"Nilisikia sauti zikinitaka nimchome kisu cha shingo mwanangu" - Mama

Chanzo cha picha, Getty Images
Onyo: Makala hii ina maelezo ya matukio ya kuhuzunisha na maudhui yanayoweza kusumbua hisia.
Lindsay Clancy alikuwa na ujuzi wa kuwasaidia wanawake kujifungua, akiwa amefanya kazi kama muuguzi na mama wa watoto watatu.
Hata hivyo, mnamo Januari 2023, maisha yake na ya familia yake yaligeuka kuwa mojawapo ya visa vya kuhuzunisha na vyenye utata mkubwa nchini Marekani.
Katika nyumba ya familia hiyo huko Duxbury, Massachusetts, Clancy mwenye umri wa miaka 35, aliwanyonga watoto wake watatu, Cora (miaka mitano), Dawson (miaka mitatu), na Callan (miezi minane), kwa kutumia mikanda ya mazoezi. Kisha alijaribu kujiua kwa kuruka kutoka dirishani kwenye ghorofa ya pili, jambo lililosababisha kupooza sehemu ya mwili wake.
Kesi yake kufunguliwa tena imechochea mjadala kuhusu mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya afya ya akili yanayoweza kutokea baada ya kujifungua, kuhusu mpaka uliopo kati ya ugonjwa wa akili na uwajibikaji wa uhalifu wa jinai, na jinsi hali ya ugonjwa wa akili inaweza kumfanya mama kutenda kitendo ambacho, kwa mtazamo wa moja kwa moja kinaonekana kisichowezekana kufanywa.
Clancy hakatai kuwa aliwaua watoto wake, lakini timu yake ya utetezi inajenga hoja yake kwenye msingi tofauti kabisa, kwamba hakuwa sawa kiakili wakati wa tukio hilo, na kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili unaojitokeza baada ya kujifungua kwa jina 'postpartum psychosis'.
Kadiri kesi inavyoendelea, mahakama bado itaamua ni nani anayewajibika kwa kilichotokea. Hata hivyo, kesi hii pia inaangazia umuhimu wa kuelewa tatizo hili la kisaikolojia na kutambua dalili zake mapema.
Ni ugonjwa gani huu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugonjwa huu unaotokea baada ya kujifungua humpata mwanamke mmoja au wawili kati ya kila wanawake elfu moja. Hii ni tatizo la afya ya akili "adimu" na linaathiri wengi. Pia linaweza kumpata mwanamke katika siku au wiki za kwanza baada ya kujifungua, na kusababisha kupoteza uhusiano na uhalisia.
Kulingana na Huduma ya Afya ya Taifa ya Uingereza (NHS), hali hii ni dharura ya kimatibabu inayohitaji hatua za haraka na matibabu, kutokana na hatari inayoweza kumkabili mama au mtoto wake.
Je, inatofautiana vipi na msongo wa mawazo wa baada ya kujifungua?
Msongo wa mawazo na saikosisi ya baada ya kujifungua ni hali mbili tofauti kwa dalili na ukali wake. Msongo wa mawazo baada ya kujifungua hutokea mara nyingi zaidi na hujidhihirisha kwa huzuni ya muda mrefu, kupoteza hamu au furaha katika shughuli za kila siku, wasiwasi, uchovu, kujihisi mwenye hatia, na ugumu wa kuanzisha uhusiano wa karibu na mtoto.
Ingawa saikosi baada ya kujifungua ni hali nadra lakini mbaya ya afya ya akili inayoweza kujitokeza katika siku au wiki za kwanza baada ya kujifungua, huambatana na dalili kama kuona au kusikia vitu ambavyo havipo (ndoto au maono ya uongo), kuwa na imani potofu zisizoendana na uhalisia, kuchanganyikiwa sana, mawazo yasiyopangika vizuri, pamoja na mabadiliko makubwa na ya ghafla ya hisia.
Akina mama wanasema nini kuhusu ugonjwa huu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Heba, mama wa watoto wawili, anasema: "Kwa uzoefu wangu, saikosi ya baada ya kujifungua ni mojawapo ya hali ngumu zaidi ambazo mwanamke anaweza kukabiliana nazo. Hakuna anayeelewa kile tunachohisi. "Nilikuwa nikisikia sauti zikinihimiza nimdunge mtoto wangu kisu shingoni wakati tulipokuwa tukila chakula jikoni. Sauti hizo zilikuwa karibu kunitawala kabisa."
"Katika jamii zetu, hakuna anayeelewa hali ya kisaikolojia anayopitia mama baada ya kujifungua. Wanasema: ni mawazo tu au fikra. Wanafikiri kwamba mama anapaswa kuwa na furaha kwa kumzaa mtoto wake, lakini hawafikirii kinachoendelea ndani ya ubongo wake, wala hawafikirii ugumu wa mawazo hayo yanayojirudia rudia," anasema Farah.
Farah anaelezea mateso yake kutokana na unyogovu wa baada ya kujifungua, akiuita "wakati mgumu zaidi," na kuongeza: "Siwezi hata kuwazia jinsi ilivyo vigumu kwa wagonjwa wenye saikosi ya baada ya kujifungua; mimi mwenyewe nilikaribia kuwa kichaa."
Kuhusu Hamsa, ambaye aliwahi kupata saikosi au kichaa cha baada ya kujifungua, anasema: "Sisahau yale yaliyonipata, na nahisi hofu kila ninapokumbuka kipindi hicho cha baada ya kujifungua. Mtoto wangu alilia bila kukoma, kujifungua kwangu kulikuwa kugumu na kulichosha sana, na sikuweza kulala.
Watu walikuja kunitembelea kuanzia wakati nilipotoka chumba cha uangalizi baada ya kujifungua, na hawakuacha kuja katika kipindi chote hicho. Nilihisi kama ninachanganyikiwa kutokana na uchovu, sikuweza kulala, na niliteseka kwa maumivu ya mishono, maumivu ya kujifungua, mshtuko, na mambo yote hayo kwa wakati mmoja."
Mama huyo wa mtoto mmoja anaongeza kuwa "Alilia sana kiasi kwamba nilihisi siwezi kumnyamazisha. Nilikuwa nikizunguka zunguka ndani ya nyumba nikiwa na maumivu, nikimtikisa mtoto kwa nguvu sana, huku nikisema, 'Jamani, tafadhalini, nataka tu anyamaze.' Nilikuwa nikipiga kelele na kulia huku nikisema, 'Imetosha, mchukueni mtoto huyu kutoka kwangu.'"
"Kisha mama yangu alikuja na kumchukua mtoto kutoka kwangu, na hapo nikagundua kuwa sikuwa sawa. Nilikaa pale nikipiga kelele na kusema, 'Simtaki, mchukueni kutoka kwangu, naogopa nitamfanyia kitu kibaya.'"
"Kisha nilijifungia chumbani kwangu kwa wiki nzima, nikijaribu kuelewa nilichokuwa nikimfanyia, huku nikilia na kujiuliza: Kwa nini nilifanya hivyo? Zilikuwa siku ngumu sana; namwomba Mungu zisirudi tena," Hamsa anaeleza.
Hali ya tahadhari yafaa itangazwe muda upi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanasaikolojia wa kitabibu Dima Haddad anasema kuwa katika visa vingi, dalili za ugonjwa huo hazianzi moja kwa moja kwa maono au sauti za uongo au imani potofu. Badala yake, mara nyingi hutanguliwa na viashiria vya tahadhari ambavyo baadhi ya watu wanaweza kuvichukulia kimakosa kama uchovu wa kawaida baada ya kujifungua.
Dalili hizo ni pamoja na matatizo ya kukosa usingizi kwa usiku kadhaa mfululizo, kuchanganyikiwa kwa mawazo, mabadiliko makubwa ya hisia, kuongezeka kwa mashaka au kutowaamini wengine, kuzungumza mambo yasiyoeleweka vizuri, au kuonyesha tabia zisizo za kawaida.
Mtaalamu huyo anaongeza kwamba kadiri hali inavyozidi kuwa mbaya, mama anaweza kuanza kusikia sauti ambazo hazipo, au kuwa na imani potofu na zisizobadilika ambazo haziendani na uhalisia. Kwa mfano, anaweza kuamini kwamba mtoto wake yuko katika hatari ambayo haipo kabisa, au kwamba amepewa ujumbe maalumu au jukumu la kipekee ambalo lazima litekelezwe.
Kwa hivyo mama anayesumbuliwa na ugonjwa wa akili baada ya kujifungua anapaswa kushughulikiwaje? Na ni nini kinachohitajika kutoka kwa wale walio karibu naye?
Dima anasema ni muhimu kwanza kutambua mama hachagui dalili hizi, na kwamba anapitia ugonjwa mbaya wa kisaikolojia unaoathiri mtazamo wake wa ukweli, kwa hivyo haifai kumlaumu au kujaribu kumshawishi kwa lazima kuwa mawazo yake si sahihi.
Anaongeza kuwa jukumu la familia ni kudumisha usalama wa mama na mtoto mchanga, sio kumwacha peke yake ikiwa dalili za kisaikolojia zitaonekana, kuwasiliana na mtaalamu wa magonjwa ya akili au idara ya dharura mara moja, kumpa mazingira tulivu na ya usaidizi, na kuzingatia mpango wa matibabu uliowekwa na timu ya matibabu.
Mwanasaikolojia wa kimatibabu anaelezea kwamba kuna viashiria vilivyo wazi vinavyohakikisha hali ya mama kuangaziwa kama dharura, hasa ikiwa dalili zozote za kisaikolojia zinajitokeza, kama vile kusikia sauti au kuona vitu ambavyo havipo, kuwa na imani zisizo za kweli na zisizobadilika, au kupoteza uwezo wa kutofautisha kati ya ukweli na njozi. Ishara zingine za tahadhari ni pamoja na kuzungumza kuhusu kujidhuru mwenyewe au mtoto mchanga, msisimko mkali, na tabia ya kushtukizia au fujo.
Tunawezaje kuwalinda watoto?
Prabha S. Chandra, mtaalamu wa afya ya akili ya wanawake pamoja na afya ya akili wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, alifanya utafiti kwa wanawake 108 waliokuwa na matatizo makubwa ya afya ya akili baada ya kujifungua na kugundua kuwa asilimia 53 yao walikuwa na mawazo potofu yanayohusiana na mtoto mchanga.
Mama walioamini, kwa mfano, kwamba mtoto ni pepo au ni mtoto wa mtu mwingine, pamoja na wale waliokuwa na mawazo potofu kumhusu mtoto, walikuwa na uwezekano mkubwa wa kumdhuru mtoto, kwani walionekana kutokuwa katika hali salama ya kumlea mtoto peke yao.
Dkt. Amrita Bhatt, kutoka Idara ya Saikiatria na Sayansi ya Tabia katika Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Washington, anaeleza kuwa kumpeleka mama hospitalini hakumaanishi lazima atenganishwe na mtoto wake.
Katika nchi zenye vitengo maalum kwa ajili ya mama na mtoto, mama anaweza kulazwa kwa ajili ya matibabu ya afya ya akili huku mtoto akiendelea kuwa naye katika mazingira salama.
Bhatt anaeleza kuwa vitengo hivi vimeundwa ili kuzingatia usalama, usaidizi, na elimu, na kwamba kumwacha mtoto na mama yake, pale ambapo ni salama kufanya hivyo, kunaweza kupunguza hatari ya kuharibika kwa uhusiano wao.
Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, uchambuzi huo unapendekeza mpango maalum wa matibabu na udhibiti wa hatari ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.














