Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Safari ya ajabu ya miaka 8 ya Mwafrika huyu kutoka Afrika hadi Greenland
Mwaka 1965, Teté-Michel Kpomassie aliondoka nchini kwao Togo barani Afrika na kuanza maisha mapya huko Greenland, akibadilisha fukwe zenye jua kwa fjord zenye barafu na chakula chenye viungo kwa nyama ya sili iliyochemshwa. Sasa akiwa na umri wa miaka 80, anapanga kustaafu na kurejea katika 'nyumbani kwake kiroho'.
Katika sebule yenye joto ya nyumba ya Tété-Michel Kpomassie jijini Paris, ambayo kwa ujumla imepangwa kwa ustadi, kuna meza ndogo katikati iliyosheheni kumbukumbu mbalimbali mlundikano wa picha za zamani za rangi nyeusi na nyeupe, barua na shajara zilizoandikwa kwa mkono.
Ni kumbukumbu za maisha ya mtu mmoja jasiri, msafiri na asiye wa kawaida.
Juu ya mafaili na makabrasha hayo yaliyosheheni meza, kuna kitabu chakavu, ambacho kurasa zake zimefifia. Jalada lake lina picha ya MInuk aliyevaa koti lililotengenezwa kwa ngozi ya sili, akiwa amesimama kando ya bahari yenye barafu.
Kichwa cha kitabu hicho kinasomeka Les Esquimaux du Groenland à l'Alaska (Waeskimo kutoka Greenland hadi Alaska). Ni kitabu cha utafiti kisicho cha kubuniwa kilichoandikwa mwaka 1947 na mwanaanthropolojia wa Ufaransa, Robert Gessain.
Ingawa miongo kadhaa imepita tangu siku ambayo Kpomassie alipoliona kwa mara ya kwanza akiwa kijana nchini Togo, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 80 bado anakumbuka tukio hilo kwa usahihi kana kwamba lilitokea dakika chache zilizopita.
Angewezaje kulisahau? Kile alichokiona ndani ya kitabu hicho tangu siku hiyo kilimvutia kabisa na kuanza kuunda kila hatua ya maisha yake.
Akiwa na umri wa miaka 16, alitoroka nyumbani na kuanza safari kubwa iliyomvusha mabara kadhaa hadi kufika Greenland, eneo lililo kaskazini kabisa duniani.
Alikuwa mwanamume wa kwanza kutoka Afrika kufika huko.
Safari hiyo ilisababisha kuandikwa kwa kitabu chake cha safari, kurejea kwake Greenland mara kadhaa na kupokea mialiko mingi ya kutoa hotuba na kusimulia uzoefu wake.
Katika miaka ya hivi karibuni, maisha yake pia yamepitia talaka yenye mzozo mkubwa.
Sasa, koti lake mwenyewe lililotengenezwa kwa ngozi ya sili limetundikwa karibu na mlango wa nyumba yake, likiwa katika sehemu ya heshima.
Haijulikani ni kwa nini utafiti wa kitaaluma kuhusu jamii ya Inuit uliwekwa kwenye rafu za duka dogo la vitabu la wamisionari wa Kikristo huko Lomé katika miaka ya 1950. Kpomassie alikikuta kitabu hicho alipokuwa akipona baada ya kukutana na nyoka akiwa juu ya mti.
Baada ya miaka mingi ya kutafakari, maelezo pekee anayoweza kutoa ni kwamba kukipata kitabu hicho ilikuwa hatima yake matokeo yasiyoweza kuepukika ya majaaliwa yaliyokuwa tayari yamepangwa.
"Nilikiokota, bila kuelewa maneno yaliyokuwa mbele yangu," Kpomassie anasema, macho yake yakimulika anaposimulia tukio hilo la asubuhi. "Lakini yule mtu aliyekuwa kwenye jalada alikuwa akinitabasamia moja kwa moja. Tulikuwa na uhusiano, mawasiliano fulani."
Akiwa amevutiwa, Kpomassie alinunua kitabu hicho, akaenda kuketi ufukweni na kukisoma kuanzia mwanzo hadi mwisho. Alipomaliza, alikisoma tena na tena.
"Kuanzia dakika nilipokimaliza," anasema, "sikuacha kamwe kufikiria kuhusu Greenland, nchi yangu. Ilikuwa ikiendelea kuvuma ndani yangu. Sielewi kwa nini. Lakini nilihisi kama sumaku ilikuwa ikinivuta, hivyo nikapakia mizigo yangu na kuondoka kwa siri."
Safari iliyofuata ni ya kushangaza kiasi kwamba ni vigumu kuamini. Kama si kwa vitu na kumbukumbu zilizowekwa mbele yangu, huenda ningekuwa na mashaka iwapo simulizi hili si hadithi ya kubuni aliyojitengenezea akilini.
Safari hiyo ilimpeleka kupitia Côte d'Ivoire, Ghana, Mauritania na Senegal. Alifanya vituo vifupi nchini Morocco na Algeria, kabla hatimaye kushuka kutoka kwenye meli kusini mwa Ufaransa.
Kutoka hapo, safari yake kupitia Ulaya iliwezeshwa na ukarimu usio na kikomo wa watu aliokutana nao, hasa ukarimu wa Jean Callaut ambaye Kpomassie alimtungia kitabu chake.
Callaut alikuwa Mfaransa ambaye baadaye akawa kama baba wa kumlea msafiri huyo kijana aliyekuwa mbali sana na nyumbani.
"Watu waliposikia hadithi yangu," Kpomassie anasema, "kila mmoja aliamini kwamba walikuwa wakishughulika na mtu mwenye dhamira kubwa. Lakini kama wasingenisaidia, msijali ningetafuta njia nyingine."
Muda mfupi kabla ya saa sita mchana, tarehe 27 Juni 1965, meli aliyokuwa amepanda Kpomassie mjini Copenhagen siku nane mapema ilitia nanga katika mji wa Qaqortoq, kusini mwa Greenland.
Miaka minane ilikuwa imepita tangu aliposema kwaheri kwa Togo kwa mara ya kwanza.
Hatimaye, Kpomassie ambaye sasa alikuwa na umri wa miaka 24 alikuwa amefika katika makazi yake mapya.
"Lilikuwa tukio la kushangaza," anasema huku akitabasamu. "Kupitia dirisha dogo la meli, niliwaona watu wote wakikusanyika bandarini wakisubiri meli yetu ifike."
Ndani ya sehemu ya chini ya meli kulikuwa na bidhaa, hasa kahawa na pombe, ambazo wenyeji walikuwa wamezingoja kwa hamu kipindi chote cha majira ya baridi. Hawakujua kwamba meli hiyo ilikuwa imebeba pia mshangao wa aina nyingine.
"Nilichukua muda wangu kabla ya kushuka," anaendelea, "kwa sababu sikuwa na uhakika watu wangetendaje waliponiona. Nilidhani huenda hakuna hata mmoja aliyewahi kukutana na mtu mweusi hapo kabla."
"Niliposhuka, kila mtu aliacha kuzungumza na wote wakaanza kunitazama. Hawakujua kama nilikuwa mtu halisi au nilikuwa nimevaa barakoa. Watoto walijificha nyuma ya mama zao. Baadhi yao walilia, wakidhani kwamba nilikuwa roho kutoka milimani."
Baadaye aligundua kwamba mwanamke mmoja katika umati huo alipiga kelele akimwita "mrembo".
Bila shaka, hali ya hewa na mandhari ya Aktiki aliyokutana nayo alipokuwa akisafiri katika maeneo mbalimbali ya Greenland zilikuwa tofauti kabisa na zile za Togo. Pia alivutiwa na tofauti za tamaduni.
"Jinsi kila jamii ilivyowatendea watoto ilinivutia tangu mapema," anakumbuka. "Nchini Togo, watoto walichukuliwa kuwa chini ya mamlaka ya wazee wao, huku kukiwa na mfumo mkali wa uongozi wa kifamilia. Huko Greenland, kwa upande mwingine, wazazi waliwatii watoto wao."
Katika kitabu alichokuja kuandika baadaye, Kpomassie anachunguza na kulinganisha mila za nchi zake hizo mbili, akitazama jinsi wazee wanavyotendewa, mila za uwindaji, maombi na kifo, pamoja na mifumo ya familia na ndoa za wake au waume wengi, ambazo katika maeneo hayo yote zilitofautiana kwa kiasi kikubwa na mtindo wa maisha wa Ulaya ya kisasa.
Kisha kulikuwa na chakula. Vyakula vyenye viungo vikali alivyokulia akila vilikuwa tofauti kabisa na nyama ya sili iliyochemshwa aliyohudumiwa karibu kila usiku, pamoja na samaki wabichi walioliwa moja kwa moja kutoka baharini.
Hata hivyo, baada ya muda, Kpomassie alianza kuona pia ufanano kati ya mataifa hayo mawili ambao, kwa mtazamo wake, uliwaunganisha.
Kufanya hivyo kulimsaidia kuutazama uamuzi wake wa kuondoka Togo kwa mtazamo tofauti.
"Niliondoka kwa sababu wakati huo nilikuwa nimefundishwa kuichukia tamaduni yangu, kutokana na yaliyokuwa yakitokea Afrika," anasema.
Alipoondoka Lomé, nchi hiyo bado ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa.
"Wakristo walijaribu kumbadilisha baba yangu kuwa Mkristo," anasema. "Majina ya Kiafrika yalipigwa marufuku na tulilazimishwa kutumia majina ya Kikristo kabla ya kuruhusiwa kujiunga na shule."
Kpomassie alitumaini kwamba Greenland ingempa maisha yasiyokuwa na aina hiyo ya ukandamizaji, ambako mila na desturi zingeachwa kustawi.
"Tatizo lilikuwa kwamba niligundua Greenland pia ilikuwa nchi iliyotawaliwa kikoloni," anasema. "Utamaduni wake ulikuwa tayari ukipoteza baadhi ya sifa zake kutokana na ushawishi wa Ulaya. Waliabudu mungu wao wa bahari, lakini hapa pia wamisionari walidhoofisha imani za wenyeji."
Ilikuwa katika maeneo ya kaskazini kabisa aliyotembelea ambako Kpomassie angepata uhuru aliokuwa akiutafuta.
Kwa kweli, mwanzoni alikatishwa tamaa na kile alichokikuta kusini mwa Greenland.
"Hakukuwa na igloo, wawindaji wala mbwa wa kuvuta sled," anasema. "Kila mtu alikuwa akinywa bia na kahawa muda wote, na kununua vyakula vya Denmark katika maduka makubwa."
Baada ya miaka minane ya safari na kusafiri maelfu ya kilomita, ndipo alipotambua kwamba kufika Greenland kulikuwa mwanzo tu wa safari yake.
Kwa sababu alipowauliza wenyeji wake waliko WaInuit wanaoishi kwenye igloo na wawindaji wa sili, aliambiwa aende kaskazini kabisa.
Ilikuwa huko kaskazini kabisa, wakati majira ya vuli na baadaye majira ya baridi yalipoanza, na nchi pamoja na watu wake wakazama katika usiku wa ncha ya dunia ulioonekana kutokuwa na mwisho, ndipo Kpomassie alihisi kwamba hatimaye alikuwa amefika kweli.
"Wakati theluji ya kwanza inaponyesha," anasema, "ndipo unaiona Greenland halisi. Joto linaposhuka kwa kasi na bahari kuganda, ndipo Wagreelanders wanakuwa wafalme wa nchi yao. Wageni wanaondoka, na maarifa ya kale yanatawala. Ni uhuru huo ndio nilioupenda zaidi."
Chini ya mwanga wa aurora borealis, akiwa mbali zaidi na Afrika kuliko alivyowahi kuwa, hatimaye Kpomassie alipata mwanga aliokuwa akiutafuta.
Maisha ya Kpomassie leo
Leo, Kpomassie anaishi Nanterre, kitongoji cha kihistoria magharibi mwa Paris. Licha ya kuwa na umri wa zaidi ya miaka 50 kuliko yeye, ninapata ugumu kumfuata, kwa kasi ya kutembea na hata katika mazungumzo, tunapoelekea kwenye mgahawa wa karibu kwa chakula cha mchana.
Kpomassie ananiambia kwamba, kama ilivyobainika, safari yake ya kwanza kwenda Greenland haikuwa ya kudumu.
Miezi 18 tu baada ya kufika huko, alirejea Togo bila kupenda, ili kuwashirikisha raia wenzake simulizi za safari yake na kukutana tena na familia yake ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imeamini kwamba alikuwa amefariki.
"Mwanzoni," anasema huku akiangalia orodha ya mvinyo, "niliporudi kutoka Greenland, nilitaka kuitupa shajara yangu baharini. Sikutaka kuandika kitabu."
Aliona uzoefu wake kuwa jambo la kibinafsi, karibu takatifu.
"Kwa kweli, hata sikutaka kuondoka, lakini sikuweza kupata meli iliyofaa kwa wakati unaofaa ili kuendelea kuelekea kaskazini zaidi. Hivyo nilitembelea mataifa 16 ya Afrika nikitoa mihadhara. Niliandika kitabu. Kwa namna fulani nilifunga ndoa nchini Ufaransa na nikapata watoto wawili."
"Lakini wakati wote huo nilijua nilikopaswa kuishia hatimaye."
Zaidi ya miaka 40 imepita tangu kitabu chake kilipochapishwa kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kifaransa. Tangu wakati huo, kimechapishwa tena katika matoleo 22 zaidi na kutafsiriwa katika lugha 10. Toleo jipya la Kiingereza linatolewa mwaka huu, huku matoleo ya Kireno na Mandarin pia yakiwa yanaandaliwa. Bila shaka, umaarufu wake wa kudumu unaweza kuhusishwa na ustadi wa Kpomassie wa kusimulia hadithi, lakini hiyo si sababu pekee iliyofanya kazi yake idumu kwa muda mrefu.
Ingawa simulizi nyingi kama hizi za safari zilizoandikwa miongo kadhaa iliyopita na "wagunduzi" sasa zinaonekana kupitwa na wakati zikiwa na mtazamo wa Ulaya, wa kuwadharau au kuwatazama watu wengine kama watu wa kigeni kazi ya Kpomassie haiwezi kuwa na umuhimu zaidi kwa wakati huu. Ukaribu aliouhisi na watu wa Inuit katika ziara yake ya kwanza uliwezesha kuzaliwa kwa kazi ya kifasihi iliyokuwa mbele sana ya wakati wake.
Tangu wakati huo, Kpomassie amerudi Greenland mara tatu zaidi, ziara yake ya hivi karibuni ikiwa mwaka 2007 alipokuwa mhadhiri kwenye meli ya kitalii ya Norway. Septemba mwaka huu atafanya safari yake ya mwisho kwenda katika nchi hiyo aliyokuja kuichukulia kuwa nyumbani kwake, ambako akiwa na umri wa miaka 81, anakusudia kuishi miaka yake iliyosalia. Anasema huo umekuwa mpango wake kwa miongo yote iliyopita.
Kwa bahati mbaya, hilo ndilo lililosababisha mwaka jana yeye na mke wake wa miaka 46 ambaye ni mama wa watoto wake kuachana na kuvunja ndoa yao.
"Nilikuwa nimeoa kwa muda mrefu, lakini kwa masikitiko, kutengana kwetu kukawa jambo lisiloepukika," anasema. "Alijua tangu mwanzo kwamba Greenland ndiyo jambo muhimu zaidi katika maisha yangu."
Anasema walikuwa wamekubaliana kwamba siku moja wangeacha maisha yao ya starehe nchini Ufaransa na kustaafu kwa kuishi maisha ya uwindaji chini ya milima ya Greenland. Lakini wakati fulani, mke wake wa zamani ambaye sasa ni nyanya bila kushangaza alibadili mawazo. Hilo likasababisha pengo ambalo halingeweza kuzibwa.
"Sasa anataka kutumia maisha yake ya kustaafu akitembelea Roma, Florence na Venice," anasema kwa sauti yenye dalili ya kutoridhika. "Tangu mwanzo nilikuwa mkweli kuhusu mahali moyo wangu ulipo. Daima tulikubaliana kwamba tutaenda pamoja. Ninaelewa, bila shaka, kwamba matakwa yake yalibadilika. Lakini yangu hayajabadilika."
Na watoto wake wanaichukuliaje hali hii yote? Naam, hawajavutiwa sana na mpango huo. Kpomassie anaamini kwamba kosa lake kubwa lilikuwa kuwaambia watoto wake kuhusu mipango yake tangu mwanzo.
"Kama ningeliwaambia nilipokuwa na umri wa miaka 16, nisingewahi kuondoka Togo," anasema. "Kila mtu angejaribu kunishawishi nibadili mawazo, na kunizuia. Sasa wanangu wanafanya vivyo hivyo, lakini hilo si jambo ninalotaka. Watoto wangu wananiheshimu, lakini wana hofu na wanahisi wanapaswa kunikatisha tamaa."
Anasema atawakumbuka, lakini mlango wake utakuwa wazi daima iwapo watataka kwenda kumtembelea.
Atakapowasili Greenland, Kpomassie anatarajia kutumia mwaka mmoja kuzunguka nchini humo, akiwapa wanafunzi wa shule mazungumzo kuhusu safari na matukio yake nchini humo na barani Afrika. Baadaye ataelekea kaskazini, ambako atabaki moja kwa moja.
"Nitakuwa na sleji ya mbwa na mbwa wa Husky," anasema huku akitabasamu. "Nitatafuta boti ndogo ya uvuvi. Na hapa nitatumia kwa furaha siku zangu zilizosalia, na hatimaye nitapata muda wa kuandika kitabu changu cha pili, kuhusu utoto wangu barani Afrika."
Hilo, bila shaka, litategemea iwapo mamlaka zitamruhusu. Kwa sasa, mbali na wenyeji, ni raia wa Denmark pekee wanaoruhusiwa kununua mali nchini Greenland.
"Nadhani wanaweza kunifanyia ubaguzi wa kipekee," anasema huku akikonyeza jicho. "Naam, angalau ninatumaini hivyo."
Anataka kuzikwa chini ya jabali kubwa la barafu. "Katika imani za jadi za Kiafrika, tunaamini kwamba kuna roho katika miti, bahari na milima," anaendelea. "Wagreelanders pia wanaamini kwamba majabali ya barafu yana roho. Ninapoketi na kuyatazama majabali hayo ya barafu, ninaweza kuwasiliana na roho hizo. Ninawapata mababu zangu barani Afrika, lakini nawapata zaidi huko Greenland."
Kpomassie ananihakikishia kwamba kuishi bila anasa za maisha ya sasa hakutakuwa tatizo, wakati mhudumu anatuletea sahani ya nyama ya bata na kujaza tena glasi zetu za mvinyo wa Côte du Rhône.
"Haya yote? Ni mambo ya juu juu tu," anasema. "Siku nitakapovaa koti langu la ngozi ya sili linaloning'inia kwenye korido yangu, nitasahau yote haya na kusema kwaheri. Ni kwa sababu tu ya kuishi ndiyo imenilazimu kuzoea."
Anaendelea, huku macho yake yakimetameta, "Unapofuatilia ndoto, ndoto ambayo imekua pamoja nawe kwa maisha yako yote, unaishi na kuipumua. Iko ndani yangu. Kuitimiza si suala la kuchagua. Mtu yeyote angesema safari yangu ya kwanza kwenda huko haingewezekana, lakini niliwathibitishia kwamba walikosea. Kwa nini iwe tofauti safari hii kwa sababu tu nimezeeka?
"Hiyo ndiyo hatima yangu. Hakuna njia nyingine."