Nchi hizi 5 Afrika mafuta huuzwa kwa bei ya 'chapati'

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati wananchi wa Tanzania na Kenya wakiendelea kulalamikia kupanda kwa bei ya mafuta kuanzia mwezi April na sasa Mei mwaka huu, baadhi ya mataifa ya Afrika bado yanaendelea kuuza mafuta kwa bei ya chini sana kulinganisha na wastani wa dunia.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji Tanzania (EWURA), bei ya petroli Dar es Salaam mwezi Mei 2026 imefikia Sh4,115 kwa lita, sawa na takribani dola 1.58 kwa lita. Nchini Kenya, mamlaka ya nishati ya EPRA Kenya ilitangaza bei ya petroli Nairobi kufikia takribani Sh214 za Kenya kwa lita, sawa na karibu dola 1.66 kwa lita.

Kupanda huku kwa bei kunachangiwa na mivutano ya kisiasa Mashariki ya Kati, hasa vita vinavyohusisha Iran, Israel na Marekani. Vita hivyo vimeongeza hofu ya usumbufu katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha karibu asilimia 20 ya mafuta yote duniani.

Lakini wakati Afrika Mashariki ikiendelea kubeba gharama hizo, kuna mataifa ambayo bado wananchi wake wananunua mafuta kwa bei ya chini sana kutokana na uzalishaji mkubwa wa mafuta, ruzuku za serikali na sera maalum za nishati.

Bei hizi za chini zinaweza kulinganishwa na bei kununua chapati moja ama mbili kulingana na bei ya chapati na ukubwa wake katika nchi za Afrika.

5. Sudan - Dola 0.700 kwa lita

Licha ya migogoro ya kisiasa na vita vya ndani, Sudan bado imo kwenye orodha ya mataifa yenye mafuta ya bei nafuu zaidi Afrika. Hii ni kutokana na uwepo wa uzalishaji wa mafuta katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo pamoja na mifumo ya udhibiti wa bei.

Kwa miaka mingi, Sudan imekuwa ikitegemea sekta ya mafuta kama chanzo muhimu cha mapato ya serikali. Ingawa uzalishaji wake ulipungua baada ya kujitenga kwa Sudan Kusini, taifa hilo bado lina miundombinu ya mafuta inayosaidia upatikanaji wa bidhaa za petroli kwa gharama nafuu.

Pia, serikali ya Sudan imekuwa ikijaribu kupunguza athari za kupanda kwa bei ya mafuta duniani kwa kuingilia soko la ndani mara kwa mara, hasa wakati wa misukosuko ya kiuchumi na kisiasa.

4. Misri - Dola 0.454 kwa lita

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Misri imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye mafuta ya bei nafuu Afrika licha ya changamoto za kiuchumi zinazowakabili wananchi wake. Serikali ya Cairo imekuwa ikiingilia mara kwa mara sekta ya nishati ili kuzuia bei kupanda kwa kasi kubwa.

Taifa hilo lina uzalishaji wake wa mafuta na gesi asilia katika maeneo ya Mediterranean na Jangwa la Sinai, jambo linalosaidia kupunguza utegemezi wa kuagiza mafuta kutoka nje.

Mbali na hilo, serikali ya Misri hutumia sera za kudhibiti bei za mafuta kwa kuangalia hali ya uchumi wa wananchi na mfumuko wa bei. Hii imeifanya nchi hiyo kuendelea kuwa na mafuta nafuu zaidi kuliko mataifa mengi ya Afrika Mashariki.

3. Algeria - Dola 0.355 kwa lita

Algeria ni moja ya mataifa makubwa zaidi ya mafuta na gesi katika eneo la Afrika Kaskazini. Uchumi wa taifa hilo unategemea kwa kiwango kikubwa mauzo ya mafuta na gesi asilia kwenda Ulaya.

Serikali ya Algeria imeendelea kuweka ruzuku kubwa kwenye bidhaa muhimu kama mafuta, gesi, unga na huduma nyingine za msingi ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi. Mfumo huo wa ruzuku umeifanya Algeria kuwa miongoni mwa nchi zenye mafuta ya bei ya chini kwa muda mrefu.Kwa mwezi Mei, nchi hii inashika nafasi ya 8 kwa kuuza mafuta ya bei nafuu duniani.

Aidha, Algeria inaendelea kuongeza uzalishaji wake wa mafuta na gesi mwaka 2026 ili kuimarisha mapato yake ya nishati na kuongeza ushawishi wake kwenye soko la dunia.

2. Angola - Dola 0.327 kwa lita

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Angola ni moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara. Taifa hilo huzalisha zaidi ya mapipa milioni moja ya mafuta kwa siku, jambo linaloliwezesha kuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti bei za ndani.

Serikali ya Angola imeendelea kuwekeza katika viwanda vya kusafisha mafuta ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mafuta yaliyosafishwa kutoka nje. Miradi ya kisasa ya kusafisha mafuta inalenga kuongeza uwezo wa taifa hilo kujitosheleza kwa bidhaa za petroli.

Ingawa Angola bado huagiza sehemu ya mafuta yaliyosafishwa, serikali yake imekuwa ikidhibiti bei kupitia ruzuku na sera za nishati zinazolenga kupunguza presha ya maisha kwa wananchi. Bei ya mafuta katika nchi hiyo ni wastani wa dola 0.327 kwa lita ikishika nafasi ya pili Afrika na ya nne duniani kwa kuuza mafuta kwa bei nafuu.

1. Libya - Dola 0.024 kwa lita

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Libya ndiyo nchi yenye mafuta ya bei ya chini zaidi Afrika na hata duniani kwa sasa. Bei hiyo ni ndogo sana kiasi kwamba lita moja ya mafuta nchini humo ni chini ya hata maji ya kunywa katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

Sababu kubwa ni kwamba Libya ina moja ya akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani. Taifa hilo lina zaidi ya mapipa bilioni 48 ya akiba ya mafuta yaliyothibitishwa, kiwango kinacholiweka miongoni mwa nchi 10 duniani zenye mafuta mengi zaidi.

Mbali na kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta, serikali ya Libya imeendelea kutoa ruzuku kubwa kwa mafuta ya ndani ili kupunguza gharama kwa wananchi. Serikali hutumia fedha nyingi kufidia bei ya mafuta sokoni, jambo linalofanya wananchi kununua mafuta kwa bei ya chini sana licha ya changamoto za kisiasa zinazoikumba nchi hiyo.

Dola 0.024 kwa lita ni sawa na shilingi 52 ya kitanzania au Shilingi 3 ya Kenya ambayo haupati, andazi, kitumbua, aua unaweza usipate hata 'Bi G', labda pipi katika baadhi ya maeneo.