TB ina chanjo na tiba, kwa nini bado inaua mamilioni?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Madame de Pompadour, mmoja wa makahaba maarufu zaidi nchini Ufaransa na aliyekuwa mpenzi na mshauri wa Mfalme Louis XV, alifariki mjini Versailles mwaka wa 1764, huku Simón Bolívar, aliyejulikana kama "Mkombozi" wa sehemu kubwa ya Amerika Kusini, akifariki akiwa eneo la Santa Marta, Colombia, mwaka 1830.

Wote wawili walikuwa wahanga wa kifua kikuu, ugonjwa uliokuwa ukijulikana pia kama white plague kuurejelea ugonjwa ulioua vizazi vya wasanii, wanasiasa na watafiti, wakiwemo waandishi Emily na Anne Brontë, mtunzi wa muziki Frédéric Chopin, mwandishi wa tamthilia Anton Chekhov na wengine wengi.

Ugonjwa huo ulikuwa umeenea sana kati ya karne ya 18 na 19 kiasi kwamba uliingia mara kwa mara katika fasihi na hadithi za kubuni.

Mpenzi wa mwandishi Alexandre Dumas fils, kahaba maarufu wa Paris Marie Duplessis, kwa mfano, alifariki kutokana na kifua kikuu akiwa na umri wa miaka 23 pekee. Kisa chake kikawa chanzo cha kuibuka kwa mhusika Marguerite Gautier, shujaa wa kitabu The Lady of the Camellias.

Kufikia wakati huo, uovu huo ulikuwa tayari umepewa jina jingine.

Uweupe uliokithiri wa ngozi, mwili mwembamba na macho yenye kung'aa vilihusishwa na hisia za kisanii, usafi wa nafsi na uzuri wa kupindukia, na hivyo kugeuza dalili ya ugonjwa huo kuwa kipimo cha urembo katika tabaka la juu la jamii.

Nadharua hiyo iliisha mwaka 1882, wakati daktari na mtaalamu wa viumbe vidogo wa Ujerumani Robert Koch alipothibitisha kwamba ugonjwa huo haukuwa ishara ya ustaarabu wa kiroho au kipaji cha kisanii, bali ulisababishwa na bakteria anayeambukiza, Mycobacterium tuberculosis, ambao alihusishwa na umaskini.

Ugunduzi huo ulisababisha mabadiliko makubwa sana ya kijamii na kiafya katika historia.

Hofu na unyanyapaa wa kijamii vilichukua nafasi ya ugonjwa ambao awali ulikuwa unatukuzwa

Mwonekano uliokuwa ukihusishwa na wagonjwa wa kifua kikuu haukuonekana tena kuwa wa kuvutia. Madaktari walionya kwamba nguo zenye na ndevu nyingi zilikuwa mazingira mazuri ya kuhifadhi vijidudu, na mitindo hiyo yote miwili ikatoweka mara moja.

Mtazamo kuhusu nafasi na mazingira pia ulibadilika kwa kiasi kikubwa.

Kwa kuwa tiba pekee iliyojulikana mwishoni mwa karne ya 19 ilikuwa mapumziko, mwanga wa jua na hewa safi, zilijengwa hospitali maalum za wagonjwa wa kifua kikuu, zilizojulikana kama sanatorium, eneo la milimani zikiwa na muundo safi na wa kitabibu.

Msisitizo huo wa usafi na mwanga wa jua uliweka msingi wa usanifu wa kisasa wa karne ya 20: paa tambarare, matuta ya wazi na madirisha makubwa yakawa maarufu ili kunufaika na miale ya jua, ambayo ilionekana kuwa kiua vijidudu cha asili chenye nguvu zaidi, pamoja na miundo ya ndani iliyozuia maeneo ambayo yangekusanya vumbi na ambako bakteria wa Koch Bacillus angeweza kujificha.

Licha ya mabadiliko hayo makubwa, bado kulikuwa na kitu muhimu kilichokosekana, mafanikio ya kitabibu.

Siku moja katika kiangazi cha mwaka 1921, katika hospitali moja mjini Paris, mtoto mchanga ambaye mama yake alikuwa amefariki kutokana na kifua kikuu alipewa dozi ya kwanza ya chanjo ya majaribio.

Muujiza wa kimya

Yote yalianza kwa utulivu.

Wanasayansi wa Ufaransa Albert Calmette na Camille Guérin walikuwa wametumia zaidi ya muongo mmoja kudhoofisha bakteria inayosababisha kifua kikuu, ili kupunguza makali yake.

Katika kutengeneza chanjo ya Bacillus Calmette-Guérin, au BCG, walikuza na kuhamisha aina hiyo ya bakteria mara 230, hadi walipopata bakteria ambaye alikuwa hai vya kutosha kuufundisha mfumo wa kinga wa watoto wachanga, lakini dhaifu kiasi cha kutowaua.

Chanjo ya BCG iliundwa kuwalinda watoto wachanga kwa sababu kwao, kifua kikuu kilikuwa kama hukumu ya kifo cha haraka; bakteria hao wangeweza kusambaa kwa kasi mwilini na kusababisha tuberculous meningitis or miliary tuberculosis zilizokuwa zikisababisha kiwango cha juu cha vifo.

Katika miaka ya mwanzo, matumizi ya chanjo hiyo yalikuwa karibu yamewekewa makundi madogo ya watoto nchini Ufaransa pekee. Hakukuwa na matangazo makubwa ya kimataifa wala sherehe za umma, kwa sababu jumuiya ya kimataifa ya kitabibu ilitaka kufanya miaka kadhaa ya majaribio kabla ya kuthibitisha chanjo hiyo kuwa salama.

Wanasayansi wakati huo walikuwa na mashaka makubwa kuhusu kuingiza bakteria hai mwilini, ingawa alikuwa amedhoofishwa, ndani ya mwili wa binadamu.

Kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, kati ya mwaka 1929 na 1930, katika jiji la Lübeck nchini Ujerumani, watoto wachanga 251 walipewa chanjo ya BCG. Kutokana na hitilafu ya maabara, dozi hizo zilichafuliwa na aina hatari ya bakteria wa kifua kikuu.

Matokeo yalikuwa mabaya sana watoto 72 walifariki na 173 waliugua vibaya.

Tukio hilo liliripotiwa kwa hofu kubwa katika magazeti na kusababisha woga mkubwa miongoni mwa umma, jambo lililoharibu sifa ya chanjo hiyo kote Ulaya.

Chanjo ya BCG haikufikia hadhi ya kuwa nyenzo ya afya ya umma duniani hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wakati uharibifu uliosababishwa na vita ulisababisha ongezeko kubwa na la kutisha la kifua kikuu barani Ulaya.

Hali hiyo ilizilazimisha mashirika ya kimataifa kuendesha kampeni kubwa za chanjo na kuwapatia mamilioni ya watoto chanjo hiyo ili kudhibiti mlipuko huo.

"Chanjo ya BCG ilileta mapinduzi, kwa maana hatimaye tulikuwa na chanjo dhidi ya kifua kikuu," alisema Claas Kirchhelle, mwanahistoria katika Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Utafiti wa Tiba ya Ufaransa (INSERM), katika mahojiano na BBC.

"Hata hivyo, tangu mwanzo haikuwa wazi kikamilifu ni kwa kiwango gani chanjo hiyo ilikuwa na ufanisi katika kuwalinda watu dhidi ya ugonjwa huo."

Kilichokuwa hakijulikani kilianza kufahamika zaidi hatua kwa hatua

Changamoto kubwa

"Kifua kikuu huathiri zaidi mapafu, bakteria hao huingia mwilini kupitia njia ya hewa hadi kufikia kwenye mapafu," alieleza Maximiliano Gutiérrez, Naibu Mkurugenzi wa Utafiti katika Taasisi ya Francis Crick jijini London.

"Wanapofika huko, huingiliana na seli za mfumo wetu wa kinga. Mwingiliano huo ndio huamua iwapo seli zetu zitaweza kuwaua bakteria hao, au ikiwa bakteria wataweza kuzaana, na kuongezeka, na hatimaye kusababisha kifua kikuu."

Chanjo inapaswa kuusaidia mwili kuwa na mfumo wa kinga unaoweza kuwaangamiza bakteria hao.

Hata hivyo, chanjo hiyo iliyotarajiwa kuokoa mamilioni ya watoto dhidi ya kufariki kutokana na aina kali zaidi za ugonjwa huo ilikuwa na udhaifu ambao ulichukua miaka kuonekana; iliwaacha watu wazima bila ulinzi wa kutosha.

"Watu waliopatiwa chanjo wakiwa katika umri mdogo sana walilindwa. Lakini ulinzi huo hupungua kadiri muda unavyopita. Idadi ya visa vya kifua kikuu tunavyoendelea kurekodi kila mwaka inaonyesha wazi kwamba chanjo hiyo haina ufanisi wa kutosha katika kuzuia ugonjwa huo kwa muda mrefu," Gutiérrez alisema.

Lakini chanjo si njia pekee tuliyonayo.

Streptomycin, antibiotiki ya kwanza iliyothibitishwa kuwa na ufanisi dhidi ya bakteria wanaosababisha kifua kikuu, iligunduliwa mwaka 1943. Kwa kipindi fulani, ilikuwa muhimu sana katika kukabiliana na kifua kikuu, lakini ikaibuka suala la usugu wa bakteria dhidi ya dawa hiyo kufanya iwe muhimu kutumia mchanganyiko wa dawa mbalimbali.

Leo hii, kifua kikuu hutibiwa kwa kutumia antibiotiki kadhaa kwa pamoja, na matibabu yake ni ya muda mrefu , huchukua takriban miezi sita.

Katika Taasisi ya Francis Crick, mojawapo ya maabara kubwa zaidi za utafiti wa tiba na biolojia barani Ulaya, watafiti wanajaribu kuelewa sababu ya hali hiyo.

"Tunataka kufahamu kwa nini inahitajika kutumia angalau antibiotiki tatu tofauti na matibabu ya miezi sita ili kumponya mtu, ikiwa tunaweza kufupisha muda huo na kupata antibiotiki zinazofanya kazi kwa ufanisi zaidi," anasema Gutiérrez.

"Pia tunavutiwa sana kuelewa kinachotokea katika hatua za mwanzo za maambukizi, zile dakika na nyakati za awali zinazoamua iwapo mtu ataishia kupata ugonjwa huo au, ataweza kuuondoa mwilini."

Kwa muhtasari, mtaalamu huyo anasema, "biolojia ya kifua kikuu ni changamano sana, na bado kuna mambo mengi ya msingi ambayo hatuyaelewi."

Maisha ya ndani ya bakteria

"Mycobacterium tuberculosis ni kiumbe kigumu sana kufanyia utafiti kwa sababu hukua polepole sana, na kwa hiyo utafiti katika eneo hili pia huendelea kwa kasi ndogo. Zaidi ya hayo, ni bakteria hatari sana," alisema Dany Beste, mhadhiri mkuu wa Viumbe Vidogo katika Chuo Kikuu cha Surrey.

Bakteria hao pia wanaweza kuishi katika aina nyingine za seli na hata nje ya seli hizo.

Inakadiriwa kuwa takriban mtu mmoja kati ya watu wanne duniani ana maambukizi yaliyofichika ya kifua kikuu, ikimaanisha kwamba watu hubeba bakteria hao mwilini bila kuugua kifua kikuu.

Sababu kuu

Licha ya juhudi zote, kifua kikuu bado ndicho chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na vimelea vya magonjwa ya kuambukiza, na ni miongoni mwa sababu 10 kuu za vifo duniani, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ugonjwa huo upo katika nchi zote na huathiri watu wa rika zote.

Ni nchi chache tu, zikiwemo Cuba, Bolivia na Suriname, ambazo zimeweza kurekodi kupungua kwa visa vya kifua kikuu katika miaka ya hivi karibuni.

Msongamano mkubwa wa watu magerezani, msongamano wa makazi mijini, umaskini na uhamaji wa watu unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa ugonjwa huo.

Kifua kikuu kinaonekana kuwa ugonjwa ambao tunapaswa kuwa na uwezo wa kuuzuia: kinadharia, tuna chanjo na matibabu ya kukabiliana nao. Lakini kwa vitendo, vyote viwili bado havitoshelezi kukabiliana na changamoto hiyo.

Zaidi ya hayo, jibu kuhusu kwa nini bado hatujaweza kutokomeza kifua kikuu halipo katika nyanja ya sayansi pekee.

"Upatikanaji wa antibiotiki na huduma za afya unaohusishwa na umaskini ni miongoni mwa vikwazo vikuu tunavyokabiliana navyo. Na ufadhili wa utafiti na maendeleo ya dawa na matibabu mapya pia umepungua," anasisitiza Max Gutiérrez, mtaalamu wa baiolojia ya seli.

Kumaliza kifua kikuu kunamaanisha kuboresha hali ya maisha ya watu, hali yao ya lishe, upatikanaji wa maji safi na makazi bora... na hilo ni mojawapo ya changamoto ngumu zaidi zinazokabili afya ya dunia.