Je, China inaweza kusaidia kumaliza vita kati ya Marekani na Iran?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ingawa matarajio ya mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran bado hayana uhakika, China polepole inaibuka kuwa mpatanishi mwenye nguvu anayefanya kazi kwa siri, huku Washington na Tehran zote zikitafuta upatanishi wa Beijing ili kumaliza vita.
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, mjini Beijing tarehe 6 Mei, wakati Washington ilipowasilisha pendekezo jipya la amani, ilitafsiriwa na wachambuzi kama jaribio la kupata uungwaji mkono wa China kwa mazungumzo hayo.
Suala la Iran linatarajiwa kuwa moja ya ajenda kuu katika ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump, nchini China na mkutano wake na Rais Xi Jinping tarehe 14 na 15 Mei.
Kwa mtazamo wa juu juu, Beijing inaweza kutumia ushawishi wake nchini Iran kusaidia kufanikisha makubaliano ya kina na ya kudumu, kama ilivyofanya katika mazungumzo ya Islamabad, kwa kuishinikiza Tehran kukubali kusitisha mapigano, jambo ambalo licha ya kuwa dhaifu sana bado linaendelea.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa China wamepunguza uzito wa nafasi ya Beijing, wakielekeza kwenye kusita kwa pande zote kufanya maridhiano pamoja na tofauti zilizopo ndani ya uongozi wa Iran.
Msimamo wa China kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na Mlango wa Hormuz ni upi?
Wakati huo huo wa mkutano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China, Abbas Araghchi na Wang Yi, uliofanyika tarehe 6 Mei, Marekani iliwasilisha rasimu yenye vipengele 14 iliyolenga kumaliza rasmi vita na kuweka mfumo wa muda mrefu wa mazungumzo.
Ingawa Donald Trump alisema makubaliano yako karibu kufikiwa, vyombo vya habari vya China vilinukuu vyanzo vya Iran vikisema kuwa Tehran bado haijajibu rasmi pendekezo jipya la Marekani, kwa kuwa inaona baadhi ya vipengele vyake kuwa "havikubaliki."
Mpango wa nyuklia wa Iran bado ni moja ya maeneo makuu ya kutokubaliana kati ya pande hizo mbili, huku kila upande ukipendekeza ratiba tofauti za kusimamisha urutubishaji wa urani wa Iran, pamoja na kuhamisha akiba yake ya urani iliyoboreshwa kwa kiwango cha juu kwenda nje ya nchi, jambo ambalo Tehran imewahi kulikataa hapo awali.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Beijing imeendelea kuwa na msimamo wa utulivu kuhusu suala la nyuklia. Wang Yi alisema katika mkutano wake na Abbas Araghchi kwamba China inaheshimu ahadi ya Iran ya kutotengeneza silaha za nyuklia, lakini pia inaamini kuwa Iran ina haki halali ya kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani.
Kuhusu kufunguliwa tena kwa Mlango bahari wa Hormuz, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilizitaka pande husika "kujibu haraka matakwa makubwa ya jumuiya ya kimataifa" na kurejesha "upitaji na usafiri wa kawaida na salama" kupitia njia hiyo ya maji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alisema kuwa suala la Mlango bahari wa Hormuz linaweza "kutatuliwa haraka," kauli ambayo ilionekana kama ishara kwamba Tehran iko tayari kufungua tena njia hiyo ya baharini.
Inaonekana pia kwamba Marekani imepunguza kwa kiasi fulani msimamo wake mkali, na imependekeza kuwa hati ya makubaliano ijumuishwe kuondolewa kwa mzingiro wa majini mara tu Iran itakapofungua tena Mlango bahari wa Hormuz.
China ina ushawishi gani kwa Iran?

Chanzo cha picha, IRANIAN FOREIGN MINISTRY OFFICE HANDOUT/EPA/Shutterstock
Ziara za Abbas Araghchi na Donald Trump nchini China zinaonesha kuwa nchi hiyo inazidi kuwa mpatanishi muhimu mwenye msimamo tofauti, kutokana na ushawishi wake maalum mjini Tehran.
Inakadiriwa kuwa kabla ya vita, China ilikuwa ikiagiza kwa njia isiyo rasmi asilimia 80 hadi 90 ya mafuta yote yaliyouzwa nje na Iran, kupitia "meli za siri" na viwanda binafsi vya kusafisha mafuta vinavyojulikana kama "teapots," na iliendelea kutoa msaada wa kifedha kwa Iran.
Hivi karibuni Washington iliweka vikwazo vya ziada dhidi ya kampuni za China ili kuvuruga mapato ya mafuta ya Iran, lakini Beijing ilijibu kwa ukali, ikitoa kwa mara ya kwanza amri inayozuia taasisi za China kutambua au kutekeleza "vikwazo vya upande mmoja" vilivyowekwa na Marekani.
Vyombo vya habari vya Magharibi pia vimeishutumu China kwa kuipatia Iran makombora yanayobebwa begani, kemikali zinazoweza kutumika kutengeneza mafuta ya roketi ya aina ya solid fuel, pamoja na vifaa na teknolojia nyingine zinazoweza kutumika kwa madhumuni ya kiraia na kijeshi.
China inaweza kusaidia kupatanisha makubaliano ya amani ya kudumu kati ya Iran na Marekani?
China inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kurahisisha njia kuelekea makubaliano ya kina na ya kudumu. Wakati Beijing ikiendelea na juhudi zake za kuzikaribisha Iran na nchi za Ghuba kwenye meza ya mazungumzo, pia imejaribu kutumia ushawishi wa upande wa tatu kama Saudi Arabia.
Wakati wa ziara yake mjini Beijing, Abbas Araghchi pia alifanya mazungumzo kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan. Pande hizo mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendelea na diplomasia pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya nchi za Asia Magharibi ili kupunguza mvutano na kuzuia migogoro kuongezeka.
Mazungumzo ya simu hiyo ilifanyika muda mfupi baada ya mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na China, ambapo Wang Yi alizitaka nchi za Mashariki ya Kati kuhimiza Iran pamoja na nchi nyingine za Ghuba kushiriki katika mazungumzo. Pia aliunga mkono kuanzishwa kwa "mfumo wa kikanda wa amani na usalama."
China imekuwa mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa maridhiano kati ya Iran na nchi za Kiarabu katika miaka ya hivi karibuni.
Mwaka 2023, Beijing ilisimamia makubaliano ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tehran na Riyadh, ingawa mchakato huo wa maridhiano baadaye ulitikiswa na mvutano wa kikanda uliotokana na vita kati ya Israel na Hamas.













