Matumaini ya Trump ya kuafikia makubaliano ya amani na Iran yana uhalisia kiasi gani?

Chanzo cha picha, Reuters
Madai ya rais wa Marekani Donald Trump kwamba wamepiga hatua kuafikia makubaliano na Iran, pamoja na uamuzi wake wa kusitisha 'Project Freedom' ilituliza masoko ya mafuta ya kimataifa.
Hata hivyo, matarajio hayo yalizimwa haraka na Rais huyo wa Marekani mwenyewe.
Iran ilitangaza siku ya Jumatano kuwa ilikuwa ikichunguza pendekezo jipya kutoka Washington baada ya vyombo vya habari vya Marekani, kusema kuwa pande hizo mbili zilikuwa karibu kukubaliana juu ya pendekezo la ukurasa mmoja wa wa kumaliza vita eneo la Ghuba.
Hata hivyo, saa chache baada ya kuchapisha kwenye mtandao wa Truth Social siku ya Jumanne jioni kwamba alikuwa "anasitisha project Freedom ili kuona kama makubaliano yanaweza kukamilishwa na kusainiwa," Trump alibadilisha ghafla msimamo wake na kutishia kuishambulia Iran iwapo hawatakubali pendekezo la Marekani.

Chanzo cha picha, Justin Sullivan/Getty Images
Grant Rumley, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa sera za Mashariki ya Kati wakati wa utawala wa Rais Joe Biden na pia katika utawala wa Donald Trump, aliiambia BBC kuwa "kusitisha ghafla kwa project freedom saa chache tu baada ya kutangazwa, inaashiria kuwa makubaliano yalikuwa yamepiga hatua."
Rumley aliongezea kuwa "tumeona hali kama hizi hapo awali, na mazungumzo kutibuka dakika za mwisho kutokana na sababu mbalimbali."
Tangu kusitishwa kwa mapigano kulipotangazwa tarehe 7 mwezi Aprili, Trump amekuwa akitoa ishara mara kwa mara kwamba makubaliano yako karibu kuafikiwa.
"Hakuna mchakato wa kweli wa sera"
Rumley alisema kwamba hata kama makubaliano yatapatikana ni "vigumu sana" kuyatatatua masuala yote, hasa kutokana na ugumu wa kiufundi wa makubaliano yanayohusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Wakati wa utawala wa Rais Barack Obama, ilichukua zaidi ya miezi 20 kukamilisha mkataba wa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Wataalamu wa masuala ya baharini walisema kuwa Project Freedom, iliyotangazwa Jumapili, ilikuwa na athari ndogo katika muda mfupi uliotekelezwa na ni meli chache tu zilipita katika mlango bahari wa Hormuz.
Ali Vaez, mkurugenzi wa miradi katika taasisi ya International Crisis Group, alisema kuwa majibu ya Iran kwa operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kushambulia meli na kulenga maeneo tofauti katika Falme za Kiarabu, yalimshawishi Trump kutatua changamoto hiyo.
Kulingana na Rumley "Hakuna mchakato wa kweli wa sera katika utawala huu. Rais hufanya maamuzi kwa misingi ya hisia zaidi ndiyo maana kuna mabadiliko kila wakati"













