Kwanini uhusiano kati ya UAE na mataifa ya Kiarabu umezorota?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Falme za Kiarabu ni taifa la pili lenye idadi kubwa ya watu katika nchi za Kiarabu eneo la Ghuba baada ya Saudi Arabia, ikiwa na zaidi ya wakazi milioni 11.

Hata hivyo, 90% ya wakazi hao ni raia wa kigeni kutoka zaidi ya mataifa 200.

Wengi wa wahamiaji hao walikuja kufanya kazi na wanatokea mataifa ya India, Pakistan, na Bangladesh. Wahamiaji wa asilia ya Kihindi pekee ni 38.45% ya idadi ya watu wa nchini humo.

Idadi ya raia wa Emirati ni milioni 1.31 pekee, kulingana na takwimu za mwaka wa 2025. Wanaume ni 63.80% ya jumla ya idadi ya watu, huku wanawake wakiwa 36.20%. Hali hii imechangiwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wahamiaji wasioishi pamoja na familia zao.

Pato la kitaifa la Falme za Kiarabu, ambalo ni kiashiria cha ukubwa na ukuaji wa uchumi, linafikia dola bilioni 504.

Uchumi wa Falme za Kiarabu unategemea sana mafuta. Sekta hiyo inachangia 30% ya pato la taifa na 41% ya mapato yote ya serikali. Falme za Kiarabu huzalisha mapipa milioni 3.38 ya mafuta ghafi kwa siku na ina akiba iliyothibitishwa ya mapipa bilioni 113.

Abraham Accords

Mwaka 2020, Falme za Kiarabu ilitia Saini mkataba wa 'Abraham Accords' ili kurejesha na kuhalalisha uhusiano wake na Israel, pamoja na Bahrain, Morocco, na Sudan.

Falme za Kiarabu ilisema hatua hiyo ililenga "kuzuia Israel kutwaa eneo la Ukingo wa Magharibi na kuleta suluhu kati ya mataifa mawili ya Wapalestina na Israel."

Mahusiano kati ya Falme za Kiarabu na Israel yaliimarishwa baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya biashara huru mwaka wa 2022. Biashara ya mafuta kati ya nchi hizo mbili iliongezeka kutoka dola milioni 160 mwaka wa 2020 hadi dola bilioni 2.3 mwaka 2023.

Wakati vita vilianza eneo la Gaza, Falme za Kiarabu ililaani shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba mwaka wa 2023. Pia ilitoa wito wa "usitishaji wa mapigano wa haraka na wa kudumu."

Mahusiano na Iran

Falme za Kiarabu iliungana na Saudi Arabia, Bahrain na Misri katika kuisusia na kuiwekea vikwazo Qatar kuanzia mwaka 2017 hadi 2021, kwa madai ya "kuunga mkono na kufadhili ugaidi" na kuwa na "uhusiano wa karibu na Iran."

Falme za Kiarabu inadai umiliki wa visiwa vitatu katika Ghuba ya Uajemi vinavyodhibitiwa na Iran, Abu Musa, Greater Tunb na Lesser Tunb.

Umuhimu wa visiwa hivyo vidogo unatokana na eneo lao la kimkakati katika Mlango bahari wa Hormuz, ambako takriban robo ya biashara ya mafuta inayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani hupitia, pamoja na kiasi kikubwa cha gesi asilia iliyoyeyushwa na mbolea.

Falme za Kiarabu ndiyo taifa la Ghuba lenye uhusiano na ushirikiano mkubwa zaidi na Iran, kwani takwimu za mwaka 2023 na 2024 zinaonyesha kuwa UAE ni mshirika mkubwa zaidi wa biashara na Iran baada ya China, kulingana na takwimu zilizotolewa na Idara ya Forodha ya Iran.

Biashara kati ya nchi hizo mbili iliongezeka hadi dola bilioni 24 mwaka 2020/2021 kutoka dola bilioni 11.

Mamluki wa Yemen

Mwaka wa 2015, Falme za Kiarabu ilijiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen, dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Falme za Kiarabu imekuwa ikilengwa mara kwa mara na makombora ya wahouthi yanayodaiwa kutoka Iran.

Mwaka wa 2019, Falme za Kiarabu ilitangaza kuondoa majeshi yake kutoka Yemen. Hata hivyo, iliendelea kudumisha uwepo wa vikosi maalum,ili kupambana na ugaidi.

Uchunguzi wa BBC ulifichua kuwa UAE imekuwa ikiwaajiri mamluki wa Marekani tangu mwaka wa 2015 kutekeleza mauaji yaliyochochewa kisiasa nchini Yemen. Mauaji mengi yalilenga viongozi wa Islah Party, kundi la Kiislamu la Kisunni ambalo linatajwa kuwa tishio kwa familia tawala ya Abu Dhabi.

Falme za Kiarabu imekanusha kuwaua raia, ikisema operesheni zake zinawalenga wanachama wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda na Islamic State kusini mwa Yemen.

Lakini uchunguzi wa BBC ulifichua kuwa UAE imewaajiri baadhi ya wanachama wa zamani wa Al-Qaeda na ISIS ambao wameunda vikosi vyake vya usalama nchini Yemen.

Mapema mwaka huu, serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia iliishutumu UAE kwa kuendesha gereza la siri katika mji wa pwani wa Mukalla.

kutengwa kwa Bashar al-Assad

Mwaka wa 2011,muungano wa Arab League ulisitisha uanachama wa Syria na kuitaka serikali ya rais wa zamani Bashar al-Assad "kuwalinda raia" dhidi ya makundi yaliyojihami.

Saudi Arabia na Qatar zilikuwa miongoni mwa mataifa ya Kiarabu ambayo yalikuwa yakitaka Assad kuondolewa madarakani.

Lakini mwaka wa 2018, UAE ilifungua tena ubalozi wake mjini Damascus. Kiongozi wa nchi hiyo wakati huo, Mohammed bin Zayed Al Nahyan, alizungumza kwa njia ya simu na Bashar al-Assad mwezi Machi 2020 na kuwapa msaada kipindi cha janga la Covid 19.

kumuunga mkono Khalifa Haftar katika mzozo wa Libya.

Kufuatia kuuawa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mwaka wa 2011, nchi hiyo ilizama katika vita kati ya makundi mbalimbali yenye silaha.

Falme za Kiarabu ilikuwa miongoni mwa nchi za Kiarabu zilizoingilia kati ili kuunga mkono makundi yaliyojihami katika mgogoro wa kugombea madaraka.

Mwezi Agosti 2014, ndege za kivita za Falme za Kiarabu, zilitekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya Libya Dawn, katika uwanja wa ndege wa Benghazi. Vikosi vya Libya Dawn, vilivyokuwa vikiungwa mkono na vyama vya Kiislamu, vilikuwa vikipigana dhidi ya vikosi vya Khalifa Haftar, ambaye alikuwa akiungwa mkono na Falme za Kiarabu, Ufaransa na Urusi.

Falme za Kiarabu imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuhusika kwake kijeshi nchini Libya, ikisema kuwa inaunga mkono mchakato wa amani wa Umoja wa Mataifa.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan

Shirika la habari la Reuters, iliripoti kuwa Falme za Kiarabu imeanzisha kituo cha mafunzo ya kijeshi kwa maelfu ya wapiganaji wanaohusishwa na Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF)

Kituo hicho, kwa mujibu wa Reuters, kiko katika eneo la Benishangul-Gumuz, karibu na Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance, na inaaminika kufadhiliwa na Falme za Kiarabu.

Reuters inasema uchunguzi wake ulitegemea vyanzo vinane tofauti, uchambuzi wa picha za setilaiti, na nyaraka za siri za kidiplomasia zinazoashiria kuhusika kijeshi kwa UAE, katika kuunga mkono vikosi vya Rapid Support Forces. Hata hivyo, Abu Dhabi imekanusha kuhusika na vita vya Sudan.

Somalia na Israel

Mwezi Januari, serikali ya Somalia ilitangaza kusitisha makubaliano ya ushirikiano wa usalama na usimamizi wa bandari ambayo ilikuwa imeafikiana na Falme za Kiarabu.

Katika hotuba ya televisheni, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliishutumu Abu Dhabi kwa "kukiuka uhuru wa taifa lake."

Hatua hii inakuja baada ya utambuzi wa Somaliland na Israel kama taifa huru, hatua ambayo serikali ya Mogadishu inaiona kama ukiukaji wa uhuru wake kama taifa.

Somalia inaamini kuwa Falme za Kiarabu ilihusika pakubwa katika hatua iliyochukuliwa na serikali ya Benjamin Netanyahu.

Mwezi Disemba mwaka uliopita, Israel ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuitambua Somaliland kama taifa huru.

Mzozo na Algeria

Mvutano kati ya Algeria na Falme za Kiarabu umeendelea kujirudia tangu kujiuzulu kwa Rais Abdelaziz Bouteflika, ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa UAE.

Algeria ilitangaza kusitisha makubaliano yake ya huduma za anga na Abu Dhabi baada ya Rais Abdelmadjid Tebboune kuishutumu UAE kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake.

Mahusiano kati ya nchi hizo mbili yamekuwa ya mvutano baada ya Abu Dhabi kumuunga mkono Khalifa Haftar kusini mwa Libya, pamoja na uhusiano wa UAE na nchi kadhaa eneo la Sahel.

Algeria pia inaamini kuwa UAE inashirikiana na Morocco na Israel "kuunga mkono na kufadhili" harakati ya kujitenga ya kundi la Waberber inayojulikana kama Movement for the Autonomy of Kabylie, ambayo inadai uhuru wa eneo la Kabylie kutoka Algeria.

Mamlaka za Algeria limetaja kundi hilo kuwa la kigaidi.