Mzozo wa Iran: Tunachojua kuhusu shambulio la Marekani dhidi ya Bandar Abbas

,

Chanzo cha picha, IRNA

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Marekani haukuwa katika pwani ya kusini ya Iran pekee. Katika wiki iliyopita, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kwamba madaraja sita yalishambuliwa mapema Ijumaa, Julai 17, katika jiji la Khamir, Hormozgan.

Ijumaa hiyo hiyo usiku, vyombo vya habari viliripoti tena kwamba handaki mbili na madaraja mawili katika jimbo la Hormozgan yalishambuliwa.

Vyombo vya habari vya Iran na maafisa wa eneo hilo wamesema kwamba mashambulizi ya Marekani yalilenga mitambo ya umeme, mitambo ya kuondoa chumvi, madaraja, barabara, na njia za reli kusini mwa Iran.

Msemaji wa Ikulu ya White House, akijibu BBC, alikanusha kulenga miundombinu ya raia katika mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Iran, akisema mashambulizi ya Washington yanalenga "kudhoofisha uwezo wa kijeshi na vifaa vya Walinzi wa Mapinduzi."

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Iran, miundombinu ya kiraia iliyolengwa katika mashambulizi ya Marekani ni pamoja na Daraja la Giriveh kwenye njia ya Bandar Abbas-Khamir-Lar, daraja lililo karibu na kijiji cha Latidan (Kalmatli), njia ya kurejea ya Bandar Abbas-Khamir-Lar, madaraja mawili kwenye njia ya Kohourestan-Lar, daraja la kijiji cha Nimekar kwenye mhimili wa Bandar Khamir-Keshar-Bandar Abbas, na daraja la kijiji cha Maru katika wilaya ya Khamir.

Baadaye tangazo lilitolewa kuthibitisha shambulizi dhidi ya Handaki ya Shahid Mirzaei, Daraja la Mto Shur kwenye njia ya Bandar Abbas-Sirjan, na daraja la kutokea la njia tatu la Minab kuelekea Rodan,

Kuchunguza makumi ya video na picha za mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu ya Iran hutupatia picha sahihi zaidi ya ukubwa wa uharibifu huo.

Tulitambua maeneo ya baadhi ya madaraja haya kulingana na picha zilizochapishwa.

Kulingana na picha tulizopata, inaonekana kuwa, madaraja yaliyoko magharibi na kaskazini mwa Bandar Abbas yaliharibiwa katika wimbi la kwanza la mashambulizi. Katika wimbi la pili, daraja moja la upande wa mashariki na jingine la upande wa kaskazini, pamoja na mahandaki mawili yaliyo kaskazini mwa Bandar Abbas, yaliharibiwa.

Mbali na madaraja na mahandaki, njia ya reli iliyo magharibi mwa Bandar Abbas pia ilishambuliwa, na sehemu ya njia za reli iliharibiwa.

Njia zote tulizochunguza zinaelekea Bandar Abbas au ni njia za kutoka katika jiji hilo.

Vyombo vya habari vya Iran vimesema kuwa shughuli za kujenga upya miundombinu hiyo inaendelea.

Picha za baadhi ya madaraja hayo zinaonyesha kuwa lori zikichimba njia kando ya barabara ili kuwezesha magari kupita kwenye njia ya muda.

Njia ya muda kando ya madaraja yaliyoharibiwa
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Huenda ukame wa muda mrefu umesaidia Iran—bila kukusudia—kukwepa barabara zilizoharibika kwa kupita moja kwa moja kwenye njia za mtoni," Arman Mahmoudian, mtafiti katika Taasisi ya Usalama wa Kitaifa na Kimataifa katika Chuo Kikuu cha South Florida, aliambia Kitengo cha BBC Verify.

"Njia mbadala kwa kawaida huwa nyembamba, zinaweza kuhudumia magari machache, na mara nyingi huwalazimu madereva kusafiri umbali mrefu zaidi," Bw. Mahmoudian alitueleza. Matokeo yake ni kwamba shughuli za usafirishaji na mashambulizi zitaendelea, lakini kwa kwa kasi ndogo. Hali hiyo itaathiri shughuli za usafirishaji na ugavi kwa pande zote mbili, za kiraia na za kijeshi, mtafiti huyo alisema, lakini athari yake "itamaanisha kupungua kwa kasi ya usafiri wa nchi kavu na mawasiliano, japo haitasitisha kabisa shughuli hizo."

Baadhi ya njia hizi mbadala zinaonekana kuwa zilikuwa karibu na mito iliyokauka, na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na njia za muda zilizotengenezwa kando ya mito hiyo.

Afisa mmoja mwandamizi wa Marekani aliliambia gazeti la Marekani la The Wall Street Journal kuwa mashambulizi hayo yalilenga "kuziba njia za usafirishaji wa vifaa kuelekea Bandar Abbas."

Mji huu wa bandari una sifa ambazo zinaweza kuwa muhimu kwa Marekani. Bandar Abbas, ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Hormozgan kusini mwa Iran, inajulikana kama bandari kubwa zaidi ya kibiashara nchini Iran na mojawapo ya nguzo za uchumi wa baharini wa nchi hiyo.

Ukaribu wa Bandar Abbas na Lango la Bahari la Hormuz umeupa mji huu umuhimu wa kipekee kisiasa na kijeshi.

Kwa upande wa kijeshi, makao makuu ya eneo la kwanza kati ya maeneo matano ya Jeshi la Wanamaji la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yanapatikana Bandar Abbas, na hili ndilo eneo la amri ya jeshi hilo la wanamaji lililo karibu zaidi na Lango la Bahari la Hormuz.

Ni wangapi waliofariki?

Kufikia sasa, vyombo vya habari vya Iran vimetangaza kuwa watu wanane wamefariki dunia na wengine 19 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi dhidi ya madaraja katika mkoa wa Hormozgan.

Shirika la Ustawi wa Jamii la Hormozgan lilitangaza kuwa "ndugu wawili, walio na umri wa miaka 11 na 32, ambao walikuwa wanufaika wa shirika hilo, waliuawa katika shambulio dhidi ya gari kwenye daraja la kijiji cha Nimekar, Wilayani Khamir."

Shirika hilo lilisema kuwa wawili hao walipoteza maisha kutokana na "athari ya mlipuko" na walitambuliwa kuwa Maziar na Homayoun Chaterzarin.

Mohammad Moayedi, dereva wa lori la mafuta la Kampuni ya Kitaifa ya Usambazaji wa Mafuta ya Iran, pia alikuwa miongoni mwa waliofariki.

Kulingana na mmoja wa ndugu zake, alifariki katika shambulio dhidi ya Daraja la Girveh, upande wa magharibi wa Bandar Abbas. Katika video zilizotolewa kutoka eneo la daraja hilo, lori la mafuta linaonekana pia likiwa limeharibiwa vibaya.

Picha ya uharibifu baada ya shambulio dhidi ya Daraja la Girveh, magharibi mwa jiji la Bandar Abbas.

Chanzo cha picha, IRNA

BBC imeona bango la shughuli ya mazishi ya watu saba waliouawa katika mashambulizi hayo, likiorodhesha majina ya Mazyar na Homayoun Chaterzarin, Mohammad Moayedi, Abdolrahim Jafarifard, pamoja na wanawake watatu walioitwa Fatemeh Zahra Akbari, Sogand Dardemand, na Maryam Parshad Del—majina yaleyale ambayo vyombo vya habari vya Iran vilikuwa vimeyataja awali.

Siku ya Jumamosi, Julai 17, shughuli ya mazishi ya watu hao saba ilifanyika katika Msikiti wa Jameh katika kijiji cha Nimekar, Wilayani Khamir, Bandar Abbas.

Picha ya tangazo la mazishi iliyotolewa na vyombo vya habari vya Iran.

Chanzo cha picha, PGNEWS.IR

Maelezo ya picha, Picha ya tangazo la mazishi iliyotolewa na vyombo vya habari vya Iran.

Wizara ya Afya ya Iran ilisema kuwa watu 50 waliuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa katika mashambulio ya anga yaliyofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 28 Julai.

Mbali na njia za usafirishaji kuelekea Bandar Abbas, maeneo mengine ndani ya jiji hilo yenyewe pia yameshambuliwa katika siku za hivi karibuni.

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa, Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji Farzaneh Sadegh, alitembelea Bandari muhimu ya Shahid Bahonar mjini Bandar Abbas jioni ya Jumapili (tarehe 19 Julai) kutathmini shughuli zinazoendelea bandarini hapo.

.

Chanzo cha picha, CENTCOM

CENTCOM, Kamandi Kuu ya Marekani, mnamo Jumatatu (Julai 13) ilitoa video ya shambulio dhidi ya Bandar Abbas.

Uchunguzi wa BBC unaonyesha kuwa video hii ni ya wakati wa shambulio la lango kuingia Bandari ya Shahid Bahonar na Bandar Abbas.

Kiwango kamili cha uharibifu katika bandari hii na baadhi ya maeneo mengine ya Iran wakati wa mashambulizi ya hivi karibuni bado hakijajulikana kutokana na ukosefu wa picha za satelaiti, lakini Iran imelipiza kisasi kwa kushambulia baadhi ya kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Shirika lisilo la kiserikali la "Armed Conflict Location and Incident Data Project" (ACLED) lilitangaza katika ripoti kwamba Iran imelenga maeneo 35 ya kijeshi katika eneo la ghuba, ikiwa ni pamoja na Iraq, Syria na Kuwait.