Vyama vya upinzani Namibia vyapinga uteuzi wa jaji kwenye tume ya uchunguzi Tanzania

Vyama vya Affirmative Repositioning (AR) na Independent Patriots for Change (IPC) vimesema uteuzi huo unaweza kuibua maswali kuhusu uhuru wa mahakama ya Namibia na nafasi ya nchi hiyo katika mjadala kuhusu haki za binadamu nchini Tanzania.

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu & Beldeen Waliaula

  1. Kufikia hapo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Iran yaikosoa Saudi Arabia baada ya kutia saini mkataba wa ulinzi na Pakistan na Uturuki

    Picha ya Ebrahim Rezaei

    Chanzo cha picha, Mehr

    Maelezo ya picha, Picha ya Ebrahim Rezaei

    Iran imekosoa makubaliano mapya ya pamoja ya ulinzi kati ya Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki, ikisema makubaliano hayo hayawezi kuhakikishia Saudi Arabia usalama wake.

    Ebrahim Rezaei, ambaye ni mwanachama wa kamati ya usalama wa taifa katika bunge la Iran, amesema kuwa,

    "Saudi Arabia inapaswa kutambua kuwa makubaliano na Uturuki na Pakistan hayawezi kuwahakikishia usalama wake, kama ambavyo kutegemea Marekani pekee haikuipa usalama."

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Rezaei aliwaambia kuwa, "Badilisheni sera zenu ili msilazimike kuomba usalama kutoka kwa wengine."

    Kauli hiyo imekuja baada ya Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki kutia saini hii leo mkataba wa pamoja wa ulinzi ujilikanao kama 'Mecca Mutual Defense Agreement.'

    Kulingana wa makubaliano hayo, shambulio la kijeshi dhidi ya moja ya nchi hizo tatu litachukuliwa kuwa ni shambulio dhidi ya mataifa hayo yote, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na usalama kati ya mataifa hayo.

    Soma pia:

  3. Vyama vya upinzani Namibia vyapinga uteuzi wa jaji kwenye tume ya uchunguzi Tanzania

    .

    Chanzo cha picha, Instagram

    Na Humphrey Mgonja

    Vyama viwili vya upinzani nchini Namibia vimepinga uteuzi wa Naibu Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Petrus Tileinge Damaseb, kuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi inayochunguza waliohusika na makosa ya jinai na ukiukwaji wa sheria uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025.

    Vyama vya Affirmative Repositioning (AR) na Independent Patriots for Change (IPC) vimesema uteuzi huo unaweza kuibua maswali kuhusu uhuru wa mahakama ya Namibia na nafasi ya nchi hiyo katika mjadala kuhusu haki za binadamu nchini Tanzania.

    Katika taarifa yake, chama cha AR kimemtaka Jaji Damaseb kukataa uteuzi huo, kikisema kushiriki kwake kunaweza kuathiri taswira ya uhuru wa mahakama ya Namibia.

    Kiongozi wa chama hicho, Job Amupanda, amesema ushiriki wa jaji anayehudumu katika mahakama ya Namibia kwenye tume ya nchi nyingine utaharibu sifa ya mahakama ya Namibia na kuibua taswira kwamba mahakama za nchi hiyo zinahusishwa na masuala ya kisiasa nje ya mipaka yake.

    AR pia imeitaka Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kueleza msingi wa kisheria na kimaadili uliotumika kumruhusu Damaseb kushiriki katika tume hiyo, na imeonya kuwa inaweza kuchukua hatua za kisheria kupinga uteuzi huo.

    Kwa upande wake, chama cha Independent Patriots for Change (IPC) kimesema ushiriki wa Damaseb haupaswi kuchukuliwa kama mbadala wa mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu masuala ya haki za binadamu nchini Tanzania, ikiwemo kuzuiliwa kwa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.

    Chama hicho kimeitaka pia serikali ya Namibia kueleza msimamo wake kuhusu ushiriki wa jaji huyo katika tume hiyo.

    Malalamiko hayo yanakuja wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, tayari ameshazindua rasmi Tume ya Rais ya uchunguzi wa wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa Sheria katika matukio yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

    Tume hiyo ya makamishna sita imepewa miezi mitano kukamilisha kazi yake na inajumuisha majaji kutoka Tanzania, Uganda na Namibia.

    Mbali na Damaseb, mjumbe mwingine kutoka nje ya Tanzania ni Cheborion Barishaki, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda.

    "Tumeamua kuwashirikisha wenzetu (Namibia, Uganda) ili kupata muono mpana na kwamba tume hii inakwenda kuingia kwa undani zaidi, kutafuta nani hasa waliochochea, waliohusika, waliotoa fedha ili mambo yale (ghasia) yatokee ndani ya nchi yetu", alisema Rais Samia akizindua Tume hiyo Ikulu, Dar es Salaam Agosti 7, 2026

    Kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa, tume hiyo itachunguza waliohusika na makosa ya jinai na ukiukwaji wa sheria uliotokea wakati wa uchaguzi na kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa.

    Kuundwa kwa tume hiyo kunatekeleza moja ya mapendekezo ya tume iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, iliyochunguza matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Matukio hayo yalisababisha vifo vya watu 518 na kujeruhi maelfu ya wengine.

    Soma pia:

  4. DRC yawaachilia huru wafungwa 15 wanaohusishwa na M23

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imewaachilia huru wafungwa 15 wanaohusishwa na kundi la waasi la March 23 (M23), katika zoezi lililoratibiwa na Shirika ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).

    Msafara uliowabeba wafungwa hao ulisafiri kutoka Beni kupitia Uganda kabla ya kuwasili Rutshuru, ambako walikabidhiwa rasmi kwa muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC), ambao M23 ni tawi lake la kijeshi.

    Operesheni hiyo ilifanyika chini ya mfumo wa makubaliano ya amani ya Doha uliotiwa saini mwezi Septemba mwaka 2025, na inaonekana kama hatua muhimu ya kujenga imani kati ya pande zinazohusika katika juhudi za kupunguza mvutano mashariki mwa DRC.

    ICRC, iliyotekeleza zoezi hilo kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote, ilisema uhamisho huo ulifanyika kwa kuzingatia hatua kali za afya, ikiwa ni pamoja na tahadhari za kuzuia maambukizi ya Ebola.

    Shirika hilo lilieleza matumaini kuwa hatua hiyo itasaidia kuwaunganisha wafungwa hao na familia zao, pamoja na kufungua njia kwa kubadilishana wafungwa zaidi siku zijazo.

    Hatua ya leo inatajwa kuwa utekelezaji wa kwanza unaoonekana wa ahadi zilizowekwa katika makubaliano ya Doha, ambayo pia yanajumuisha kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia kwa waathiriwa wa vita mashariki mwa DRC.

    Soma pia:

  5. Zaidi ya watu 4,000 wathibitishwa kuambukizwa Ebola DRC

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kesi zilizothibitishwa za ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimepita 4,000 kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mlipuko wa sasa, kulingana na takwimu zilizotolewa na serikali ya taifa hilo.

    Mlipuko huo, ambao ni wa pili kwa ukubwa kuwahi kurekodiwa duniani, umetajwa pia kuwa unaenea kwa kasi zaidi kuliko milipuko yote ya awali.

    Wataalamu wanaamini maambukizi yalianza kusambaa miezi kadhaa kabla ya mlipuko kutangazwa rasmi tarehe 15 mwezi Mei, na kwamba idadi halisi ya walioambukizwa huenda ni kubwa zaidi kuliko takwimu rasmi.

    Taasisi ya Afya ya Umma ya DRC imesema katika taarifa yake ya hivi karibuni kuwa jumla ya maambukizi yaliyothibitishwa imefikia 4,053, huku watu 1,850 wakifariki dunia.

    Maambukizi yameripotiwa katika majimbo matano ya nchi hiyo ambayo ni Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Haut-Uele na Tshopo.

    Soma pia:

  6. Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan kutia saini makubaliano ya pamoja ya ulinzi

    Picha ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdoğan na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Picha ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdoğan na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman

    Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan zinatarajiwa kutia saini makubaliano ya pamoja ya ulinzi mjini Makka siku ya hii leo.

    Hatua hiyo inakuja wakati eneo la Mashariki ya Kati inaendelea kukumbwa na vita, huku baadhi ya mataifa ya Ghuba yakishambuliwa na Iran kulipiza kisasi mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake na Marekani na Israel.

    Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo matatu yenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni na pia ni washirika wa Marekani.

    Hata hivyo, bado haijabainika wazi kila taifa itachangia nini au jinsi makubaliano hayo yatakavyoathiri mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

    Mataifa hayo matatu yameonyesha kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya usalama Mashariki ya Kati, nafasi ya Iran ya Kishia katika siasa za eneo hilo, pamoja na kuongezeka kwa ushawishi wa Israel.

    Uturuki ina jeshi la pili kwa ukubwa ndani ya muungano wa NATO. Saudi Arabia ndiyo taifa lenye nguvu zaidi katika eneo la Ghuba na linahifadhi maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu, huku pia likiwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani. Pakistan, kwa upande wake, ndiyo nchi pekee yenye idadi kubwa ya Waislamu inayomiliki silaha za nyuklia.

    Soma pia:

  7. Trump apiga marufuku 'utalii wa kujifungua' nchini Marekani

    Picha ya Donald Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri mbili mpya, zinazolenga kupunguza haki ya uraia wa kuzaliwa nchini Marekani, hatua inayokuja wiki chache baada ya Mahakama Kuu kukataa jaribio lake la awali la kufuta haki hiyo.

    Amri ya kwanza inapanua orodha ya raia wa kigeni ambao watoto wao wanaozaliwa Marekani, kuwa hawatapata uraia wa moja kwa moja wa Marekani.

    Amri ya pili inapiga marufuku kile kinachoitwa "utalii wa kujifungua"ambapo wanawake wajawazito husafiri kwenda Marekani kujifungua ili watoto wao wapate uraia wa Marekani kwa kuzaliwa.

    Akizungumza katika Ofisi ya Oval, Trump alisema,"Hatua hii ilipaswa kuchukuliwa miaka mingi iliyopita, lakini sasa tunatatua tatizo hili."

    Pia aliikosoa Mahakama Kuu kwa kukataa jaribio lake la awali la kufuta haki ya uraia wa kuzaliwa, ambayo imekuwepo kwa karibu miaka 150.

    Kwa mujibu wa amri hiyo mpya, watoto wanaozaliwa Marekani hawatapata uraia wa kuzaliwa ikiwa wazazi wote wawili si raia wa Marekani na mmoja wa wazazi hao:

    • Ni mwanachama wa kundi la kigaidi la kigeni
    • Ni mfanyakazi wa serikali ya kigeni
    • Alijaribu kupata uraia wa Marekani kwa udanganyifu au ulaghai
    • Au anaishi katika maeneo ya Marekani ambako uraia kwa njia ya kuasili hautolewi chini ya sheria za shirikisho.

    Hata hivyo, uraia wa watu wanaozaliwa katika maeneo ya Marekani kama Puerto Rico unaendelea kutambuliwa chini ya sheria za shirikisho.

    Trump na maafisa wengine wa utawala wake wamekuwa wakikosoa mara kwa mara utalii wa kujifungua. Pia wamezituhumu nchi kama Urusi na China kwa kutumia sheria za uraia wa kuzaliwa kupata ushawishi nchini Marekani.

    Wakati wa kutangaza amri hizo, Trump alidai kuwa mamilioni ya watoto wamezaliwa Marekani kupitia utalii wa kujifungua.

    Hata hivyo, taasisi huru ya utafiti ya Migration Policy Institute inakadiria kuwa kati ya watoto 22,000 na 26,000 huzaliwa kila mwaka nchini Marekani kupitia utalii wa kujifungua.

  8. Iran: Hatutaruhusu njia ya pili kufunguliwa katika Mlango-Bahari wa Hormuz

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mohsen Rezaei

    Mohsen Rezaei, mshauri wa kijeshi wa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu amesema: "Hatutaruhusu kufunguliwa kwa njia ya pili kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz."

    Aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X: "Ikiwa kizuizi kitaendelea, meli na vikosi vya Marekani vitakabiliwa na hatari kubwa na majeruhi."

    Kauli za Mohsen Rezaei zinakuja wakati ambapo usafiri wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz bado ni mdogo sana.

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema jana (Alhamisi) kwamba anadhani Mlango-Bahari wa Hormuz "upo wazi kwa kiasi fulani" lakini kwamba Iran daima inaweza "kufanya mashambulizi au kutega bomu majini."

  9. Habari za hivi punde, Watu kadhaa wafariki baada ya kijana wa Thailand kuwapiga risasi wazee na walimu wa shule

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Watu wengine 15 wamejeruhiwa, wawili kati yao wakiwa katika hali mbaya, kufuatia tukio la ufyatuaji risasi katika shule moja iliyo nje kidogo ya Bangkok

    Ripoti za milio ya risasi zilitoka katika tawi la Nonthaburi la Shule ya Debsirin, iliyo nje kidogo ya mji mkuu wa Bangkok, muda mfupi baada ya saa 10:00 kwa saa za huko (saa 03:00 GMT).

    Video kutoka eneo la tukio zinaonyesha wafanyakazi wakiwatoa wanafunzi haraka kutoka darasani huku maafisa wa polisi wakijaribu kumtafuta mpiga risasi huyo.

    Kwa mujibu wa polisi, mhusika alikuwa mwanafunzi wa shule hiyo mwenye umri wa miaka 14, ambaye aliwafyatulia risasi walimu na wanafunzi wenzake kabla ya kujitoa uhai.

    Waliopata majeraha walipatiwa huduma ya kwanza na wahudumu wa dharura kabla ya kupelekwa hospitalini.

    Tukio hili la ufyatuaji risasi linafuatia tukio jingine katika shule iliyo kusini mwa Thailand mwezi Februari.

    Tukio hilo liliibua maswali—ambayo bila shaka yataulizwa tena sasa—kuhusu urahisi wa kupatikana kwa bunduki nchini Thailand.

    ..

    Chanzo cha picha, Reuters

  10. Infantino apata uungwaji mkono wa Afrika, huku England (FA) ikimkataa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Infantino

    Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alipata ahueni kubwa siku ya Alhamisi baada ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuunga mkono uongozi wake kwa kauli moja.

    Hata hivyo, uungwaji mkono huo kutoka kwa mojawapo ya makundi makubwa zaidi ya wapiga kura katika soka hautarajiwi kukomesha uchunguzi kuhusu namna mchezo huo unavyoendeshwa duniani kote.

    Hatua hiyo ya CAF—ambayo vyama vyake 54 wanachama vinawakilisha zaidi ya robo ya wanachama 211 wa FIFA—ilimpa Infantino msukumo muhimu sana wakati akijitahidi kupata muhula wa nne madarakani.

    Hathivyo timu za Ulaya bado zinaweza kususia mashindano, ikiwemo Kombe la Dunia, huku UEFA ikisema kuwa utetezi wa FIFA kwa rais wake Gianni Infantino "hauleti mabadiliko yoyote".

    Chama cha Soka cha Uingereza (FA) kimetuma barua ya kuondoa uungaji mkono wake kwa Infantino kufuatia mpango wa kuuza hisa za Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

    Shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA) lilisema katika taarifa yake kuwa masharti yake hayakutimizwa, licha ya mpango wa Infantino kusitishwa.

    "Kwanza, mapendekezo ya kuuza mashindano makubwa yalipaswa kuondolewa na pili," ilisema taarifa ya UEFA. "Lazima kuwe na uhakikisho kwamba majaribio kama hayo ya kuharibu mchezo kwa namna hiyo hayatafanyika tena.

    "Masharti haya hayajatimizwa."

    UEFA tayari imesema imepoteza imani na Infantino, ikilitaja pendekezo la 'Fifa Forward Enterprise' (FFE) kuwa "mpango mbovu, uliofanywa kwa siri na usio wazi".

    Infantino alikuwa ameahidi vyama vyote vya soka dola milioni 40 (pauni milioni 30) iwapo vingeliunga mkono pendekezo la uwekezaji binafsi katika mashindano yake, ikiwemo Kombe la Dunia la wanaume na wanawake, kupitia kampuni tanzu ya FFE.

    Shirikisho la soka duniani (FIFA) lilisema katika mkutano wa Jumatano kuwa "makosa" kuhusiana na FFE "yalikubaliwa", na kusema kuwa "haikuwa nia" ya Baraza la FIFA na vyama wanachama "kuhisi kutoshirikishwa katika mchakato huo na kwamba mchakato huo ulipaswa kushughulikiwa kwa namna tofauti".

    Taarifa ya UEFA ya kujibu hilo iliongeza: "UEFA iliweka wazi kabisa katika taarifa yake ya Jumamosi kwamba imepoteza imani na uongozi wa Gianni Infantino. Msimamo huo bado upo palepale.

    "Tangazo la jana kwamba baadhi ya watu walioajiriwa na rais wa FIFA (na ambao taaluma zao zinategemea upendeleo wake) wanakubaliana naye, halibadilishi chochote."

    FIFA imeombwa kutoa maoni yake kuhusu suala hili.

  11. Reuters: Wahouthi wauwa "takriban wanajeshi 58" wa serikali katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Wahouthi

    Wanamgambo wa Houthi wa Yemen waliua takriban wanajeshi 58 wa serikali katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani siku ya Alhamisi, chanzo cha kijeshi kiliiambia Reuters, katika mojawapo ya siku zenye maafa makubwa zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka minne nchini humo.

    Wizara ya Ulinzi ilisema kuwa makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani (drones) zililenga kambi kadhaa katika mikoa ya Marib na Hadramawt, na kusababisha vifo na majeraha kwa idadi ya askari wa Yemen.

    Wizara hiyo haikutaja idadi kamili ya waathiriwa.

    Wizara hiyo ililaani mashambulizi hayo na kuyaelezea kuwa ya "hila na usaliti" na kuahidi "kujibu uchokozi huu wakati na mahali mwafaka".

    Kundi la Houthi, ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya kaskazini-magharibi mwa Yemen na kuungwa mkono na Iran, lilisema kuwa lililenga "vikosi vikubwa vya kijeshi vya Saudi Arabia" vilivyokuwa vikijiandaa kwa operesheni ya kijeshi.

    Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukiunga mkono serikali wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    Katika shambulio jingine tofauti, msemaji wa muungano huo alisema kuwa raia 11 walijeruhiwa katika eneo la mpakani la Najran nchini Saudi Arabia, katika tukio walilolielezea kuwa shambulio la Houthi.

    Katika taarifa yao iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, walisema kuwa miongoni mwa waliojeruhiwa kulikuwa na raia saba wa Saudi Arabia, akiwemo mwanamke na mtoto wa miaka minne ambao wote walipata majeraha ya kuungua ngozi kwa kiwango cha pili.

    Raia wengine wanne walikuwa kutoka Yemen, Pakistan na Misri.

    Mashambulizi ya Houthi katikati mwa Yemen yalifanyika saa 10:40 kwa saa za eneo hilo (saa 07:40 GMT) siku ya Alhamisi, kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Yemen.

  12. Meta yatozwa faini ya dola milioni 567 katika uamuzi mkubwa zaidi kuhusu usalama wa watoto

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mmiliki wa Meta Mark Zuckerbag

    Siku ya Alhamisi, jaji wa Marekani katika jimbo la New Mexico aliiamuru kampuni ya Meta kulipa kiasi kingine cha dola milioni 567 (pauni milioni 421) kwa kushindwa kuionya jamii kuhusu hatari ambazo majukwaa yake yanawaweka watoto nazo; hii ikiwa ni hukumu kubwa zaidi dhidi ya kampuni hiyo kuhusiana na usalama wa watoto.

    Jaji Bryan Biedscheid alisema kuwa kampuni hiyo kubwa ya mitandao ya kijamii ni "kero kwa umma" inayofanana na uchafuzi wa hewa, na kwamba lazima iweke fedha hizo kwenye mfuko unaolenga kupunguza madhara ya baadaye.

    Hukumu hiyo inaongezeka juu ya faini ya dola milioni 375 ambayo Meta ilikuwa tayari imeamriwa kulipa katika kesi hiyo, na kufanya jumla ya malipo kuwa dola milioni 942.

    Jaji Biedscheid aliifananisha Meta na kiwanda, ambapo matangazo na maudhui ndiyo bidhaa zake, huku "madhara ya kisaikolojia na unyonyaji wa kingono dhidi ya watoto vikiwa ndivyo uchafuzi unaopaswa kudhibitiwa."

    Msemaji wa Meta—kampuni inayomiliki na kuendesha Instagram, Facebook, WhatsApp na Threads—alisema siku ya Alhamisi: "Hatukubaliani na hukumu hiyo na tutakata rufaa."

    "Tunajitahidi sana kuhakikisha usalama wa watu kwenye majukwaa yetu na tumekuwa wazi kuhusu changamoto za kubaini na kuondoa watu wenye nia mbaya pamoja na maudhui hatari. Tunaendelea kujiamini katika rekodi yetu ya kuwalinda vijana mtandaoni na tutaendelea kujitetea dhidi ya madai yanayopotosha ukweli."

    Kuhusu uamuzi wa awali wa kulipa dola milioni 375 katika kesi hiyo, Meta ilikuwa imesema ina nia ya kukata rufaa na kutoa maelezo kama hayo. Ilikuwa mara ya kwanza kwa jimbo kufanikiwa kuishitaki Meta kuhusiana na masuala ya usalama wa watoto.

    Kwa sasa, Meta inakabiliwa na maelfu ya kesi nchini Marekani kuhusiana na masuala kama hayo. Mbali na hukumu hizo za New Mexico, mapema mwaka huu Meta ilishindwa kesi huko Los Angeles iliyohusisha madai ya aina hiyo.

  13. Trump: Mlango-bahari wa Hormuz uko wazi, lakini Iran inaweza wakati wowote kushambulia au kutega mabomu majini

    .

    Chanzo cha picha, NurPhoto/Getty images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwa mara nyengine tena siku ya Alhamisi kuwa anaamini Mlango-bahari wa Hormuz "uko wazi kwa kiasi," lakini hakufikia hatua ya kutangaza makubaliano ya kuufungua kikamilifu njia hiyo ya maji.

    "Sitaki kusema kuwa kuna makubaliano, lakini (Mlango-bahari wa Hormuz) sasa uko wazi kwa kiasi fulani," Bw. Trump aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi (Agosti 5) baada ya kutia saini amri kadhaa za kiutendaji katika Ikulu ya White House.

    "Tunaudhibiti, lakini wakati wowote wanaweza kurusha kitu au kuweka mabomu majini. Hata bomu moja linatosha kuharibu mambo, kwa sababu hakuna anayetaka kuhatarisha meli yake yenye thamani ya mabilioni ya dola kwa kugonga mabomu yaliotegwa. Hata hivyo, nadhani mambo yanaenda vizuri sana," aliongeza.

    Rais huyo wa Marekani pia alisema anashiriki katika mazungumzo yanayoendelea na Iran, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu namna anavyoshiriki.

    Katika kauli nyingine, alisisitiza tena imani yake kuwa vita na Iran vitakwisha hivi karibuni kwa sababu, kama alivyosema, "hafikiri" kama Iran inaweza "kuendelea kwa muda mrefu zaidi."

    Licha ya kauli hizi, usafiri wa meli kupitia Mlango-bahari wa Hormuz bado una vikwazo vikali. Iran inataka meli zipite karibu na pwani yake na zipate kibali kabla ya kupita hapo.

    Kulingana na takwimu kutoka kampuni ya uchambuzi wa data za baharini ya Kepler, ni chini ya meli 10 zilizopita katika Mlango-bahari wa Hormuz kwa siku kuanzia Jumapili hadi Jumanne.

  14. Trump akanusha kuwepo kwa uhaba wa silaha nchini Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Donald Trump

    Rais Donald Trump amekanusha ripoti kwamba Marekani inakabiliwa na uhaba wa zana za kivita na kuahidi kupitia ujumbe wa mitandao ya kijamii kutaka "vifungo virefu gerezani" kwa wale wanaoshukiwa kuvujisha taarifa.

    "Marekani ina akiba kubwa ya 'zana za kivita,' hasa za aina fulani," Trump aliandika kwenye mtandao siku ya Alhamisi asubuhi. "Aidha, kiasi kikubwa kinatengenezwa na kusafirishwa kuja Marekani kadiri ya mahitaji."

    Trump na Pentagon wanakabiliwa na maswali yanayoongezeka kuhusu hali ya akiba ya silaha za jeshi, huku vita hivyo vikiwa sasa katika mwezi wa sita na makubaliano ya amani yakionekana kutofikiwa.

    Iran ilijibu ripoti kuhusu kupungua kwa akiba ya Marekani kwa kusema kuwa silaha zake zinazotengenezwa nchini humo zinaiwezesha kukabiliana na "tishio lolote".

    "Kila siku, dalili za kupungua kwa uwezo wa adui zinazidi kudhihirika," Waziri wa Ulinzi Majid Ibn-e-Reza aliandika kwenye mtandao wa X. "Lakini Majeshi yetu - yakisaidiwa na sekta ya ulinzi ya taifa - yana vifaa vya kutosha kukabiliana na tishio lolote."

    Aliongeza kuwa "wale wanaotaka kununua usalama na ubora wa kijeshi kupitia mifumo iliyoagizwa kutoka nje hivi karibuni watagundua kuwa teknolojia ya ndani ya Iran ni bora zaidi kuliko mfumo wowote katika eneo hili".

    Baada ya Marekani kutumia kiasi kikubwa cha silaha ambazo ni ngumu kutengenezwa wakati wa operesheni ya kivita inayojulikana kama 'Operation Epic Fury' na mashambulizi ya kulipizana kisasi yaliyofuata, utawala wa Trump umejaribu kuwahakikishia Wamarekani kuwa akiba ya makombora ya nchi hiyo bado ni imara.

  15. Natumai hujambo na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja