Je, Saudi Arabia inanufaika na vita vya Iran?

Chanzo cha picha, Reuters
Kampuni ya mafuta ya Saudi Aramco imetangaza kuwa faida yake katika robo ya pili ya mwaka 2026 ilifikia kiwango cha juu zaidi tangu mwaka 2022, licha ya mzozo unaoendelea katika eneo la mashariki ya kati kutokana na vita Iran vilivyoathiri usafiri wa majini katika Ghuba ya Uajemi.
Faida hii ilirekodiwa wakati ambapo uzalishaji na usafirishaji wa mafuta wa Saudi Arabia umepungua, na sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya nchi hiyo imeelekezwa kwenye njia ya Bahari ya Shamu.
Faida ya Aramco kwa robo hiyo pia ilizidi dola bilioni 33, ikiwa ni ongezeko la takriban theluthi moja ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, faida ya kampuni hiyo iliongezeka kwa asilimia 44.
Takwimu hizo mbili zinatokana na vigezo tofauti, lakini zote zinaashiria ongezeko kubwa la faida ya Aramco.
Ongezeko hili la faida sambamba na vita vya Iran kunazua swali iwapo utendaji wa kampuni kubwa zaidi ya mafuta duniani unaonyesha kuwa serikali ya Saudi Arabia imefaidika kutokana na vita hivyo, na iwapo taarifa za kifedha za Aramco zinaakisi kwa usahihi hali ya uchumi wa Saudi Arabia.
Kwa nini faida ya Aramco iliongezeka sana licha ya kushuka kwa uzalishaji?

Chanzo cha picha, Reuters
Uzalishaji wa mafuta na gesi wa Aramco katika robo ya pili ya mwaka 2026 ulikuwa chini kwa takriban asilimia 25 ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka uliopita, lakini bei ya mafuta iliyouzwa na kampuni hiyo ilipanda kwa zaidi ya asilimia 60, na mapato kutokana na ongezeko hili la bei yalifidia athari za kupungua kwa uzalishaji na mauzo ya nje.
Carol Nakhleh, mchumi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ushauri ya Crystal Energy, aliambia BBC Idhaa ya Kiajemi kwamba kampuni hiyo kubwa ya mafuta ya Saudi Arabia si kampuni pekee iliyonufaika na hali hii. "Aramco, kama kampuni nyingine yoyote ya mafuta ambayo imeendelea kusambaza bidhaa katika masoko ya kimataifa wakati wa mivutano ya hivi karibuni, imenufaika na ongezeko la bei ya mafuta," alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bi. Nakhleh anasema kuwa gharama nafuu ya uchimbaji wa mafuta pia imekuwa na umuhimu mkubwa kwa Aramco: "Kwa mzalishaji mwenye gharama nafuu kama Aramco, kupanda kwa bei sio tu kunafidia kikamilifu athari mbaya za kupungua kwa uzalishaji na mauzo ya nje, bali pia kunazalisha mapato zaidi."
Katika ripoti yake ya kifedha, Aramco pia ilitaja ongezeko la bei ya mafuta ghafi, bidhaa za petroli, na bidhaa za kemikali kama sababu kuu ya ukuaji wa faida.
Kitengo cha usafishaji na uuzaji cha Aramco pia kimenufaika na bei ya juu ya bidhaa kama vile dizeli na mafuta ya ndege pamoja na kuboreka kwa faida katika shughuli za usafishaji.
Faida yake ya uendeshaji ilikaribia kuongezeka maradufu, na mtandao wa Aramco wa viwanda vya kusafisha mafuta, mitambo ya kemikali za petroli, maghala na shughuli za biashara ndani na nje ya Saudi Arabia umeiwezesha kampuni hiyo kubwa ya nishati kupata mapato zaidi kutokana na bei ya juu ya bidhaa za mafuta.
Ongezeko hili la mapato halikuishia kwa Aramco pekee. Wakati matokeo ya robo mwaka ya Aramco yakitangazwa, kampuni ya BP nayo iliripoti faida ya dola bilioni 73.5 katika robo ya pili ya mwaka 2026—kiasi kinachozidi mara mbili ya faida ya kipindi kama hicho mwaka uliopita na kuwa faida ya juu zaidi ya robo mwaka kwa kampuni hiyo tangu mwaka 2022.
Kampuni za ExxonMobil, Chevron na Shell nazo ziliripoti faida kubwa zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hata hivyo, sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya Aramco kwa kawaida hupitia njia iliyoathiriwa moja kwa moja na vita.
Wataalamu wanasema kuwa ongezeko kubwa la faida katika robo mwaka moja halimaanishi kuwa mwenendo huo utaendelea katika miezi ijayo. Kurejea kwa usafirishaji wa bidhaa kupitia Lango la Hormuz kunaweza kupunguza bei ya mafuta, huku kuongezeka kwa mgogoro—ingawa kuna uwezekano wa kupandisha bei ya mafuta—kukweza pia kuathiri zaidi mauzo ya nje ya Aramco.
Je, Bomba la Mashariki-Magharibi lilipunguza vipi shinikizo kwenye mauzo ya nje?

Chanzo cha picha, Gallo Images/Orbital Horizon/Copernicus Sentinel Data 2026 via Getty Images
Mojawapo ya mambo yaliyoisaidia Aramco kuendelea na usafirishaji wa mafuta nje ya nchi ni Bomba la Mafuta la Mashariki-Magharibi, ambalo husafirisha mafuta kutoka kituo cha Abqaiq mashariki mwa Saudi Arabia hadi bandari ya Yanbu iliyopo pwani ya Bahari ya Shamu.
Carol Nakhleh aliambia BBC kuwa bomba hilo linaipa Saudi Arabia fursa nzuri zaidi kuliko baadhi ya majirani zake: "Saudi Arabia inaweza kusafirisha sehemu kubwa ya mafuta yake ghafi kwenda Bahari ya Shamu kupitia bomba la Mashariki-Magharibi na kupunguza utegemezi wake kwa Lango la Hormuz; ingawa haiwezi kuepuka kabisa utegemezi huo."
Nchi kama Iraq na Kuwait zina njia chache mbadala na ziko katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na usumbufu katika usafirishaji wa baharini.
Bomba la Mashariki-Magharibi, lenye uwezo wa kusafirisha takriban mapipa milioni tano kwa siku, likawa njia muhimu mbadala kwa Aramco wakati wa vita vya Iran na migogoro ya Mashariki ya Kati. Kulingana na gazeti la New York Times, Saudi Arabia ilielekeza zaidi ya asilimia 70 ya usafirishaji wake wa mafuta kwenye njia hiyo baada ya vita kuanza.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aramco, Amin Nasser, alisema baada ya kampuni hiyo kutoa taarifa zake za kifedha kwamba uwezo wake wa kuhifadhi mafuta, vituo vingi vya kusafirisha mafuta, na bomba la mashariki-magharibi kuelekea bandari ya Yanbu vilikuwa vimewezesha Aramco kuendelea na shughuli zake.
Alisema kampuni hiyo iliendeleza shughuli zake "licha ya usumbufu usio na kifani katika usambazaji wa mafuta kupitia Mlango wa Bahari la Hormuz" kwa kutegemea rasilimali zake mbalimbali na "mipango yake ya miongo kadhaa."
Hata hivyo, bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi halina uwezo wa kusafirisha kiasi chote cha mafuta kilichokuwa kikisafirishwa kutoka Ghuba ya Uajemi kabla ya vita, na sehemu ya uwezo wake hutumika kusambaza mafuta kwa viwanda vya kusafisha mafuta vilivyoko magharibi mwa Saudi Arabia. Kupungua kwa uzalishaji wa Aramco katika robo ya pili ya mwaka kulionyesha mapungufu ya njia hii mbadala. Ingawa bomba hilo lilipunguza ukubwa wa athari za usumbufu huo, halikuondoa utegemezi wa Saudi Arabia kwa usalama wa njia za maji katika eneo hilo.
Mnamo mwezi Julai, tishio hilo lilienea hadi Bahari ya Shamu. Kundi la Houthi la Yemen lilitangaza kuzuia meli za Saudi Arabia na kufanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Saudi Arabia katika bandari mbili za pwani.
Aramco ilisema inaweza kushughulikia kwa haraka usumbufu huo, lakini matukio hayo yalionyesha kuwa kuhamisha usafirishaji wa mafuta ili kuepuka Lango la Hormuz hakukuondoa kabisa mafuta ya Saudi Arabia katika eneo la vita.
Shirika la Fedha Duniani (IMF) pia limeeleza kuwa hatua ya Saudi Arabia ya kuboresha na kuongeza aina mbalimbali za miundombinu ya mafuta na usafirishaji imechangia katika uwezo wake wa kuhimili usumbufu huo.
Shirika hilo lilisema kuwa usafirishaji wa haraka wa mafuta kupitia bomba la Mashariki-Magharibi na bandari za Bahari ya Shamu, pamoja na matumizi ya akiba ya fedha za kigeni na Aramco, vilisaidia kupunguza kushuka kwa mauzo ya mafuta nje ya nchi, mchanganyiko wa mambo haya pia unaonekana katika taarifa za kifedha za Aramco.
Je, ongezeko kubwa la faida ya Aramco ni kielelezo cha hali ya uchumi wa Saudi Arabia?
Kuongezeka kwa faida ya Aramco kunaathiri moja kwa moja mapato ya serikali ya Saudi Arabia, kwani serikali na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa nchi hiyo ndio inaomiliki karibu hisa zote za kampuni hiyo. Aramco iliidhinisha mgao wa msingi wa takriban dola bilioni 22 kwa robo ya pili, ambapo sehemu kubwa huenda kwa serikali na mfuko huo, hivyo kutoa rasilimali za ziada kwa bajeti ya umma na miradi mikubwa ya Saudi Arabia.
Hata hivyo, wakati faida ya Aramco ikiongezeka kwa kasi, uchumi wa Saudi Arabia umepungua. Makadirio ya awali ya Ofisi Kuu ya Takwimu ya nchi hiyo yanaonyesha kuwa Pato la Taifa (GDP) lilipungua kwa karibu asilimia 5 katika robo ya pili ikilinganishwa na mwaka uliopita. Shughuli zinazohusiana na mafuta zilipungua kwa takriban asilimia 25, na sekta isiyo ya mafuta haikuonyesha ukuaji mkubwa.
Kuongezeka kwa faida ya Aramco hakumaanishi uchumi wa Saudi Arabia pia unakua. Kupanda kwa bei ya mafuta kuliimarisha mapato ya Aramco, huku Pato la Taifa la nchi hiyo likitegemea zaidi kiasi cha bidhaa na huduma zinazozalishwa.
Aramco inaweza kupata pesa zaidi kwa kuuza mafuta kwa bei ya juu, lakini kupungua kwa uchimbaji na mauzo ya nje kutapunguza ukubwa wa sekta ya mafuta katika uchumi wa Saudi Arabia. Gharama zilizoongezeka za bima, usafirishaji na ulinzi wa njia za usafirishaji wa bidhaa nje wakati wa vita pia zitachukua sehemu ya mapato hayo ya ziada.
Athari ya vita haishuhudiwi na sekta ya mafuta pekee. Mpango wa "Vision 2030" wa Saudi Arabia unategemea kuvutia uwekezaji wa kigeni, kuendeleza utalii na kupanua shughuli zisizo za mafuta. Sekta hizi hutegemea zaidi utulivu wa kikanda na uwezo wa kupanga mipango ya muda mrefu kuliko mapato ya mafuta. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linasema kuwa vita vimeathiri biashara, shughuli zisizo za mafuta na imani ya wawekezaji, na kuendelea kwa vita hivyo kunaweza kudhoofisha ukuaji na uwekezaji katika miaka ijayo.
"Ni upotoshaji kuashiria kuwa Saudi Arabia imefaidika na mgogoro huo kwa sababu tu faida ya Aramco imeongezeka," anasema Bi. Nakhleh. Anasema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kwa muda mfupi kumeongeza mapato ya wazalishaji ambao wameweza kuendelea kuuza bidhaa nje, lakini kuendelea kwa ukosefu wa utulivu kunaweza kuchochea vitisho vya kiusalama, kuwakatisha tamaa wawekezaji na kufanya mazingira ya biashara kutotabirika zaidi.
Matokeo ya robo ya pili yanaonyesha kuwa kupanda kwa bei ya mafuta na kuhamisha sehemu kubwa ya mauzo ya nje kupitia bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi kumefidia kupungua kwa uzalishaji na mauzo ya nje na kuongeza faida ya Aramco. Hata hivyo, katika kipindi hicho hicho, uzalishaji wa mafuta na uchumi wa Saudi Arabia vilipungua, huku hatari kwa njia zake za biashara na mipango isiyohusisha mafuta ikiongezeka. "Aramco inaweza kufaidika na bei ya juu ya mafuta kwa muda mfupi, lakini Saudi Arabia ingefaidika zaidi na utulivu wa kikanda kuliko kipindi kirefu cha vita," anasema Bi. Nakhleh.















