Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nani aliwafanya wanawake kuzionea aibu sehemu zao za siri?
Wanadamu wamekuwa wakizungumzia maeneo ya nje ya uke au vulva kwa maelfu ya miaka.
Hapo awali, sehemu hiyo ya uke ilikuwa ishara ya uzazi, lakini baadaye ilionekana kuwa kitu cha hatari, cha aibu na kinachopaswa kufichwa.
Leo hii, kuna tasnia nzima inayozunguka eneo la nje la uke, ikitoa huduma za "kuufanya iwe changa", Pamoja na taratibu zingine za urembo na upasuaji.
Kwa sasa wasanii wanaonyesha sehemu hiyo katika kazi zao za sanaa, wanaharakati wanaitumia kama ishara ya maandamano, huku madaktari wakijaribu kueleza kwamba maumbile ya kawaida ya sehemu za siri za mwanamke yanaweza kutofautiana kwa kiasi kikubwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Je, ni kwa nini sehemu hii ya mwili wa binadamu ilitoka kuwa ishara ya uzazi hadi kuwa kitu cha aibu, kutoka kuwa ishara ya urembo hadi kuwa alama ya kisiasa?
Gazeti la Ufaransa Le Monde limejaribu kufuatilia historia hii, huku gazeti la Uingereza The Guardian likitoa takwimu kuhusu athari za ponografia na mitandao ya kijamii.
Kwa pamoja, zinaonyesha kwamba mjadala kuhusu sehemu za siri za mwanamke hauhusu mwili pekee. Pia unahusu mamlaka, aibu, urembo na haki ya mtu kuamua nini cha kufanya na mwili wake.
Sehemu ya nje ya uke kama ishara ya uzazi
Ni vigumu kufikiria leo kwamba sehemu ya nje ya uke au vulva ulikuwa unaonyeshwa waziwazi katika sanaa bila aibu wala nia ya kuuficha.
Maelfu ya miaka iliyopita, wanadamu walitengeneza michoro na sanamu za mwili wa mwanamke, wakisisitiza hasa eneo la sehemu za siri. Ushahidi wa hili umeonekana nchini Ufaransa, katika eneo la kale la La Ferrassie na kwenye Pango la Chauvet, ambako baadhi ya michoro ya kale zaidi ya miambani duniani imehifadhiwa.
Kuna pia ugunduzi mwingine wa kuvutia. Kwa mfano, katika sanamu ndogo ya Venus kutoka Monpazier, sehemu za siri za mwanamke zilitengenezwa kwa ukubwa mkubwa kimakusudi. Inaaminika kuwa huenda watu wa kale walitaka kusisitiza uwezo wa mwanamke wa kuzaa.
Katika Mesopotamia ya kale, jinsia ya mwanamke pia haikuonekana kama jambo la aibu. Katika maandishi ya kale, mungu wa kike Ishtar anamwambia mteule wake "Panda mbegu katika uke wangu, mpenzi!"
Lakini baada ya muda, kila kitu kimebadilika.
Mwanahistoria wa zama za kale, Christian-Georges Schwentzel, aliiambia Le Monde kwamba mabadiliko makubwa yalianza Ugiriki ya kale na baadaye Roma, wakati jinsia ya mwanamke ilipoanza kuonekana kama jambo hatari.
"Nchini Ugiriki, na baadaye Roma, sehemu ya nje ya uke ulianza kuchukuliwa kama kitu cha kudharauliwa," mwanahistoria huyo anasema.
Mwanamke mwenye matamanio yake polepole alianza kuonekana kama mtu anayehitaji kuzuiwa na kudhibitiwa.
Na wazo hili limeendelea kuwepo kwa muda mrefu.
Mchambuzi wa saikolojia Sarah Piazza anazungumzia "hofu ya sehemu za siri za mwanamke," ambayo, kwa maoni yake, imepitia katika historia nzima ya jinsi wanawake wamekuwa wakionyeshwa, kuanzia zama za kale hadi sasa.
Udhibiti unaofichwa nyuma ya urembo
Tamaa ya kubadilisha mwonekano wa sehemu za siri za mwanamke pia haikuanza katika zama za kisasa.
Katika tamaduni mbalimbali, kumekuwa na desturi zinazohusisha kuondoa sehemu ya viungo vya uzazi au kubadilisha mwonekano wake.
Tiba ya Ulaya ilielezea upasuaji wa kupunguza labia au mashavu ya uke kabla ya kuibuka kwa upasuaji wa kisasa wa urembo.
Leo hii, wanawake wana uhuru wa kuamua wenyewe kile wanachotaka kufanya na miili yao. Lakini hilo linaibua swali: chaguo hili lina uhuru kiasi gani ikiwa jamii inaendelea kuwaambia wanawake mwili wa kike "unaofaa" unapaswa kuonekanaje?
Jibu la kitabibu ni kwamba hakuna umbo moja sahihi la sehemu ya uke ya nje.
Mtaalamu wa masuala ya ngono Joel Mignot anasisitiza kwamba hakuna kiwango cha kitabibu kinachoweza kuweka mwonekano unaopaswa kuwa nao sehemu za siri za mwanamke. Kuna tofauti kubwa kati ya wanawake, kama ilivyo kwa wanaume.
Hata hivyo, mwanamke anaweza kuutazama mwili wake ambao ni wa kawaida kabisa na kufikiri kwamba kuna tatizo nao.
Nani alibuni "sehemu bora ya uke wa nje"?
Katika miongo ya hivi karibuni, shinikizo hili limeongezwa na tasnia ya ponografia, mitandao ya kijamii, matangazo ya taratibu na upasuaji za urembo na mtindo wa kuondoa kabisa nywele za sehemu za siri.
Hatua kwa hatua, picha finyu ya "uke bora" imejengwa; wenye ulaini, usio na nywele, usio na mikunjo inayoonekana, wenye kunyumbulika, wa rangi ya waridi na usio na harufu.
Daktari wa magonjwa ya wanawake Sophie Berville anaita hali hii aina ya "kiwango cha dhahabu" kilichoibuka katika miaka ya 2000.
Gazeti la The Guardian linaongeza kuwa tatizo ni kwamba vijana hawaoni kwa urahisi jinsi maumbile ya kawaida ya sehemu za siri za mwanamke yanavyoweza kutofautiana.
Mwaka 2024, gazeti hilo lilinukuu matokeo ya utafiti uliofanywa Australia, yaliyoonyesha kuwa miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 24, asilimia 23 walihisi wasiwasi au aibu kuhusu mwonekano wa labia zao au mashavu ya nje ya uke wao, na nusu yao wanafikiria kufanyiwa upasuaji
Wakati huohuo, si kila mwanamke anayetaka kubadilisha mwili wake amekuwa tu mwathirika wa matangazo, mitandao ya kijamii au ponografia.
Daktari wa magonjwa ya wanawake Sophie Berville aliiambia Le Monde kwamba baadhi ya wagonjwa wake walikuwa na wasiwasi kuhusu mwonekano wa sehemu zao za siri kwa miaka mingi. Baadhi yao waliona aibu kuvua nguo mbele ya wenza wao au waliepuka mahusiano ya kimapenzi.
Baada ya kufanyiwa upasuaji, alisema, baadhi yao walijisikia vizuri zaidi kisaikolojia na maisha yao ya ngono yakawa bora.
Kwa hiyo, suala hilo si tu "kufanyiwa upasuaji au kutofanyiwa upasuaji." Jambo muhimu ni ikiwa mtu anaelewa hatari na madhara yanayoweza kutokea, na ikiwa kweli huo ni uamuzi wake mwenyewe.
Chama cha Madaktari wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake cha Marekani (ACOG) kinaonya kwamba intaneti na ponografia vinaweza kumfanya mtu ahisi kwamba maumbile ya kawaida ya mwili wake si sahihi. Pia, ushahidi kuhusu usalama na ufanisi wa taratibu nyingi za urembo zinazofanywa katika eneo hili bado hautoshi.
Kutoka aibu hadi maandamano na maarifa
Simulizi hii inachukua mkondo usiotarajiwa.
Mwili ambao kwa karne nyingi ulilazimishwa kufichwa, imegeuka kuwa njia ya kutoa ujumbe hadharani.
Mwaka wa 1969, msanii wa Austria Vali Export aliingia katika ukumbi wa sinema mjini Munich akiwa amevalia mavazi yaliyokuwa na uwazi katika eneo la sehemu za siri.
Ilikuwa ni hatua ya makusudi ya kuchochea mjadala na kupinga namna mwili wa mwanamke unavyogeuzwa kuwa kitu cha kutazamwa na wanaume.
Export aliwapa watazamaji fursa ya kuona si tu picha nyingine ya kuchochea hisia kwenye televisheni, bali mwanamke halisi aliyekuwa mbele yao na kuingiliana naye moja kwa moja.
Katika miaka ya 1970, wasanii wanawake wa kifeministi walianza kutumia waziwazi picha za sehemu za siri za mwanamke katika kazi zao za sanaa kama njia ya kuzungumzia jinsia ya mwanamke, mwili wake na haki yake ya kuamua namna ya kuonyesha mwili huo.
Miongoni mwa wasanii waliohusishwa na harakati hii alikuwa Judy Chicago.
Mwanahistoria na mkosoaji wa sanaa Cindy Nemser pia alikuwa na mchango muhimu katika kueneza harakati hii. Aliandika kuhusu sanaa ya kifeministi na kuwaunga mkono wasanii wanawake waliokuwa sehemu ya mkondo huo.
Baada ya muda, mada hii ilivuka mipaka ya sanaa.
Mwaka 2019, msanii Deborah de Robertis alionekana akiwa uchi nje ya Bunge la Ulaya, katika maandamano dhidi ya uwakilishi mdogo wa wanawake katika nafasi za madaraka.
Wakati huohuo, miradi ilianza kuibuka ikiwa na lengo la kubadilisha aibu kuwa maarifa.
Mwaka 2011, msanii Jamie McCartney alitengeneza Great Wall of Vagina, kazi ya sanaa iliyojumuisha vielelezo vya sehemu za siri za wanawake 400, kwa lengo la kuonyesha utofauti wa maumbile ya mwili wa mwanamke.
Mwaka 2016, The Vulva Gallery ilianzishwa, mradi wa mtandaoni unaoonyesha jinsi maumbile ya sehemu za siri za wanawake yanavyoweza kutofautiana.
Na mwaka 2019, Vagina Museum ilifunguliwa jijini London jumba la makumbusho linalolenga kuelimisha watu kuhusu maumbile ya mwanamke, afya na namna jamii inavyoutazama mwili wa mwanamke.
Leo, uke wa nje unaonyeshwa tena hadharani lakini kwa sababu tofauti.
Unaonyeshwa ili kuzungumzia uhuru.
Unachunguzwa ili kupambana na aibu.
Unaonyeshwa katika sanaa ili kuzungumzia mamlaka na haki ya mtu kuamua mwenyewe kile anachotaka kufanya na mwili wake.
Swali sasa si tena "sehemu ya nje ya uke unapaswa kuwa wa aina gani?"
Unaweza kuwa wa maumbo na mwonekano tofauti.
Na hilo ni jambo la kawaida.