Harvard yafichua siri rahisi ya kuishi maisha marefu

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Wataalamu wametumia muda mrefu kufuatilia kwa kina undani wa jambo hili

.

Linapokuja suala la afya, si teknolojia mpya, virutubisho au uanachama wa gym wa gharama kubwa unaoweza kuwa na athari kubwa zaidi kwa afya yako kwa muda mrefu. Badala yake, kuna jambo rahisi zaidi na la gharama nafuu zaidi: kuwa na mahusiano na watu wengine.

Kitendo cha msingi cha kujenga uhusiano na binadamu wengine kinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa si tu muda wa maisha yako, bali muhimu zaidi, kinaweza kuongeza idadi ya miaka utakayoishi ukiwa na afya njema. Mahusiano mazuri ya kijamii yanaweza kukusaidia kuishi maisha bora kwa muda mrefu, na kuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha hilo.

Uchambuzi wa tafiti 148 uliochapishwa mwaka 2019, uliowahusisha zaidi ya watu 300,000, ulibaini kuwa watu wenye mahusiano imara ya kijamii wana uwezekano mkubwa kwa asilimia 50 wa kuishi zaidi ikilinganishwa na wale wasio na mahusiano hayo.

.
Maelezo ya picha, Kuweka ratiba ya shughuli za kijamii za mara kwa mara, kama vile kucheza michezo pamoja na marafiki, kunaweza kusaidia kudumisha mahusiano muhimu.

Inaaminika kuwa kuwa na kundi la watu wa karibu kunaweza kuwa na athari ya kinga kiafya inayolingana au hata kuwa kubwa zaidi kuliko baadhi ya vihatarishi vinavyojulikana vya vifo, ikiwemo uvutaji sigara, unywaji pombe na maisha ya kukaa bila kufanya mazoezi.

Kwa upande mwingine, kutengwa na jamii kwa muda mrefu kunaweza kuwa na athari inayolinganishwa na kuvuta sigara 15 kwa siku, kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Kuzeeka nchini Marekani (National Institute on Aging), na kunaweza kupunguza muda wa maisha kwa miaka 15.

"Binadamu kimsingi ni viumbe wa kijamii, hivyo ubongo na miili yetu imeundwa ili kuungana na wengine na kujiona kuwa sehemu ya makundi ya kijamii – kama familia, vikundi vya kazini, vikundi vya shughuli tunazopenda na mengine," anasema Profesa Tegan Cruwys, mtafiti na mwanasaikolojia wa tiba katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia mjini Canberra.

Watu wanawahitaji watu

Mahusiano ya kijamii si jambo la ziada tu – ni hitaji la kibayolojia kwa afya na yanaweza kubadilisha hali ya mwili wako mara moja.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Mtu anapohisi kuwa ana uhusiano salama na wengine, mwitikio wa mwili dhidi ya msongo wa mawazo hutulia, kiwango cha homoni ya cortisol hushuka, na hali ya 'pigana au kimbia' inayochangia kwa kiasi kikubwa wasiwasi huanza kupungua," anasema Dkt Ahmed Shoka, daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Medical Express Clinic mjini London.

"Uhusiano chanya, iwe ni kukumbatiana, kutazamana machoni, kucheka pamoja au hata kupiga simu, huongeza oxytocin, ambayo husaidia kujenga uaminifu na kuufanya mfumo wa fahamu kuingia katika hali ya kupumzika na kumeng'enya chakula."

Takwimu nyingi zinaonyesha kuwa athari chanya ya mwingiliano wa kijamii katika kudhibiti msongo wa mawazo wa muda mrefu ni miongoni mwa sababu kuu zinazofanya mahusiano yawe na mchango mkubwa katika muda ambao mtu anaweza kuishi akiwa na afya njema. Tafiti zimeonyesha uhusiano kati ya matatizo yanayosababishwa na msongo wa mawazo na kuongezeka kwa hatari ya kifo kutokana na sababu mbalimbali.

Hata hivyo, kuhisi uko salama katika mahusiano yako ya karibu kunaonekana kusaidia kupunguza mwitikio wa mwili dhidi ya msongo wa mawazo, anasema Profesa Robert J Waldinger, profesa wa magonjwa ya akili katika Shule ya Tiba ya Harvard na mkurugenzi wa Harvard Study of Adult Development.

"Watu wanaohisi kuwa wako salama, kwa maana kwamba wanaweza kuwategemea wengine wakati wa mahitaji, huonyesha dalili chache za msongo wa mawazo wa muda mrefu. Kinyume chake, upweke wa muda mrefu huufanya mfumo wa mwili wa kutambua vitisho ubaki katika hali ya tahadhari kwa muda mrefu – hali inayofanana na aina nyingine za msongo wa mawazo wa muda mrefu," anasema.

Mahusiano imara ya kijamii yamehusishwa na maboresho mbalimbali katika viashiria muhimu vya afya, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa viwango vya kisukari na kupungua kwa kasi ya kudhoofika kwa uwezo wa kufikiri kadiri mtu anavyozeeka. Kwa mujibu wa Shoka, watu walio na mahusiano mazuri ya kijamii huwa na shinikizo la damu la chini na viwango vidogo vya uvimbe mwilini, huku kutengwa na jamii kukihusishwa na kuzeeka kwa mwili kwa kasi zaidi, ikiwa ni pamoja na kudhoofika kwa mfumo wa kinga.

Aidha, tafiti zinaonyesha kuwa kushiriki katika shughuli za kijamii kunaweza kuboresha afya ya ubongo kwa watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa wa shida ya akili.

"Mahusiano mazuri, kwa namna fulani, hufanya kazi kama dawa ya muda mrefu ya kupunguza msongo wa mawazo," anasema Shoka.

.
Maelezo ya picha, Mahusiano machache ya karibu na yenye kina yana thamani kubwa zaidi kuliko mahusiano mengi yasiyo na kina.

"Kwa upande wangu kama daktari anayewahudumia wagonjwa, faida za afya ya akili pia ni kubwa: watu walio na mahusiano thabiti na ya kuaminika hupona vizuri zaidi na huwa na uwezekano mdogo wa kurejea katika hali ya awali," anasema.

Kwa upande mwingine, watu wanaohisi kutengwa au kuwa wapweke huwa na furaha kidogo, hasa wanapozeeka. Harvard Study of Adult Development imewafuatilia wanaume 724 pamoja na vizazi vyao tangu mwaka 1938, kwa lengo la kubaini mambo yanayoweza kuchangia maisha marefu.

Moja ya matokeo yake makuu ni uhusiano kati ya mahusiano mazuri na maisha marefu. Washiriki waliokuwa na afya bora zaidi walipofikisha umri wa miaka 80 hawakuwa wale waliokuwa wamejikusanyia mali nyingi zaidi au walioonekana kuwa wamefanikiwa zaidi, bali wale ambao waliridhika na mahusiano yao tangu walipokuwa na umri wa miaka 50.

"Utafiti wetu, pamoja na tafiti nyingine, umeonyesha kuwa watu wanaohisi wametengwa zaidi kuliko wanavyotamani huwa na furaha kidogo, afya zao hudhoofika mapema katika umri wa kati, uwezo wao wa ubongo hupungua mapema na huishi maisha mafupi zaidi kuliko watu ambao hawana upweke," anasema Waldinger.

Anasema upweke hufanya kazi kama hatari ya kiafya inayojengeka taratibu, na si tu hali ya kihisia. "Kwa muda mfupi, kutokuwa na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu kunahusishwa na hali mbaya ya hisia, kuvurugika kwa usingizi na kuongezeka kwa mwitikio wa msongo wa mawazo. Kwa muda mrefu, takwimu za utafiti zinahusisha kutengwa kwa muda mrefu na kudhoofika mapema kimwili, kupungua mapema kwa uwezo wa utambuzi na maisha mafupi."

Kukabiliana na janga la upweke

Tatizo ni kwamba, licha ya kuwa ni rahisi zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuwasiliana na watu wengine, wengi wetu tunapata changamoto ya kuwa na mwingiliano wa kijamii wenye maana. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa mtu mmoja kati ya watu wazima watatu wenye umri mkubwa na kijana mmoja kati ya wanne huathiriwa na kutengwa na jamii, huku watu kutoka makundi madogo katika jamii mara nyingi wakikabiliwa na vikwazo zaidi katika kuungana na wengine.

"Jamii yetu imebadilika kwa namna ambayo imepunguza ulazima wa kuingiliana na watu wengine," anasema Dkt Gillian Sandstrom, mwandishi na profesa msaidizi wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Sussex.

Tunafanya kazi kwa njia ya mtandao. Tunachagua kujihudumia wenyewe tunapokwenda dukani au tunaamua kutokwenda kabisa na badala yake kuagiza bidhaa mtandaoni. Tunatazama mitandao ya kijamii wakati tungeweza kuwa tunasimulia siku yetu kwa mtu tunayempenda.

.
Maelezo ya picha, Kujiunga na kikundi, kama vile kwaya, kunaweza kukusaidia kutenga muda kwa ajili ya kushirikiana na watu wengine.

"Kuendelea kuepuka mwingiliano huu mdogo mdogo hujikusanya na hatimaye kutengeneza maisha ambayo yanaweza kuwa na usumbufu mdogo, lakini pia yakawa na utajiri mdogo, uzoefu tofauti kidogo na maisha yasiyo na kina," anasema Sandstrom.

Si suala la kuhitaji tu mwingiliano wa kijamii wa mara kwa mara, ingawa wengi wetu tunahitaji hilo – tunahitaji pia mahusiano yenye kutosheleza.

"Utafiti wetu unaonyesha kwamba si kuwa tu karibu na watu wengine ndiko kunakokuwa na umuhimu – bali ni kuhisi umeunganishwa nao kisaikolojia na kuwa sehemu ya makundi yenye maana ambayo hutoa manufaa makubwa zaidi kwa afya ya akili na ustawi," anasema Cruwys.

Shoka anashauri kuzingatia ubora badala ya wingi. "Mahusiano machache ya karibu na ya kuaminika pamoja na jamii ambayo unahisi kwa dhati kuwa wewe ni sehemu yake huwa na kinga kubwa zaidi kuliko kuwa na mtandao mkubwa wa watu unaowafahamu juu juu," anasema.

Hata hivyo, mawasiliano madogo ya kila siku yana umuhimu mkubwa kuliko tunavyoweza kufikiria.

"Kuongea na jirani, kutazamana machoni, kumshukuru mtu au kumsaidia mtu. Kila moja ya mambo haya ni ishara fupi ya kumfanya mtu ajisikie kuwa sehemu ya jamii."

Kujiunga na kundi au jamii, iwe ni kwaya, timu ya michezo au klabu ya vitabu, kunaweza kusaidia kujenga hali ya kuwa sehemu ya jamii. Kwa mujibu wa Cruwys, hilo linaweza kuwezesha baadhi ya manufaa makubwa zaidi.

"Kama tayari huna mtandao imara wa kijamii, anza kidogo na uchague shughuli zinazohusisha kukutana mara kwa mara na watu wale wale kuhusu jambo au lengo mnaloishirikiana," anasema.

"Kwa sababu ni utambulisho unaoshirikishwa, na si tu mawasiliano ya kijamii, ambao una uwezekano mkubwa wa kujenga urafiki wa kudumu na afya bora."

Inaweza kuonekana kuwa jambo kubwa kujaribu kupanua mduara wako wa kijamii – hasa ikiwa shughuli za makundi katika eneo lako ni chache. Sandstrom anasema baadhi ya watu ni rahisi kuzungumza nao wakati unapoanza kujenga ujasiri.

"Watu wenye mbwa wamezoea watu wengine kuingiliana nao, huku wahudumu wa huduma mbalimbali wakiwa wamefundishwa kuzungumza kwa urafiki na wateja."

Huenda jambo bora zaidi unaloweza kufanya ili kuimarisha ustawi wako wa kijamii ni kuwa na mpango na kuchukua hatua katika mahusiano yako.

"Tunaweka ratiba ya kufanya mazoezi na kupanga milo, lakini tunaacha mahusiano yatokee tu yenyewe," anasema Shoka.

Anashauri kupanga muda wa kuwasiliana na watu mara kwa mara na kuulinda muda huo kama unavyolinda muda wa kulala au wa kutekeleza majukumu ya kazi.

"Uhusiano wa kidijitali una nafasi muhimu, hasa kwa watu wanaokabiliana na ugonjwa, ulemavu au kutengwa na jamii, lakini manufaa makubwa zaidi bado hupatikana tunapokuwa pamoja ana kwa ana."

Hata hivyo, Cruwys anasisitiza kwamba jukumu la kukabiliana na tatizo la upweke haliwezi kuwa la watu wanaopitia hali hiyo pekee.

"Ni jukumu la kila mmoja wetu kujenga jamii zinazowajumuisha wote, ambako sote tunaweza kupata manufaa ya kiafya."