Majaji wa Uganda, Namibia kuchunguza wahusika wa ghasia za Oktoba 29 Tanzania

Chanzo cha picha, Fullshangwe
Majaji wawili kutoka Uganda na Namibia ni miongoni mwa makamishna sita watakaochunguza waliohusika na makosa ya jinai na ukiukwaji wa sheria uliotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi tume hiyo Ijumaa.
Tume hiyo, iliyopewa muda wa miezi mitano kukamilisha kazi yake, inaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shabani Ally Lila, huku Rais Samia akisema muda huo unaweza kuongezwa endapo kutakuwa na sababu za msingi.
"Kama kutakuwa na ombi la kuongezewa muda, tutaliangalia baadaye," alisema Rais Samia wakati wa uzinduzi uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Majaji wa nje walioteuliwa ni Petrus Tileinge Damaseb wa Namibia na Cheborion Barishaki wa Uganda.
Damaseb ni Naibu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Namibia na pia Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo. Barishaki ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda, ambayo pia hufanya kazi kama Mahakama ya Kikatiba ya Uganda, na ni Jaji wa Kitengo cha Rufani cha Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Makamishna wengine ni Jaji Mstaafu Gad John Mjemmas, Jaji Mstaafu Awadh Mohamed Bawazir na Jaji Mstaafu Aishieli Nelson Sumari.
Akizindua tume hiyo, Rais Samia aliwataka Watanzania kushirikiana na makamishna ili waweze kutekeleza majukumu yao bila vikwazo.
"Niwasihi sana Watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika na tume katika kutekeleza majukumu yao. Tuisaidie tume hii iweze kufanya kazi yake na tusiisumbue," alisema.
Tume itachunguza nini?
Kwa mujibu wa hadidu za rejea zake, tume hiyo itachunguza wahusika wa makosa ya jinai na ukiukwaji wa sheria uliotokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, kubaini mazingira yaliyopelekea matukio hayo na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya waliohusika.
Kuundwa kwa tume hiyo kunatekeleza moja ya mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, iliyowasilisha ripoti yake kwa Rais mwezi Aprili.
Miongoni mwa mapendekezo yake ilikuwa kuundwa kwa chombo maalumu cha kuchunguza viashiria vya uhalifu na kubaini wahusika wa matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.
Tume ya Jaji Chande Othman ilisema baadhi ya matukio yaliyochunguzwa yalihitaji uchunguzi wa kina wa jinai ili kubaini waliohusika na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria, hatua ambayo sasa itafanywa na tume mpya iliyozinduliwa na Rais Samia














