Moja kwa moja, Serikali ya Kenya yaonya wageni kuwa kuingia bila viza hakumpi haki ya kufanya biashara

“Tunawahakikishia wafanyabiashara na wafanyakazi wa mataifa yote kwamba, wakiwa na nyaraka zinazohitajika, zikiwemo vibali vya kazi na leseni, wanalindwa kisheria kuendesha shughuli zao nchini Kenya”, asema Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’oei.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. UAE iliwazuia mabahari 10 wa Iran kurejea nyumbani - Iran

    .

    Chanzo cha picha, Sailor provided to BBC News

    Iran imesema mamlaka za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zilizuia kurejea kwa mabaharia 10 wa Iran waliokuwa wanashikiliwa nchini humo, licha ya maandalizi yote ya safari yao kukamilika.

    Kwa mujibu wa Ofisi ya mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika mkoa wa Hormozgan, tiketi za kurejea Bandar Abbas zilikuwa tayari zimetolewa na uratibu wote muhimu ulikuwa umefanyika kati ya maafisa wa Iran na UAE.

    Hata hivyo, ofisi hiyo ilisema kuwa katika dakika za mwisho, upande wa UAE ulisitisha kuondoka kwa wavuvi hao bila kutoa sababu yoyote rasmi.

    "Tiketi za kurejea Bandar Abbas kwa ajili ya mabaharia waliokamatwa UAE zilikuwa zimetolewa, na uratibu wote muhimu ulikuwa umefanyika kwa ajili ya kurejea kwao. Hata hivyo, katika dakika za mwisho, upande wa UAE ulizuia kuondoka kwa raia hao wa Hormozgan bila kutoa sababu ya msingi," taarifa hiyo ilisema.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema wmabahariai hao 10, ambao waliripotiwa kupotea katika maji ya Ghuba ya Uajemi wiki chache zilizopita, wako hai na wako nchini UAE.

    Mamlaka za Iran zilisema zinatarajia mabaharia hao kurejea nyumbani hivi karibuni.

    Habari za kupotea kwao zilianza kuripotiwa mwishoni mwa mwezi Agosti. Mashuhuda waliiambia Iran News Network kwamba mabaharia hao walionekana mara ya mwisho karibu na Kisiwa cha Siri.

    Kisiwa hicho ni miongoni mwa visiwa vya kusini mwa Iran vilivyopo katika Ghuba ya Uajemi, karibu na Kisiwa cha Abu Musa.

    Wakati huo, Shirika la Utangazaji la Iran liliripoti kuwa kuvuka bila ruhusa katika maji ya nchi jirani ni tukio linalojitokeza mara kwa mara kwa baadhi ya mabaharia katika eneo hilo. Hata hivyo, lilisema hali ya mvutano wa kikanda ilikuwa imeongeza wasiwasi kuhusu usalama wao.

  2. Mume wa Rais Samia kuzikwa leo Zanzibar

    .

    Chanzo cha picha, CCM

    Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atazimwa leo saa kumi Kizimkazi, visiwani Zanzibar. Mzee Hafidh alifariki dunia leo katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Zanzibar.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Hafidh alikuwa akitibiwa ugonjwa wa moyo na alifariki dunia majira ya saa mbili asubuhi.

    Licha ya kuwa mwenza wa Rais wa Tanzania, Hafidh Ameir Hassan hakuwa mtu aliyezoeleka kuonekana hadharani.

  3. Tanzania yarekodi tukio nadra la tembo mapacha kuzaliwa kwa miaka 3 mfululizo

    .

    Chanzo cha picha, TAWIRI

    Tanzania imerekodi tukio nadra la kuzaliwa kwa tembo mapacha kwa miaka mitatu mfululizo katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, jambo ambalo watafiti wanasema ni nadra kutokea kwa tembo wa Afrika.

    Utafiti unaofanywa kupitia Mradi wa Tembo Tarangire (TEP) umebaini kuzaliwa kwa tembo hao mapacha katika miaka ya 2024, 2025 na 2026.

    Mtafiti wa tembo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Revocatus Meney, amesema mradi huo unaofuatilia zaidi ya tembo 800 kutoka makundi 29 umeweza kurekodi matukio hayo katika kipindi hicho.

    Kwa mujibu wa Meney, mwaka 2024 tembo aitwaye Sakina alizaa mapacha.

    Mwaka uliofuata, tembo mapacha walionekana katika kundi linaloongozwa na tembo jike mkubwa anayejulikana kama Joyce, huku mwaka 2026 mapacha wengine wakirekodiwa katika kundi linaloongozwa na Eva.

    Meney amesema kuzaliwa kwa mapacha kwa tembo wa Afrika ni jambo nadra sana.

    “Kwa tembo wa Afrika (Loxodonta africana), uzao wa mapacha ni nadra sana kutokea, ni karibu asilimia 1 tu ya uzao wote.

    Pia, ifahamike kuwa makundi ya tembo kwa kawaida huongozwa na tembo jike mzee na mwenye uzoefu (matriarch).”

    Tembo na ndama wake

    Chanzo cha picha, TAWIRI

    Eneo la mfumo Ikolojia wa Tarangire-Manyara, ambao unajumuisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, ni miongoni mwa maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa tembo katika eneo dogo duniani.

    Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 35,000 na ni makazi ya zaidi ya tembo 4,200.

    Hii inaifanya Tarangire kuwa eneo lenye msongamano mkubwa wa tembo, huku katika baadhi ya maeneo ukikutana na tembo ndani ya kila kilomita moja ya mraba.

    Tarangire pia inafahamika kwa kuwa na tembo wakubwa na wa kipekee, wakiwemo wale wenye meno marefu yanayovunja rekodi.

    Miongoni mwao ni Ophelia, tembo jike mzee mwenye umri wa zaidi ya miaka 65, ambaye anatajwa kuwa na meno marefu zaidi nchini humo.

  4. Raia wa Burundi wamiminika ubalozini Nairobi kutafuta nyaraka

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Mamia ya raia wa Burundi wanaoishi nchini Kenya wamejitokeza katika Ubalozi wa Burundi jijini Nairobi na katika vituo mbalimbali vya huduma za intaneti wakitafuta nyaraka muhimu za usafiri na utambulisho.

    Ripoti za awali zinaarifu kuwa ubalozi huo umeanza kutoa hati za dharura za kusafiria kwa raia wa Burundi ambao hawawezi kutumia pasipoti zao, jambo lililochangia kuongezeka kwa idadi ya wanaohitaji huduma hizo.

    Hata hivyo, afisa mmoja wa ubalozi aliyezungumza na Citizen Digital amesema utoaji wa nyaraka hizo ni sehemu ya huduma za kawaida zinazotolewa kwa raia wa Burundi.

    "Sio kwa sababu ya hali ya sasa. Tunafanya hivi kila siku. Tunatoa hati muhimu za kusafiria kwa wale wasio nazo au ambao nyaraka zao zimekwisha muda wa matumizi. Hizi ni huduma za kawaida za kibalozi," alisema afisa huyo.

    Mbali na ubalozi, raia wengi wa Burundi walionekana wakijazana katika vituo vya intaneti katika maeneo mbalimbali ya Nairobi wakikamilisha taratibu zinazohusiana na nyaraka zao.

    Kwenye Barabara ya Dennis Pritt, watu kadhaa walionekana wakiwa kwenye foleni katika moja ya vituo hivyo, wakiwa na pasipoti, vitambulisho na vibali vingine vinavyohitajika katika mchakato huo.

    Mmoja wa raia hao, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema wameagizwa kuhakikisha nyaraka zao ziko sawa ili kujiandaa kwa uwezekano wa kurejea Burundi.

    Alisema wengi wao wanakamilisha taratibu za kisheria na kiutawala ili kuwa tayari kusafiri iwapo itahitajika, ingawa haikufahamika mara moja sababu ya hatua hiyo kwa idadi kubwa ya watu kwa wakati mmoja.

  5. Saudi Arabia imefanya mashambulizi nchini Yemen- Wahouthi

    Wahouthi

    Chanzo cha picha, EPA

    Wapiganaji wa Kihouthi wanadai kuwa Saudi Arabia imefanya mashambulizi ya anga katika maeneo mbalimbali nchini Yemen.

    Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saba, linaloendeshwa na Wahouthi, maeneo katika majimbo ya Al Jawf, Al Bayda, Marib na Taiz yalilengwa katika mashambulizi hayo ya anga pamoja na makombora ya kurushwa kutoka kwenye meli.

    Madai hayo hayajathibitishwa kwa njia huru, na Saudi Arabia haijatoa tamko rasmi kuhusiana na madai hayo.

    Hatua hiyo inakuja wakati Wahouthi wanavyoendelea na operesheni yao katika maeneo yaliyo karibu na Mlango Bahari wa Bab al-Mandab, njia muhimu ya usafiri wa majini inayounganisha Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden.

    Kwa mujibu wa taarifa za pande zinazohusika, mamia ya watu wameuawa katika mapigano kati ya Wahouthi na vikosi vya serikali ya Yemen tangu operesheni hiyo ilipoanza siku ya Alhamisi.

    Wahouthi, wanaojulikana pia kama Ansar Allah, ni kundi linaloungwa mkono na Iran kwa mujibu wa hasimu wao, na limekuwa likipambana kwa miaka kadhaa na vikosi vya serikali ya Yemen vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia.

    Kwa sasa, Wahouthi wanadhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen, ikiwemo mji mkuu wa Sanaa na maeneo ya pwani ya Bahari ya Shamu.

    Kwa upande mwingine, Baraza la Uongozi wa Rais wa Yemen, ambalo linatambuliwa na jumuiya ya kimataifa kama mamlaka halali ya nchi hiyo, linadhibiti maeneo ya mashariki mwa Yemen, sehemu kubwa ya pwani ya kusini na mji wa bandari wa Aden.

    Wahouthi wamesema operesheni yao inalenga kuvunja kile wanachokitaja kuwa mzingiro unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi yao. Kundi hilo pia limekuwa likidai kuyalenga masilahi ya Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu, ikiwemo meli za mafuta.

    Soma pia:

  6. Iran yaonya Korea Kusini kutoshiriki operesheni za kijeshi katika Ghuba ya Uajemi

    A

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imeionya Korea Kusini kuwa itakabiliwa na “madhara makubwa” iwapo itashiriki katika operesheni za kijeshi katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Hormuz.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baqaei, amesema Iran itachukulia uwepo wa Korea Kusini katika operesheni hizo kuwa ni shambulio na ushiriki katika kile alichokiita uchokozi wa Marekani.

    Onyo hilo linakuja wakati Korea Kusini ikizingatia njia mbalimbali za kushiriki katika juhudi za kuhakikisha usalama na uhuru wa meli kusafiri kupitia Mlango wa Hormuz.

    Soma pia:

  7. Kenya yaomboleza kifo cha mume wa Rais Samia

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Kenya William Ruto ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha mumewe, Hafidh Ameir Hassan.

    Katika ujumbe wake, Rais Ruto amesema amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Hafidh, akitoa pole kwa Rais Samia, familia yake na Watanzania wote.

    Amesema kifo hicho kimemnyang'anya Rais Samia mwenza wake wa maisha, watoto wake baba yao mpendwa, na Tanzania imepoteza mwananchi wake mashuhuri.

    “Kenya iko pamoja na ndugu na dada zetu wa Tanzania katika kipindi hiki cha majonzi,” amesema Rais Ruto.

    Ameomba Mungu awape Rais Samia na familia yake faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu, na amuimarishe Hafidh Ameir Hassan katika pumziko la milele.

    Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, pia ametuma salamu za rambirambi, akieleza kuwa anasimama na familia ya rais na wananchi wa Tanzania katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

    Hafidh Ameir Hassan amefariki Septemba 7 akiwa Zanzibar, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.

    Maelezo zaidi:

  8. Habari za hivi punde, Mume wa Rais Samia aaga Dunia

    Rais Samia

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

    Mume wa Rais Samia Suluhu Hassan, Bw.Hafidh Ameir Hassan ameaga dunia hii leo tarehe 07 Septemba, 2026.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Bw. Hafidh alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya kumbukumbu ya Emilio Mzena visiwani Zanzibar.

    Bw. Hafidh alikuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo, ambapo aliaga dunia majira ya saa mbili asubuhi.

    Mipango ya mazishi inaendelea kufanyika Kizimkazi Zanzibar.

    Zaidi soma hapa:

  9. Qatar yasema inahitaji uwezo wa kujilinda licha ya kuwa na washirika wa kimataifa

    Rais wa Marekani Donald Trump na Emir Tamim bin Hamad Al Thani wa Qatar

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump na Emir Tamim bin Hamad Al Thani wa Qatar

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majid Ansari, amesema kuwa kuwa na ushirikiano wa kimkakati na Marekani ni muhimu, lakini hakutoshi kuhakikisha usalama wa nchi hiyo.

    Akizungumza katika mkutano nchini Umoja wa Falme za Kiarabu, Ansari amesema nchi za Ghuba ya Uajemi zinapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda zenyewe licha ya kuwa na washirika wa kimataifa.

    “Kuwa na muungano wa kimkakati na Marekani ni jambo zuri, lakini hautoshi,” alisema.

    Ameongeza kuwa Qatar inaweza kuwa na washirika na washirika wa kimkakati, lakini inapaswa kujitegemea katika masuala ya usalama.

    “Kujitegemea katika usalama ndiyo njia pekee ya kusonga mbele,” alisema Ansari.

    Kauli hiyo inakuja wakati Iran ikiendelea kulenga miundombinu ya mafuta na gesi nchini Qatar tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi yake.

    Katika moja ya mashambulizi hayo, Iran ililenga kituo kikubwa cha kusafirisha gesi asilia iliyoyeyushwa nchini Qatar, hatua iliyozua wasiwasi kuhusu usalama wa usambazaji wa nishati duniani.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Serikali ya Burundi yakosoa msimamo wa Kenya kuhusu wafanyabiashara wa kigeni

    s

    Chanzo cha picha, X/MOFA BURUNDI

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Édouard Bizimana, ameikosoa serikali ya Kenya kwa kusema kuwa maelezo yake kuhusu vibali vya kazi na biashara hayajajibu madai ya vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa kigeni, hususan raia wa Burundi.

    Katika ujumbe kupitia mtandao wa X, Bizimana amesema Wakenya wanaishi kwa amani nchini Burundi na kuitaka serikali ya Kenya kuhakikisha usalama wa raia wa Burundi wanaoishi nchini humo.

    Kauli hiyo imekuja baada ya mkutano wa dharura alioufanya mwishoni mwa wiki na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akiwemo Kenya.

    Bizimana amesema aliombwa kuwasilisha wasiwasi wa Burundi kwa serikali ya Kenya na kuhakikisha raia wa Burundi hawanyanyaswi.

    Alipoulizwa na BBC Gahuza kuhusu hatua ambazo serikali ya Burundi inapanga kuchukua, Bizimana amesema ujumbe wake kupitia X ulikuwa wazi na kwamba serikali inafuatilia kwa karibu hali hiyo.

    Amesema Burundi haitasita kuchukua hatua iwapo raia wake watadhulumiwa.

    Bizimana pia amekosoa wazo la kuwaruhusu raia kufanya majukumu ya polisi, akisema hatua hiyo inaweza kuchochea ghasia, uporaji na chuki dhidi ya wageni.

    Serikali ya Kenya imesema wageni wenye vibali halali vya kazi na biashara wanaweza kuendelea na shughuli zao. Hata hivyo, wageni wanaotumia viza za utalii kufanya kazi au biashara wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

    Pia Unaweza Kusoma;

  11. Meli ya USS Ross yafika Mombasa baada ya kushiriki operesheni za Marekani dhidi ya Iran

    G

    Chanzo cha picha, US NAVY

    Meli ya kivita ya Marekani yenye uwezo wa kurusha makombora, USS Ross, imewasili katika bandari ya Mombasa kwa ziara iliyopangwa, huku Marekani na Kenya zikisisitiza ushirikiano wao katika masuala ya usalama wa baharini na utulivu wa kikanda.

    USS Ross, aina ya Arleigh Burke, iliwasili Mombasa Septemba 5 ikiwa katika operesheni za Jeshi la Wanamaji la Marekani katika eneo la Afrika na Ulaya.

    Kaimu Balozi wa Marekani nchini Kenya, Susan M. Burns, amesema ziara hiyo inaonyesha nguvu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

    “Ziara hii inaonyesha nguvu ya ushirikiano wa Marekani na Kenya na historia yetu ndefu ya kufanya kazi pamoja katika masuala ya kikanda yenye maslahi ya pamoja,” alisema.

    Burns amesema bandari za kikanda kama Mombasa zinawezesha vikosi vya Marekani kupata huduma za vifaa, kuongeza mafuta na mahitaji mengine muhimu, huku ziara za meli zikisaidia pia kubadilishana uzoefu kati ya wanajeshi wa Marekani na wenzao wa Kenya.

    Kamanda wa USS Ross, Cmdr. Pia Chapman, amesema ziara hiyo pia inawapa wanajeshi wa meli hiyo nafasi ya kupumzika baada ya muda wa operesheni.

    “Wanajeshi wetu wamefanya kazi kwa bidii kubwa katika kipindi hiki cha operesheni, wakitekeleza majukumu yao kwa nidhamu na mshikamano,” alisema Chapman.

    Ameongeza kuwa wanajeshi hao wanathamini mapokezi waliyopewa na wakazi wa Mombasa na fursa ya kushirikiana na jamii pamoja na washirika wao wa Kenya katika masuala ya baharini.

    Kenya hushiriki kila mwaka katika zoezi la Cutlass Express, linaloongozwa na Marekani na kuwaleta pamoja washirika wa kimataifa katika kuimarisha usalama wa baharini Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi.

    Marekani imesema inaendelea kushirikiana na Kenya kukabiliana na vitisho vya pamoja, vikiwemo kundi la al Shabaab na Islamic State.

    USS Ross imekuwa katika eneo la operesheni la Fifth Fleet ya Marekani tangu Aprili, ambako kwa mujibu wa taarifa hiyo imekuwa ikiunga mkono Operation Epic Fury na kizuizi cha Marekani dhidi ya Iran.

    Meli hiyo ilianza safari yake ya operesheni mwezi Machi ikiwa sehemu ya George H.W. Bush Carrier Strike Group, inayojumuisha meli ya kubeba ndege USS George H.W. Bush pamoja na meli nyingine za kivita.

    Kwa sasa USS Ross inaendesha shughuli katika eneo la Sixth Fleet ya Marekani, inayohusika na operesheni za kijeshi na majini barani Ulaya na Afrika kwa kushirikiana na washirika na mataifa mengine.

    Soma Pia:

  12. Watu watano wafariki dunia baada ya ndege ya mizigo ya Amazon kupata ajali Miami

    n

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ndege ya mizigo ya kampuni ya Amazon Air imepata ajali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami nchini Marekani, na kusababisha vifo vya watu watano na wengine watano kujeruhiwa vibaya.

    Ndege hiyo aina ya Boeing 767 300 ilitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luis Muñoz Marín mjini San Juan, Puerto Rico, kabla ya kupita nje ya njia ya kutua ilipokuwa ikitua Miami, na kugonga magari kadhaa yaliyokuwa ardhini.

    Ajali hiyo ilitokea muda mfupi kabla ya saa 14:00 kwa saa za huko, sawa na saa 19:00 GMT.

    Meya wa Kaunti ya Miami Dade, Daniella Levine Cava, amesema watu watano wamefariki na wengine watano wamejeruhiwa.

    Watatu kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.

    Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani, FAA, ilisimamisha safari zote za ndege huku vikosi vya uokoaji vikikabiliana na eneo la ajali lililokuwa likitoa moshi.

    Amazon imesema inashirikiana kwa karibu na mamlaka za eneo hilo kubaini chanzo cha ajali.

    “Kwa sasa, tunalenga zaidi familia za waathiriwa, waliojeruhiwa na shughuli zinazoendelea za uokoaji,” alisema Mkuu wa Zimamoto wa Miami, Raied Jadallah.

    Ajali hiyo imetokea wakati wa wikendi ya Sikukuu ya Wafanyakazi nchini Marekani, kipindi ambacho ni miongoni mwa nyakati zenye wasafiri wengi zaidi kwa mwaka.

    Soma Pia:

  13. Serikali ya Kenya yaonya wageni kuwa kuingia bila viza hakumpi haki ya kufanya biashara

    Waziri Lee Kinyanjui

    Chanzo cha picha, Wizara ya Biashara ya Kenya

    Serikali ya Kenya imekanusha taarifa kwamba Rais William Ruto ameamuru wafanyabiashara wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo nchini kufunga shughuli zao.

    Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’oei, amesema kauli ya Rais Ruto ilichukuliwa nje ya muktadha, akieleza kuwa ilikuwa katika mjadala kuhusu Muswada wa maudhui ya ndani ambao kwa sasa uko bungeni.

    Sing’oei amesema raia wa Burundi, mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, wako huru kuishi na kufanya biashara Kenya, mradi wazingatie sheria za nchi.

    Amesema:

    “Tunawahakikishia wafanyabiashara na wafanyakazi wa mataifa yote kwamba, wakiwa na nyaraka zinazohitajika, zikiwemo vibali vya kazi na leseni, wanalindwa kisheria kuendesha shughuli zao nchini Kenya.”

    Hata hivyo, serikali ya Kenya imesisitiza kuwa kuingia nchini bila viza, au kutohitajika kupata idhini ya kielektroniki ya kusafiri, hakumpi mgeni haki ya moja kwa moja ya kufanya biashara au kuajiriwa nchini.

    Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Lee Kinyanjui, amesema baadhi ya wageni wamekuwa wakitumia vibaya hadhi zao za utalii au uwekezaji kufanya shughuli ambazo haziruhusiwi chini ya masharti ya vibali vyao.

    Amesema:

    “Kuingia nchini bila viza au kutohitajika kupata idhini ya kielektroniki ya kusafiri, hakumpi mtu haki ya kuajiriwa, kufanya biashara au shughuli za kibiashara nchini Kenya.”

    Serikali imesema wanaotaka kufanya biashara au kuajiriwa Kenya lazima wazingatie masharti ya uhamiaji, wapate vibali vinavyohitajika na kufuata sheria zinazosimamia shughuli zao.

    Aidha, wageni watakaobainika kukiuka masharti ya viza au vibali vyao wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kufutiwa hadhi au vibali vyao.

    Wakati h uo huo, Ubalozi wa Burundi nchini Kenya umewafahamisha raia wote wa Burundi wanaotaka kurejea nchini kwao kuwa umeandaa utaratibu wa kuwapatia hati ya kusafiria ya muda, yaani laissez passer, bila malipo kuanzia leo Jumatatu.

    Kauli hizi zinakuja baada ya Rais William Ruto kuzungumzia ushiriki wa wageni katika biashara ndogo nchini Kenya, suala lililozua mjadala kuhusu nafasi ya wafanyabiashara wa kigeni katika uchumi wa Kenya.

    Soma Zaidi Hapa:

  14. Bomu la Marekani huenda lilipiga harusi nchini Iran kimakosa - Gazeti la Washington

    s

    Chanzo cha picha, Iranian Red Crescent Society

    Gazeti la Washington Post limeripoti kwa njia ya kipekee siku ya Jumapili kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha shambulio lililosababisha vifo katika harusi katika mji wa Kohstak, kusini mwa Iran, huenda lilitokea baada ya moja ya mabomu sita yaliyoongozwa kwa usahihi, yaliyorushwa na ndege za kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani, kupotoka na kukosa shabaha iliyokusudiwa.

    Kwa mujibu wa gazeti hilo, silaha sita za Marekani zililenga jengo la mawasiliano na huduma za simu lililokuwa karibu na eneo la sherehe, lakini moja ya mabomu hayo ilikosa shabaha na kulipiga jengo ambako sherehe ya harusi ilikuwa ikiendelea.

    Washington Post, likimnukuu mtu anayefahamu kwa karibu maelezo ya operesheni hiyo, liliripoti kuwa tathmini ya awali ya jeshi la Marekani ilionyesha kuwa tukio hilo lilisababishwa na "kosa la kombora" na si "kulengwa kwa makusudi kwa jengo ambako sherehe ilikuwa ikiendelea."

    Ripoti hiyo imechapishwa wakati Kamandi Kuu ya Marekani, CENTCOM, ikisema inachunguza taarifa kuhusu vifo vya raia vilivyosababishwa na shambulio hilo. Maafisa wa Marekani wamesema matokeo ya mwisho ya uchunguzi huo bado hayajatolewa.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Kombora la Iran la "kukabiliana na meli za kivita" latumika dhidi ya Marekani kwa mara ya kwanza: Mohsen Rezaei

    j

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amedai kuwa Iran imetumia kwa mara ya kwanza kombora lililotengenezwa nchini humo, linalolenga kukabiliana na meli za kivita za Marekani.

    "Masaa 48 yaliyopita, tulifanyia majaribio kwa mara ya kwanza kombora la Iran la kukabiliana na meli za kivita dhidi ya meli ya Marekani. Kombora hilo liliwasababishia Wamarekani hali ngumu sana na wakakimbia," Mohsen Rezaei alisema katika mahojiano na televisheni.

    Kamandi Kuu ya Marekani, CENTCOM, haikujibu moja kwa moja madai ya Iran. Hata hivyo, katika ujumbe uliowekwa kwenye mtandao wa X jana, ambao unaonekana kurejelea shambulio dhidi ya meli zake mbili, iliandika: "Ujumbe kwa Walinzi wa Mapinduzi uko wazi: mkifyatua mashambulizi dhidi ya meli zetu mbili, tutawawekea gharama kubwa zaidi za kiuchumi na kuharibu meli zenu tatu."

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa "hatutasita kuwalinda wanajeshi wa Marekani na, ikibidi, kuharibu meli chache za kubeba mafuta za Iran zilizo katika mazingira hatarishi."

    Aliyekuwa kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran alisema kuhusu madhara yanayoweza kuwakabili wanaosafirisha bidhaa katika eneo hilo: "Meli zitakazokiuka masharti na kufanya shughuli bila kushauriana na Iran zitaongezwa kwenye orodha ya vikwazo ya Iran na zitakabiliwa na madhara mengine, yakiwemo masuala ya bima na ugumu wa kupita katika eneo hilo baadaye."

    Soma zaidi:

  16. Iran yatangaza kuweka vizuizi nje ya Mlango wa Hormuz

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mohsen Rezaei, katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, ametangaza kuwa nchi hiyo inapanga kuanzisha eneo la "marufuku ya kuingia" nje ya Mlango wa Hormuz katika siku chache zijazo. Hatua hiyo ni ya hivi karibuni zaidi kuchukuliwa na Tehran wakati mvutano wa kijeshi na kiuchumi kati yake na Marekani ukizidi.

    Akizungumza na televisheni ya taifa ya Iran siku ya Jumapili, Mohsen Rezaei alisema eneo hilo litaanzia kwenye mstari wa kizuizi uliowekwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani na kuenea hadi katika maeneo ya Ghuba.

    Aliongeza kuwa "meli yoyote itakayoingia katika eneo hilo jipya itaongezwa kwenye orodha ya vikwazo ya Iran", lakini hakufafanua hatua ambazo Tehran itachukua dhidi ya meli zitakazokiuka vikwazo hivyo.

    Rezaei pia alisema kuwa Mlango wa Hormuz "umefungwa kabisa" na uko chini ya udhibiti wa majeshi ya Iran.

    Hata hivyo, kauli hiyo inakinzana na msimamo wa Marekani, ambao unasema kuwa meli za kubeba mafuta zinaendelea kupita katika njia hiyo muhimu ya majini.

    Zaidi ya mapipa milioni tisa ya mafuta hupita katika Mlango wa Hormuz kila siku, Waziri wa Nishati wa Marekani Chris Wright alisema Jumapili. Aliongeza kuwa usafirishaji wa mafuta kupitia njia mbadala za usambazaji umeongezeka na kufikia takriban theluthi mbili ya viwango vilivyorekodiwa kabla ya mvutano wa sasa kuanza.

    Katika hali ya kawaida, takriban moja ya tano ya mafuta na gesi asilia iliyosafishwa duniani hupita katika Mlango wa Hormuz. Hivyo, usumbufu wowote katika usafirishaji kupitia njia hiyo ya majini unaweza kuwa na athari kubwa kwa masoko ya nishati duniani.

    Kauli ya Mohsen Rezaei inatolewa wakati Marekani imezidisha shinikizo dhidi ya Iran na kukaza vikwazo dhidi ya nchi hiyo, sambamba na kuweka kizuizi cha majini kinacholenga mauzo yake ya mafuta.

    Soma Zaidi Hapa:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 7/09/2026.