J-10C Fighters: Nini kinazifanya ndege hizi za kivita kuwa hatari zaidi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Anga la China limeendelea kuonyesha nguvu zake kupitia ndege za kisasa aina ya J-10C, ambazo zimekuwa sehemu muhimu ya mazoezi makubwa ya kijeshi yanayofanyika katika mazingira yanayofanana na vita halisi.
Katika mazoezi hayo, ndege hizo zimekuwa zikifanya mashambulizi ya anga, kuruka kwa kasi katika vikosi vya pamoja pamoja na kushirikiana na mifumo mingine ya kijeshi ya China.
Mazoezi hayo yamelenga kupima uwezo wa marubani kufanya maamuzi ya haraka vitani, kutumia teknolojia za kisasa za rada pamoja na kushambulia malengo ya mbali kabla ya kuonekana na adui. Wachambuzi wa kijeshi wanaeleza kuwa uwezo huo ndio unaozifanya ndege hizo kupewa heshima kubwa ndani na nje ya Asia.
Katika miaka ya karibuni, China imewekeza nguvu kubwa katika utengenezaji wa ndege za kivita za kisasa ili kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje. J-10C imekuwa moja ya ndege zilizofanikiwa zaidi kutokana na mchanganyiko wa teknolojia ya kisasa, gharama nafuu na uwezo mkubwa wa kivita.
Licha ya kuwa na injini moja pekee, ndege hiyo imeonyesha uwezo mkubwa katika mapambano ya anga dhidi ya baadhi ya ndege kubwa zaidi duniani, jambo ambalo limeifanya kutajwa kuwa miongoni mwa ndege hatari zaidi katika kundi la ndege za kizazi cha nne "4+ generation".
Uwezo wa kivita unaofanya J-10C kuwa hatari

Chanzo cha picha, Getty Images
Moja ya sababu kubwa zinazofanya J-10C kupewa hadhi ya ndege hatari ni uwezo wake wa kushambulia adui kabla hata ya kuonekana kwenye rada za kawaida. Ndege hiyo imefungwa rada ya kisasa ya AESA, teknolojia inayoweza kufuatilia maeneo inayoyalenga kwa mengi na kwa wakati mmoja huku ikiwa vigumu kugunduliwa mapema na adui. Mfumo huo huipa nafasi ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza angani.
J-10C pia hubeba kombora la PL-15, ambalo linatajwa kuwa moja ya makombora yenye uwezo mkubwa zaidi duniani katika mashambulizi ya mbali ya anga. Kombora hilo linaaminika kuwa na uwezo wa kulenga shabaha kutoka zaidi ya kilomita 200, hatua inayomruhusu rubani kushambulia ndege ya adui kabla hata ya kuingia kwenye eneo hatari la mapambano.
Katika mapambano ya karibu angani, ndege hiyo hutumia kombora la PL-10 ambalo lina uwezo mkubwa wa kubadili mwelekeo kwa kasi na kufuatilia shabaha hata ikiwa ipo pembeni mwa ndege. Mfumo huo huifanya J-10C kuwa hatari sana katika "dogfight" - mapambano ya karibu kati ya ndege mbili angani.
Mbali na silaha zake, J-10C imeundwa kwa uwezo mkubwa wa kufanya mizunguko ya haraka angani na kubadilisha mwelekeo kwa kasi kubwa wakati wa mapambano. Uwezo huo huipa nafasi ya kukwepa mashambulizi ya adui na kujipanga upya ndani ya sekunde chache.
Ripoti za kijeshi zimewahi kueleza kuwa katika mazoezi kadhaa ya anga, J-10C ilifanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa dhidi ya ndege kubwa zaidi kama Su-35 ya Urusi kutokana na mchanganyiko wa teknolojia yake ya rada, kasi ya kufanya maamuzi pamoja na matumizi ya makombora ya kisasa.
Jambo jingine linaloifanya kuwa tishio zaidi ni uwezo wake wa kushirikiana kidigitali na ndege nyingine za China kama J-20 na J-16. Mfumo huo huruhusu ndege kubadilishana taarifa za kivita kwa wakati halisi, jambo linalosaidia marubani kuona nafasi ya adui mapema na kufanya mashambulizi ya pamoja kwa ufanisi mkubwa.
Mafunzo ya marubani wa J-10C ni 'vita'

Chanzo cha picha, Getty Images
China imeongeza kiwango cha mafunzo kwa marubani wake wa kivita katika miaka ya karibuni, hatua inayotajwa kuongeza uwezo wa kutumia ndege hizo katika mazingira magumu ya vita.
Mazoezi mengi yanayohusisha J-10C hujengwa katika mazingira yanayofanana na vita halisi, yakiwemo mashambulizi ya usiku, vita vya kielektroniki pamoja na operesheni za kushambulia malengo mengi kwa wakati mmoja.
Marubani wa China pia hupata muda mkubwa zaidi wa mazoezi ya kuruka ukilinganisha na baadhi ya mataifa mengi duniani, hali inayowasaidia kuzoea matumizi ya mifumo ya kisasa ya ndege hizo.
Uwezo wa marubani kufanya maamuzi ya haraka pamoja na kutumia teknolojia za kisasa kwa ufanisi ndio unaoifanya J-10C kuwa tishio kubwa zaidi katika mapambano ya kisasa ya anga.
Gharama nafuu lakini teknolojia kubwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Tofauti na ndege kubwa zaidi kama J-20 au J-16, J-10C imeundwa kwa gharama nafuu zaidi huku ikiwa bado na uwezo mkubwa wa kivita.
Kutumia injini moja kunapunguza gharama za matengenezo, matumizi ya mafuta pamoja na muda wa maandalizi kabla ya operesheni za kijeshi.
China imefanikiwa kuzalisha ndege hizi kwa idadi kubwa kwa muda mfupi, hali iliyosaidia kuliboresha jeshi lake la anga kwa kasi kubwa.
Wataalamu wa kijeshi wanaamini kuwa uwezo wa kuzalisha ndege nyingi za kisasa kwa gharama ndogo ni moja ya silaha kubwa za China katika ushindani wa kijeshi duniani.
Makala hii imeandaliwa kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo Military Watch Magazine.










