Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rui Pinto: Mdukuzi aliyefichua siri zilizoingiza Man City matatizoni
- Author, Laura Scott
- Nafasi, Sports news correspondent
- Author, Sarah Dawkins
- Nafasi, BBC Sport Senior Journalist
- Author, Patrick Nathanson
- Nafasi, BBC Sport
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rui Pinto ni jina ambalo huenda mashabiki wengi wa Manchester City hawalijui na wasilipende kuliskia, lakini nyaraka za siri alizovujisha zilisaidia kufichua mambo ya ndani ya klabu hiyo na zikahusishwa na uchunguzi mkubwa wa masuala ya fedha katika soka la England.
Pinto, raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 37, alianzisha tovuti yake ya Football Leaks mwaka 2015 akisema alitaka kufichua "upande wa pili wa soka usiojulikana".
Kupitia Football Leaks, alianza kuchapisha nyaraka za siri kutoka ndani ya vilabu, zikiwemo barua pepe na taarifa kuhusu mikataba ya udhamini, malipo na miamala mingine ya kifedha.
Miaka kadhaa baadaye, mamilioni ya nyaraka hizo ziliingia mikononi mwa waandishi wa habari wa uchunguzi barani Ulaya na kufichua taarifa kuhusu baadhi ya majina makubwa katika soka.
Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa ni taarifa zilizohusisha Manchester City na masuala ya fedha, ambayo baadaye yakawa sehemu ya mazingira ya uchunguzi mkubwa wa Ligi Kuu ya England.
Lakini Pinto mwenyewe amekuwa mtu wa utata: kwa baadhi ya watu ni mtoa taarifa aliyefichua mambo ambayo umma ulipaswa kuyajua, huku wengine wakimwona kama mdukuzi aliyepata taarifa hizo kwa njia haramu.
Alivyoanza na alivyotaka haki ionekane
Safari ya Pinto ilianza katika mji wa Vila Nova de Gaia, upande wa pili wa Mto Douro kutoka Ureno. Baba yake alifanya kazi katika kiwanda cha viatu kabla ya kujihusisha na biashara ya vitu vya kale, huku mama yake akifariki, Pinto akiwa na umri wa miaka 11.
Mwalimu wake wa zamani, Mario Falcao, anamkumbuka kama kijana aliyekuwa mchangamfu, mwenye uwezo wa kutumia kompyuta na aliyekuwa na udadisi mkubwa. Wakati mwingine alikuwa akikosa masomo, lakini uwezo wake wa teknolojia ulionekana mapema.
Mnamo Septemba 2015, Football Leaks ilimtafuta mwanahabari Antonio Varela wa gazeti la michezo la Record nchini Ureno. Pinto alitumia jina bandia "John" alipowasiliana naye kwa mara ya kwanza.
Varela na wenzake walipoanza kuchunguza nyaraka walizotumiwa, waligundua kuwa zilikuwa na taarifa muhimu sana. Hata hivyo, walijiuliza: je, ni sahihi kuchapisha taarifa ambazo zimepatikana kwa njia isiyo halali? Hatimaye waliamua kuwa maslahi ya umma wafanyae hivyo kwa kuwa ilikuwa taarifa muhimu zaidi.
Wengi wanaona labda alitaka haki itendeke kwneye soka.
"Mmoja wa watoa taarifa muhimu zaidi barani Ulaya"
Taarifa za Pinto hazikuishia katika chumba kimoja cha habari nchini Ureno. Baadaye alikabidhi makumi ya mamilioni ya nyaraka kwa mwanahabari Rafael Buschmann wa jarida la Ujerumani, Der Spiegel.
Timu ya waandishi wa habari mjini Hamburg ilianza kazi kubwa ya kuchambua nyaraka hizo. Walitumia muda mwingi kuzipanga, kuzilinganisha na taarifa nyingine na kuzihakiki kabla ya kuchapisha masuala muhimu.
Kwa ujumla, Pinto alitoa mamia ya taarifa kwa Der Spiegel na vyombo vingine vilivyoshirikiana katika mtandao wa waandishi wa habari wa uchunguzi wa Ulaya. Kiasi hicho ni kikubwa kiasi cha kulinganishwa na takribani nakala 3,000 za Encyclopaedia Britannica.
Taarifa hizo zilihusu baadhi ya watu na taasisi kubwa zaidi katika soka, wakiwemo Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Neymar, pamoja na vilabu, mawakala na mikataba yao.
Christoph Winterbach, mmoja wa waandishi waliohusika kuzichambua taarifa hizo, anamwelezea Pinto kama mtu mwenye umakini mkubwa, akili na msimamo wa kuamini kwamba anachofanya kina umuhimu.
Winterbach alimwita Pinto "mmoja wa watoa taarifa muhimu zaidi barani Ulaya", mtazamo unaoonyesha kwa nini baadhi ya waandishi wa habari wanamwona Pinto kama mtu aliyesaidia kufungua milango ya siri za biashara ya soka.
"Shujaa au mwizi?"
Hata hivyo, si kila mtu anamwona Pinto kwa mtazamo huo. Mjadala mkubwa unaomzunguka ni kama anapaswa kuonekana kama mtoa taarifa aliyefichua mambo yenye maslahi kwa umma au mdukuzi aliyepata taarifa hizo kwa kuvunja sheria.
Ana Gomes, mwanasiasa na mwanadiplomasia wa zamani wa Ureno, alikutana na Pinto akiwa gerezani na baadaye akatoa ushahidi wa kumtetea. Anaamini alipaswa kulindwa kama mtoa taarifa badala ya kushtakiwa.
Kwa upande wake, mwanahabari wa zamani Jose Carlos Freitas anasema wengi nchini Ureno wanamwona Pinto kama mwizi wa taarifa. Lakini pia kuna watu wanaomchukulia kama shujaa.
Antonio Varela, mwanahabari aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupokea taarifa za Football Leaks, anasema Pinto hawezi kuwekwa upande mmoja tu wa mjadala huo.
Kwa mtazamo wake, njia iliyotumiwa kupata taarifa hizo ilikuwa kinyume cha sheria, lakini taarifa zilizofichuliwa zilikuwa na manufaa kwa jamii. Hilo ndilo linalofanya suala la Pinto kuwa tata.
Hata wakili wake baada ya kukamatwa Pinto na kusekwa ndani, Francisco Teixeira da Mota, hakumwelezea kama shujaa au mtakatifu. Hoja yake ni kwamba, licha ya njia alizotumia kuwa tata, taarifa alizofichua zilileta manufaa kwa jamii.
"Maisha ya Pinto yamebadilika sana miaka 6 iliyopita"
Maisha ya Pinto yalibadilika kabisa mwaka 2019 alipokamatwa nchini Hungary na baadaye kurejeshwa Ureno. Kuanzia wakati huo, amekuwa akihusishwa na kesi kadhaa za kisheria zinazotokana na shughuli zake za Football Leaks.
Amewahi kufungiwa peke yake, kuwekwa kizuizini nyumbani na baadaye kuingia katika mpango wa ulinzi wa mashahidi. Katika moja ya kesi zake, alifika mahakamani akiwa ameandamana na kikosi cha ulinzi na polisi wenye silaha.
Katika kesi yake ya kwanza nchini Ureno mwaka 2023, alihukumiwa kifungo cha miaka minne baada ya kupatikana na hatia ya makosa yaliyohusisha jaribio la unyang'anyi, kuingia kwenye mifumo ya taarifa bila ruhusa na kuvunja usiri wa mawasiliano.
Pia alikabiliwa na kesi nchini Ufaransa, ambako alifungwa miezi sita. Kesi nyingine nchini Ureno bado inaendelea.
Mwanahabari Miguel Dantas anasema hali ya ulinzi wakati wa kesi za sasa ni tofauti na ilivyokuwa katika kesi yake ya kwanza, ambapo Pinto alivaa koti la kuzuia risasi na kulikuwa na askari wenye silaha juu ya paa la mahakama.
Katika maisha yake ya sasa, Pinto anaishi kwa kiasi kikubwa akiwa amefichwa kutokana na mpango wa ulinzi wa mashahidi. Hata hivyo, bado anafuatilia kesi na mijadala inayotokana na taarifa alizowahi kutoa miaka iliyopita.
"Football Leaks imekuwa na athari gani?"
Takribani miaka 10 baada ya kuanzishwa kwa Football Leaks, athari za taarifa alizokuwa akizitoa bado zinaonekana katika soka la Ulaya. Moja ya mifano mikubwa zaidi ni sakata linaloihusu Manchester City na masuala ya fedha.
Nyaraka zilizovujishwa na Pinto zilikuwa sehemu ya taarifa na uchunguzi mpana uliosaidia waandishi wa habari na mamlaka kuchunguza namna baadhi ya vilabu vilivyokuwa vikisimamia fedha, mikataba na mahusiano yao ya kibiashara.
Manchester City baadaye ilishtakiwa na Ligi Kuu ya England kwa mashitaka 115 yanayohusiana na madai ya kuvunja kanuni za kifedha. Kesi hiyo imekuwa mojawapo ya kesi kubwa zaidi za masuala ya fedha katika historia ya ligi hiyo.
Stefan Borson, aliyewahi kuwa mshauri wa masuala ya fedha wa Manchester City, anaonya dhidi ya kumchukulia Pinto kama "mpigania uhuru", akisema udukuzi wenyewe ulikuwa kitendo cha jinai. Hata hivyo, anasema baada ya taarifa hizo kufika hadharani, mamlaka zilikuwa na wajibu wa kuzichunguza.
Kwa upande wa Pinto, matokeo ya uchunguzi na kesi zinazotokana na taarifa hizo yana umuhimu wa kipekee. Wakili wake amesema Pinto anaishi maisha magumu ya kujificha na angependa kuona kwamba mambo aliyoyafichua yalikuwa na manufaa kwa jamii.
Kwa ujumla Pinto aliyekuwa na kompyuta huko Budapest ameweza kusababisha mtikisiko mkubwa katika ulimwengu wa soka, kutoka vyumba vya habari vya Ulaya hadi vilabu vikubwa na mahakama. Kwa sasa inaelezwa Man City imekutwa na hatia na iko katika wakati mgumu wa adhabu kali kisoka.
Inaweza kupigwa faini kubwa ya fedha, kupokwa alama nyingi kwenye ligi, kushushwa daraja kwenda Championship au madaraja ya chini zaidi, kufungiwa kusajili wachezaji, kunyang'anywa mataji ya nyuma. Yote yanategemea uamuzi wa mwisho wa kisheria.