Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nguvu ya jeshi la Iran na namna lilivyojiimarisha tangu vita kuanza
- Author, Juan Francisco Alonso
- Nafasi, BBC News Mundo
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ulinzi wa mapinduzi hili ndilo jukumu lililoainishwa katika Ibara ya 150 ya Katiba ya Iran kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), taasisi iliyoanzishwa na Ayatollah Ruhollah Khomeini mara tu baada ya mapinduzi ya mwaka 1979 yaliyomng'oa Shah Reza Pahlavi madarakani. Tangu wakati huo, IRGC imekuwa ikijiona kama nguzo kuu ya kulinda mfumo wa mapinduzi na kuhakikisha utawala wa Kiislamu unaendelea kuwepo.
Leo, baada ya takribani wiki sita za mashambulizi kutoka Marekani na Israel, wataalamu wanasema IRGC imefikia kiwango cha juu cha ushawishi wake. Licha ya mashambulizi hayo makali, serikali ya Iran bado imesimama imara na haionekani kuwa katika hatari ya kuanguka, jambo ambalo linaonyesha uimara wa mfumo uliowekwa na IRGC.
Wachambuzi wa masuala ya ujasusi na masuala ya Mashariki ya Kati wanasema mfumo wa Iran ungekuwa na wakati mgumu kuhimili mashambulizi hayo ya anga bila udhibiti mkali wa IRGC katika jamii, udhibiti ambao unaonekana kuimarika zaidi. Hii imeifanya taasisi hiyo ionekane kama mhimili mkuu wa uhai wa taifa la Iran.
Kwa miaka mingi, IRGC imeendelea kupanua ushawishi wake kutoka uwanja wa vita hadi katika siasa na uchumi wa nchi. Hali hii imeifanya isiwe tu jeshi, bali pia chombo cha kisiasa na kiuchumi chenye nguvu kubwa ndani ya mfumo wa Iran.
Jeshi ndani ya jeshi
IRGC iliundwa kwa sababu ya kutokuwa na imani na jeshi la kawaida la Iran lililorithiwa kutoka enzi ya Shah. Kwa mujibu wa wataalamu wa siasa za kimataifa, Khomeini alitaka chombo kingine cha kijeshi kitakachomtii moja kwa moja Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi badala ya serikali ya kawaida au wizara ya ulinzi.
Tofauti kubwa ni kwamba IRGC inaripoti moja kwa moja kwa Kiongozi Mkuu wa nchi, jambo linaloifanya kuwa na nguvu kubwa kuliko hata jeshi la kawaida. Hii imeifanya kuwa si taasisi ya kijeshi pekee, bali pia chombo cha kulinda itikadi ya mapinduzi ya Kiislamu ndani ya Iran.
Wataalamu wanasema muundo huu umeifanya IRGC kuwa huru zaidi kuliko taasisi nyingine za serikali. Hii inamaanisha inaweza kufanya maamuzi makubwa bila kuingiliwa moja kwa moja na taasisi za kiraia za serikali.
Kwa muda mrefu, hali hii imeongeza mvutano kati ya jeshi la kawaida na IRGC, lakini baada ya muda IRGC imeibuka kuwa taasisi yenye nguvu zaidi ndani ya mfumo wa ulinzi wa Iran.
Jeshi lililojijenga kupitia vita na historia
Vita vya Iran na Iraq (1980–1988) vilikuwa hatua muhimu sana katika kuipa IRGC nguvu na uzoefu mkubwa wa kijeshi. Katika kipindi hicho, IRGC ilijionyesha kama jeshi lenye utii mkubwa kwa serikali na uwezo wa kupigana vita virefu.
Tangu wakati huo, nguvu zake zimeendelea kukua. Leo, inakadiriwa kuwa na kati ya wanajeshi 125,000 hadi 200,000, huku jeshi la kawaida la Iran likiwa na zaidi ya wanajeshi 350,000. Hata hivyo, wachambuzi wanasema nguvu ya IRGC haipimwi kwa idadi pekee bali kwa ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi.
Katika miongo iliyofuata, IRGC imekuwa ikijenga uwezo wake wa kiteknolojia, hasa katika makombora na droni. Hii imeifanya Iran kuwa na uwezo wa kujibu mashambulizi ya nje kwa haraka na kwa nguvu.
Kwa hiyo, licha ya kuwa na idadi ndogo kuliko jeshi la kawaida, IRGC imekuwa ikionekana kuwa na nguvu kubwa zaidi kimkakati na kiutendaji.
Matawi maalum ya vikosi vya Basij na Quds
IRGC ina matawi kadhaa maalum ambayo yanaipa uwezo mkubwa wa ndani na nje ya Iran. Miongoni mwao ni Basij na Quds, ambayo yana jukumu tofauti lakini muhimu sana katika mfumo wa usalama wa nchi.
Basij ni vikundi vya kujitolea vinavyohusika na usalama wa ndani na kudhibiti maandamano. Kundi hili limekuwa likilaumiwa kwa kushiriki katika ukandamizaji wa maandamano ya wananchi katika miaka ya hivi karibuni, ambapo mamia ya watu wameripotiwa kupoteza maisha.
Kwa upande mwingine, kikosi cha Quds ni kitengo cha operesheni za nje ya nchi kinachojihusisha na vita visivyo vya moja kwa moja, intelijensia na kusaidia makundi washirika wa Iran katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati kama Lebanon, Gaza na Yemen.
Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yamekuwa yakiona kama kikosi cha Quds ni kama moja ya vitengo hatari zaidi vya kijeshi vya Iran kutokana na shughuli zake za kimataifa.
Mfumo wa "Mosaic" na mbinu mpya za kivita
Baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel, IRGC ilibadilisha mfumo wake wa uendeshaji na kuanza kutumia "Mosaic System", unaoruhusu kila mkoa kufanya maamuzi ya kijeshi kwa uhuru zaidi bila kusubiri amri kutoka Tehran.
Katika mfumo huu, Iran iligawanya nchi katika mikoa 31, kila moja ikiwa na jukumu la kijeshi na akiba ya makombora na droni. Hii imeifanya Iran kuwa na uwezo wa kujibu mashambulizi haraka hata kama miundo ya mawasiliano ya kitaifa imeathiriwa.
Wachambuzi wanasema mfumo huu umejengwa kutokana na uzoefu wa kuona kushindwa kwa mataifa makubwa kama Marekani katika vita vya Iraq na Afghanistan, ambapo Iran imejifunza umuhimu wa vita vya mgawanyo badala ya uongozi wa kati pekee.
Hii pia imeifanya IRGC kuwa na uwezo wa kuendelea na mashambulizi hata kama sehemu ya uongozi wake mkuu inalengwa na adui.
Nguvu nje ya uwanja wa vita
Mbali na kijeshi, IRGC imekuwa na ushawishi mkubwa katika uchumi wa Iran. Inamiliki hisa katika sekta ya mafuta, ujenzi, benki na miradi mikubwa ya kitaifa.
Hii imeifanya kuwa si tu taasisi ya ulinzi, bali pia mchezaji mkubwa wa kiuchumi. Wataalamu wanasema ushawishi huu wa kiuchumi unaipa nguvu zaidi ya kisiasa ndani ya serikali ya Iran, ambapo majenerali wake mara nyingi hushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kitaifa.
Pia imeingia katika miradi ya miundombinu na biashara kubwa, jambo linaloifanya iwe na mtandao mpana wa kifedha ndani ya nchi.
Kwa hiyo, IRGC imekuwa taasisi inayochanganya nguvu za kijeshi, kisiasa na kiuchumi kwa wakati mmoja.
Kuongezeka kwa ushawishi baada ya mashambulizi
Baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel, IRGC imeonekana kuimarisha nafasi yake zaidi ndani ya mfumo wa utawala. Viongozi wake wamekuwa wakihusika moja kwa moja katika mazungumzo ya kimataifa na maamuzi ya kijeshi.
Baadhi ya majenerali wake wamepata nafasi kubwa katika bunge na serikali, na wengine wamekuwa wakipewa nafasi za juu za ushawishi wa kisiasa. Hii inaonyesha jinsi taasisi hiyo ilivyopanua nguvu zake zaidi ya uwanja wa vita.
Aidha, uwepo wake umeimarika zaidi katika usalama wa taifa, ambapo sasa inaonekana kuwa na sauti kubwa kuliko taasisi nyingi za kiraia.
Wataalamu wanasema hali hii imeongezeka hasa baada ya shinikizo la kijeshi kutoka nje.
Je, kuna mabadiliko ya mfumo wa utawala?
Wachambuzi wengine wanaamini Iran inaweza kuingia katika mfumo ambapo jeshi, hasa IRGC, linakuwa na nguvu kubwa nyuma ya pazia la siasa. Hii inaweza kumaanisha kuwa jeshi litakuwa na "kura ya veto" juu ya maamuzi makubwa ya nchi bila kuchukua rasmi utawala.
Hata hivyo, wataalamu wengine wanasema bado ni mapema kuzungumzia mabadiliko ya utawala. Badala yake, wanasisitiza kuwa IRGC sasa imekuwa nguzo kuu ya kuendesha na kulinda mfumo wa Iran kuliko hapo awali.
Wengine wanailinganisha hali hiyo na nchi ambazo jeshi lina ushawishi mkubwa lakini si lazima lichukue moja kwa moja madaraka ya kisiasa.
Kwa sasa, mjadala bado unaendelea kuhusu mustakabali wa mfumo wa utawala wa Iran.