'Lango la Kuzimu la Turkmenistan:' Shimo linalowaka moto kwa miaka 40

n

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Kwa kawaida moto unaowaka kutokana na nishati kama mafuta au gesi, huwaka kwa saa chache, siku au wiki. Hata hivyo, moto unaowaka kutokana na nishati iliyo chini ya ardhi, unaweza kuwaka kwa miongo kadhaa.

Shimo la Gesi la Darvaza, ambalo pia linajulikana kama 'Lango la Kuzimu', ni shimo lenye upana wa mita 60 (futi 196) katika Jangwa la Karakum nchini Turkmenistan, ambalo linawaka moto kwa miaka 40.

Asili ya shimo hili inabishaniwa. Baadhi wanadai lilizuka miaka ya 1970 wakati mashine ya kuchimba gesi ya Kisovieti ilipotoboa gesi asilia chini ya ardhi kwa bahati mbaya; wengine wanaamini lilitokea tu wenyewe miaka ya 1960.

Lakini wanajiolojia walipogundua methane ikivuja kutoka kwenye shimo hilo, waliwasha moto kwa lengo la kuepuka janga la kimazingira. Walidhani ingeungua baada ya wiki chache na kuisha, lakini shimo hilo bado linawaka moto miongo kadhaa baadaye.

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kreta ya Gesi ya Darvaza ni shimo lenye upana wa mita 60 (futi 196) katika Jangwa la Karakum nchini Turkmenistan. - Picha kwa hisani ya: Getty Images

Shimo hilo liko juu ya uwanja mkubwa wa mafuta na gesi unaopitia Turkmenistan hadi Uzbekistan, ikimaanisha kuwa huenda limeungana na akiba kubwa ya methane chini ya ardhi, na kutoa nishati isiyo na kikomo kuwasha moto.

2013, mchunguzi wa Canada George Kourounis alianza safari ya kuchunguza shimo hilo. Akiwa amevaa suti inayostahimili joto, alishuka hadi chini ya shimo ili kukusanya sampuli za udongo. Aligundua viumbe ambavyo vinaweza kuishi katika hali ngumu ya hewa kwenye shimo hilo.

Mlango huu wa Kuzimu unaweza kuwa moto maarufu zaidi, lakini sio moto wa zamani zaidi unaoendelea kuwaka. Tabaka nene za makaa ya mawe ya chini ya ardhi, zinaweza kuwasha moto unaodumu kwa karne nyingi.

Moto mmoja wa makaa ya mawe chini ya Mlima Wingen nchini Australia umekuwa ukiwaka kwa zaidi ya miaka 5,000. Hadi ugavi wao wa nishati chini ya ardhi utakapokwisha, moto huu huenda utaendelea kuwaka kwa muda usiojulikana.