Wachezaji wa Ireland wakataa kusalimiana na timu ya Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha wa Jamhuri ya Ireland, Heimir Hallgrímsson, amesema wachezaji wake walivutia hisia duniani baada ya kukataa kutekeleza baadhi ya taratibu za kawaida kabla ya mechi yao dhidi ya Israel.
Kabla ya mchezo huo uliochezwa Hungary na kumalizika kwa ushindi wa mabao 3-0 kwa Ireland, wachezaji wa Jamhuri ya Ireland na Israel hawakusalimiana kwa kupeana mikono. Aidha, wachezaji wa Ireland waliinamisha vichwa vyao wakati wimbo wa taifa wa Israel ukipigwa.
Nahodha wa Ireland, Dara O'Shea, na mwenzake wa Israel, Manor Solomon, pia hawakusalimiana kabla ya mechi, huku timu hizo mbili zikikosa kubadilishana bendera za kumbukumbu kama ilivyo kawaida.
Tangu droo ya Kundi B3 ilipofanyika mwezi Februari, mechi kati ya timu hizo zimezua mjadala kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Gaza.
Awali, baadhi ya wachezaji wa Ireland walikabiliwa na wito wa kujiondoa kwenye mashindano hayo, huku kampeni ya "Stop the Game", iliyoandaliwa na kundi la Irish Sport for Palestine, ikipata uungwaji mkono mkubwa katika wiki za hivi karibuni.
Pia unaweza kusoma:





















