Iran v Marekani: Wahamishia vita UN

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema Iran haitawahi kujisalimisha, lakini iko tayari kufikia suluhu la kidiplomasia ili kumaliza mzozo unaoendelea.

Baada ya karibu miezi saba ya vita kati ya Marekani, Israel na Iran,Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, alijibu tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kutaka kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, iwapo makubaliano hayatafikiwa haraka.

"Anapaswa kujua kwamba vikwazo, kuongeza shinikizo na vitisho vitaongeza tu upinzani wa wananchi wa Iran" alisema Rais huyo

Pezeshkian pia alisisitiza kwamba makubaliano yoyote yanapaswa kujumuisha kuondolewa kwa kizuizi cha Marekani dhidi ya meli na bandari za Iran.

"Haiwezekani kila mtu kunufaika na Mlango wa Hormuz, huku sisi tukinyimwa fursa ya kuutumia,"aliongezea.

Mlango Bahari wa Hormuz, ambao kabla ya vita ulikuwa njia ya kupitisha takribani asilimia ishirini ya usafirishaji wa mafuta na gesi asilia duniani, umekuwa kitovu cha mvutano kati ya Iran na Marekani.

Usafirishaji katika eneo hilo umevurugika tangu kuanza kwa vita, huku Iran na Marekani zikichukua hatua zinazoathiri usafiri wa kibiashara.

Iran imesema iko tayari kufungua tena Mlango wa Hormuz ndani ya siku saba iwapo Marekani itapunguza shinikizo la kijeshi na kuondoa vizuizi dhidi ya bandari za Iran.

"Hakuna mtu katika eneo hili atakayekuwa salama akiwa peke yake. Aidha tutajenga usalama pamoja, au tutakabiliana na ukosefu wa usalama pamoja" alisema Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.

Rais huyo wa Iran pia alikosoa utendaji wa jumuiya ya kimataifa kuhusu Iran. Akirejelea Israel, alisema kuwa "Bomu la nyuklia liko Israel, huku wakaguzi wakiwa Iran."

Pezeshkian aliongezea kuwa "Israel yenyewe ina bomu la nyuklia, lakini haijawahi kukaguliwa, huku Iran ikikaguliwa. Israel inaua, lakini Iran inawekewa vikwazo."

Rais wa Iran aliongeza kuwa Tehran haitasitisha mpango wake wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia.

Katika hotuba yake siku ya kwanza ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Marekani Donald Trump alisema yuko katika hatua ya kufanya "maamuzi makubwa" kuhusu iwapo afikie makubaliano na Iran na kuiruhusu nchi hiyo kujijenga upya, au "kuiangamiza."

Iran na Marekani zilifikia makubaliano ya awali mwezi Juni ya kumaliza vita na kufungua tena Mlango wa Hormuz, lakini makubaliano hayo yalivunjika ndani ya wiki chache baada ya Iran kuanza tena mashambulizi dhidi ya meli na Marekani kurejesha kizuizi cha kijeshi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi na Balozi wa Marekani Steve Witkoff walifanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyosimamiwa na Qatar, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York.

Steve Witkoff alisema ana matumaini kuwa mazungumzo hayo, ambayo yalikuwa duru ya kwanza ya mazungumzo tangu mwezi Juni, yatakuwa yataleta matumaini, akiongeza kuwa wasuluhishi wataendelea na juhudi zao.

Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmail Baghaei alisema mazungumzo hayo hayakuhusisha mada mpya zozote, na kwamba Araqchi alisisitiza masharti ya Iran, yakiwemo kuondolewa kwa kizuizi cha kijeshi cha Marekani na kuachiliwa kwa mali za Iran zilizozuiliwa.

Wakati huohuo, afisa mmoja wa ngazi ya juu nchini Iran aliiambia shirika la habari la Reuters kwamba Iran na Marekani bado zinatofautiana pakubwa kuhusu namna ya kumaliza vita, lakini diplomasia inapaswa kuendelea.

Afisa huyo wa Iran, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema Tehran inachunguza majibu ya Washington kuhusu mapendekezo yake ya amani, ambayo yanatoa kipaumbele kwa kuondolewa kwa kizuizi cha kijeshi cha Marekani baharini dhidi ya bandari za Iran na kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz.

Afisa huyo aliongezea kuwa,"Bado kuna tofauti nyingi kati ya misimamo ya Iran na Marekani, lakini diplomasia inaendelea."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba kufikia makubaliano na Iran kutahitaji juhudi za ziada na muda, akiongeza kuwa Donald Trump pia ana chaguo za kijeshi alizo nazo.