wa Krismasi katika Uwanja wa Ndege wa Gatwick akiwa amevaa fulana tu, anasema, akiwa ameshtushwa na baridi kali lakini mwenye furaha kwa kupata nafasi ya kuanza maisha mapya. Alihamia kuishi kwa ndugu wa mbali.

"Uingereza ilikuwa neema yangu kubwa. Nilipokwenda England, nilipata sauti yangu," alisema mke huyo wa rais. "Nilipata uhuru wangu, na ndipo nikaweza kujitetea mwenyewe. Na sasa ninaweza kupigania vijana wengi iwezekanavyo."

Kitu kingine alichopata nchini Uingereza ni nyumba ya makazi ya serikali huko Southwark katikati mwa London, nyumba ambayo bado anayo hadi leo na ambayo watoto wake wanaishi humo.

Kwa kuwa ni aina ya makazi ya kijamii, nyumba za serikali kwa kawaida huwa na kodi nafuu kuliko nyumba za binafsi, na waombaji wanapaswa kutimiza vigezo fulani ili kuzipata.

Wanawake saba kwenye picha ya pamoja katika chumba cha kifahari chenye michoro iliyowekwa kwenye fremu za dhahabu.: Sophie, Duchess of Edinburgh wa Uingereza, Malkia Mathilde wa Ubelgiji, Malkia Camilla wa Uingereza,Malkia Rania wa Jordan, Mary, Binti mfalme wa Denmark, Fatima Bio, na mke wa rais wa Ukraine Olena Zelenska.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake saba kwenye picha ya pamoja katika chumba cha kifahari chenye michoro iliyowekwa kwenye fremu za dhahabu.: Sophie, Duchess of Edinburgh wa Uingereza, Malkia Mathilde wa Ubelgiji, Malkia Camilla wa Uingereza,Malkia Rania wa Jordan, Mary, Binti mfalme wa Denmark, Fatima Bio, na mke wa rais wa Ukraine Olena Zelenska.

Ukweli kwamba mke wa rais anayehudumu madarakani, ambaye anaishi katika ikulu ya rais katika mji mkuu wa Freetown, bado anaendelea kumiliki nyumba ya makazi ya serikali umeibua ukosoaji katika vyombo vya habari vya Uingereza na Sierra Leone.

Kwa kuwa zaidi ya watu 18,000 wako kwenye orodha ya kusubiri makazi katika eneo hilo, tovuti ya halmashauri hiyo inaeleza kwamba "hata watu wenye mahitaji makubwa zaidi wanaweza kusubiri kwa miaka kadhaa."

Lakini hali hiyo anaendelea kuitetea.

"Watoto wangu wote ni raia wa Uingereza," alisema Fatima Bio. "Ninalipia mwenyewe nyumba yangu. Sijafanya kosa lolote."

Katika taarifa yake, Halmashauri ya Southwark iliiambia BBC kwamba haitoi maoni kuhusu upangaji wa nyumba za watu binafsi, lakini "ikiwa kuna shaka kuwa wapangaji hawatimizi wajibu wao chini ya mkataba wa upangaji, tunafanya ukaguzi na uchunguzi wa mara kwa mara kubaini kama masharti hayo yanazingatiwa."

Tulikuwa katika shamba la familia hiyo, takriban saa moja kwa gari kutoka Ikulu ya Rais mjini Freetown, ambako kwa kawaida huishi na mume wake.

Julius Bio, ambaye ni mwanajeshi wa zamani, alikua rais mwaka 2018 na kuchaguliwa tena mwaka 2023.

 Bio
Maelezo ya picha,

Hapa shambani, Fatima Bio anaonekana kuwa huru zaidi kuliko katika shughuli rasmi tulizokuwa tumemfuatilia hapo awali. Akiwa amevaa jeans na jezi ya mpira wa miguu ya Arsenal F.C., alitupeleka kutembea kuangalia wanyama wake wengi, wakiwemo kuku, ng'ombe na mbuzi.

Ni taswira hii ya ukaribu na watu pamoja na matumaini, sura mpya kwa Sierra Leone, ambako simulizi za kimataifa kwa muda mrefu zimejikita katika wanajeshi watoto, utawala wa kikoloni wa Uingereza na almasi za damu, iliyomfanya kupata mamilioni ya watu wanaomfuatilia kwenye mitandao ya kijamii. Huchapisha mara kwa mara, mara nyingi akicheza na kuwasiliana moja kwa moja na wafuasi wake.

Anazungumzia pia mada ambazo mara nyingi huonekana kuwa mwiko kama umasikini wa hedhi. Sierra Leone haina sera ya kitaifa inayohakikisha upatikanaji wa taulo za kike bure mashuleni, tofauti na Kenya, Botswana, Afrika Kusini na Zambia.

Makundi mbalimbali, yakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, yamesema kuwa wasichana nchini Sierra Leone mara nyingi hukosa shule wanapokuwa kwenye hedhi kwa hofu ya kuchafua sare zao.

"Wasichana walikuwa wanakosa takribani siku 80 za shule kila mwaka kutokana na hedhi," alisema Bio. "Ukikosa siku 80 za mwaka wa shule, ni karibu sawa na kukosa muhula mzima. Bado hawapati usawa wanaostahili. Ndiyo maana mimi hutembelea maeneo mbalimbali kugawa taulo za kike bure. Nataka wasichana wapate elimu ili waweze kuwa mezani wakifanya maamuzi yao wenyewe."

Ingawa hatua hizi zimemletea wafuasi wengi, na hata kuchaguliwa kuwa mkuu wa Organization of African First Ladies for Development, watu wengi wanaamini kuwa anavuka mipaka ya nafasi ambayo kwa kawaida huonekana kuwa ya kiitifaki zaidi.

 Julius Bio

Chanzo cha picha, JOHN WESSELS/AFP via Getty Images

Maelezo ya picha,

Fatima Bio ni mwanachama hai wa chama tawala cha Sierra Leone People's Party, na huwatetea waziwazi wanasiasa anaowaunga mkono. Pia huzungumza katika mikutano ya kampeni hata pale ambapo mume wake hayupo. Aidha, amewahi kutoa taarifa za video kupitia mitandao yake ya kijamii akiwapinga wanasiasa, wakiwemo wale wa chama chake mwenyewe, pamoja na Spika wa Bunge.

Wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge tarehe 7 Agosti 2025, Fatima Bio alizomewa na baadhi ya wabunge. Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa waliimba wimbo wa kumdhalilisha uliowahusu wafanyakazi wa ngono. Yeye alijibu kwa kuvaa earphones zake na kusikiliza muziki.

Mke huyo wa rais anasisitiza kuwa kuzomewa huko hakukumuumiza.

"Inaonesha tu kwamba si wanaume wote wameelimika," alisema. "Si wanaume wote wanaoamini katika kuwawezesha wanawake na usawa wa wanawake."

"Nimekuwa mwanaharakati kwa muda mrefu sana kiasi kwamba siwezi kuwa mke wa kupanga ratiba tu," alisema, akimaanisha kuwa anafanya zaidi ya kuandaa shughuli za familia.

"Ninawasikiliza wananchi na kupeleka mawazo yao serikalini. Ninaisikiliza serikali na kupeleka ujumbe wake kwa wananchi. Hivyo ndivyo tunavyofanya kazi."

 Fatima Bio anasema amepigania elimu ya wasichana “ili waweze kuwa mezani wakifanya maamuzi yao wenyewe.”
Maelezo ya picha, Fatima Bio anasema amepigania elimu ya wasichana "ili waweze kuwa mezani wakifanya maamuzi yao wenyewe."

Katika siku tulizotumia pamoja naye, Fatima Bio alisema anataka kubadilisha taswira ya nchi yake.

Tulipohudhuria sherehe ya mahafali katika Choithram International School, shule ya kisasa iliyopakwa rangi mpya ambapo alikuwa mzungumzaji mkuu, wasichana walikuwa wakisimama kuzungumza naye walipokuwa wakipokea vyeti vyao.

Alisisitiza kuwa shule ya kwanza ya sekondari ya wasichana katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ilijengwa nchini humo, na akaielezea Sierra Leone kama taifa lenye uvumilivu wa kidini.

Kama asilimia 77 ya watu wa Sierra Leone, Bio ni Muislamu. Hata hivyo, mume wake Julius Bio ni miongoni mwa asilimia 21 ya Wakristo nchini humo. Alituambia kuwa wao wawili huhudhuria ibada za msikitini na kanisani.

Ilikuwa baada ya ibada ya kanisani ndipo alipokosolewa vikali zaidi.

Mnamo Januari 2025, shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa Jos Leijdekkers, anayejulikana pia kama "Chubby Jos", mmoja wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaotafutwa zaidi Ulaya, alionekana katika video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya Fatima Bio.

Video hiyo inadaiwa kumuonesha Leijdekkers mwenye umri wa miaka 34 akiwa amesimama mistari michache nyuma ya mke wa rais na rais wakati wa ibada hiyo ya kanisani.

Leijdekkers amehukumiwa kifungo cha miaka 24 jela na mahakama ya Rotterdam akiwa hayupo mahakamani, kwa kosa la kusafirisha kokeini kwenda Uholanzi.

Mataifa ya Afrika Magharibi mara nyingi hutumika kama njia ya kusafirisha dawa za kulevya kutoka Amerika Kusini kwenda Ulaya.

BBC haijaweza kuthibitisha video hiyo kwa uhuru, na sasa imefutwa.

Alipoulizwa na BBC jinsi mmoja wa wafalme wa biashara ya dawa za kulevya wanaotafutwa zaidi Ulaya aliweza kuwa karibu na familia ya kwanza ya Sierra Leone, Fatima Bio alikana kumfahamu.

"Siwezi kujua kwa sababu mimi si mhalifu," alisema Fatima Bio. "Mimi sileti watu kanisani. Mimi si Mkristo. Mimi ni Muislamu. Kwa hiyo sijui nani alikuwa ndani ya kanisa hilo. Huzungumzi kuhusu jambo usilolijua."

Pia alikanusha uvumi kwamba Jos Leijdekkers anadaiwa kuwa na mtoto na binti wa kambo wa Fatima Bio, ambaye ni binti wa rais kutoka uhusiano wa awali.

"Huo wote ni uongo ambao sitaki kuuthibitisha kwa kuujadili," alisema.

Wachambuzi wanasema kuwa watu wengi nchini Sierra Leone wanajali zaidi mapambano ya kila siku ya kujikimu kuliko kumfikiria Leijdekkers.

Tangu wanajiolojia wa Uingereza walipoanza kuchimba almasi katika miaka ya 1930, utajiri wa madini wa nchi hiyo haujawanufaisha sana wananchi wa kawaida.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kikatili vilivyodumu kuanzia mwaka 1991 hadi 2002, vilivyochochewa kwa sehemu na biashara ya almasi na kuungwa mkono na vikosi vya Charles Taylor kutoka Liberia, viliua makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni wengine kukimbia makazi yao.

Juhudi za kuijenga upya nchi hiyo zimekuwa zikikwamishwa mara kwa mara na mlipuko wa Ebola wa mwaka 2014, janga la Covid-19, pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta na chakula baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Mwaka 2022, maandamano kuhusu gharama ya maisha yalizuka mjini Freetown na takribani raia 20 pamoja na polisi sita waliuawa.

 Masuala ya kimataifa yamechangia mfumuko wa bei na kuongezeka kwa gharama za maisha.

Chanzo cha picha, SAIDU BAH/AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Masuala ya kimataifa yamechangia mfumuko wa bei na kuongezeka kwa gharama za maisha.

Katika mazingira hayo, ambapo changamoto za kila siku za kiuchumi ndizo zinazotawala mawazo ya wananchi, ukosoaji mwingine kuhusu utajiri wa mke wa rais umejitokeza, ukiwemo kuhusu mali kadhaa anazodaiwa kumiliki.

Fatima Bio alikataa kueleza kwa undani alipoulizwa kama familia yake inaishi katika majumba makubwa nchini Gambia, na jinsi yalivyolipiwa.

"Sihitaji kukanusha. Sihitaji kukubali. Wakileta ushahidi kwamba wanachosema ni kweli, ndipo tutakapozungumza," alisema.

Ni hali hii ya kujiamini iliyowafanya wachambuzi wengi wa siasa nchini Sierra Leone na kwingineko kujiuliza kama Bio anaandaa mazingira ya kuwania urais siku moja, huenda baada ya muhula wa mume wake kuisha mwaka 2028, kwani hastahili kugombea tena.

Mume wake, Julius Bio, naye amekumbwa na mijadala mbalimbali, ikiwemo ukosoaji kuhusu namna alivyosimamia uchumi na maswali kuhusu uwazi wa uchaguzi wa mwaka 2023. Tume ya uchaguzi ilisisitiza kuwa kulikuwa na mifumo iliyowekwa kuhakikisha uchaguzi wa haki.

"Sina tamaa ya kuwa rais," alisema Fatima Bio. "Itabidi iwe mapenzi ya Mungu. Mimi ni muumini mkubwa sana kwamba Mungu anapotaka jambo, hulifanya… Ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, hakuna mwanadamu anayeweza kulizuia."

Graphic with Global Women written in white on a purple background, with blueish-purple arcs taken from concentrically arranged circles on the right.