Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini kujicheka si jambo zuri kila wakati?
- Author, BBC Future
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 10
Kwa nini baadhi ya watoto hutengwa shuleni?
Katika miaka ya 1990, wanasaikolojia walianza kuchunguza kwa nini baadhi ya watoto hutengwa na wenzao.
Walibaini makundi mawili ya msingi. Baadhi ya watoto waliotengwa walikuwa wakorofi na wenye tabia za ukatili. Wengine walikuwa waoga na wanyenyekevu. Makundi yote mawili yalikuwa na sifa moja kwa pamoja: hawakuweza kuvumilia utani.
Kundi la kwanza lilijibu utani kwa hasira au vurugu, huku kundi la pili likiumia na kujitenga. Makundi yote mawili yaliuchukulia ucheshi uliokusudiwa kama tusi, kana kwamba haungeweza kufanywa kwa nia njema. Kwa upande mwingine, watoto waliokuwa na kujiamini zaidi kijamii ama walipuuza utani huo au waliucheka tu na kuendelea na maisha.
Uwezo wa kujicheka unaweza kuwa na athari kubwa, kuanzia utotoni.
Utafiti unaonyesha kwamba kuwa na mtazamo mchangamfu na wenye ucheshi kuhusu maisha kuna manufaa zaidi kwa afya ya akili, mahusiano na hata uwezekano wa kuishi maisha marefu.
Hata hivyo, kwa muda mrefu kumekuwa na mitazamo tofauti, hasa kuhusu iwapo kujicheka ni jambo zuri.
Lakini sasa watafiti wanaanza kuelewa kwa undani maana halisi ya uwezo wa kujicheka, na ni wakati gani na kwa namna gani jambo hilo linaweza kuwa na manufaa.
Mada yenye utata
Je, kweli mtu anaweza kujicheka mwenyewe?
Plato hakuona uwezekano huo kuwa mkubwa. Mwanafalsafa huyo wa kale wa Ugiriki aliamini kwamba ucheshi ulitokana na hisia ya kujiona bora kuliko wengine; hasa watu waliojidanganya kwamba walikuwa warembo au werevu zaidi kuliko walivyokuwa kwa hakika.
Karibu miaka elfu moja baadaye, mwaka 1651, mwanafalsafa wa Kiingereza Thomas Hobbes kwa kiasi kikubwa aliunga mkono mtazamo huo, isipokuwa kwa jambo moja.
Kwa mujibu wake, wakati mwingine watu hujicheka wanapokumbuka upumbavu waliowahi kufanya. Bila shaka, hilo hutegemea jinsi walivyokomaa na kujifunza kuhusu maisha katika kipindi kilichopita tangu walipofanya jambo hilo.
Kadiri muda ulivyopita, wanafalsafa walianza kukubali kwamba si kila aina ya ucheshi huwa na nia mbaya. Kwa mfano, "nadharia ya kutokulingana" (incongruity theory) iliyoibuka katika karne ya 18 na kupata umaarufu mkubwa, ilieleza kwamba hisia ya kucheka mara nyingi hutokana na kuvunjwa kwa matarajio au kanuni za kijamii kwa namna isiyotarajiwa.
Hata hivyo, suala la iwapo watu wanaweza kweli kujicheka lilibaki kuwa na utata hadi hivi karibuni.
Tafiti nyingi kuhusu ucheshi zilizofanywa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita zilitumia kuwauliza watu iwapo wanaweza kujicheka na kisha kukubali majibu yao kuwa sahihi.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa takwimu za kiasi cha pombe wanachokunywa kila wiki ambazo watu huandika kwenye fomu wanazopewa na madaktari, majibu hayo yanaweza kuonyesha "kile kinachodaiwa kuwa" badala ya "kile kilicho kweli". Huenda watu wasiweke uvumilivu na uwezo wao wa kujichekesha katika kiwango wanachodai.
Hata hivyo, mwaka 2011, watafiti wa Ulaya walijaribu uwezo huo kupitia jaribio la kisayansi.
Washiriki waliitwa kwenye maabara, ambako nyuso zao zilirekodiwa kwa siri. Waliporudi, walionyeshwa picha zao zilizopotoshwa, zinazofanana na zile zinazoonekana kwenye vioo vya kuchekesha katika viwanja vya burudani, huku miitikio yao ikirekodiwa.
Ingawa si kila mtu alifurahia, asilimia 80 ya wale waliokumbana bila kutarajia na picha hizo walitabasamu angalau, huku asilimia 40 wakicheka kwa nguvu na kuonekana kufurahia hali hiyo.
Sonja Heintz, mhadhiri wa saikolojia na mtafiti wa ucheshi katika Chuo Kikuu cha Plymouth nchini Uingereza, anasema: "Sasa kuna makubaliano katika jumuiya ya wanasayansi kwamba watu wanaweza kujicheka na kwamba jambo hilo lina manufaa mengi."
Gelotophobes
Mwaka 2010, mtafiti wa ucheshi wa Marekani Paul McGhee alipendekeza kwamba uwezo wa kujicheka ni miongoni mwa aina ngumu zaidi za ucheshi kujifunza.
Katika mpango wake wa hatua saba wa kujifunza ucheshi, uliolenga watu wenye "umakini uliopitiliza" kama Plato, kujifunza kujicheka ilikuwa hatua ya pili kutoka mwisho. Kitu pekee kilichoonekana kuwa kigumu zaidi ni uwezo wa kuona ucheshi katika hali zenye msongo wa mawazo.
McGhee aliona kujicheka kuwa lango la kuelekea aina nyingine za ucheshi na "sehemu ya msingi" ya maisha yenye furaha zaidi.
Heintz anaeleza: "Kwa sababu mtu anapojichukulia kwa uzito kupita kiasi, inakuwa vigumu kwake kuhusiana na ucheshi kwa ujumla."
Kwa baadhi ya watu, kujifunza kujicheka ni rahisi zaidi kuliko kwa wengine.
Ikiwa kwa kweli unachukia watu wanapokucheka, huenda ukawa na "gelotophobia", yaani hali ya kuwa na kujihisi vibaya watu wakicheka.
René Proyer, profesa wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Martin Luther Halle-Wittenberg nchini Ujerumani, anasema: "Unaweza kuwa umeketi katika mkahawa ukifanya mzaha na marafiki zako, kisha mtu akaja na kukuuliza, 'Kwa nini unaniongelea kwa kucheka?'" Kwa watu wenye gelotophobia, hata tabasamu kwenye uso wa mtu mwingine linaweza kumaanisha kwamba mtu huyo anawaona wao kuwa watu wa kuchekesha au wa kudharauliwa.
Hakuna sababu moja inayoweza kueleza kwa nini mtu huwa na gelotophobia.
Hata hivyo, Proyer anaeleza kwamba malezi yenye ukali mkubwa na adhabu nyingi ni mojawapo ya sababu zinazoweza kuongeza hatari hiyo.
Sababu nyingine ni tukio la kutisha la zamani lililohusisha watu wengine kumcheka mtu huyo.
Proyer anatoa mfano: "Kwa mfano, unaweza kuwa ulikumbana na hali ya aibu sana shuleni ambapo ulikuwa mlengwa wa utani kwa wiki, miezi au hata miaka."
Ugonjwa wa usonji pia unachukuliwa kuwa sababu nyingine inayoweza kuongeza hatari hiyo.
Pia kunaonekana kuwa na tofauti za kitamaduni. Viwango vya gelotophobia katika nchi za Asia Mashariki kwa ujumla viko juu zaidi ikilinganishwa na nchi za Magharibi. Watafiti wanaeleza kwamba huenda hii ni kwa sababu watu kutoka tamaduni zinazosisitiza zaidi mshikamano wa kundi huwa na uwezekano mdogo wa kujitokeza ili kuvutia umakini au kutumia ucheshi kama njia ya kukabiliana na changamoto.
Katika tamaduni hizo, inaaminika kwamba ucheshi unapaswa kuachwa kwa wataalamu. Kwa mfano, nchini China, watu huwa wanahusisha ucheshi na "wataalamu", yaani wachekeshaji, badala ya raia wa kawaida.
Kama ilivyo kwa watoto wasioweza kuvumilia kudhihakiwa, watu wenye gelotophobia mara nyingi huwa na hali mbaya zaidi ya kisaikolojia. Tabia hii imehusishwa na wastani mfupi zaidi wa muda wa kuishi, tabia ya kuepuka urafiki, pamoja na kuongezeka kwa upweke na msongo wa mawazo.
Kinyume cha hali hiyo ni "gelotophilia", yaani kufurahia watu wengine wanapokukecheka, hali ambayo imehusishwa na mahusiano imara zaidi ya kijamii.
Njia mojawapo hali hii inavyojitokeza ni kutokuwa na mtazamo wa kujichukulia mwenyewe au dunia kwa uzito kupita kiasi, na badala yake kuichukulia kwa mtazamo mwepesi—sifa inayojulikana kama "playfulness", yaani tabia ya kucheza na mambo au kuyachukulia kwa uchangamfu.
Proyer anasema: "Watu wenye uwezo mkubwa wa kuona mambo kwa mtazamo wa kiuchezaji wanaweza kuyatafsiri upya au kuyaweka katika muktadha mwingine ili kuyafanya matukio ya kila siku yawe ya kufurahisha, yenye kuchochea fikra au ya kuvutia kwao binafsi."
"Mtu mwenye uwezo huo anaweza kuchukua kazi inayochosha au kazi za nyumbani na kuitazama upya kwa mtazamo unaoifanya iwe ya kufurahisha zaidi."
Tafiti zinaonyesha kwamba uwezo huu unahusishwa na kujithamini zaidi na kuridhika zaidi katika mahusiano.
Wataalamu wengi wanakubaliana kwamba ucheshi una manufaa kwa mahusiano yetu. Hata hivyo, aina ya ucheshi pia ni muhimu.
Mwaka 2003, watafiti wa Canada walitengeneza "Kipimo cha Mitindo ya Ucheshi" (Humor Styles Scale), ambacho huainisha aina kuu ya ucheshi ya mtu katika makundi manne:
- Ucheshi wa kujenga mahusiano
- Ucheshi wa kujitia moyo
- Ucheshi wa kuwaudhi wengine
- Ucheshi wa kujidhalilisha
Kipimo hicho kilikuwa na athari kubwa na kwa haraka.
"Wazo kwamba ucheshi unaweza kuwa na aina zinazosaidia au zinazodhuru lilichunguzwa kwa mara ya kwanza katika utafiti huu," anasema Claire Fox, profesa wa Saikolojia ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza.
Watu wanaotumia ucheshi wa kujitia moyo hutambua upuuzi na udhaifu wa maisha ya binadamu na uwepo wetu.
Watu hawa hukubaliana na kauli kama: "Ninapohisi huzuni au kutokuwa na furaha, kwa kawaida hujaribu kujisikia vizuri kwa kufikiria jambo la kuchekesha kuhusu hali hiyo."
Watu wa aina hii pia hupunguza uzito wa matatizo yao kama njia ya kukabiliana nayo. Aina hii ya ucheshi huchukuliwa kuwa ucheshi unaosaidia kukabiliana na changamoto.
Kwa upande mwingine, "ucheshi wa kujidhalilisha" huchukuliwa kuwa aina inayoweza kudhuru.
Wanaotumia mtindo huu wa ucheshi hukubaliana na kauli kama: "Mara nyingi hujaribu kuwafanya watu wanipende au wanikubali zaidi kwa kusema jambo la kuchekesha kuhusu udhaifu, makosa au kasoro zangu."
Wakati utafiti huo ulipofanywa, aina hii ya ucheshi ilionekana kuwa ishara ya hitaji la kupata umakini na kukubalika kutoka kwa wengine, pamoja na kujithamini kwa kiwango cha chini.
Je, ni bora kujicheka au kujitesa?
Heintz alipoanza kufanya utafiti kuhusu ucheshi katika miaka ya 2010, alishangazwa kuona jinsi ucheshi wa kujidhalilisha ulivyokuwa ukitazamwa vibaya katika nyanja hiyo.
"Kwa sababu mtindo wangu binafsi wa ucheshi unategemea kujifanyia mzaha kila mara," anasema. "Sijichukulii kwa uzito."
Alipokuwa akipitia tafiti zilizokuwepo, Heintz aligundua kwamba mtu kama yeye alichukuliwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata wasiwasi, msongo wa mawazo na mawazo ya kujiua.
Ili kubaini kama watu wanaotumia mtindo wa ucheshi wa kujidhalilisha kwa kweli hujichukia kwa kiwango hicho, Heintz aliwakusanya watu wa kundi hilo na kuwalinganisha na watu waliokuwa na mitindo mingine ya ucheshi.
Heintz anasema: "Ikiwa mtazamo uliokuwepo ulikuwa sahihi, watu hawa walipaswa kuwa na matatizo makubwa ya afya ya akili." Lakini hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na matatizo hayo.
Badala yake, aligundua kwamba ucheshi wa kujidhalilisha ulihusishwa na kujithamini zaidi na mahusiano bora zaidi na watu wengine.
Kwa mujibu wa Heintz, tafiti nyingi zinazoonyesha uhusiano kati ya ucheshi wa kujidhalilisha na matokeo mabaya zaidi katika afya ya akili na mahusiano zinategemea tu uhusiano wa kitakwimu, badala ya kuonyesha kwamba jambo moja linasababisha jingine.
Tafiti nyingine zimeonyesha kwamba athari za ucheshi wa kujidhalilisha zinaweza kutofautiana kulingana na mazingira.
Utafiti wa Fox wa mwaka 2014 ulibaini kwamba watoto wa umri wa kwenda shule wanaodhulumiwa na wenzao hutumia ucheshi wa kujidhalilisha zaidi kuliko wengine, na tabia hiyo huongezeka kadiri muda unavyopita.
Hata hivyo, utafiti mwingine wa Fox uliofuata mwaka 2016 uliongeza mtazamo mpya katika suala hilo.
Utafiti huo uliwaainisha watoto kulingana na aina ya ucheshi waliopendelea.
Kundi lililoitwa "self-defeaters", yaani watu wanaojidhoofisha wenyewe, lilitumia pekee ucheshi wa kujidhalilisha. Kundi hili lilionekana kuwa katika hali mbaya zaidi; lilikuwa na kiwango cha chini zaidi cha kujiamini na lilizidi kujitenga na wengine kadiri muda ulivyopita.
Kwa upande mwingine, baadhi ya watoto walitumia ucheshi wa kujidhalilisha hata zaidi kuliko kundi la "self-deprecating", lakini hawakupata madhara kama hayo.
Tofauti ilikuwa kwamba watoto hawa, walioitwa "humour endorsers", walitumia aina zote nne za ucheshi. Wakati wale waliotegemea pekee ucheshi wa kujidhalilisha walikumbana na madhara ya kijamii, hali hiyo haikutokea kwa wale waliotumia aina mbalimbali za ucheshi.
Fox anasema: "Hii inaonyesha kwamba mradi tu utumie ucheshi wa kujidhalilisha pamoja na aina nyingine za ucheshi, kwa kweli hakuna tatizo kufanya hivyo."
Hii haimaanishi kwamba ucheshi wa kujidhalilisha hauwezi kamwe kusababisha matatizo.
Heintz anasema: "Ikiwa unajifanyia mzaha na mzaha huo unatokana na hisia za maumivu au kujichukia, basi ndiyo, huenda hilo si jambo zuri kwako."
Hata hivyo, Heintz sasa anaamini kwamba mtazamo mwingi hasi kuhusu ucheshi wa kujidhalilisha unaweza kuwa umetokana na kasoro katika mbinu iliyotumiwa kwenye dodoso la Mitindo ya Ucheshi.
Anaeleza kwamba maswali kuhusu ucheshi wa kujidhalilisha mara nyingi huwa na hukumu ya thamani ndani yake, kupitia kauli kama "Ninafanya hivi kupita kiasi" au "Ninafanya hivi zaidi kuliko ninavyopaswa."
Je, upendeleo huu hasi dhidi ya nafsi unaweza kuwa unapotosha matokeo?
Makala ya Heintz inayotarajiwa kuchapishwa, ambayo bado anaifanyia kazi, inatathmini historia ya miaka 25 ya dodoso hilo na kupendekeza kutathminiwa upya kwa kipimo cha ucheshi wa kujidhalilisha.
Watafiti wengine tayari wanaandaa vipimo vipya vinavyotofautisha kati ya ucheshi unaomdhoofisha mtu mwenyewe na aina zake zinazoweza kuwa na manufaa, kama vile mtindo maarufu wa Waingereza wa kujifanyia mzaha.
Kujifunza kujicheka
Kama wachekeshaji wazuri wanavyojua, unapaswa kujifanyia mzaha tu pale unapokuwa umetulia na kukubali kasoro au kosa unalolifanyia mzaha.
Heintz anaeleza kwamba ikiwa mzaha wako unatokana na hali ya kutokuwa na raha, watu wataitambua hali hiyo na kujisikia vibaya.
"Watu wanapofanya mzaha, tunahitaji kujua kwamba hawapaswi kuchukuliwa kwa uzito. Lazima kuwe na kiwango fulani cha kuaminiana ili mtu aweze kuitikia ucheshi huo."
Kiasi pia ni jambo la kuzingatia. Fox anasema tofauti kati ya ucheshi wa kujikosoa na ucheshi wa kujidhalilisha "inaonekana kuwa kwenye kuzidisha na kuvuka mipaka."
Hata hivyo, ni wazi kwamba kujifunza kujicheka kunaweza kuwa na manufaa ya kisaikolojia na kijamii.
Kutokujichukulia kwa uzito kupita kiasi kumeonekana kusaidia mtu kukabiliana na changamoto na misukosuko ya maisha.
Heintz anasema: "Hii inahusiana na dhana ya 'kujivuka nafsi' (self-transcendence), ambayo inamaanisha kuwa na uwezo wa kuweka umbali fulani kati yako na hali unapokumbana na mambo yanayokwenda vibaya na kuziangalia kwa mtazamo wa kiuhalisia zaidi... kuwa na uwezo wa kuona upande wa kufurahisha au mwepesi wa mambo."
"Pia tunajua kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mambo kama kuridhika na maisha, uwezo wa kukabiliana na changamoto na hali ya jumla ya ustawi."
Kwa upande wa mahusiano na watu wengine, uwezo wa kujicheka unaweza kuwa nyenzo muhimu katika kukuza ujuzi wa kijamii.
Heintz anasema: "Unapokuwa na watu usiowajua na bado hujaelewa kikamilifu aina yao ya ucheshi, kutumia ucheshi katika mazingira mapya ni njia salama sana ya kuanzisha mawasiliano."
Njia hii inaweza kuwa muhimu hasa katika mazingira ambako kuna tofauti za mamlaka.
Utafiti mwingine uliofanywa na Fox ulibaini kwamba walimu wanaotumia "ucheshi wa kujidhoofisha" huonekana kuwa na mtazamo chanya zaidi machoni pa wanafunzi.
Aidha, watu wanaocheka makosa madogo wanayofanya, mradi tu makosa hayo hayawaathiri wengine vibaya, huonekana kuwa wenye moyo wa upendo zaidi na wenye uwezo zaidi.
Jinsi ya kuboresha ucheshi
Kwa hiyo, ikiwa wewe ni mtu mwenye tabia ya kuchukulia mambo kwa uzito kupita kiasi, unawezaje kujenga mtazamo mwepesi zaidi kuhusu nafsi yako?
McGhee alipendekeza kuanza kwa kuangalia udhaifu wako, kama vile urefu, uzito, upara au kutokuwa na ustadi, na kukabiliana moja kwa moja na "maeneo ambayo kwa kawaida hayapaswi kufanyiwa mzaha."
Ingawa mwanzoni inaweza kuwa vigumu, alisema kwamba "unapoanza kujisikia vizuri kufanya mzaha kuhusu mambo ambayo zamani yalikuwa yakukera au kukuaibisha, utaanza kupata hisia ya furaha na uhuru."
Hatua ya kwanza ni kuwaambia wengine mambo ambayo huyapendi kuhusu nafsi yako, ukianza na yale madogo zaidi.
Kisha anza kuyafanyia mzaha.
Heintz anasema: "Tuseme hupendezwi sana na mitindo ya mavazi; unaweza kujifanyia mzaha kwa kusema, 'Lo, nimevaa tena jeans zile zile za zamani.'"
"Au unaweza kusema, 'Angalia, nimefanya manunuzi yangu Temu.'" Kadiri muda unavyopita, utakuwa tayari pia kufanya mzaha kuhusu tabia zako zinazokuudhi au kukutia wasiwasi zaidi.
Ikiwa kuchunguza mambo yako nyeti kunaonekana kuwa kugumu, unaweza kuanza kwa kujenga mtazamo wa jumla wa uchangamfu na kucheza na mambo.
Proyer alifanya utafiti wa kuchunguza iwapo ingewezekana kuboresha uwezo wa washiriki wa kuchukulia mambo kwa mtazamo wa kiuchezaji ndani ya wiki moja kupitia shughuli rahisi.
Kwa mfano, unaweza kutumia dakika 10 kila jioni kuandika mambo matatu yaliyokuwa ya kufurahisha au ya kuchekesha zaidi yaliyokutokea siku hiyo, "iwe ni wazo lililokujia akilini au jambo uliloliona njiani kwenda kazini," kama Proyer anavyosema.
Kwa ujumla, washiriki waliripoti kwamba waliendelea kujiona kuwa watu wenye uchangamfu na uwezo wa kucheza na mambo hadi miezi mitatu baada ya utafiti. Pia walisema kwamba hali zao za huzuni zilipungua na viwango vyao vya furaha viliongezeka.
Kwa hiyo, ni jambo gani la kufurahisha zaidi lililokutokea leo? Liandike na ujitabasamie.