Moja kwa moja, Iran yaweka masharti ya kufungua Mlango wa Hormuz

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema Tehran bado haijapokea majibu rasmi kutoka Washington kupitia wapatanishi.

Muhtasari

  • Tetesi za soka Ulaya: Barcelona yamtaka Haaland
  • Iran yaweka masharti ya kufungua Mlango wa Hormuz

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliuaula

  1. Tetesi za Soka Ulaya Jumapili: Barcelona yamtaka Haaland

    ,

    Barcelona inaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Norway, Erling Haaland, huku ikitarajia mchezaji huyo mwenye miaka 26 kuwa chaguo lao namba moja katika dirisha la usajili la majira ya joto. (El Nacional)

    Real Madrid imesema Trent Alexander-Arnold, mwenye miaka 27, hana mpango wa kuondoka klabuni hapo, licha ya Arsenal na Liverpool kuonyesha nia ya kumsajili beki huyo wa England (TeamTalk)

    Manchester United inamfuatilia kwa karibu beki wa kushoto wa Hispania, Alejandro Balde, mwenye miaka 22, ambaye huenda akaondoka Barcelona mwezi Januari (Mundo Deportivo).

    Bayern Munich iko tayari kutoa ofa ya pauni milioni 69 kumsajili mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Dani Olmo, mwenye miaka 28. (Sport)

    Liverpool na Manchester United zote zinamvizia beki wa Uholanzi Micky van de Ven, lakini itahitaji kiasi kikubwa cha fedha kuishawishi Tottenham kumuuza mchezaji huyo mwenye miaka 25 (Caught Offside).

    Beki Fikayo Tomori, mwenye miaka 28, na kiungo Ruben Loftus-Cheek, mwenye miaka 30, wanatarajiwa kuondoka AC Milan mwakani baada ya mikataba yao kumalizika Juni (Gazzetta - kwa Kiitalia).

    Bayern Munich inamuwania pia beki wa Ureno wa Benfica, Tomas Araujo, mwenye miaka 24 (Bild)

    AS Roma inatarajiwa kuongeza mara mbili bei ya kiungo wake Manu Kone hadi pauni milioni 86 mwezi Januari, baada ya Chelsea kuripotiwa kukataa nafasi ya kumsajili mchezaji huyo wa Ufaransa kwa pauni milioni 43 katika dirisha la usajili la majira ya joto. (La Gazzetta dello Sport)

    Beki wa Real Madrid, Raul Asencio, mwenye miaka 23, alipokea ofa tatu kubwa wakati wa dirisha la usajili la majira ya joto, zikiwemo kutoka Chelsea na Liverpool, lakini akaamua kubaki klabuni hapo. (Marca)

    Beki wa Hispania Alex Jimenez, mwenye miaka 21, amejiunga kwa mkopo Fiorentina kutoka Bournemouth, huku mkataba huo ukiipa klabu hiyo ya Italia chaguo la kumsajili kwa pauni milioni 17. (Tuttomercatoweb)

  2. Iran yaweka masharti ya kufungua Mlango wa Hormuz

    .

    Iran imesema suluhisho la mazungumzo pekee ndilo linaloweza kusababisha kufunguliwa tena kwa Mlango bahari wa Hormuz, siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema amekataa pendekezo la Iran la kufungua njia hiyo ya majini ndani ya wiki moja.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema Tehran bado haijapokea majibu rasmi kutoka Washington kupitia wapatanishi.

    Trump amesema Iran ilitoa pendekezo hilo kwa sababu inaona inapoteza vita.

    Hata hivyo, Araqchi amesema Iran haitarejea nyuma kuhusu masharti iliyoweka katika pendekezo hilo.

    Miongoni mwa masharti hayo ni kusitishwa kwa uhasama wote katika eneo hilo, ikiwemo mzozo unaoendelea nchini Lebanon, pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

    Wakati huohuo, mamlaka za Iran zimeonya meli kutotumia njia ambazo zimezieleza kuwa "hazijaidhinishwa" kupita katika Mlango wa Hormuz.

    Mlango huo ni njia muhimu ya majini kwa usafirishaji wa mafuta duniani, huku sehemu kubwa ya mafuta na gesi inayosafirishwa kimataifa ikipitia katika eneo hilo.

  3. Salamu na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Septemba 27, 2026