Nchi hizi 9 zilipataje silaha za nyuklia?

دو عکس کنار هم از قارچ هسته‌ای

Chanzo cha picha, Universal History Archive/Universal Images Group via Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Silaha za nyuklia zimebadili kabisa namna mataifa yanavyofikiria kuhusu vita na usalama.

Leo, kuna nchi tisa zinazojulikana kuwa na silaha hizo: Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini.

Lakini nchi hizi hazikufikia hatua hiyo kwa njia moja. Baadhi zilianza kutengeneza silaha za nyuklia wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, nyingine wakati wa Vita Baridi, huku kwa baadhi mashindano ya kikanda na hofu za kiusalama yakiwa sababu muhimu.

Zilipataje silaha za nyuklia?

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwaka 1953, Dwight Eisenhower, katika hotuba yake iliyopewa jina "Atoms for Peace" (Atomu kwa Amani), alipendekeza huko Umoja wa Mataifa kuwepo kwa juhudi za kimataifa za kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Marekani ilikuwa nchi ya kwanza duniani kutengeneza silaha za nyuklia kupitia mpango wa siri wa Manhattan Project wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mnamo Agosti 1945, ilitumia mabomu mawili ya atomiki dhidi ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan. Hatua hiyo ilionyesha uwezo mkubwa wa silaha hizo na kuanzisha mashindano ya nyuklia.

Umoja wa Kisovieti ulianza juhudi zake za kutengeneza bomu la atomiki wakati wa vita na kufanikiwa kufanya jaribio lake la kwanza mwaka 1949. Hilo lilimaliza ukiritimba wa Marekani na kuanzisha mashindano makubwa ya silaha za nyuklia kati ya mataifa hayo mawili. Uingereza, ambayo ilikuwa imeshirikiana na Marekani katika juhudi za wakati wa vita, ikawa nchi ya tatu yenye silaha za nyuklia mwaka 1952.

Ufaransa na China zilifuata katika miaka ya 1960, zikifanya majaribio yao ya kwanza mwaka 1960 na 1964 mtawalia. Kufikia hapo, Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza, Ufaransa na China zilikuwa zimejiimarisha kama mataifa yenye silaha za nyuklia. Hofu ya nchi nyingine kufuata njia hiyo ilisababisha kuanzishwa kwa Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia, NPT, mwaka 1970.

India iliingia kwenye kundi hilo mwaka 1974, licha ya kutokuwa imesaini NPT. Pakistan nayo haikusaini mkataba huo na ilifuata njia hiyo, huku ushindani wake wa kiusalama na India ukiwa sehemu muhimu ya mazingira yaliyopelekea kuendeleza silaha hizo. Pakistan ilifanya majaribio yake ya kwanza mwaka 1998.

Israel ni kesi tofauti. Haijawahi kuthibitisha wala kukana rasmi kwamba ina silaha za nyuklia, ikifuata sera inayojulikana kama nuclear ambiguity. Israel pia haijasaini NPT. Taarifa zilizovuja na makadirio ya wataalamu zimeifanya ihesabiwe miongoni mwa mataifa yenye silaha za nyuklia, huku makadirio yakionyesha inaweza kuwa na takriban vichwa 90.

Korea Kaskazini nayo iliwahi kuwa mwanachama wa NPT lakini ilijiondoa mwaka 2003, ikitaja miongoni mwa sababu zake mvutano wa kijeshi na Marekani na Korea Kusini. Mwaka 2006 ilifanya jaribio lake la kwanza la nyuklia na tangu wakati huo imeendelea kukuza uwezo wake wa nyuklia na makombora.

Kwa nini nchi nyingine ziliacha mpango wa nyuklia?

جی اف کندی، رئیس‌جمهور آمریکا در حال سخنرانی مقابل دوربین‌های شبکه‌های تلویزیونی

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati wa vita baridi, kulikuwa na vitisho kadhaa vya mashambulizi ya nyuklia

Kuwa na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia hakumaanishi kwamba nchi itaendelea nao hadi mwisho.

Nchi kama Brazil, Sweden na Uswisi ziliwahi kuanzisha mipango ya kutengeneza silaha hizo lakini baadaye ziliacha.

Mfano wa kipekee zaidi ni Afrika Kusini, ambayo ilifanikiwa kutengeneza silaha za nyuklia kisha ikazivunja na kusitisha mpango wake. Uamuzi huo ulihusishwa na mambo kadhaa, yakiwemo mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi, kupungua kwa migogoro ya kikanda na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa duniani.

Baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, Ukraine, Belarus na Kazakhstan pia zilirithi sehemu za silaha za nyuklia za Kisovieti zilizokuwa katika maeneo yao, lakini baadaye zote ziliacha silaha hizo. Ukraine ilikabidhi silaha hizo chini ya makubaliano ya Budapest Memorandum ya 1994, ikipokea ahadi za usalama kutoka Marekani, Uingereza na Urusi.

Dunia bado ina silaha ngapi?

مرد بر ویرانه‌های ناشی از بمب اتمی ایستاده است به عمارت بزرگ تقریب ویاران نگاه می‌کند

Chanzo cha picha, Universal History Archive/Universal Images Group via Getty Images

Maelezo ya picha, Matumizi ya mabomu ya atomiki katika miji ya Hiroshima (pichani) na Nagasaki ndiyo matukio pekee ambapo silaha za nyuklia zimetumika vitani

Kwa sababu serikali nyingi hazitangazi kikamilifu ukubwa wa maghala yao, hakuna idadi inayojulikana kwa uhakika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa SIPRI, nchi tisa zenye silaha za nyuklia zilikuwa na takriban vichwa 12,187 vya nyuklia Januari 2026. Kati ya hivyo, takriban 9,745 vilikuwa katika maghala ya kijeshi kwa matumizi yanayoweza kutokea, huku karibu 4,012 vikiwa tayari vimewekwa kwenye makombora au ndege.

Ingawa idadi ya jumla ya silaha za nyuklia imekuwa ikipungua kwa muda mrefu, SIPRI inaonya kwamba mataifa yenye silaha hizo yanaendelea kuziboresha na kutengeneza mifumo mipya ya kuzifikisha.

Marekani na Urusi bado zinamiliki sehemu kubwa zaidi ya silaha hizo duniani.

Je, nchi nyingine zinaweza kujiunga na klabu hiyo?

Swali hilo limekuwa muhimu zaidi kutokana na mjadala kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Iran ni mwanachama wa NPT na imesisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia una madhumuni ya amani na kwamba haitafuti kutengeneza silaha za nyuklia.

Lakini wataalamu wanaonya kwamba iwapo Iran itapata silaha za nyuklia, hatua hiyo inaweza kubadili hesabu za usalama katika Mashariki ya Kati na kuchochea nchi nyingine kufikiria kuhusu uwezo wao wa nyuklia.

Hata hivyo, kuingia katika klabu hiyo si jambo rahisi. Nchi inayotaka kutengeneza silaha za nyuklia inahitaji rasilimali, teknolojia na vifaa vinavyodhibitiwa kwa karibu kimataifa. Mchakato huo ni wa gharama kubwa na unaweza kuchukua miaka.

Kwa hiyo, licha ya kuwepo kwa hofu kwamba idadi ya mataifa yenye silaha za nyuklia inaweza kuongezeka, vikwazo vya kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia bado vinafanya safari hiyo kuwa ngumu.